Monday, December 12, 2011

TUANZE JUMATATU HII KWA MWANAMTINDO HUYU JE UNAMFAHAMU?

Kuna siku mtu lazima ujifurahishe na huyu mwanadada aliamua kujifurahisha au kuwa modo wa kijapani kwa siku moja kama mnavyomwona. Huhitaji kwenda mpaka Japani na kuwa mwana mtindo:-)


Mmmmmhhh! kweli ninafaa kuwa mJapani? mbona mie MTZ.. Aaahh kwa siku moja nafaa....





あなたについて= habari zenu. Ni raha kweli kuwa mJapani kwa siku moja. Dada Mariamu upoo???

Sunday, December 11, 2011

NAWATAKIENI WOTE JUMAPILI NJEMA...


JUMAPILI NJEMA KWA WOTE AMANI NA UPENDO VITAWALE NYUMBANI MWENU

Friday, December 9, 2011

SALAMU ZA KUSHUREKEA MIAKA 50 YA UHURU TANZANIA KUTOKA SWEDEN...

Familia hii haiko nyumba katika siku hii ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru. Ingawa mwanafamilia mmoja hayupo katika picha. MUNGU IBARIKI TANZANIA, WABARIKI VIONGOZI WAKE, HEKIMA UMOJA NA AMANI MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE IBARIKI TANZANIA ....

Thursday, December 8, 2011

KUJIFUNZA/KUJITEGEMEA MAISHA/KAZI ZA NYUMBANI!! AU MTOTO UMLEAVYO NDIVYO AKUAVYO!!

Tulipokuwa nyumbani mwezi wa sita mwishoni mpaka wa nane mwanzoni bahati nzuri ulikuwa ni msimu wa kuvuna. Tulimkuta Mzee ngonyani/babu amevuna mahindi. Na hapa mnamwona kijana Erik akimsaidia babu kupiga mahindi, kwa babu Songea Ruhuwiko.



Baada ya kazi nzito ya kupiga mahindi nguo zilikuwa zimechafuka kwa hiyo ni lazima kufua na hapa mnamwona anafua nguo zake....hapa ni Songea Ruhuwiko ....


Dada mtu naye siku yake ya dobi ikaja kama mnavyoona naye anafua nguo zake. Hii /hizi kazi ni moja ya kujifunza kuishi kwa kujitegemea.Uzuri wake maji tulikuwa nayo humu humu uani.

MAISHA NI KUJIFUNZA.

Wednesday, December 7, 2011

KWELI MAMA NI NGUZO YA FAMILIA/JAMII INATAKIWA KUBADILIKA ILIKUWASAIDIA AKINA MAMA!!


Duh! kaazi kwelikweli najiuliza mpaka sasa kesho kutwa ni miaka 50 ya UHURU lakini...MWANAMKE KWELI NI MWANAMKE..
Picha inamuonesha mama mmoja kutoka katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma akikabiliwa na majukumu mazito kama anavyoonekana katika picha hii.Ingawa mama huyu anakabiliwa na changamoto mbalimbali bado anaonekana mwenye furaha.

HIVI HUKU SIO KUBAKA KWELI?

KAMA KAWAIDA YETU NI ILE JUMATANO YA KIPENGELE CHA MARUDIO NA LEO KAPULYA UMEFANYA UKAPULYA WAKE NA KUKUTANA NA MADA HII AMBAYO AMEIPATA HAPA. Haya karibuni.
Kama kubaka ni hali ya mwanaume au mwanamke kulazimisha kufanya tendo la ndoa bila hiyari ya mwingine, basi wanawake wengi sana walioko kwenye ndoa hubakwa na waume zao kila siku.
Kubakwa huku kunatokana na ukweli kwamba wanawake wengi hulazimika kukubali kufanya tendo la ndoa na waume zao kutokana na mazingira mbalimbali yaliyo nje ya upendo.
Kuna ndoa nyingi ambazo zimekufa, ingawa wanandoa wanaishi pamoja. Zimekufa kwa sababu hazina mawasiliano kabisa. Lakini cha ajabu ni kwamba, watu hawa wanakutana kimwili na pengine kuzaa watoto. Kwa sehemu kubwa kwenye ndoa za aina hii, wanawake huwa hawako kwenye ukamilifu wao kimawazo.
Mara nyingi athari huwa ni kwa wanawake kwa sababu wao kimaumbile huishi kihisia. Kutokana na kuathirika kimawazo hamu yao ya kushiriki tendo la ndoa nayo hupotea.
Kwa kuwa hawana hamu ya kushiriki tendo la ndoa, waume zao wanapowaambia, ‘geuka huku’ (hawaongei zaidi ya hapo kwa sababu hakuna mawasiliano), hufanya hivyo. Na hufanya hivyo huku wakiwa hawataki.
Sio wengi wanaoweza kukataa kwa sababu hawakulelewa katika mazingira yanayoweza kuwafanya wakatae. Wamelelewa kwenye mazingira ambayo yamewaambia, miili yao hawana haki nayo mbele ya utashi wa waume zao!
Ukiacha mawasiliano kuna ndoa ambazo wanaume ni Malaya sana, walevi, au wapigaji. Kwenye ndoa za aina hii unaweza kukuta mwanamke bado anaendelea kuwepo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ya utegemezi au watoto. Pamoja na kuendelea kwao kuwepo, hamu ya tendo la ndoa na waume zao nayo inakuwa haipo
Lakini mwanaume hatakiwi kunyimwa mwili wake anapouhitaji. Kwa hiyo, kinachotokea ni mwanamke kufanya mapenzi kwa kujilazimisha au kulazimishwa..
Kuna kesi nyingi ambapo tumesikia juu ya wanaume kuwauwa wake zao kutokana na kuwakatalia unyumba au wakiwa wanapigana baada ya mwanamke kukataa kushiriki tendo la ndoa.
Kwenye ndoa nyingi wanawake hubakwa, yaani hushiriki tendo la ndoa bila hiyari zao. Hulazimishwa au hujilazimisha kutokana na nafasi ambayo jamii imewapa.

