Mbeya. Hospitali ya Rufaa Mbeya (MRH), imeteuliwa rasmi kuwa na maabara maalumu ya kuwapima watu watakaohisiwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa ebola.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Mpoki Ulisubisya alisema hayo jana jioni alipozungumza mambo mbalimbali kuhusu changamoto zinazoikabili hospitali yake.
"Ni kweli Serikali imeiteua maabara yetu ya hospitali kuwa maabara maalumu ya kupima virusi vya ebola nchini na kwa sasa maandalizi yote yanakamilishwa na tutaanza kazi mwishoni mwa mwezi huu au mapema Februari’’ alisema.
Kwa kipindi cha miaka mitano sasa, Maabara ya Hospitali ya Rufaa Mbeya ni maabara ambayo imethibitishwa kimataifa kwa ubora na kwamba vipimo vikitolewa kwenye maabara hiyo vinakubalika hata nchi za Marekani na Uingereza.
Akizungumzia uboreshaji wa utendaji kazi amesema wafanyakazi kupitia kwa viongozi wao kwa sasa wameimarisha utendaji kazi.
Kuhusu chumba cha kuhifadhi maiti kwenye Hospitali hiyo, Ulisubisya amesema Serikali imempata mtu atakayejenga jengo kubwa la kuhifadhi maiti na kuliboresha ili kuendeshwa kwa ubia katika hali ya usafi na kisasa zaidi.
‘’Bila shaka unakumbuka , mfanyakazi wa chumba cha maiti aliwahi kumweleza Waziri kwamba ukifariki dunia ukiwa Mbeya maiti yako italazwa chini. Sasa Serikali imeamua kuchukua hatua ili kuboresha nyumba hizo ingawa wahusika watatakiwa kutoa mchango kidogo’’alisema.
Mapema mwaka jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Seif Rashid wakati huo akiwa Naibu Waziri alitembelea hospitali hiyo ambapo mfanyakazi wa Chumba cha maiti, Vuruga P Vuruga alimweleza kiongozi huyo kwamba maiti zinalazwa mbili mbili kwenye chumba chenye uwezo wa kuhifadhi watu sita.
Vuruga amesema kutokana na kasi ya kufa, hivi sasa maiti zinalazwa chini na kwamba hata Naibu Waziri angefariki akiwa Mbeya ajue maiti yake ingelazwa chini.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment