Friday, April 23, 2010

HIVI NI KWANINI TUWE WATU WA MAJUNGU?


“Wanawake wakipeana michapo”

Kuna mada moja nimeisoma katika blog ya Je huu ni uungwana, ya Mfalme Mrope. Mada hiyo imenivutia sana kwa kuwa yaliyoelezwa humo, ni mambo ambayo binafsi nimeyashuhudia huku ughaibuni. Kwa kuisoma mada hii unaweza kubofya hapa

Kwa kawaida zipo tabia mbazo katika kila jamii inajulikana kuwa nazo, kwanza zipo tabia za kimakabila, kiukoo na za kijamii yaani za nchi kwa ujumla. Kwa sisi Watanzania tunajulikana kwa wenzetu huku ughaibuni kuwa ni wakarimu, wapole na wanyenyekevu kupindukia, japokuwa unyenyekevu wenyewe hauna hata tija lakini kwa kweli tumevikwa sana kilemba hiki cha ukoka, tukitofautishwa na jirani zetu wa Kenya na Uganda.

Lakini sifa hizo zinavuma kwa kuwa aidha tunawafanyia wageni au zinaonyeshwa sana kwa wageni. Hata wewe unayesoma hapa unaweza kushangazwa na sifa hizo kwa kuwa huenda zikakuacha mdomo wazi kutokana na kile unachokishuhuda au ulichokishuhudia hapo nyumbani.

Hebu jiulize kwa nini siku hizi hapo nyumbani magazeti yanayoongoza kwa mauzo ni yale yanayoandika habari za umbeya na majungu yaani magazeti ya udaku? Tuache magazeti ya udaku tuje kwenye Mitandao, hivi umeshawahi kujiuliza ni kwanaini habari au mada zinazopata wachangiaji wengi kupindukia ni zile za majungu umbeya na fitina?

Labda kama hujui leo nitakujuza maana hili nimekaa nalo mwishowe nimeona potelea mbali ngoja niliseme.

Kuna baadhi yetu sisi Watanzania tuna tabia mbaya sana ya umbeya na majungu. Ndio lazima niseme ukweli. Kama huamini hebu fanya utafiti kwa kupitia magazeti ya udaku na mitandao yenye habari za udaku utakubaliana na mimi.

Kama hutakuta habari za kujadili maisha ya mtu, basi utakuta kuna mtu kazushiwa kashfa makusudi ili kumdhalilisha au kumshusha. Kutokana na magazeti hayo kuruhusu kuletewa habari, kuna watu wanakesha usiku kucha kutafuta namna ya kumkomoa mtu ili mradi apate jambo ambalo kama likiandikwa huyo muhusika ni lazima litamuharibia.

Wakati naondoka nyumbani miaka 15 iliyopita kuja huku Ughaibuni hali haikuwa kama ilivyo leo hii. Kulikuwa hakuna mitandao na wala magazeti ya udaku. Na sifa kuu niliyoondoka nayo ni ile ya ukarimu, upole na unyenyekevu tuliyo nayo Watanzania.

Kwa kawaida unapoishi mbali na nyumbani kwenu ulipozaliwa, hususana huku ughaibuni, unapata shauku sana ya kuwajua wenzako mliotoka nchi moja au hata mji mmoja, kabila moja na kadhalika lengo ni kukumbushana habari za nyumbani kubadilishana mawazo na kutembeleana.

Lakini kumbe kukaa kwangu huku sikujua kama mambo yamegeuka, kwani, nilishangaa sana kuona kuwa kila niliyejaribu kuwa naye karibu, mweh!. Mazungumzo niliyokutana nayo yalikuwa ni ya kujadili watu. Unaweza kumtembelea mtu kwa minajili ya kubadilishana mawazo tena ukiwa umeambatana labda na familia yako lakini utashangazwa na mazungumzo ya mwenyeji wako, unaweza kukuta muda wote tangu ufike hapo ni mazungumzo ya umbeya na majungu. Hapo watazungumziwa watu mwanzo mwisho, mpaka unajiuliza hivi na mimi kesho si itakuwa ni zamu yangu hapa akija mwingine.

Unaweza kushangaa mtu anaweza kumzungumzia mtu jinsi anavyoishi na familia yake huku ughaibuni mpaka hali ya kijijini kwao alikozaliwa utadhani wametoka kijiji kimoja, kumbe siyo.

Awali nilikuwa nikishangaa hii tabia imetoka wapi, lakini baada ya kuanza kublog na Kutembelea mitandao mbali mbali ndio nikaaanza kupambazukiwa. Nilipokwenda nyumbani likizo ndio nikakutana na magazeti ya udaku. Kuanzia hapo nikajua kumbe tatizo hili limeanzia nyumbani.

Kwa huko nyumbani inawezekana ni kutokana na watu kukosa shughuli za maana za kufanya, au kutokana na ulimbukeni wa uhuru wa vyombo vya habari, na kurasa za mitandaoni, hivi vitu bado ni vigeni kwetu, lakini je kwa sisi tunaoishi huku ughaibuni hili linawezekana kweli?

Mahali ambapo kuna ushindani mkubwa wa ajira na gharama za maisha zilivyokuwa juu, bado mtu unapata muda wa kukaa na kumchunguza mtu, maisha yake na kupata muda pia wa kumjadili. Huo muda kama ungetumika katika kubuni mambo yenye kuleta tija tungekuwa wapi kimaendeleo au tungekuwa tumewawezesha ndugu zetu au familia zetu huko nyumbani kwa kiasi gani.

Sikatai zipo baadhi ya familia na marafiki ambao wamestaarabika na wanajistahi, hawa wameendelea kuwa marafiki zetu wazuri huku tukitembeleana na kubadilishana mawazo.
Tumeendelea kushirikiana kwa kila hali na mali, bila kusigishana.