Ni kwa nini basi tunapozungumzia kubaka tusiwaambie wanawake na kuwashauri wawe macho na ubakaji huu ambao una athari kubwa kwao na kwa jamii wakiwemo watoto wanaozaliwa kwenye ndoa hizi za kibabe?
MWENYEZI MUNGU AKIPENDA BASI TUONANE TENA JUMATANO IJAYO...NA WOTE MNAOPITA HAPA MBARIKIWE SANA .

TAARIFA ZA MSIBA WA BABU WA BLOGA WENZETU KAKA BARAKA CHIBIRITI HUKU NYUMBANI TANZANIA!!

Picha ya Babu Blezi Chibiriti, akiwa na mwanae wa mwisho mpendwa wake Fabiani Chibiriti


Kwa habari zaidi basi soma hapa. Babu yetu ustarehe kwa amani.

Tuesday, December 6, 2011

NAWATAKIENI JIONI NJEMA WOTE:- WATU WANAJUA KUUNGANISHA MANENO /KUAMSHA HISIA EBU SIKILIZA WIMBO/MANENO HAYA



JIONI NJEMA....ILA WIMBO HUU HAKIKA...

MIMI NAAMINI ANAYETAFUTA ATAPATA ANCHOTAFUTA/ANAYEULIZA ATAPATA JIBU!!

Nimelipenda swali hili: "Jamaa aliniuliza hivi; Bro hebu nijibu swali hili....au waulize hata wana blog wenzio wa kiume; Ni kweli supu ya pweza huchajisha?
- Mimi kwakweli sijui swali hili kulijibu." swali/maelezo kutaoka hapa.


Monday, December 5, 2011

MIMI NAISHI LEO, SIISHI KESHO, WEWE JE?

Watu wengi siku hizi wanaishi katika hofu kubwa, wanahofu kuhusu familia, majirani, kazi na matarajio ya maisha yao ya baadae. Hofu imekuwa ni kubwa katika maisha ya watu wengi hivi sasa, kwa sababu ya ushindi wa kuuridhisha mwili.

Tunaweza kuondoa hofu iwapo tunatabadili mfumo wetu wa kufikiri kwa kuanza kufikiri vizuri. Kwa kawaida hofu huwa zinatuletea matokeo hasi, kwa sababu kwa kutawaliwa kwetu na hofu, tunajenga woga kwa kuiogopa kesho, na hiyo ndio sababu watu wengi huanguka katika maisha.

Woga kuhusu kesho hauna maana, kwani kesho huwa haiji kwa namna tunavyotarajia. Sisi huwa hatuishi kesho bali tunaishi leo. Wakati unawaza nini kitakachokutokea kesho, mwezi ujao au mwaka ujao, unakuwa unajiwekea vikwazo katika kufikia malengo yako kwa kuvuruga mfumo wako wa kufikiri.

Kwa hiyo si vyema kutumia hata sekunde yako moja kuhofu kuhusu kesho, ishi leo. Kimsingi huwezi kufanikiwa na kufikia matarajio yako iwapo maisha yako yatakuwa yametawaliwa na hofu za kesho, na maisha yako yatakuwa yamewawaliwa na hofu za kesho basi utakuwa unapoteza muda wako bure, na matokeo yake unakufa ukiwa hujayafikia malengo yako ya kuwepo hapa duniani.

Lakini hata hivyo ni vyema ukumbuke kuwa katika kufikia malengo yako, ukubaliane na changamoto za maisha, kamwe zisikutie hofu, cha kufanya ni wewe kuyaona matarajio yako kwa taswira ya jicho lako, jiamini na lione kabisa kwamba lengo lako limefanikiwa. Ishi kila siku kwa namna inavyokuja, kwani kesho ni jina tu la siku inayofuata, kuihofia na kuiogopa ni UJINGA tu.
Kwa nini nasema ni UJINGA? Ni kwa sababu hakuna hata mmoja wetu anayejua kesho au kesho itakuwaje.

