Wednesday, August 24, 2011

Unajifunza nini toka kwa umchukiaye?

Kama kawaida leo ni siku ya Jumatano na ndiyo ile siku ya kipengele chetu cha marudio ya mada/makala, picha pia matukio mbalimbali. Na leo katika kupekua pekua nimekutana na makala hii ambayo binafsi imenigusa sana na pia imenifunza kitu. Nadhani nanyi ndugu zanguni mtajifunza kitu...Makala hii inatoka kwa Mzee Wetu Wa Changamoto. Kribuni sana.




Photo Credits: Relationshipplaybook.com


Kuchukia si kitu kizuri. Lakini ukweli haupingiki kuwa watu wanawachukia wenzao. Na wengine wanawachukia watu kwa kuwa wanahisi watu hao wanawachukia wao. Sijui hapo nani anatibu nini!!! Nakumbuka kusoma nukuu ya mtu mmoja ikisema "huwezi kutatua tatizo kwa kutumia njia iliyopelekea tatizo hilo kutokea." Ina maana kwa kumchukia umdhaniaye anakuchukia nawe unakuwa na chuki kama yeye. Na kwa undani zaidi ni kama vile unataka kumdhihirishia kuwa nawe unaweza na pengine unasikitika kuwa hukuanza wewe kumuonesha hivyo. Tayari umeshakuwa kama yeye. Kisha nikasoma nukuu nyingine isemayo "If you hate a person, you hate something in him that is part of yourself. What isn't part of ourselves doesn't disturb us." Hermann Hesse Swiss author (1877 - 1962)
Lakini kuna binadamu aliye sahihi katika kila atendacho? HAPANA. Hata mapacha walioungana wana tofauti japo ya fikra (na twajua kuwa fikra hufuatwa na matendo) kwa hiyo lazima tukubali kuwa hatuwezi kuwa kama kila mtu na si kila mtu anaweza kuwa kama sisi. Na Je! Kuna binadamu asiye sahihi katika kila kitu? HAPANA. Hata umuonaye si sahihi ana wafuasi wamuonaye sahihi. Ukimuona adui wengine wanamuona shujaa kwao na wanamuiga.
Sasa kama kila mtu si kamili na si kila mtu ana mapungufu kama tuyaonayo sisi (na pengine tunaona hivyo kwa kuwa tuna mapungufu kwenye sehemu hizo) unadhani wao wanatuonaje katika misimamo yetu? NAO WANATUONA TUNA MAPUNGUFU.
Sasa kama ni mtu ambaye huna nafasi yoyote ama uwezo wa namna yoyote kum'badili tabia ama mwenendo utaendelea kuumia kwa chuki ndani mwako? Si suluhu ya tatizo na pengine usipokuwa makini utajikuta unakutana na mwingine kama wa awali na kama hukujifunza kitu toka kwa huyo wa mwanzo utaendelea kuwa mhanga wa watu hao. Ni kama waibiwavyo watu kwa kuwekewa "kanyaboya" na bado hawawi makini wanapofungiwa walichonunua.
Kubwa ni kwamba kila mtu ana kitu unachoweza kujifunza toka kwake. Uwe unampenda ama unamchukia. Ni namna tunavyojijengea utashi wa kujifunza kutoka kwa watu. Na kama kuna mtu m'baya kuliko wote uliowahi kukutana nao duniani, funzo la kwanza ni kuwa "kumbe wapo wabaya zaidi ya nilivyokuwa nafikiria!?"na kuanzia hapo unaweza kuamua kujifunza kujiepusha na / kukabiliana nao.
Ukikutana na mchoyo jifunze kwamba si kila mahali utakuwa na aliye tayari kukupa.
Ukikaa na mlafi jifunze kuwa usipokuwa makini utalala na kufa njaa.
Ukimuona muuaji jifunze kuwa maisha ya binadamu hayana thamani sawa machoni pa wengi.
Ukimuona fisadi jifunze kuwa tunaweza kutafsiri tofauti neno "mali ya umma."
Na mengine mengi.
Lengo kuu hapa ni kujua kuwa kila anguko lina nafasi ya kukupa funzo la ulipoanguka na ukiamua utajifunza kuwa makini usianguke tena, na hata ikitokea ukaangua basi isiwe kwa sababu iliyokuangusha awali.

Labda ni namna nionavyo tatizo, maana namna uonavyo tatizo ......................
Jumatatu njema.

-----------------------------------------------------------------------------------------

TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO... !!!!!

9 comments:

Fadhy Mtanga said...

nimeipenda sana makala hii. ahsante sana.

Anonymous said...

kama binaadamu,kuchukia kupo,amakumchukia mtu ni jambo la kawaida.Lamuhimu hapa ni kumchukia huko ama kumchukia mtu huyo kuna tija.Yawezekana ikawa nichuki yakumsaidia,kutokana na kile unachokiona wewe usinge penda kiwe au kitokee,na hakikupotezei muda kukiendelezea kama chuki, kama adhabu.mfano mtu mlevi kupindukia na akilewa anatukana ,nk.Kwa uzoefu wangu mimi kama 'Sam' huchukia,huchukizwa, ama na kitu,au na watu.matokeo ya halihi,muhimu huwa najiuliza itanisaidia nini nikiitekeleza chuki hii? jibu hulipata kuwa, hainisaidii kitu, bali ni kujongezea,msongo wa mawazo,nakupunguza raha ambayo natakiwa kuipata niwapo hapa duniani. haraka sana husamee.Hivyo basi sipendi kumchukiza mtu,na yeye sipendi anichukize,ila hapa utakuta kutekeleza inatakiwa kweli uwe mjasiri sana,katika kuangalia maisha ya mwanadamu kwa ujumla .mfano katika msahafu wa kikristo neno,'mpende jirani yako kama unavyo jipenda'nk ,nimambo ambayo kwa hali ya kawaida ningumu,lakini taratibu unaweza kufika halihii ninayo iona mimi,ambayo haitofautiani na,usemi huu,mpende adui yako. Kaka .S.

