Sunday, July 11, 2010

Jumapili njema na ujumbe huu:-Tenda wema

Kuna wengi walimwengu, kujaa dunia nzima,
Muumba ni yeye Mungu, kila moja na karama,
Wenye maisha machungu, huhitaji tendwa mema,
Tenda wema nenda zako.

Wale walio shidani, kamwe sije watupa,
Waondoe majonzini, usijaribu wakwepa,
Wafanye was'ende chini, maisha wakaogopa,
Tenda wema nenda zako.

Yale walopungukiwa, ambayo wewe unayo,
Usisite kuyatowa, kadiri uyawezayo,
Upate kuwaokowa, yale yawasumbuayo,
Tenda wema nenda zako.

Wale walio na njaa, usisite kuwalisha,
Waso nguo za kuvaa, ukapate kuwavisha,
Waliokata tamaa, imani kuwahuisha,
Tenda wema nenda zako.

Wale wanaoumia, ukawafute machozi,
Ili waache kulia, wayahimili majonzi,
Hao 'sije wakimbia, peke yao hawawezi'
Tenda wema nenda zako.

Ila utendapo wema, usingoje shukurani,
Tena 'sigeuke nyuma, ungoje kitu fulani,
Tena usije kupima, ujuwe yake thamani,
Tenda wema nenda zako.

Kamwe usihesabu, Mungu ndiye anajuwa,
Kwa hilo ukawe bubu, nawe utabarikiwa,
Timiza wako wajibu, moyo kutopungukiwa,
Tenda wema nenda zako.

Ukitaka mashairi zaidi gonga hapa
JUMAPILI NJEMA KWA WOTE NDUGU ZANGUNI!!!!!

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

Da Yasinta ahsante sana kwa ujumbe huu.

Nawe uwe na Jumapili njema.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Nimerudi kwenye chakula kitamu rasmi sasa. Tuko pamoja.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

aksante dugu!

Unknown said...

ahsante sana dada Yas. Sikujua kuwa na ni malenga. Ujumbe umefika..