Sunday, December 4, 2011

HONGERA KWA SIKU YAKO YA KUZALIWA YASINTA MDOGO (KIBIBI)



Hongera kwa siku ya kuzaliwa Wajina wangu. Huyu binti ni binri wa kaka yangu. Kaka ambaye aliniachia ziwa na huyu ni mtoto wake wa pili na leo anatimiza miaka 8. Ila nampa pole kwa kuitwa YASINTA...najua mnajua kwanini nasema hivyo. HONGERA WAJINA:-)

Saturday, December 3, 2011

NATAMANI NINGEPATA MLO HUU MCHANA WA JUMAMOSI HII LAKINI....SINA. SIJUI NIFANYEJE?

UGALI......




......KWA DAGAA´


Nimepita mara mia kwa dada Rachel na kumezea meta au kujaribu kula kwa macho na nimeshindwa maana nina unga lakini sina dagaa...

JUMAMOSI NJEMA KWA WOTE HATA KAMA BILA UGALI NA DAGAA:-)

Friday, December 2, 2011

TUWE PAMOJA NA KAKA Addson Noel Omari ( Mfalme Mrope ) KWA MAOMBI YA MSIBA WA MAMA MZAZI HUKO NYUMBANI TANZANIA!!

Kaka Mrope pole sana kwa msiba wa mama yetu mzazi kwani naamini mama yako ni mama yetu.Katika pita pita zangu nimekutana na habari hii ya kusikitisha.
-----------------------------------------------------------------------------------------------
TAARIFA YA MZIBA
Napenda kuwataarifu ndugu zangu na marafiki popote mlipo kuwa nimepatwa na msiba wa mama yangu mzazi Shamsa binti Hassan aliyefariki huko nyumbani Tanzania leo tarehe 2/12/2012. Habari za kisomo na dua zitawajia baadae. BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA...Kwa pole napatikana 301 222 7739.... nahitaji maombi yenu.Wenu, Addson Noel Omari ( Mfalme Mrope ) http://tustaarabike.blogspot.com/

UJUMBE WANGU WA IJUMAA YA LEO UNASEMA!!!!

Ndoto zetu ndizo zinazotufanya tusonge mbele.
NAWATAKIENI IJUMAA NJEMA NA MWANZO WA MWISHO WA JUMA PIA. NA WOTE MTAKAOPITA HAPA MUWE NA AMANI.

NI IJUMAA YA MAJONZI MSANII MR EBBO AFARIKI DUNIA


Nimepatwa na mstuko pia majonzi makubwa sana baada ya kusikia kifo cha msanii huyu kwani ni moja ya wasanii niliokuwa nikiwasdikiliza kila mara. NAPENDA KUTOA POLE KWA FAMILIA YA MR EBBO NA NDUGU PIA MARAFIKI WOTE. MAREHEMU NA ASTAREHE KWA AMANIPEPONI AMINA. TUTAKUKUMBUKA DAIMA.

Thursday, December 1, 2011

PICHA YA WIKI:- SARE SARE MAUA ASIYEJUA KUCHAGUA!!

huyu ni Yasinta Ngonyani (Kapulya) picha imepigwa jana 30/11/2011.
Nilipoina picha hii ya chini nikatamani kama ndiyo ningekuwa mie kwani napenda sana mvao huu/vazi hili la asili ya kimasai. Nikaona ngoja nami nivae mgololi wangu..... ila naona kama naogopa kitu katika picha hii...mmmmhhh!!!

huyu ni ..Mhe. Namelo Sokoine
...ila naona mwenzangu mgolori wake una urembo, halafu ana mkoba, pia zaidi ya yote hiyo ya shingoni /hiyo nimeivizia kila mara lakini sijaipata bado.... Ila nadhani kidogo picha zinafanana.. Au?

Wednesday, November 30, 2011

SWALI LILILONIKERA KWA MIAKA MINGI!!!

Nimeshindwa kuvumilia mwenzenu, kwani hili jambo/swali limekuwa likinikera miaka sasa.

Ni hivi:- Hivi kwanini mwanamke mjane anweza kuishi peke yake mudamrefu au hata milele bila kuolewa tena na mwanamume mwingine? Maana ukiangalia asilimia kubwa ya wanaume wajane huwa hawaishi muda mrefu peke yao huwaa wanaoa tena.

Nina mfano mmoja, bibi yangu mzaa mama:- Babu alifariki mwaka 1980 na bibi amekuwa mjane mpaka Mwenyezi Mungu alipomchukua 2005. Na mafano mwingine nilionao ni baba mmoja nimfamuye mkewe alifariki 2004 na yeye 2006 tayari alipata mwanamke mwingine na kufunfa naye ndoa 2008.
Je?Hapa ndo kusema wanawake wanawapenda zaidi waume zao/wana uchungu zaidi kuliko wanaume?
NAOMBA TUJADILI KWA PAMOJA SWALA HILI JAMANI... KAPULYA WENU!!!!!

HISTORIA :-SONGEA MBANO KIONGOZI SHUJAA WA WANGONI ANAYESTAHILI KUENZIWA DAIMA.

