Wednesday, April 14, 2010

KWA NINI WATU WANAOANA?

Kama ukimuuliza au ukiwauliza watu wanaooana, kwamba kwa nini wanaoana au ni kwa nini wako kwenye ndoa? Utapata majibu tofauti tofauti kulingana na namna watu hao wanavyotafsiri neno ndoa. Mimi sitajibu swali hilo lakini labda kile ninachokusudia kukiandika hapa huenda kikakusaidia kupata jibu la kwa nini watu wanaoana.

Kuna ukweli kwamba binadamu wamefanya kuoana kama jambo la kimaumbile, na wakilifunganisha na tendo la ndoa. Mtu anajikuta akioa au kuolewa tu. Hana haja ya kujiuliza ni kwa nini anaoa au kuolewa, kwa sababu anaona watu wanoa na kuolewa na akiangalia umri wake anaona kwamba amefikia umri wa kuoa au kuolewa hana haja ya kutaka kujua sababu. Hivi ni nani aliyepanga umri wa kuoa au kuolewa? Na umri wa kuoa au kuolewa umapangwa kwa kuzingatia vigezo gani? Je kupitisha umri huo kuna athari gani?

Ipo sababu nyingine inayotajwa kuwa watu wanoana kwa sababu wamependana, upendo ninaouona hapa ni wa mtu kumtamani mwenzie awe mwanamke au mwanaume, kwani kwetu sisi tunaamini kuwa kutamani ndio kupenda.

Hivi kama watu wanoana kwa sababu ya kupendana kungekuwa na talaka kweli? Naamini kama kungekuwa na talaka basi zingekuwa ni chache sana, na wanaoachana wasingeachana kwa ugomvi na visasi, bali wangeachana kwa upendo na wangeendelea kupendana na kuheshimiana, kwa sababau upendo ni tofauti na kutamani, upendo upo na utaendelea kuwepo na si vinginevyo.

Utakuta wanandoa wanasema “sisi tumeoana kwa sababu tunapendana” lakini baada ya mwaka wanandoa hao hawaelewani na wanakuwa na ugomvi wa mara kwa mara mpaka kufikia mmoja kumuua mwenzie, huu ndio upendo wa aina gani?

Ndoa za namna hii, hazikuwa ni za upendo bali watu kutamaniana au mtu kutamani mwili wa mwenzie, lakini kulikuwa hakuna upendo miongoni mwao.

Wengi wameoana kwa kufuata mnyororo ule ule wa kuoana kwa kufuata dhana iliyowekwa na jamii kuwa ni lazima watu waoana bila kutafuta tafsiri ya kufanya jambo hilo. Na mara waingiapo katika ndoa huona kama wamejitwisha mzigo mzito wasioweza kuubeba. Kuna zile kauli zinazotolewa ambazo wengi huita usia kwa wanandoa kwamba ndoa ni kuvumialiana, lakini watu hawajiulizi ni nini maana ya kuambiwa ndoa ni kuvumiliana, kuvumiliana kwa lipi? Kuna kitu gani katika ndoa kinachohitaji watu kuvumiliana?

Haya maswali inapaswa watu wajiulize kabla hawajaingia katika ndoa maana kuna mambo mengine hayafai kuvumilia, sasa itakuwaje nikishindwa kuvumilia? Na kuvumilia huko ni mpaka wapi?

Kuna watu wengi wanapata shida katika ndoa kwa sababu hawakujua ni kwa nini wanaoa au kuolewa, inawezekana, waliunganishwa na tendo la ndoa zaidi na sio upendo, na hapo ndipo wanpokuja kugundua kuwa walifanya makosa.

Nadhani imefikia wakati sasa ya watu kujiuliza ni kwa nini wanaoa au kuolewa, kwani ni hii itapunguza magomvi na talaka katika ndoa.Inabidi kila mtu awe na sababu yake mwenyewe ya kuamua kufanya hivyo sio kwa kuangalia sababu zilizowekwa na jamii au kusukumwa na matakwa ya jamii bali uwe ni uamuzi wake mwenyewe bila kushurutishwa au kusukumwa na matakwa ya jamii.

