Saturday, June 5, 2010

Sweden yaibana zaidi Tanzania

BALOZI wa Sweden aliyememaliza muda wake, Staffan Herrstrom

BALOZI wa Sweden aliyememaliza muda wake, Staffan Herrstrom jana alitoa hotuba kali ya kuitaka serikali kutekeleza ahadi inazozitoa, ikiwemo kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote wa kesi kubwa za rushwa na kuondokana na utamaduni wa kulipana posho.

"(Serikali) isiache hata jiwe moja juu ya jiwe jingine," ameeleza balozi huyo katika hotuba yake iliyokuwa na ujumbe mzito kwa serikali wakati wa hafla ya maadhimisho ya siku ya Sweden ambayo ilitumiwa kumuaga.

Katika hotuba hiyo kali inayosisitiza msimamo wa Sweden katika vita dhidi ya rushwa, Balozi na Herrstrom alitaja mambo mawili makubwa muhimu katika kuondoa umaskini ambayo yanatakiwa kushughulikiwa kuwa ni utekelezaji wa maamuzi yaliyokwishafikiwa na sera pamoja na haki za watoto.

Hotuba yake imekuja zaidi ya wiki moja baada ya Sweden na nchi nyingine wahisani kutangaza kuzuia theluthi moja ya mchango wao kwenye bajeti kuu ya serikali ya Tanzania, kufuatia kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na kubadilisha mfumo wa usimamizi wa fedha za umma na utekelezaji wa mazimio yaliyofikiwa wakati wa kusaini makubaliano ya kutoa fedha hizo.

Nchi hizo zilitangaza kuwa zimezuia Sh297 bilioni kwenye bajeti kuu ya serikali ya mwaka 2010/11 na kwamba, zinaendelea na mazungumzo na serikali, huku zikisema kuwa iwapo serikali haitatekeleza ahadi zake fedha hizo ambazo ni za walipa kodi wa nchi hizo zitahamishiwa kwa taasisi zisizo za kiserikali ili ziendelee kusaidia katika kupunguza umaskini.

Jana Balozi Herrtsron, ambaye nchi yake inachangia dola 45 milioni za Marekani kwenye bajeti hiyo, alikuwa mkali zaidi.

"Tekelezeni nia iliyoelezwa ya kushughulikia kesi zote kubwa za rushwa mkihakikisha kuwa watuhumiwa wote wa rushwa wanafikishwa mahakamani na kesi zote zinatolewa maamuzi muafaka. Iwe ni moja au zote, bila ya kuacha jiwe moja juu ya jingine," alisema balozi huyo katika hafla hiyo.

Kauli hiyo imetolewa wakati vita dhidi ya rushwa ikionekana kupoa, huku watuhumiwa wa rushwa kubwa wakianza kujitokeza hadharani baada ya kupotea kwa kipindi kirefu kutokana na kuelekezewa tuhuma kali kwa takriban miaka miwili.

Baada ya wahisani kuzuia fedha kwa mara ya kwanza takriban miaka mitatu iliyopita, serikali iliamka na kuwafikisha mahakamani watu wanaotuhumiwa kuiba fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), kushughulikia ubadhirifu wa fedha za walipa kodi kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa na kushughulikia tuhuma za rushwa kwenye wizara iliyosababisha mawaziri wawili wa zamani kufikishwa mahakamani.

Lakini hatua hizo za serikali zimeonekana kutowagusa watuhumiwa wakubwa hasa kwenye suala la EPA, ambalo baadhi ya watuhumiwa walipata msamaha wa Rais baada ya kutakiwa kurejesha fedha hizo kabla ya Novemba mwaka 2008, huku tuhuma nzito kama za Meremeta Gold zikiwa hazijashughulikiwa kisheria.

Hata hivyo, vita hiyo inaonekana kupungua nguvu na wahisani wameonyesha kuwa na wasiwasi na mwenendo huo, ikiwemo Sweden.

