Tuesday, January 26, 2016

SIRI 8 ZA KUISHI MAISHA YA MAFANIKIO NA USHINDI


ENDELEZA MAMBO CHANYA SIKU ZOTE.
Mafanikio ni safari. Tena ni safari ambayo wakati mwingine inahitaji uvumilivu mkubwa wa kutosha ili kufika mwisho. Kutokana na umuhimu wa safari hii ni lazima kwako uwe na nguvu, dira, mwelekeo pamoja na hamasa kubwa siku zote bila kuchoka. Kama utakosa hamasa hii ya kufikia mafanikio yako basi elewa hutafika mbali ni lazima utakwama.
Hivyo, ili kufanikiwa ni lazima kujifunza kila siku na kujua mbinu mbalimbali za kuhamasika na ambazo zitakufanya usonge mbele bila kusimama. Kwa kufanya hivyo utajikuta ukiishi maisha ya mafanikio na ushindi siku zote. Je, hivi unajua siri ya maisha ya ushindi ipo wapi? Bila kupoteza muda, leo nakukumbusha siri chache za kuishi maisha ya ushindi katika maisha yako.
1. Acha kujilisha na kuendeleza vitu dhaifu katika maisha yako.
Kama ni ubora endeleza ubora siku zote, acha kubeba udhaifu mwingi katika maisha yako usio na maana. Kwa mfano unaweza ukawa ni mvivu, acha kuendeleza uvivu huo. Unaweza ukawa una matumizi mabovu ya pesa acha kuendeleza tabia hiyo. Hayo ni mambo dhaifu unayotakiwa kuyaacha mara moja ili kujihakikishia mafanikio yako.
2. Kuwa makini na maisha yako.
Siku zote kuwa makini na maisha yako. Jitahidi kila siku asubuhi kuandika kile ulichojifunza kwa siku ya jana kupitia dunia, kiwe kizuri au kibaya kisha kifanyie kazi. Hakikisha siku isipite bila kujifunza kitu cha kubadili maisha yako. Hiyo haitoshi usiruhusu mtu achezee maisha yako kwa namna yoyote ile. Kuwa makini siku zote, itakusaidia kuishi maisha ya ushindi.
3. Acha kusubiri kitu, kuwa mtendaji.
Ni bora kuanza na kitu kidogo kuliko ukakaa na kuendelea kusubiri. Kama ni malengo anza kuyatekeza kidogo kidogo mpaka yatatimia. Kama ni kuandika andika kidogo mwisho wa siku utaandika kitabu kizima. Je, bado unaendelea kusubiri? Usisubiri huo si wakati wake kwa sasa.
4. Shauku na hamasa ni msingi mkubwa wa mafanikio yako.
Watu wanaofanikiwa sio kwamba wana akili nyingi sana kuzidi wengine, hapana. Kinachowafanya wafanikiwe ni kwa sababu ya SHAUKU ya kutaka kufanikiwa kwao na MAARIFA wanayowekeza kila siku. Ukijijengea shauku na hamasa kubwa hakuna kitu cha kukuzuia lazima ufanikiwe.
5. Jijengee mtazamo chanya ili kufanikiwa kwa viwango vikubwa.
Kama unafikiri huwezi kufanikisha ama kufikia kiwango fulani cha mafanikio katika maisha yako, basi hakuna njia nyingine ya kukutoa hapo, ndivyo itakavyokuwa.  Kwa sababu kila hatua utakayochukua itaendana sawa sawa na kile unachoamini katika maisha yako siku zote.
6. Kila siku tafuta kubadilika kwanza wewe.
Ikiwa unataka maisha yako yabadilike. Anza kwanza kubadilika wewe. Hiyo ni njia rahisi ya kufikia mafanikio yoyote unayoyahitaji. Lakini ikiwa utakazana sana kubadili mambo ya nje na kujisahau wewe, itakuwa ni ngumu sana kwa wewe kuweza kubadilisha maisha yako zaidi utaendelea kubaki hivyo ulivyo.
7. Hakuna kukata tamaa kwenye mafanikio.
Kitu cha kutambua hapa huwezi kupata mafanikio kwa mara moja. Mafanikio yanakuja hatua kwa hatua kama tulivyosema mwanzoni. Kuna wakati tunakuwa tunashindwa sana lakini tunanyanyuka na kusonga mbele. Hivyo kwa namna yoyote ile hutakiwi kukata tamaa pale unaposhindwa.
8. Tafuta wazo moja na lifanyie kazi.
Najua unaweza ukawa unaweza mawazo mengi ambayo unataka kuyatendea kazi. Acha kuhagaika sana mara huku mara kule. Chagua wazo moja na kisha ulifanyie kazi. Ishi na wazo hilo na liwe kama sehemu ya maisha yako.
Hizo ni sehemu ya sheria ambazo unaweza ukazitumia zikakupa mafanikio makubwa katika maisha yako.
Katika pitapita zangu nimekutana na hii hapa nikaona niiweke hapa ili nisifaidike peke yangu.
PAMOJA DAIMA....KAPULYA!

5 comments:

Ayubu Chewale said...

So courage thanx my friend

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ayubu Ahsante sana na karibu tena..

Denis Ntyangiri said...

Asante. Ni maelekezo Mazuri

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante kaka Denis...na karibu sana hapa kibarani

Unknown said...

Mungu akubatiki sana