Monday, February 14, 2011

Swali la JUMATATU HII!!!

katika ukuaji wangu sikuwahi kusikia watu wakitakiana siku ya kuzaliwa na kuna wengine hata hawajui lini wamezaliwa.

Pia sikuwahi kusikia watu wakitakiana siku ya wapendanao. Au siku ya "Halowini" Hivi ni kwa nini imekuwa hivi? Nimewaza tu kwa sauti!!!

12 comments:

Mrs. F said...

Mm naona watu kusahau kutokana na majukumu ya maisha, kutojaliana,kupuuza kutokana na kutokuona umuhimu wa sikukuu hizi. Asante kwa swali zuri dadaaaa!

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Vyote hivi ni mambo ya kizazi kipya, kizazi cha kisasa kinachojaribu zaidi kujifungamanisha na utamaduni wa Kimagharibi.

Zamani pengine hakukuwa na umuhimu sana wa kujua siku ya kuzaliwa; na watu wengi hawakuwa na kumbukumbu sahihi. Ukiwauliza wazee kuhusu siku yao ya kuzaliwa, watakwambia kwa kurejelea matukio muhimu ya wakati ule mf. vita, nzige, mvua kubwa n.k. Na hii ilitosha!

Kuhusu Valentine Day - mimi sijui ni kwa nini inasherehekewa!

Rachel Siwa said...

Da yasinta niwakati wa dot com huu mwenagu!!!!!kama hii Valentine Day mimi nimeijua au kuisikia ukubwani kabisaaaaaaaaa!

Anonymous said...

Kwa maoni yangu, sikukuu ya valentine ni sikukuu ya watengenezaji wa kadi za salamu kama Hallmark. Wamejihakikishia siku hiyo watauza kadi nyingi sana. Kama una mpenzi, ifanye kila siku iwe sikukuu ya mapenzi yako wewe na mpenzio.

Goodman Manyanya Phiri said...

Naam, kama Mrs F alivyosema: ni usahaulifu unaosababisha kutomtakia mwenzio heri kwa siku yake ya kuzaliwa.

Kingine kinachosababisha hiyo hali ni kutokuwa na pesa za kutosha kusherehekea au kupeyana ujumbe huo wa ukumbusho.

Lakini pia na mambo ya utamaduni yapo. Haya mambo ya kutakiana heri kwa siku ya kuzaliwa ninahisi chimbuko lake Ulaya, lakini naweza nikakosea.

Naweza nikakosea pia kwamba huko Japan hawana kitu kama hicho, bali kila mtu humtakia mpendwa wake heri ya siku ya kuzaliwa KILA MWANZO WA MWAKA MPYA (january 01)!!! Na kama ni kweli, ninahisi Mrs F (nami pia) tungefurahia utamaduni kama huo, maana yake haiwezekani tukasahau tena.


Ya Valentine ni makubwa mno, madogo yana nafuu hata kwa watoto washule! Ijumaa niliwauliza wasichana wawili mtu (umri: 7) na dada yake (umri: 10) 'kwanini Valentine itakuwa siku maalum shuleni kwao, inawahusu nini wao kama watoto washule za jiji Pretoria?'

Basi kicheko cha watu wazima kilizuka ndani yaTAXI kwani waliniambia kwa uhakika: "VALENTINE NI SIKU YA KITU KIMOJA TU MUHIMU: MASHINDANO YA MAVAZI!"

Unknown said...

Historia Ya Sherehe Ya Siku Ya Valentine

Sherehe hii ya wapendanao ni sherehe ya wapagani wa Kirumi wakati dini yao ya upagani ilikuwa ni dini iliyotapakaa kwa Warumi karne zaidi ya kumi na saba zilizopita. Na fikra zao ilikuwa ni kuelezea hisia ya 'mapenzi ya kiroho'

Kulikuwa na visasili (uongo) zilizohusishwa na sherehe hii ya upagani ya Warumi ambao umeendelea kutoka warithi wa Kikiristo. Miongoni mwa uongo huo ni kuamini kwao Warumi kuwa Romulus, aliyevumbua Rome, alinyonyeshwa siku moja na mbwa mwitu mwanamke, hivyo akampa nguvu na hikma.
Warumi walikuwa wakisherehekea tukio hili katikati ya Februari kila mwaka kwa kufanya sherehe kubwa. Na mojawapo ya tambiko katika sherehe hii ni kuchinja mbwa au mbuzi.

Vijana wawili wenye nguvu hujipaka damu ya mbwa au ya mbuzi katika miili yao, kisha huiosha damu hiyo kwa maziwa.