Balozi Herrstrom, ambaye mapema wiki hii alizungumzia ugoigoi huo wa serikali katika kutekeleza ahadi zake, alizungumzia pia uhuru wa habari katika hotuba hiyo.

"Tekelezeni ahadi zote mlizotoa za kupata njia ya kisasa itakayohakikisha haki ya kupata habari inakuwepo; kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari na hivyo kuwa na uwazi na uwajibikaji, kutekeleza mabadiliko sita muhimu yanayotakiwa kwa haraka sana, kama mabadiliko katika serikali za mitaa na usimamizi wa fedha za umma" alisisitiza balozi huyo.

"Tekelezeni azma mliyoeleza ya kuachana na utamaduni wa kulipana posho ambao ni hatari sana katika suala la ufanisi na utawala."

Balozi huyo pia ameitaka serikali kuwasilisha muswada wa Sheria ya Watoto na kusema: "Tafadhali tekelezeni ahadi mliyoweka ya kuruhusu wanafunzi wanaopata mimba ambao wanakuwa wazazi mapema, kuendelea na shule badala ya kutimuliwa hivyo kunyimwa haki yao ya kupata elimu".

Alisema jambo la pili muhimu ni haki za watoto, akitaka walindwe, wasikilizwe na kupewa uwezo na kutaka adhabu kali dhidi ya watoto ziondolewe.

"Tuweke ahadi ya pamoja kwa niaba ya watoto wa nchi hii. Watoto wote wa Tanzania Bara na Zanzibar wasipigwe na tuhakikishe kuwa Zanzibar inakuwa na sheria nzuri ya haki za watoto kabla ya uchaguzi mkuu," alisema.

Hotuba yake ya jana haitofautiani sana na hotuba aliyoitoa mwezi mmoja uliopita katika mkutano wa kitaifa wa kupambana na rushwa ulioandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Balozi Herrstrom alisema hakuna nafasi ya kupunguza kasi katika vita dhidi ya rushwa na kuitaka serikali kumsikiliza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) na kwamba ifanyie kazi mambo yote yanayoibuliwa na ofisi hiyo katika mwaka uliopita na kutekeleza mapendekezo yake.

Mwandishi Wetu-Gazeti la Mwananchi


9 comments:

Mija Shija Sayi said...

Nashukuru Mungu kumbe hata nchi nyingine zinaona tunavyozembea. Nchi yetu kama ingekuwa haizembei hata hayo mahela ya nyongeza tusingeyahitaji maana ni nini tukosacho? kama ni mali asili tunazo za kutosha, hali ya hewa nzuri, watu wenye afya. Lakini ndo hivyo "penye miti.........."

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

kwa nini anaibana sasa hivi wakati ANAMALIZA MUDA WAKE?

Fadhy Mtanga said...

Natamani ningekuwa na uwezo wa kujibu swali la kaka Chacha.

Naunga mkono hao wote wanaoipunguzia msaada Tanzania. Kama ntaonekana siyo mzalendo potelea mbali. Tunastahili kuondolewa misaada kabisa tena siyo kupunguziwa.

Haiwezekani wanaoutupa misaada wawe na nidhamu na matumizi ya pesa za walipakodi wao, halafu sisi tunaopewa tuwe tunazifuja kifisadi.

Kateni tu.

Anonymous said...

kwanza hiyo misaada haisaidii wananchi sanasana mafisadi tu tena wangezuia misaada yote kabisa watie akili

MARKUS MPANGALA said...

CHACHA una hoja. hii ni sawa na shirika la kijasusi la CIA likabandika habari za kuonya TZ, lakini kwa mimi ninayjua kitendekacho na kwakuwa siko mbali na waandamizi wa usalama wala naona ni sawa na kumpiga kwenzi kinyago.

