Monday, June 21, 2010

WANGONI NA VISA ASILI VYAO!

Sijui nimfundishe mwanangu juu ya mila hizi?

Kuna visa asili vingi sana ambavyo nimevishuhudia katika makuzi yangu. Lakini miongoni mwa visa asili hivyo, kuna kisa asili kimoja ambacho mpaka leo bado ninakikumbuka.

Bila shaka hata wewe unayesoma hapa huenda vipo visa asili ambavyo unavikumbuka na umekuwa ukiviamini au umeachana navyo kutokana na utamaduni wetu kumezwa kwa kiasi kikubwa na utamaduni wa kigeni.

Leo nimekumbuka kisa asili kimoja ambacho ningependa kuwashirikisha wasomaji wa kibaraza hiki.

Nakumbuka nilipokuwa mdogo mama alipokuwa jikoni akipika, alikuwa na kawaida ya kuita mmoja kati ya sisi watoto wake ili kwenda kumuwekea chumvi kwenye chakula na kama tulikuwa mbali au shuleni basi atamwomba mtoto wa jirani na kama hayupo mtoto wa jirani basi atapika bila kuweka chumvi.

Hali iliendelea kuwa hivyo mpaka siku nilipovunja ungo, ndipo nami nikaingia kwenye mkumbo huo. Niliambiwa kuwa nisitie chumvi tena kwenye chakula au mboga. Lakini cha kushangaza kaka zangu pamoja na wao kubalehe lakini hawakuwekewa vikwazo kama mimi.
Kama kawaida na UKAPULYA wangu nikataka kujua KWANINI?
Jibu lake lilikuwa hili:- Niliambiwa kuwa nikitia chumvi hasa wakati ule nipo hedhini na baba yangu akila chakula kile basi atavimba miguu Nadhani kama nakumbuka vizuri niliambiwa kuwa hata kaka zangu pia mume wangu wanaweza kuathirika.
Cha kushangaza ni kwamba mila hiyo niliiacha siku nyingi huko nyumbani na nimekuwa nikimpikia mume wangu kama kawaida bila kutafuta mtu wa kuniwekea chumvi na wala haijatokea akavimba miguu. Hata hivyo sina uhakika sana kama imani hii bado ipo au la. Kwani tangu niondoke nyumbani kuna mambo mengi sana yamebadilika.
Swali langu kwa wasomaji wa kibaraza hiki. Je? hii imani ni ya wangoni tu au ipo kwenye makabila mengine?

7 comments:

EDNA said...

Haaa Da Yasinta umeniacha hoi,nafikiri kila kabila lina milana desturi zake ingawa kwa sasa zinaelekea kutokomea.Mimi ninachokumbuka siku za nyuma ilikuwa mwanandugu akifariki wote mnanyoa kipara,hii ni kwa WAHEHE lakini sikuhizi sioni watu wakinyoa vipara tena.Itabidi nimuulize mama kama kuna mila nyingine alafu nitakujulisha.

Bennet said...

Hya jamani wenye visa vingine nao watuhadithie pia

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

hapo mama alikuwa anafundisha usafi. Maadamu ushajua kuoga sasa mume hawezi dhurika ....lol!

Anonymous said...

Chacha ina maana hata mama alikuwa hajui usafi? na ilikuwaje kumuamini mpita njia au mtoto wa jirani.....
Kuna jambo hapo bado linafichwa, tatizo ni kwamba hawa wazazi wetu walikuwa ni wasiri sana, pale watoto wanapotaka kujua undani wa kile kinachoitwa MWIKO.....

Dada Yasinta endelea nautafiti, majibu ya mama bado hayaridhishi....LOL

Subi Nukta said...

Nilikokulia mimi hatuna mila wala desturi hiyo ila ilikuwepo moja.
Nililelewa na Bibi na kwa bahati alikuwa mwalimu, sasa siku moja tumekwenda kwa jirani tukakaribishwa chakula na baada ya kula, nilisikia akiwaambia watoto wake, 'msisafishe vyombo, kufanya hivyo kusafisha vyakula tumboni watu wapatwe njaa usiku waishie kupita miayo na kuhesabu misumari darini.' Siku moja nilipomwambia Bibi kuwa sisafishi vyombo jioni ile akanifahamisha kuwa angenichopeka viboko (chapa) na kwamba haraka sana niache uvivu kama wa jirani na mila zisizo na maelezo. Nikakoma.

Kisa kingine, Mama wa Babu angali bado yu hai, aliwahi kunizuia kufagia usiku. Nilitaka kufagia usiku ule ili asubuhi nisiwe na kazi kubwa ya kufanya kabla ya kwenda shuleni. Nilikwenda moja kwa moja kwa mama kumwuliza sababu ya 'Mai' kunizuia kufagia usiku akasema mila yao inasema kufagia usiku ni kufukuza wageni. Ila wewe nenda ufagie tu mimi nitazungumza na Mai.

Na nyingine Mai alikuwa akisema, usipige mbinja (mluzi) usiku, ni kuita mashetani. Na pia, wanawake hawapaswi kupiga mbinja.

Na mwisho kabisa ni mila ya kutokumchapa mtoto usiku akalia, inaashiria jambo baya kwa hivyo sisi tulikuwa tukitambua kuwa tumetenda kosa, basi tutajificha hadi kiza kiingie ndipo tuingie ndani.

Nimemaliza ninayokumbuka kwa leo!

Penina Simon said...

Duh!! hiyo sijawahi kuisikia, sasa mtu ukizaa wanajinsia wa kike ina maana inabidi kuazima mtoto wa jirani

Yasinta Ngonyani said...

Ndiyo kuna visa vingi sana na hiki je mwanamke mjamzito asile maya akila atapozaliwa mtoto atakuwa hana nywele(zitanyonyoka) Subi we una visa vingi hivyo nilivisahau asante kwa kunikumbusha.