Nadhani kuna haja ya kujikagua na kujirekebisha, kwani tunatia sana aibu machoni mwa wenzetu. Nakubali kuwa kila jamii inayo mikabala tofauti, lakini mikabala hiyo inapokuwa ni ya kuoneana kijicho, husuda na kukashifiana, tutakuwa tunajifedhehesha bure.

Ni vyema tukaunganisha nguvu na kuishi kama ndugu huku tukijadili matatizo ya nyumbani ili kusaidia kuleta maendeleo huko nyumbani tulipoacha familia zetu. Kwa mfano Blog na Mitandao ingetumika kama chachu ya kuhimiza maendeleo huko nyumbani kwa kuchukua yale mazuri ya wenzetu na kuwahabarisha watu wa nyumbani na kuibua mijadala yenye tija katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo huko nyumbani. Kama wote tunajenga nyumba moja kuna haja gani ya kugombea fito na kutiliana fitina miongoni mwetu?

8 comments:

Fadhy Mtanga said...

Da Yasinta umeongea jambo la maana sana. Jambo hilo nami linanipa taabu sana. Kama ulikuwa mawazoni mwangu. Nami naiandaa post ambayo ntazungumzia jambo kama hili. Nashukuru sasa ntakuwa na reference ya kutosha kuhusiana na majungu. Majungu ni roho mbaya. Majungu yanaendana na tabia ya kutopenda mwingine afanikiwe.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Papa Fadhy: majungu si roho mbaya bali ni ujinga.

Mwenye asili haachi asili. Inatokana na makuzi na uelewa wa jinsi ya kutenganisha watu na issues. Ukiangalia yote yanayosemwa kuhusu watu yanaenda kinyume na matazamio.

Bwana mkubwa mmoja alisema kuwa 'LOVE the SINNER, HATE the SIN'. Sasa kinachoonekana ni kuwa tunamchukia mtu ama tunapiga majungu kuhusu mtu badala ya kujadili hoja.

Ni wakati muafaka kuangalia upya juu ya mienendo yetu na kauli zetu.

Anonymous said...

Yasinta umepatia sana. Hii mada ni nzuri na kila ulichokisema ni kweli tupu. Majungu sio mtaji lakini watu hawakosi kupoteza muda kupiga majungu. Aliimba Banza Stona, "Elimu ya mjinga ni majungu" na ujinga upo katika nyanja nyingi sana dadangu!!
Ubarikiwe na Mungu.

Unknown said...

Mada hii umeilezea vizuri sana dada Yas. Ninajisikia vizuri na fahari kubwa kufyatua hiyo fyuzi kwani ulivyoiandika ndivyo hasa ilivyotakiwa iwasilishwe. Baraka nyingi kwako katika mchango kwa jamii. Wakati wengine watashangilia yale yasiyopendeza, ni vizuri wakakumbushwa kile ambacho wanakifahamu na kukipa kisogo. UADILIFU...!! Unapoyapika majungu makazini na kwenye familia... hata kanisani jamani? kule misikitini?? Ni hoja tu ndugu zangu!!

Anonymous said...

Majungu niugonjwa wa mapungufu ya hekima katika nafsi ya mwanadamu,ungonjwa huo unaweza ukasambazwa na kuenea kama magonjwa mengine.Chachandu yaani catalyst ni ufukara,ulofa maarifa duni,utawala mbovu au uongozi dhaifu.

Anonymous said...

Majungu ni mtaji mfu-:
1.Kwa maneno yake Mwl Nyerere walitengua jina la Sarwati katika kugombea ubunge kwa tiketi ya TANU na kumchukua mtu mwingine,Sarwati akagombea kwa tiketi ya chama kingine na kumbwaga yule aliyeteuliwa na Tanu,Tanu wakalikosa jimbo sababu ya kitu majungu.
2.Mwenda alikuwa Kamisheni wa forodha wakampikia majungu wakamfukuza kazi kwa mbwembwe,Raisi Museveni wa Uganda alijua umahili wa Mwenda,akamuandika kazi kama hiyo,Mwenda aliboresha mifumo ya makusanyo ya kodi Uganda na kuiimalisha uchumi wa nchi hiyo tukabakia kusema aa Mwenda ni Mtanzania.
3.Rwakatere aligombea ubunge wilaya ya Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM akamshinda aliyekuwa mbunge Kataraia lakini kwa mambo ya majungu wakampitisha Kataraia,Rwakatare akahamia CUF na kumshinda Kataraia.
4.Dr Slaa alienguliwa na CCM katika kuwania ubunge akaenda CHADEMA na kupata ushindi wa kishindo sababu ya majungu,leo anaitesa serikali ya CCM,na inajuta kwa maamuzi yake.
5.Brain drain ya watanzania mabingwa wa nyanja mbalimbali waliokimbilia nje si tu kuongeza mkate tu bali na majungu yasiokwisha.
6.Kuvunjika kwa Ndoa na mifarakano katika jamii yetu ya Tanzania,majungu yanachangia kwa kiasi kikubwa.
Samuel

Yasinta Ngonyani said...

Ni raha ya ajabu kuweza kuliandika hili jambo ambalo lilikuwa likinikera miaka yote hii. Na nawashukuruni mliochangia na pia msiochangia najua mmepita hapa na mmesoma. Natumaini wengi tutakuwa tumejifunza mawili matatu kwani ni kwanini usipende mwingine afanikiwe? majungu ya nini jamani tuache hayo na tuishi kwa upendo na furaha. UPENDO DAIMA!!

Anonymous said...

UMBEA MAJUNGU,USABABISHWA NA MTU KUA NA ROHO MBAYA;KUTO KUTENDA MWENGINE AFANIKIWE