Kauli ya balzo itaishi kusifiwa na wanahabari na kumpongeza kisha kuficha madudu yote waliyofanya. NITAJE?????

walituma majasusi wao mwaka 2009 halafu wakawafanya eti watalii na wengine kusaidia vyama vya walemavu. Kumbe walikuja kuangalia eti tunavyojipanga kutumia pes awalizotoa kwetu ili kuwezesha uchaguzi wa serikali za mitaa.
NIELENDELEE AU??? ndiyo kwahiyo kauli ya balozi kwangu mimi angewahutubia watoto au??

AU ANATAKA TUSEME MENGINE AMBAYO ANADHANI HATUJUI NA HAYAANDIKWI MAGAZETINI NA BLOGU ZET HIZI.

naacha, yako mengi ambayo yamemfanya aseme kwakuwa tu anamaliza muda wake......
NAACHA SITASEMA ZAIDI YAISHIE MOYONI

MARKUS MPANGALA said...

NIMERUDI natamani sana TUWEKEWE VIKWAZO VYA KIUCHUMI NAAMINI TUTAPATA HEKIMA NA AKILI

John Mwaipopo said...

ila inauma kuona wewe uliyetoa msaada huishi kwa kutanua kama yule uliyempa huo msaada. inauma zaidi unapodhani kuwa msaada wako ulilenga kwa masikini asiyejiweza kumbe msaada huohuo unatumika kuwahonga Brazil waje kucheza kwa dk 90 tu.

Niliwasikia hao wahisani wakisema kuwa sasa hiyo sehemu ya misaada waliyokata wakatakuwa wanapeleka wao wenyewe kwa wananchi moja kwa moja ama kwa NGOs. lakini nako kwenye NGOs (Nothing Going On) kuna kaufisadi kake. lakini haidhuru sana walau inakwenda karibu na watu husika.

nje ya mada kidogo.
paragrafu ya pili mwandishi (wetu) anaandika:
"(Serikali) isiache hata jiwe moja juu ya jiwe jingine," amefanya tafsiri sisisi ya nahau ya Kiingereza 'no stone should be left unturned'. hili ni kosa la waandishi wengi wa kiswahili. Idioms (nahau)za lugha moja haziendi katika lugha nyingine kwa kutafisri maana za maneno yanayoziumba. katika kutafsiri unachotakiwa kufanya ni kupeleka maana yake husika. sio kubeba idiom kama ilivyo. kwa mfano katika kiswahili tuna nahau 'kupiga maji' ambayo inamaanisha 'kunwa pombe (nyingi)'. kama unatafsiri kwenda kingereza unatakiwa uandike 'to drink (too much) beer' na sio 'to hit/beat water'. (unaona inavyokuwa haiji?). katika kizungu utachekesha kama alivyochekesha mwandishi wetu katika kiswahili.

nahau hazihamai kama zilivyo kwani ni language-specific. tunahamisha maana tu. kumsaidia mwandishi wetu here is a rewrite: " (Serikali) ifanye kila liwezekanalo".

msishangae jamani ni uwanda niliobobea huu.

Fadhy Mtanga said...

Kaka John bora umeliona hili. Waandishi wetu kama tu sarufi ya Kiswahili wanaiandika kwa makosa, vp lugha iliyokuja kwa meli na ndege?

Ni tatizo kubwa sana kwa idioms za Kikatoliki kuzitafsiri moja kwa moja kwa maneno yake kuja kwenye Kimadafu.

Kwa mfano, 'it's raining cats and dogs'

Na unanikumbusha mwaka 1995 Mwalimu aliposema 'I can't let this country to the dogs' kuna watu walikuja juu wakadai amewaita mbwa.

Ha ha haaaaaa! Ahsante sana mwalimu Mwaipopo.

Yasinta Ngonyani said...

Nami namshukuru sana Mungu kuona hata nchi nyingine wanaona jinsi tulivyo wazembe nikiwsema watanzania tunapenda vya bure mnalalamika sasa? Asanteni wote.