Monday, February 17, 2014

JUMATATU HII NIMEONA TURUDI NYUMA MPAKA MIAKA ILE TULIYOSOMA SHULE YA MSINGI "DARASA LA NNE" NA HADITHI HII YA SADIKI NA SIKIRI!!!

Sadiki ni mtoto anayeishi karibu na Ujiji. Anaye ndugu yake aitwaye Sikiri. Sadiki na Sikiri husoma katika shule ya Businde. Sadiki anafanya kazi zote kwa bidii. Lakini Sikiri ni mtoto mbaya kwa sababu ni mvivu, kaidi, tena hana adabu.
Siku moja wakati wa livu baba yao aliwaamsha mapema sana. Akasema, "Sadiki, chuukua hii shilingi. Nenda sokoni ukanunue samaki. Na wewe Sikiri, nenda kisimani ukateke maji." Wote wawili wakaenda. Sadiki alinunua samaki, akarudi nyumbani haraka. Lakini Sikiri alichelewa. Baba yake akamngoja mpaka akachoka.
Baba akatoka kwa hasira kumfuata Sikiri kule kisimani. Alipofika alimkuta anachezea maji. Anayateka na kuyamwaga juu ya jiwe. Baba yake akamwuliza, "Unafanya nini Sikiri? Mbona unacheza tu? Teka maji, twende nyumbani." Sikiri akateka maji, wakarudi nyumbani.
Walipofika nyumbani walimkuta mama amekwisha tayarisha uji. Wakanywa. Walipomaliza, baba yao akawaambia, "Twendeni tukapalilie bustani ya mboga. Mama atabaki hapa nyumbani. Atalisha kuku na kusafisha nyumba. Baadaye atatayarisha chakula."
Kule katika bustani kulipandwa mchicha, maharagwe, vitunguu na nyanya. Magugu na manyasi yaliota kwa wingi. Sadiki, Sikiri na baba yao walipalilia kwa uangalifu ili wasiharibu mimea ya mazao.
Sikiri hakupenda kazi. Kwa hiyo alitoroka akaenda kichakani. Kule kichakani alitafuta matunda mwitu. Sikiri alikuwa mtoto mvivu kweli. Hakutaka kufanya kazi kwa bidii. Sadiki na baba yake waliporudi nyumbani, akawafuata.
Walipofika nyumbani chakula kilikuwa tayari. Sikiri alikuwa wa kwanza kunawa mikono na kuanza kula. Siku ile mama alipika ugali na samaki alionunua Sadiki. Walipokwisha kula, baba alimwita Sikiri akamwuliza, "kwa nini leo alitoroka?" Sikiri alinyamaza tu. Sakiri alikuwa mtoto mkaidi. Baba akamwambia, "Kesho utakwenda kupalilia bustani. Usipokwenda hutapata chakula."
Siku iliyofuata Sikiri alikataa kwenda bustanini, alitoroka. Sadiki na baba yake walikwenda kupalilia peke yao. Jioni waliporudi, baba alimwuliza mama, "Sikiri amekwenda wapi?" Mama akajibu, "Mimi leo sijamwona nyumbani. Sijui amekwenda wapi." Kumbe, siku ile asubuhi Sikiri alipanda basi kwenda mjini Kigoma. Huko njiani aliulizawa nauli. Sikiri hakuwa na pesa hata kidogo. Dereva akamtelemsha pale pale. Akaachwa peke yake. Sikiri alilia sana . Mwisho akaanza kusema kwa uchungu:-
Sikiri mimi maskini,
Uvivu wangu nyumbani,
Ukiwa huu njiani,
Nakufa hapa kwa nini?

Sadiki sasa ashiba,
Chakula kingi kwa baba,
Nirudi tena kwa baba,
Nakufa hapa kwa nini?
Sikiri alirudi nyumbani. Alikuwa amechoka sana. Alipofika nyumbani aliomba radhi. akamwambia baba na mama.
Naomba radhi nimekosa,
Nitakuwa mtoto mwema sasa,
Shambani tena sitakosa,
Baba na mama nisameheni.

Nitalima kama Sadiki,
Nitalima wala sichoki,
Na nyumbani tena sitoki
Baba na mama nisameheni.
Baba hakumpiga Sikiri. Alimsamehe. Sikiri akabadili tabia yake, akawa anawasaidia wazee wake. Kila alipotumwa alikwenda upesi. Mama yake alifurahi, akamwambia, "Siku hizi wewe ni mtoto mwema kama Sadiki. Mtoto mtii hupendwa na wazazi wake. Tena hupendwa na watu wote kijijini. Endelea kuwa mtoto mwema na mtii.......MWISHO......
HADITHI HII KILA NINAPOISOMA INANIKUMBUSHA SANA NA ILE HADITHI YA MWANA MPOTEVU EBU MSIKILIZA HAPA WIMBO HUU WA EMACHICHI

NAWATAKIENI JUMATATU NJENA NA KILA LA KHERI KWA KILA MTAKACHOFANYA!!! UJUMBE WA LEO YULE AWEKAYE AKIBA BASI HUFAIDI...maana yake ukitunza ulichonacho kitawafaa wengi..Elimu ni kugawana.

3 comments:

Anonymous said...

Darasa La 3 Dada yangu Mpendwa

Yasinta Ngonyani said...

Oh...usiye na jina !...kweli muda umeenda naona ni uzee unanyemelea......usihofu nitarekebisha. Ahsante..je umeikumbukaje hadithi?

Nicky Mwangoka said...

Dah umenikumbusha mbali hadi Raha. Hilo bus tulikuwa tunaita mkate teh teh teh