Mbona Profesa Mbele anazo mvi lakini hazifichi?
Mvi ni dalili ya uzee au ni kitu gani? Kwa zamani ingekuwa ni muhali mkubwa mtu kuuliza swali la aina hii, kwa sababu mvi zinahesabiwa kama dalili ya busara, bila shaka zikihusianishwa na kuona mengi ambayo ni wenye umri mkubwa tu waliokuwa na nafasi hiyo.
Lakini leo, mvi ni kisirani na karibu kila mtu anajaribu kuzikimbia, kwani kuendalea kuwa kijana ni sifa kubwa. Kwa sasa uzee unanuka na kila mmoja anajaribu kuukimbia kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kukana umri na kujirudisha nyuma kimatendo. Kwa kifupi hii ndiyo historia ya mvi, usiziogope bure!
Karibu rangi zote asilia za nywele zinatoka kwenye kitu kiitwacho melanin, ambacho huzalishwa na mwili kutokana na seli zinazofahamika kama melenocytes. Nywele zinapobadilika na kuwa nyeupe ina maana kwamba, melenocytes haizalishi tena melanin. Mabadiliko haya ya nywele kutoka rangi nyeusi na kukosa rangi (mvi) siyo hatua ya siku moja bali mwaka na miaka, kwani nywele moja hubadilika baada ya muda mrefu na nyingine na nyingine. Siyo hatua ya siku moja tu.
Kwa kadiri mtu anavyozeeka ndivyo ambavyo uwezo wa mwili kuzalisha melanin unavyopungua. Uwezo huu huanza kupungua mtu anapofikia umri wa miaka 35 au 40. Lakini watu wengine huanza kuota mvi wakiwa na umri wa miaka hata 20 tu. Je, hii nayo inatokana na nini?
Hili kusema kwali siyo jambo la ajabu. Ingawa kuna watu ambao huwa wanalishangaa. hata hivyo wana sayansi wanasema kwamba hawajaweza hasa kujua ni kwa sababu zipi uwezo wa mwili kuzalisha melanin huwa unashuka. Lakini wana uhakika kwamba wale wanaoanza kuota mvi kabla hawajafikisha umri wa miaka 35, kwa sehemu kubwa wanaathiriwa na urithi au kizalia.
Kama mtu ataona kwamba anaanza kupata mvi mapema sana ni dhahiri kwamba akiangalia kwenye familia yao atakuta kuna mtu ambaye naye alianza mapema kuwa na mvi. Hii itasaidia kumuonyesha kwamba mvi zake ni matokeo ya kizalia.
Pengine ni jambo la ajabu kwamba kuvuta sigara kunatajwa kama sababu ya kuchochea mtu kupata mvi akiwa na umri mdogo. Ukiwachunguza wavuta wazuri, utagundua kwamba wameanza kuota mvi mapema kuliko umri wa miaka 35 au 40.
Matatizo kwenye kiungo kinachodhibiti ukuaji mwilini, yaani thyroid huweza pia kusababisha mtu kupata mvi kabla ya kufikisha umri wa miaka 35. Pia ukosefu wa vitamin B12 unatajwa kwa sababu nyingine.
Kuna watu ambao hata kama wana umri wa miaka 60 bado hawataki kuona nywele nyeupe vichwani mwao . Watu hawa huangaika huku na kule kutafuta dawa kuondoa mvi na pengine kutumia rangi ya nywele ili kufanya rangi ya nywele nyeupe zisionekane. Huu ni kama mwendawazimu kwa kiasi fulani. Kwanini?
Kwanza kuna ukweli kwamba nyingi kati ya hizo zinazodaiwa kuwa rangi za kuondoa mvi, zina athari katika mwili wa mtumiaji. Lakini wendewazimu mkubwa zaidi ni kitendo chao cha kukataa ukweli ambao inabidi waujivunie.