Kama kawaida ni JUMATANO YA KILE KIPENGELE CHETU CHA MARUDIO na leo nimeona tubaki SONGEA na kujikumbusha historia hii. Katika mipitopito nimekutana na mada hii hapa. Na nikaipenda na nimeona si mbaya nikiweka hapa Maisha na Mafanikio. Karibuni sana ndugu zanguni.



HUWEZI kuilezea na kuikamilisha historia ya vita ya Majimaji na ukombozi wa nchi yetu bila kumtaja shujaa wa kabila la wangoni Nduna Songea Mbano ambaye jina lake lilipewa hadhi ya kuuita mji wa Songea kutoka kwenye jina la Ndonde mwaka 1906.
Kiongozi huyo alikuwa ni miongoni mwa wasaidizi ( Nduna) 12 wa Chifu wa kabila la wangoni (Nkosi) chifu Mputa bin Gwezerapasi Gama.
Ambapo wasaidizi wake wengine walikuwa ni Mgendera Mawaso Gama, Kohongo Magagura, Mputa Mkuzo Gama, Magodi Mbamba Mbano, Mtekateka Muyamuya Tawete, Fratela Fusi Gama.
Manduna wengiwe ni Maji ya kuhanga Komba, Zimanimoto Gama, Mpambalyoto Soko Msalawani, Mtepa Hawaya Gama na Nduna Mkomanile ambaye alikuwa ni mwanamke pekee kuwa nduna.
Nduna Songea Mbano alikuwa ni maarufu kuliko manduna wenzake na hata chifu Mputa Gama alikuwa anamtegemea sana katika kuwaongoza Manduna wenzake na wapiganaji wa vita ya Majimaji kiujumla.
Mhifadhi kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Maji maji Songea Philipo Maligissu akizungumzia maisha ya Nduna Songea Mbano katika viwanja vya Makumbusho hayo,alisema kuwa Songea Mbano akiwa miongoni mwa manduna alitokea kuwa maarufu sana ukilinganisha na wenzake 11 ambapo sifa kubwa iliyo mpa umaarufu ili kuwa ni ueledi na ushadi wake wa kuandaa mikakati ya kivita, na maamuzi mazito yasiyoteteleka na kuyasimamia maamuzi hayo kikamilifu.
Kwa umakini mkubwa Nduna Songea Mbano aliweza kufanya kile alichokuwa akikiamini na uthibitisho wa jambo hilo ulianza kujitokeza julai 12, mwaka 1897 katika viwanja vya Bomani kwa mkuu wa Wilaya wa wajerumani luteni Engelhardt.
Maligissu anasema kuwa kwa rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa tarehe hiyo Nduna Songea Mbano alionekana kuwa ni mtu wa kipekee katika idadi ya Manduna 11 ambao walikuwa wasaidizi wa chifu Mputa Gama kwa kitendo chake cha kubisha wazi wazi tamko la utawala mpya wa wajerumani la kutaka wangoni wakomeshe biashara ya utumwa.
Siku hiyo ilikuwa ni siku rasmi ambayo utawala wa kikoloni ulikuwa unaanzishwa katika mji wa Songea wakati huo ulikuwa unaitwa Ndonde na Mkoa wa Ruvuma kiujumla chini ya Luteni Engelhardt wa Jeshi la Kijerumani ambaye alikuwa ndiye Mkuu wa Jeshi kwa kanda ya Kusini.
Wajerumani walipofika kuanzisha makoloni yao katika maeneo ya ukanda wa kusini walikutana na msuguano mkubwa kutoka kwenye tawala za kiafrika hususani tawala za wangoni.
Maligissu anasema kuwa wangoni walikuwa na tabia ya kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara kuvamia na kuchukua mateka na kuwaleta Songea kuwafanyisha shughuli mbalimbali katika maeneo yao ya utawala.
Tabia hiyo ya wangoni iliwachukiza sana wajerumani kwani wajerumani walikuwa wanaheshimu sana makubaliano yaliyofikiwa kutoka kwenye mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 hadi 1885.
Katika mkutano huo moja ya makubaliano yaliyofikiwa ni pamoja na kila nchi yenye koloni barani Afrika ni lazima ikomeshe biashara ya utumwa na kwa kuwa wajerumani walikuwa wamejiimarisha sana katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Hivyo walipokuja Ruvuma wakatoa tamko kwa wangoni kuwa hairuhusiwi na haitaruhusiwa tena kwenda Lindi,Mtwara na maeneo mengine kuchukua mateka na kwamba mateka wote waliochukuliwa na wangoni waachiwe huru.
Baada ya wajerumani kutoa tamko hilo ndipo Nduna Songea Mbano alipojitokeza waziwazi na kusimama kujibu hoja iliyotolewa na wajerumani kuhusiana na tamko hilo.
Nduna Songea Mbano alisema kuwa utawala wa kabila la wangoni hauwezi kutekeleza tamko hilo na kwamba msimamo wao ni kutoutambua utawala mpya wa kijerumani na tamko lao.
Aliendelea kusema kuwa ujio wa utawala wa wajerumani na kutoa tamko hilo kwa wangoni una lengo la kudhoofisha utawala wa Machifu na Manduna katika maeneo yao kwa kufuata kanuni zao za kimila na kitamaduni.
Kuanzia hapo wajerumani walimuona Nduna Songea Mbano kuwa ni mtu hatari sana katika utawala wao mpya na walimuweka alama maalumu na kuanza kumfuatilia nyendo zake.
Kwa sababu alionekana kuwa kiongozi shupavu na mwenye misimamo mikali na anayezingatia heshima na utu wa kabila lake bila kuyumbishwa.
Alionekana kuwa ni mtu wa pekee mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira yoyote kwa kushirikiana na wananchi wake ambao walikuwa wana mheshimu sana na kumsikiliza.
Maligissu anaeleza kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha wananchi wake na kuwa na umoja, upendo na mshikamano na kwamba alikuwa akiwaelekeza jambo wanalifanya kwa umakini na kwa ukamilifu.
Anaendelea kusema kuwa kuanzia hapo Nduna Songea Mbano aliendelea kujizolea umaarufu mkubwa na wajerumani baada ya kuona hivyo na kitendo cha nduna Songea kutamka kuwa yupo tayari kwa lolote lile na hawezi kukubali kuona tawala za kiafrka zinadharauliwa na wakoloni kwa namna yeyote ile.