Baada ya hapo, watu hufanya gwaride wakiwa vijana hawa wawilii wako mbele wakiongoza gwaride iliyokuwa ikitembea barabarani. Vijana hao wawili walikuwa wakichukua vipande vya ngozi ambavyo waliwapigia watu wanaowavuka. Wanawake wa kirumi walikuwa wakipokea mapigo hayo wakiamini kuwa yatawahifadhi na kutibu utasa.

Kuungamana Baina Mtakatifu Valentine (Saint Valentine) Na Sherehe Hii
Mtakatifu Valentine (Saint Valentine) ni jina waliopewa mashujaa wawili wakongwe waliokufa ambao ni wana wa kanisa la kikiristo. Inasemekena kwamba walikuwa ni wawili au mmoja tu. Huyo mmoja alikufa Rome kutokana na mateso ya kiongozi wa Kigothi aliyeitwa Claudius. Kanisa la Saint Valentine lilijengwa kwa ajili ya kudumisha kumbukumbu yake.

Warumi walipoingia ukristo, wakaendelea kusherehekea sikukuu ya wapendanao (valentine day) lakini wakabadilisha kutoka fikra ya upagani ya 'mapenzi ya kiroho' (spiritual love) na kuleta fikra nyingine iliyojulikana kama ni 'mapenzi ya mashujaa' yaliyowakilishwa na Saint Valentine ambaye aliuliwa kwa ajili ya kutetea mapenzi na amani. Vile vile ikajulikana ni sikukuu ya wapenzi, na Saint Valentine alifanywa kuwa ni mlezi wa mapenzi ya mtakatifu.

Miongoni mwa imani yao inayoambatana na sherehe hii ni kwamba majina ya wasichana waliofika umri wa kuolewa yaliandikwa katika vikaratasi vidogo vilivyokunjwa mviringo kisha vikawekwa katika chombo juu ya meza.

Kisha wavulana waliotaka kuoa waliitwa na kila mmoja huchagua karatasi moja ikiwa na jina la msichana. Kisha hujiambatanisha naye huyo msichana aliyempata kutokana na kura hiyo aliyochagua kwa muda wa mwaka ili wajuane vizuri kisha tena hufunga ndoa, au kama hawakuelewana hurudia tena kufanya kura inapofika siku hiyo mwaka unaofatia.

Vile vile imesemekana kwamba chanzo cha sikukuu hii, ni kwamba warumi walipokuwa wakristo baada ya ukristo kutapakaa, Mfalme wa Kirumi Claudius II alitoa hukumu katika karne ya tatu kwamba askari wasioe kwa sababu kuoa kwao kutawashughulisha na vita walivyokuwa wakipigana.

Hukumu hiyo ilipingwa na Saint Valentine ambaye alianzisha kuozesha maaskari kwa siri. Alipokuja kujua mfalme, alimfunga jela na akamhukumu kuuliwa. Huko jela akapendana na mtoto wa mkuu wa jela, lakini ikawa ni siri kwani kutokana na sheria ya ukristo, mapadri na makasisi wameharamishwa kuoa au kupenda.

Hata hivyo alipewa heshima yake na wakristo kwa sababu ya kushikilia na kujikita imara katika ukristo wakati mfalme alipotaka kumsamehe kwa sharti aache ukristo na kuabudu miungu ya Kirumi ili awe msiri wake na awe mkwe wake. Lakini Saint Valentine alikataa ahadi hiyo na akapendelea ukristo, kwa hiyo akauliwa siku ya tarehe 14 Februari 270 CE. Ndio ikaitwa siku hii kwa jina la huyo mtakatifu (Valentine).

Papa (Pope) naye akaifanya siku hiyo ya kufa Saint Valentine tarehe 14 Februari 270 CE kuwa ni sikukuu ya mapenzi. Na ni nani alikuwa Papa huyo? Ni Askofu mkuu wa kanisa la 'universal church', ambaye ni mrithi wa mtakatifu Peter.

Flora Wanna said...

sikuizi tunacopy mila na desturi za wazungu, ndio maana hapo zamani hukusikia watu wanapeana heri ya kuzaliwa, wala siku ya wapendanao, na mengineyo. kizazi cha sasahivi kinashida kwakweli yani kila kitu ni copy na paste toka kwa wazungu. ona sasa hata mimi nachanganya lugha, hahaaah! haya wazungu wametuaribia tamaduni zetu.

MARKUS MPANGALA said...