Mvi bado ni dalili ya busara. Kama umefikia umri wa kuota mvi na hujafanya jambo lolote la maana na hujatoa mchango wowote wa maana kwa familia yako au jamii unamoishi ni lazima utaficha mvi zako. Kwanini?Kwa sababu utaona haya sana kuonekana kwamba umri wako ni mkubwa lakini hujafanya lolote. Tunaposema mchango wa maana hatuna maana ya fedha au mali, bali zaidi tuna maana ya mawazo ya kujenga na pengine kuandaa misingi ya kujenga kwa nia ya kuleta maendeleo baadaye.
Hebu chunguza kwa makini, utagundua kwamba watu wote wanaojaribu kuficha mvi ni wale watu ambao wametawaliwa sana na vionjo na tamaa ya miili yao kuliko maendeleo ya binadamu. Ni wale watu ambao hata kama wana fedha, hawajajua hasa wako hapa duniani kwa sababu gani. Hivi ndivyo ilivyo kwa sababu watu wa aina hii huhofia sana umri, huhofia sana kufa kwa sababu hawajakamilisha walichokuja kukifanya duniani kwasababu hawajajua bado.
Kukosa kujiamini na kujikubali kwamba wewe ni fulani na uko katika hali fulani na kiwango fulani hupelekea watu wengi kubadili majina, kuchukua makabila yasiyo yao, kujiita maarufu au kuongopa kuhusu maisha yao kwa ujumla. Mtu anayejaribu kuficha mvi ili asijulikane kwamba ana umri mkubwa hana tofauti na watu hawa.
Mtu ambaye anajiamini hawezi kuogopa kutaja umri wala kuonyesha kwamba ana umri mkubwa. Na mtu hawezi kujiamini kama hajijui yeye ni nani na kujijua kunataka mtu asiishi kwa kutazama wengine watamuonaje, bali anajionaje.
Kuficha mvi inaweza kuwa ni dalili ya mtu kuvuka kipindi fulani bila kufanya mambo ambayo kisaikolojia alitakiwa kuyafanya wakati huo. Kama mtu alitakiwa kufanya mambo hayo katika umri wa miaka 20 hadi 25 na hakufanya, kuna kawaida ya mtu kama huyo kuja kutaka kuyafanya akiwa na umri wa juu zaidi.
Kwa kuwa wakati huu mvi ni dalili kwamba ameshapita umri wa kufanya mambo hayo, atahakikisha kwamba dalili hii inafunikwa au kufutwa ili isimfedheheshe. Wengi wetu tunawajua wa waficha mvi na vituko vyao huko mitaani kwetu. Habari hii chanzo ni Jitambue.......
10 comments:
Dada Yasinta, shukrani kwa mada yako. Nikiwa ndio mwenye hii sura hapo juu, ngoja nijikongoje niseme moja mawili.
Kwanza naona mada yako imejaa mawazo ya kufikirisha. Ni changamoto nzuri, kwa jinsi ilivyogusia vipengele vya kimaumbile, kiafya, kisaikolojia kijamii, na kitamaduni.
Ili kuanzisha mjadala, napenda tu kusema kuwa mimi nilizaliwa na kukulia kijijini. Pamoja na miaka yote niliyosoma na kufundisha, Tanzania na ughaibuni, katika nafsi yangu najitambua ni mtu wa kijijini. Mila na desturi za kule ndizo zinazogusa roho yangu na kuongoza maisha yangu.
Kuhusu mvi, ni kuwa katika utamaduni wetu wa ki-Matengo, mvi zina maana sana, kama ulvyogusia. Ni ishara ya uzee, na kwa vile uzee unahusishwa na busara zinazotokana na umri mkubwa na kuona mengi, basi unapokuwa na mvi unajikuta ukiwa na wajibu wa kuishi na kufanya mambo kufuatana na mategemeo hayo.
Mvi zinanikumbusha wajibu wa kuishi kwa misingi hii niliyoitaja. Ndio maana mtu mwenye mvi akifanya jambo ambalo haliendani na hadhi hiyo, watu wanalalamika: "Huyu mzee na mvi zote hizi kwa nini amefanya hivi!"