Waliamua kuwaalika Machifu na Manduna wote Julai 13 mwaka 1897 Bomani kwa mkuu wa Wilaya wa kwanza katika nchi ya ungoni ambaye pia mkuu wa jeshi la wajerumani katika nchi ya ungoni Luteni Engelhardt na kuwaambia kuwa mtu yoyote katika eneo lake atakaye kaidi amri yeyote kutoka kwa uongozi mpya wa wajerumani basi atapigwa risasi, kunyongwa hadi kufa au kufungwa maisha .
Siku hiyohiyo Machifu na Manduna walichukuliwa hadi juu ya mlima wa shabaha wa chandamari uliopo katikati ya mji wa Songea na kuwaonyesha nguvu ya risasi inavyoweza kufanya kazi katika mwili wa binadamu na kwamba silaha za kijadi na kimila za wangoni haziwezi kufua dafu mbele ya silaha hizo.
Licha ya wajerumani kutoa mkwara na vitisho vingi Nduna Songea Mbano aliendelea kushikilia msimamo wake wa awali wa kuchukia utawala wa wajerumani na kuutetea utawala wa kiafrika mpaka vilipo kuja kutokea vita vya Majimaji.
Nduna Songea Mbano alitoa ushindani mkubwa sana katika vita hivyo na alionyesha ustadi mkubwa kwenye mapigano na katika sehemu zote ambazo wajerumani walipigana wameandika kuwa hawakupata ushindi mkubwa kama waliopata katika Mkoa wa Ruvuma zamani nchi ya ungoni.
Ambapo viongozi wao hawa kuwa wanafiki kwani walijitoa kikwe likweli kusaka ukombozi wa kweli na hadhi ya tamaduni zao mpaka dakika ya mwisho, ndio maana idadi ya watu walionyongwa katika historia ya nchi yetu walitoka katika himaya ya Nduna Songea Mbano na ushahidi upo wazi kuwa watu 67 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa akiwemo Nduna Songea Mbano.
Katika kuonyesha kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa na uwezo wa kufanya mambo kwa uweledi mkubwa bila kusaliti dhamira yake kuanzia mwaka 1897 alianza kuandaa jeshi lake la kupambana na utawala wa wajerumani.
Akaanza kuchukua watu wake na kuwapeleka juu ya mlima wa chandamari, kufanya nao mkutano na kutoa mafunzo ya kivita na kuwaelekeza kwa nini wanawachukia wajerumani.
Katika mlima huo ndipo alipoeleza kwa kina madhara ya kuukubali utawala wa wajerumani na kutoa ahadi kwa wananchi wake ya kuwaondoa wajerumani kwa lazima na kwamba alisema kuwa eneo hilo ni lao na wamekuwa wakiishi siku zote chini ya utawala wao sasa inakuwaje waletewe utawala mpya wakati hawahuitaji.
Chokochoko hizo zilizaa vita vya Majimaji na wakati mapigano yakiendelea wajerumani walianza kumtafuta Nduna Songea Mbano ili wamkamate na kufanya nae mazungumzo ya maridhiano.
Kumbe Songea Mbano alikuwa amejificha kwenye pango kubwa lililopo kwenye mlima wa chandamari na usiku hukutana na askari wake nje ya pango hilo na kuwapa mafunzo zaidi ya kivita.
Maligissu anaeleza kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa anaishi na Ndugu zake katika eneo la Mateka lililopo katika eneo la Manispaa ya Songea na wakati wa vita ndipo Songea Mbano alikuwa anajifisha katika pango hilo ili wasimkamate mpaka atakapotimiza malengo yake.
Wajerumani walipoona wanaendelea kupata madhara makubwa kutokana na vita hivyo waliamua kuwakamata ndugu na familia yake, chifu Mputa Gama na Manduna wengine na kuwafunga gerezani kwa lengo la kumdhoofisha Nduna Songea Mbano.
Baada ya wajerumani kumdhoofisha Nduna Songea Mbano alipata taarifa zote na akaamua kutoka kwenye pango hilo na kwenda kwa wajerumani na kutaka watu wake waachiwe ili mapigano yaendelee.
Ndipo naye alipokamatwa na kuwekwa gerezani na kwamba utawala wa wajerumani waliamua kuwa hukumu wafugwa hao kunyogwa hadi kufa akiwemo chifu wa kabila la Wangoni.
Wafungwa hao waliamuliwa kuchimba shimo kubwa bila kujua kuwa shimo hilo ndilo litakalotumika kuwa kaburi lao na ilipofika siku ya kunyongwa walinyongwa kwa zamu siku mbili na maiti zao kwenda kuwekwa kwenye kaburi hilo hadi walipofikia 66 ndipo walizikwa kwa pamoja kwenye kaburi hilo.
Nduna Songea Mbano walimuacha ili aweze kuwasaidia kufikisha malengo yao kwa wananchi kwani waliamini kuwa yeye ni kiongozi jasiri na anayependwa na watu wake na kusikilizwa vizuri.
Toka siku hiyo walipomuacha bila kumnyonga Nduna Songea Mbano aliwasumbua sana wajerumani na kutaka naye anyongwe kama ndugu zake kwani haoni sababu ya yeye kuishi wakati ndugu zake wamekufa na kusema kama hawataki kumnyonga basi hataki kula wala kunywa chochote mpaka afe.
Ndipo wajerumani walipoamua kumnyonga na kumzika katika kaburi la pekee yake wakiamini kuwa ni mtu wa pekee mwenye ushujaa na maamuzi mazito na misimamo isiyoyumba na walimuenzi kwa kubadilisha jina la mji wa Ndonde na kuubatiza jina la Songea ambapo mpaka sasa linatumika kuuita mji huo wenye hazina kubwa ya historia na utalii wa kitamaduni
Kila mmoja wetu hana budi kujiuliza ni mafundisho yepi anaweza kuyapata katika historia ya nchi yetu na mchango mkubwa alioutoa Nduna Songea Mbano na je kizazi kilichopo tunao ule moyo wa ushujaa , uzalendo heshima na usawa kama ilivyo kuwa kwa mababu zetu basi inatupasa tutimize wajibu wetu kikamilifu ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na uwepo wetu duniani.
TUKUTANO TENA JUMATANO IJAYO NA NAWATAKIENI MWISHO MWEMA WA MWEZI HUU NA MWANZO MWEMA WA MWEZI WA KUMI NA MBILI.