@matondo, umenena sana. naomba uwasaidie ndugu zetu wasabato masalia wanaohubiri ujio wa jamaa mmoja aitwaye Yesu, kila mwaka. kuna jamaa wengine wa Radio Family ati wanatangaza mwisho wa dunia.
kuna uchafu mwingi tunaelezana kila kukicha. Hii Halowini ilikuwa watu ambao ni sawa na kuamua kuingiza mchezo wa KOMBOLELA KATIKA BIBLIA.
Kaka Matondo kumbuka falsafa uliyotuwekea pale kijijini kwako katika post ya MZEE WA KIYAHUDI ASIYEJUA KUSOMA.

@MCHARIA hakika umameliza kila kitu, hawa akina Cladius ni sawa na mchezo wa UKUTI kuingiza katika imani za dini.

Nashukuru mchumba wangu wala hashtuki na midubwasha iitwayo valentine kwa kukong'oli kidhungu ati ya mupenzi wake wa lundunyasa.

SHEREHE ZINGINE KAMA ZA HALOWIN NA VALENTINE NAHISI KICHEFU CHEFU NATAMANI KUTAPIKA KOOOOOOOOOOO OOOOOOOO

Mija Shija Sayi said...

mmmmmmmmmmmhhhh!!

Yasinta Ngonyani said...

Kwanza nasema ahsanteni wote na pili napenda kusema naona dukuduku/ukapulya wangu umenisaidia na naona nimepata jibu. Na ruksa mjadala kuendelea....

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

@Mwanafalsafa Kardinali Mpangala. Wasabato wasikushangaze sana. Historia yao inaonyesha kwamba wana tabia hiyo ya kukurupuka na kudakia kila tukio linalotokea hapa duniani kwamba linaashiria mwisho wa dunia.

Juzi juzi hapa Wikileaks moja ikaeneza tetesi kwamba inawezekana mafuta kule Saudi Arabia yataisha mwaka 2030 - na tayari hawa jamaa wakaidaka na kuanza kusema kuisha kwa mafuta hayo kumetabiriwa na kutakuwa ndiyo mwanzo wa machafuko duniani kote na hatimaye vita vya mwisho vya Megido (Armageddon). Baadaye imekuja kubainika kwamba wikileaks hiyo ni ya uongo na ilikuwa ni speculation tu ya mtu mmoja.

Angalia Historia yao hapa

http://en.wikipedia.org/wiki/Seventh-day_Adventist_Church

na utaona kwamba kimsingi hili ni kanisa ambalo limeegemea zaidi katika unabii hasa katika kitabu cha Daniel na Ufunuo na kila jambo linalotokea linajaribu kuoanishwa na vitabu hivi. Hata mwanzilishi wao mmoja aitwaye William Miller alitabiri kwamba dunia ingefikia mwisho wake machi 21, 1844. Watu wakauza nyumba na vitu vyao vya kidunia. Siku hiyo ikafika na kupita bila tukio lolote la maana.

Ukristo sasa umevurugika na kugeuma kuwa biashara; na huwezi kujua yupi ni yupi. Cha muhimu ni kushika na kufuata misingi iliyoainishwa katika Biblia. Kanisa linalofuata misingi hiyo hilo ndilo la kufuata (ingawa kusema kweli kanisa haliokoi). Vinginevyo mitume na manabii hawa wanaozuka kila leo na kujifanya kuwa wanafanya miujiza na wanaongea na Mungu - wakati ukiangalia wakihubiricho na matendo yao ni kinyume na maandiko - wataweza kukuchanganya.

Kadinali - shika sana ulichonacho!

Penina Simon said...

lazima ujue kuwa tupo kwenye dakika za mwisho dunia kufunga historia, mambo kama haya lazima yatokee ili kukamilisha unabii, natamani nikutafutie kitabu fulani hivi kinaitwa "MATUKIO YA SIKU ZA MWISHO" na uweje kujua kuwa haya ni mapokeao tu wanadamu huyaanzisha, je umewahi kujiuliza Bithday ya YESU ilianzaje? au umewahi kujiuliza ni mwezi gani Bikra Maria alipokea ujumbe wa kubeba mimba na ni kweli YESU alizaliwa Decemba?, na kama sio je haya yametoka wapi? na yalianzishwa na nani?
2. Umewahi kukumbuka Mungu wakati anaumba nchi alikuwa anahesabuje sku? na je ziligeukaje mpaka kuanzia Usiku? na ni nani alieanzisha hili, na kwnn? usisumbue kichwa chako Majibu yote haya unaweza kuyapata kwenye vitabu vya roho za unabii na matukio ya sku za mwisho na tumaini la vizazi vipya kama wewe ni msomaji mzuri.