Mvi zinanichunga na kunikumbusha wajibu wangu.
Nafahamu fika kuwa tuna tatizo la watu kuigaiga mambo kikasuku. Kwa mfano, huku Marekani, watu hawathamini uzee. Hamu ya kutaka kuonekana vijana zimetawala maisha ya watu. Sitashangaa iwapo mawazo hayo yataenea katika nchi yetu, kwa jinsi watu wanavyozidi kuwa kasuku wa mambo ya nje, hasa Ulaya na Marekani.
Mie kama mtu mwenye mvi tokea ze utoto kikubwa nilichokuwa nastukia ni watu kushangaa kuwa kwanini namvi.
Na sifichi kuna miaka fulani nilikuwa najaribu kuzing'oa.:-(
Ila siku hizi[aka miaka kibao] umri umekwenda na sichani nywele basi nastukia ZAIDI watu wengi wanashangaa kwanini sichani nywele zaidi ya kustukia nina mvi.
Ila sikubali kuwa kila wenye mvi wazifichao ni kwa sababu ya kukana umri kwa kuwa naamini ukienda UMRI hata ufanyaje unajulisha tu kwa kuwa sio mvi bali mwili mzima kuna namna unageuka na kujulisha tu UMATI kuwa weye MKONGWE ingawa una bonge la kalikiti na na panki lisilo na masihara.
Na kuna watu mvi hazijagawanyika vizuri kichwani .Kwa hiyo utakuta kitita hapa na kitita pale na mvi kadhaa moja moja kule ,...- kitu ambacho kuna niwajuao wenye mvi wenzangu ambao huonekana kama wana nywele chafu kitu ambacho huwafanya kuziweka rangi ili zote ziwe sawa. Kumbuka pia sio mvi zote nyeupe pee kwa baadhi ya watu .
Ukiniuliza miye ntasema kila mtu na staili yake ajisikiavyo kama unajisikia unapendeza zaidi kwa kuwa na nywele za rangi ya kijani na hazikuharibii kazi au kukutafsiria vibaya nini ni maisha yako kuwa utakavyo .
Kwa kuwa maisha yenyewe ya binadamu mafupi na yana fulu matatizo na kama hutaki uonekane unakipara na wigi lenye mvi halipatikani dukani,... vaa tu WIGI lenye rangi nyeusi tii hata kama una miaka themanini ikiwa kwa hivyo angalau siku kadhaa maishani mwako LINAKUFANYA unadunda mtaani umekenua meno kwa furaha.
Na kwa bahati mbaya miye na mvi zangu watu hawakosei sana umri wangu ki hivyo bado !:-(
Kama mvi ni kipimo cha BUSARA ni kwanini zifichwe?
Kumbuka kuna matatizo mengine ya watu ni uke na nawala sio busara ndio matibabu.:-(
Tatizo ni kuwa sasa hivi ni vitu vichache saana vijavyo kwa sababu za asili. Hivi sasa hata ukimuona binti huamini kama ni yeye. Kama ni wale wadanganywao kuwa ni "wazuri", basi adhaniaye hivyo bado atajiuliza kama ni "uzuri" wake ama wa maabara. Na pengine kujiuliza kama alizaliwa akiwa mdada ama alibadili jinsia.
Sababu ya kutothaminika kwa mvi ni kwa kuwa zaweza kumpata hata Paulina mwenye miezi sita kwa kuwa yasababishayo mvi sasa ni mengi (kama ambavyo umetaja baadhi).
Pengine ni wakati wa kutoficha kilicho nje na kwa walio nje kutotumia mtazamo wa nje kumjua mtu.
Ni hayo kwa sasa
Tuonane NEXT IJAYO
Hhahaa Da Yasinta umenikumbusha Mjomba wangu,yeye anamvi na umri umekwenda kidogo, lakini kamwe hawezi kuziachia watu wazione.