Monday, November 28, 2011

ULIJUA KAMA SONGEA KUNA HIFADHI /MBUGAYA WANYAMA?


Nimeishi miaka mingi Songea nilikuwa sina habari kama kuna mbuga ya wanyama. Mbuga hii ipo nje kidogo ya Msamala . Kwa hiyo nasi tulipata bahati na kuingia hapa kwa msaada ya mwenyeji wetu ndugu Sunday Hebuka.


Hili ni jengo/au niseme ni ofisi ndipo ambapo unalipa....Na pia unaona magari kwa ajili ya watalii........


Ila sisi tuliona ni vizuri kutembea kama unavyoona tupo katika msululu hapo...kusaka wanyama....

Msafara unaendelea hapa ni kadaraja...
Na hapa ni mto Ruhila kwa ubunifu wao wameweka mawe ni kama daraja vile. Ila inabidi uwe shupavu kwani kulikuwa na utelezi. Hapa ni lazima kuvua viatu pia...Siku hii tulifurahi sana kuwa katika eneo hili ambalo hatukujua kama lipo...Ushauri ukifika Songea usikose kuchungulia hapaa.



Sunday, November 27, 2011

NAWATAKIENI JUMAPILI HII YA KWANZA YA MAJILIO PIA YA MWISHO KWA MWEZI HUU PIA NAPENDA KUWASHUKURUNI KWA USHIRIKIANO WENU KWA SALA YA FAMILIA PAMOJA

Milango imefungwa, Ea Bwana.Yule mtoto mchanga amelala, tunajisikia salama.Tuna raha ya ndani, kwani tumeshiba, chakula kilikuwa kizuri, kinatuletea faraja.
Huu nio wakati wa kukugeukia , mwishoni mwa siku hii ya leo, kama familia-familia yako, ambapo Kristu anaishi.
Kwa ajili yetu, kila moja wetu Bwana, tunakushukuru. Kwa ajili ya siku hii ya leo, iliyojaa mambo mengi, mema na yasiyo mema sana. Kwa yote tunakushukuru.
Tunapoangalia nyuma, mara nyingine, ni rahisi kuona kwamba ingaliwezekana kuwa vizuri zaidi. Hapa na pale, tumeshindwa kukupendeza, kwa neno la hasira. Na lile ambalo hatukulitimiza.
Tunasikitika, Bwana tusamehe. Kwani tunahitaji upendo wako. Tunakuhitaji wewe, ukae nasi, ili utulinde, utubariki, kwani wewe ndiwe kuta za kweli na paa za nyumba yetu.
Utubariki tulalapo, utujalie ndoto zetu ziwe za faraha. Na utujalie tuamke kesho tukiwa na uzima mpya tele. Nguvu mpya na starehe mpya. Ili tuweze kuishi tena siku nyingine.