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

Anonymous said...

LAZIMA TUCHUKIANE ILE TUJENGE KAMA HAKUNA CHUKI WOTE TUTAKUWA MANDONDOCHA,

UCHUKULIWE KIMWANA NA MSHIKAJI WAKO USICHUKIE WEWE UTAKUWA VIPI UA SIO BINADAMU KILA BINADAMU ALIUMBWA NA WIVU NA CHUKI.

DA YASINTA WEWE UCHUKULIWE MMEO UTAKUWAJE UTAFURAHI? LA KAMWE UTAMCHUKIA TU HUO ATAKAE KUCHUKULIA. LAKINI SIKUOMBEI MABAYA

Yasinta Ngonyani said...

Mtani Fadhy! hata mie nimeipenda sana tu hii mada na ndio nikaona iwe marudio.
Kaka S.! Ulichokisema ni kweli kumchukia mtu ni kupoteaza muda na pia kuumiza kicha tu.. Mpende adui yako nimependa msemo huu:-)

Mtakatifu Simon...Naona umeguna kwelikweli ..Mmmmh!

Usiye na jina wa 2011 3:09 PM nakubaliana nawe nusu nusu ni kwamba kama mtu atanichuklulia/chukuliwa kimwana mume wangu ni lazima mume wangu au huyo kimwana atakuwa anapenda hawatachukiana tu. Kwa hiyo haitakuwa busara kuwa na chuki kwasababu kama watu wakifikia hadi hatua ya hiyo basi ujua wamapendana na wewe/mimi niliyebaki sipendwi tena. Basi hata kama nikichukia haitanirudishia mume/kimwana tena . Ni wazo langu ruksa kutofautiana.

Anonymous said...

Dah! yaani umesema/umenena haswa,juu ya kuchukuliwa,mume/mke na rafiki yako.Yasinta katika kipengere hicho ndo utapima ubinaadamu wa mtu.wengi huishia kulipiza,kujidhuru na hata kupoteza maisha kwa kujiuwa,eti sababu kakataliwa au kaachwa.ukiachwa mshukuru mungu, hujuwi ''kakuepushianini,kwa huyo jamaa.wengi husema,kwamba usikubali atakuachaje,hapo ina maana sasa unataka kulazimisha,kuwa nahuyo mume/mke au kidosho wako.haya ngoja niishie hapo. Kaka S

Salehe Msanda said...

Ni sahihi kabisa
Tulio wengi tuna tatizo la kuamini kuwa sisi tuko sahihi wakati wote na kudhani wengine wanatakiwa kuwa kama sisi
Hii inasababisha watu wengi kukosa upendo wa kweli kati yetu na kuwakubali wengine kama walivyo na kama wao wanavyotupenda sisi kama tulivyo.



Kila la kheri

emu-three said...

Imekaa vyema sana hii makala, ni shule tosaha. TUPO PAMOJA

raynjau njau said...

20 Lakini ninyi hamkujifunza Kristo kuwa hivyo, 21 mradi tu mlimsikia yeye na mlifundishwa kupitia yeye, kama vile kweli ilivyo katika Yesu, 22 kwamba mnapaswa kuuondolea mbali utu wa zamani unaolingana na mwenendo wenu wa kwanza na ambao unaharibiwa kulingana na tamaa zake za udanganyifu; 23 bali kwamba mnapaswa kufanywa upya katika nguvu zinazoendesha akili yenu, 24 na mnapaswa kuvaa utu mpya ulioumbwa kulingana na mapenzi ya Mungu katika uadilifu wa kweli na ushikamanifu.

25 Kwa hiyo, sasa kwa kuwa mmeuondolea mbali uwongo, semeni kweli kila mmoja wenu na jirani yake, kwa sababu sisi ni viungo vya mtu na mwenzake. 26 Iweni na ghadhabu, lakini msitende dhambi; jua lisitue mkiwa katika hali ya kuchokozeka, 27 wala msimpe Ibilisi nafasi. 28 Mwizi asiibe tena, bali afanye kazi ya bidii, akifanya kwa mikono yake kazi iliyo njema, ili awe na kitu cha kumgawia mtu aliye na uhitaji. 29 Neno lililooza na lisitoke kinywani mwenu, bali neno lolote ambalo ni jema kwa ajili ya kujenga kulingana na uhitaji, ili liwape wasikiaji lile linalofaa. 30 Pia, msiwe mkiihuzunisha roho takatifu ya Mungu, ambayo kupitia hiyo mmetiwa muhuri kwa ajili ya siku ya kuachiliwa huru kupitia fidia.

31 Uchungu wote wenye uovu na hasira na ghadhabu na kupiga kelele na matukano na viondolewe mbali kutoka kwenu pamoja na ubaya wote. 32 Bali iweni wenye fadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma nyororo, mkisameheana kwa hiari kama vile Mungu pia kupitia Kristo alivyowasamehe ninyi kwa hiari.