Atanyoa nywele zote au atapaka dawa ya kufanya nywele ziwe nyeusi....Baada ya mada hii imeniamsha itabidi siku nikienda TZ nimuulize kisa na mkasa cha yeye kuficha mvi.
Jamani miye napenda sana MVI lakini ukijitokeza hata u-mvi mmoja tu kuna mtu ananimonita na akiuona tu anasema hataki nionekane MZEE :-(
Sasa naomba walau ziote miguuni ili niwe naziona nikivua suruali...lol!
Tatizo ni kuwa wengi wetu tunaoficha mvi ni kwa sababu ya kutojiamini kama makala inavosema.
Kuna wengine:
1. Wakionekana na MVI wakisema umri wao utasikia mtu anamaka 'mie nilidhani mzee kumbe TOTO DOGO tu?' Hivo wale ambao hawataki kuonekana WATOTO bali wakubwa sasa wanaficha mvi kama ukoma!
2. Wakionekana na mvi hawatai kuwa wazee. Wanataka kuwa vijana na japokuwa umri unawatupa utaona mambo yao wanayofanya ni ya vijana na hata watoto.
Nakubaliana na Mzee Mbele (ktk medani ya elimu nadhani Prof=Mzee....lol) kuwa Mvi zinakumbusha majukumu ya mtu ktegemeana na mazingira (kabila na sehemu).
Tuko pamoja.
Kisa cha kuandika mada hii kwanza kabisa niliipenda nilipokuwa nasoma na pia ni kwa sababu mimi mwenyewe pia nimeshaanza kupata mvi miaka mitatu iliyopita. Na leo asubuhi nimeamka na nikaanza kujiangalia kwenye kioo....lol , nikaona uweupe wacha nishtuke nikaanza kuwaza hivi ni kweli nimefikia umri wa kupata MVI? Maana kuna usemi usemao ukiwa na MVI basi ni dalili ya uzee....lol. Ndo sababu nikaona ni lazima niiweke hii mada hapa ili kupata jibu sawasawa ingwa jibu nimelipata lakini inaweza majibu yakatofautiana.
sasa unamaanisha huyo pichani anaficha mvi???
hapo zamani ni kweli mvi zilikuwa kipimo cha busara lakini leo hii sio hivyo tena! nikiwatembelea wazee wabgu kama wajomba, dingwadogo, maza, bibi, majirani nk woote husinngizia utu uzima wao na nisipowapa pesa watanilaani
sasa nimewaonya wote wasemao watanilaani kwani mimi naweza kuwalaani kabla wao hawajafanya hivyo nani kasema laana anayo mwenye mvi tu?? \\
harafu sitaki usumbufu eti kwa sababu una mvi,
ila mvi sio kipimo tena cha busara au maarifa kama ilivyokuwa zamani kwani siku hizi maarifa yote na utajiri v imo mikononi mwa vijana na wenye mvi wanategemea huruma ya vijana
ila kuficha mvi ni uchizi, ni ujinga, ni kujikataa nk
Kuwa na mvi inategemea unaweza kuwa na mvi kuanzia umri mdogo kama alivyosema kaka Simon,pia unaweza kuwa na mvi ukianza kupata umri mkubwa, na pia inategemea na ukoo,kuna ukoo mwingine mvi huanza kuota wakifikisha miaka 20tu,mvi hizo zinaanza sasa hapo huwezi kusema ni uzee.
Pia kuna aina ya nywele ambazo huanza kuota mvi mapema, na kuna ambao hupata mvi kutokana na aina ya mafuta unayotumia.
Kwahiyo kuota mvi au kuwa na mvi sio lazima uwe na umri mkubwa tu,inategemea.
Heri ya Pasaka DADA YASINTA!
Napenda kuchukua nafasi hii na kuwashukuru wote kwa maoni yenu mazuri na piakwa kutochoka kutembelea hapa kibarazani kwangu MAISHA NA MAFANIKIO. UPENDO DAIMA!!
Post a Comment