Baada ya hapa napenda kuwashukuruni wote kwa upendo wenu, ushirikiano wenu kwa kushirikiana nami kwa Wiki hii inayokwisha leo kwa maombolezo ya mdogo wetu Asifiwe. AHSANTENI SANA. PIA NAWATAKIENI JUMAPILI HII YA KWANZA YA MAJILIO IWE NJEMA NA MBARIKIWE SANA WOTE MTAKAOPITA KATKA BLOG HII YA MAISHA NA MAFANIKIO. AMINA

Saturday, November 26, 2011

LEO NI 26/11/2011 NDIYO SIKU ALIYOZALIWA ASIFIWE NGONYANI

Tarehe 26/11/1989 ilikuwa siku ya furaha kwa familia ya Ngonyani kupata binti mwingine ambaye ni Asifiwe. Ni hisia za ajabu sana mwaka huu bila kumpigia simu na kumtakia HERI kwa siku yake ya kuzaliwa ambayo ni leo. Na hii ni sababu kubwa nikaona wiki nzima iwe yake kwa vile imekuwa wiki ya matukio matatu kwa mpigo. Kweli Mwenyezi Mungu ndiye muweza ebu jaribu kuangalia Asifiwe alizaliwa 26/11/1989 siku ya jumapili ,na leo na jumamosi 26/11/2011 ange/ametimiza miaka 22 halafu sasa siku aliyozikwa ni 26/3/2011 siku ya jumamosi tena…HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA MDOGO WETU,DADA YETU,MAMA MDOGO WETU, SHEMEJI YETU, PIA RAFIKI YETU. NA USTAREHE KWA AMANI, TUTAKUKUMBUKA DAIMA.
UA HILI NIMETUMIWA NA KAKA ISSACK CHE JIAH AMBAYE PIA NI MSOMAJI WA MAISHA NA MAFANIKIO. AHSANTE SANA.

Thursday, November 24, 2011

MWAMBA ULIOPASUKA...



TUMTEGEMEE MUNGU WETU KWA KILA TUTENDALO. PAMOJA DAIMA.

Wednesday, November 23, 2011

TUTAKUKUMBUKA DAIMA ASIFIWE NGONYANI!!!

Kwa vile leo ni JUMATANO NA NI JUMATANO YA KIPENGELE CHA MARUDIO YA mada/makala/matukio mbalimbali. Basi JUMATANO YA LEO imeangukia kuwa tarehe 23/11 ambayo si mara nyingi inakuwa hivi. nasema hivi kwasababu 23/3/2011 siku ya jumatano tuliondokewa na mpendwa wetu Asifiwe na leo imetimia miezi nane na imeangukia siku ya jumatano na tarehe 23/11-11 kusema kweli nimeshikwa na butwaa kidogo maana si mara nyingi inakuwa hivi. Kwa hiyo nimeona si vibaya kama tukimkumbuka Asifiwe wetu.

Hapa ndipo mahali alipopumzika Asifiwe katika safari yake ya mwisho. TUTAKUKUMBUKA DAIMA ASIFIWE.KWANI UPO NASI KIROHO ILA SI KIMWILI. PUMZIKA KWA AMANI MDOGO WANGU/WETU.

Tuesday, November 22, 2011

ASIFIWE NGONYANI (1989- 2011). Kioo kingine cha maisha yetu, kwa maisha yetu na wenzetu

Kama jana jumatatu nilivyosema ni wiki ya kumkumbuka mdogo wangu Asifiwe Kwa hiyo nimeona si mbaya kama tukimkumbuka Asifiwe kwa mada hii iliyoandikwa na Mzee wa changamoto.