Kama hujaoa au kuolewa isikupe shida tulia, na ukitaka kuoa au kuolewa ufanye hivyo ukiwa na sababu yako binafsi.

8 comments:

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Enheee! UPENDO!

Ni dubwana lisiloeleweka vema! Wanaosema tumeoana kwa sababu tunapendana kuna ukweli nusu na nusu nyingine ni HISIA na hisia za upendo zikiisha basi inakuwa ni kizungumkuti.

Kwa kuwa upendo haushi wala kupungua. Na kwa wengi wetu wanadhani hisia ndo upendo kwani unaweza kuwa na hisia na usiwe na upendo KATU :-(

Anonymous said...

sio mchezo, somo limekolea!

ERNEST B. MAKULILO said...

Da Yasinta, ni swali la kujiuliza kwa kweli kwanini mtu anafunga ndoa. Mimi nipo ktk maandalizi ya kuingia ndoani. Harusi yangu ni May 1st, 2010. Binafsi si "hisia" zinazonipelekea kuoa. Nimeamua kuoa, kwani naamini kabisa mapenzi ni kuamua kumpenda mtu.

Ngoja tusubirie wadau waje na mawazo mengi zaidi tupate kujifunza.

MAKULILO, Jr.
wwww.makulilo.blogspot.com
San Diego, CA

chib said...

Nakubaliana na Chacha

watila said...

hilo ni suala gumu dada yasinta labda tuangalie ilikuwa vipi mwanzo alipoumbwa babayetu Adam ikawa yupo peke yake mola alijuwa kuwa huyu hawazi kuishi pekee yake ndo akataftiwa mama yetu hawa au?kwa hivo sisi maumbile yetu kuowana bila ya hivo ni hatari ndo maana ukaona hata wanyama huwa mume na mke mimea hali kadhalika pili tunaowana kwa sababu ipatikane njia iliyo sawa tusiwe kama ngo'mbe na punda pahala popote wanaweza kushughulikiana

Anonymous said...

Yasinta nenda kwa nuru the light ukaone arusi ilivyo noga!

Simon Penina said...

Tukikumbuka kutoka mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, kama tunavyoamini sisi wakristo kwa kufuata maandiko matakatifu (Bibli), ndoa ni jambo la pili kubarikiwa na Mungu, Baada ya kuumbwa Adamu, Mungu aligundua kuwa alikuwa na hitaji la kuwa na mwenza, baada ya Adamu kuona kila mnyama ana partiner na yeye yupo mpweke alinyongonyea na ndipo Mungu alipoamua kumpatia mwenzake.

Hivyo basi Kuoana ni upendo ambao unawasukuma watu wawili kuungana, na hii huja automatic unajikuta unapata msukumo wa aina fulani kujihisi/kupenda upate mwenzako kufuatia na umri unavyosonga. Na kwa maana hiyo basi umri ukifika usipate mwenzako wengi wanajikuta kuchanganyikiwa, kuchoka,na hata kujichukia na kuishi kwa sononeko.

Kunawiri,kustawi,amani na upendo katika ndoa ndio mwanzo wa familia na jamii bora, ndoa siku hizi zimekuwa na changamoto nyingi sana hii yote ni mpango wa shetani kuvuruga na kuleta mifarakano katika ndoa, sababu anajua ndoa zote zikiwa na amani familia,jamii, nchi na mataifa hayatakuwa na mifarakano na njama zake za kupata wafuasi zitakwama. hivyo hujitahidi sana hata kama mnapendana vipi anapandikiza vijambo vidogo vidogo kuhakikisha ndoa zinafarakana.

Markus Mpangala. said...

bado swali NDOA NI NINI? ALIVHOUNGANISHA MUNGU KWELI BINADAMU HAWEZI KUKITENGANISHA eg NDOA? mmmh sina jawabu nina swali tu