"..see you in ZION, holding hands together standing by MY FATHER'S SIDE. Meet you in ZION singing songs together....." LUCIANONi mwaka mmoja na siku 24 tangu ilipobandikwa MAKALA HII YA KUMSHUKURU MUNGU KWA KUFANIKISHA UPAUSAJI WA Dada Mdogo Asifiwe Ngonyani. Leo hii NAMSHUKURU MUNGU kwa maisha na mapumziko ya Dada Asifiwe, ambaye aliaga dunia Machi 23 na kuzikwa Machi 26.Dada wa Asifiwe, ni Da Yasinta Ngonyani. Sio bloga mwenzangu tu, bali ndiye anayewasiliana na familia yangu kuliko bloga yeyote. Twawasiliana kwenye chat, kwenye simu na hata skype ambapo huwa tunaongea mara kwa mara.Mara nyingi tumezungumza kuhusu Asifiwe.Na kila mara alikuwa akitujulisha maendeleo yake. Na kwa kila wakati ambao afya ya Da Asifiwe ilikuwa ikihitaji msaada wa uangalizi wa watabibu, Da Yasinta alikuwa mnyonge. Na nakumbuka siku ambayo alisema hakuweza kuweka bandiko kwenye blogu yake kwa kuwa hakuwa na furaha. Baadae tukawasiliana kuwa ameweza kuongea na Asifiwe na alikuwa na furaha kusika maendeleo yake ni mema.Lakini juma hili, taarifa zimefika kuwa ASIFIWE HATUNAYE. Binafsi niliumia sana. Nilikuwa sijapata kuonana na Asifiwe, lakini mazungumzo juu yake kutoka kwa Dadake na Da Koero yalinifanya kuwa karibu naye kwa namna ya pekee.Lakini kwa wote hawa (Yasinta na Koero), nililogundua ni namna ambavyo FURAHA ZAO ZILIATHIRIWA NA HALI YA ASIFIWE. Kwa maongezi nao, niligundua juu ya maisha yake ambayo ndicho kilikuwa kivutio kikubwa kwa ndugu zangu hawa ambacho ni TABIA. Da Yasinta hakuwa tu akimzungumzia Asifiwe kama ndugu yake ambaye ni wao wawili pekee wa kike katika familia, lakini alikuwa akimzungumzia kama RAFIKI.NA HILI NDILO NILILOJIFUNZA NA NINALOJIFUNA.Ninapomuwaza ASIFIWE, nikimuwaza Dada Yasinta na dugu, jamaa na marafiki wakimlilia, naona AKISI YA MAISHA YA ASIFIWE. Naona jambo ambalo sisi sote twatakiwa kujifunza kutoka kwa Asifiwe, kisha kuona maisha yetu na ya wali walio kwetu yakibadilika.KILIO cha kumlilia Asifiwe ni ishara nyingine kuwa alipendwa, na licha ya kuwa ni KAZI YA MUNGU kumpumzisha baada ya kuyagusa maisha yetu kwa namna alivyoyagusa, bado tungependa kuendelea kuwa naye.Nakumbuka Juni mosi mwaka 2009, NILIBANDIKA MAKALA HAYA KUHUSU KILIO CHANGU KWA MJOMBA WANGU, ambaye nililia kwa kuwa nilimlilia, na katika makala hiyo, niliandika kuhusu kilio cangu kwa mjomba kuwa "nililia kwa kuwa kwa tafsiri yangu, kulia ni kutokubali kuwa wakati wa mjomba kupumzika ulikuwa umefika na hakika alistahili kupumzika baada ya kutenda mema mengi tena kwa mapambano ya hali ya juu. Mjomba alikuwa mtu mwema kwangu na kwa wengi..." Mtu wa kwanza kutoa maoni kwenye bandiko hilo (kama ilivyo kwa mabandiko mengi kwenye blogu nyingi) ni Dada yangu Yasinta ambaye alisema "Mzee wa Changamoto pole sana tena sana. Nalia pamoja nawe kwani nakuelewa kabisa. Na nakushauri lia sana kwani kulia ni moja ya kutoa uchungu wako. Natumanini Mjomba wako yupo nawe kila siku amini. Astarehe kwa amani."Leo hii nami namkumbuka Asifiwe, na licha ya kuwa NAMLILIA, bado nakumbuka kuwa ALISTAHILI KUPUMZIKA na kuwa aligusa maisha ya waliohusiana na kuishi naye na yetu tuliomfahamu kupitia ndugu na marafiki.Lililo kubwa kwetu tuliobaki, ni kuishi maisha sahihi na maisha yaliyo mema. Kama ambavyo aliishi ASIFIWE NGONYANI....Na ndio maana (kama kisemavyo kichwa cha post) namuona "ASIFIWE NGONYANI kama Kioo kingine cha maisha yetu, kwa maisha yetu na wenzetu"Chris Rice anasema....COME THOU FOUNT

AHSANTE MZEE WA CHANGAMOTO/KAKA MUBELWA BANDIO!!!

Monday, November 21, 2011

NI WIKI YA PEKEE KWANGU/KWETU-ITAKUWA NI WIKI YA KUMKUMBUKA ASIFIWE!!!

Natumaini wote mu-wazima wa afya njema, na mwisho wa juma umekuwa safi.
Ni hivi blog ya MAISHA NA MAFANIKIO inapenda kuwaambia kwamba wiki hii haitakuwa kama kawaida. Nitawaambia kwa nini, ila kwa kifupi ni kwamba itakuwa wiki ya kumuenzi mdogo wangu marehemu Asifiwe. Kwa namna nyingine haitakuwa kama kawaida hapa kibarazani. NINA IMANI TUTAKUWA PAMOJA /MTAKUWA PAMOJA NAMI NATANGULIZA SHUKRANI ZANGU ZA DHATI. KAPULYA.