Wednesday, February 17, 2016

WOSIA WA BABA KWA BINTI YAKE

Aliyoyasema baba siku moja kabla bintie hajafunga ndoa....

Binti yangu, kuanzia kesho hutakuwa ukiitwa tena jina langu. Utakuwa na furaha kuolewa na mwanaume uliyempenda. Usinikumbuke sana mimi kwasababu nimeshatimiza majukumu yangu. Sasa ni wakati wa kutimiza majukumu yako.



Kuanzia utoto wako, nimekulea vema kwa neema za Mungu. Ila kabla hujasema mbele ya kasisi kuwa unakubali kuolewa ningependa nikueleze kuhusu kuishi na mwanaume na maisha ya ndoa kiujumla.



Unakumbuka ulivyokua umekaribia kufanya mtihani wako wa mwisho wa kidato cha sita? Unakumbuka Ulikuja kwangu na nikakupa Tsh laki moja kwa ajili ya maandalizi ya mtihani? Sawa,  ingawa nilikupa mimi, lakini ukweli ni kwamba pesa ile ilikuwa sio yangu.



Najua siku zote ulikua ukijua kuwa mimi ndiye niliyekuwa nikikulipia ada. Ukweli ni kwamba mimi nilikuwa nimefirisika sina mbele wala nyuma...lakini mama yako alinipa pesa zake. Angeweza kukupa wewe moja kwa moja ila aliamua kunipa mimi kwanza.



Hii inamaanisha nini mwanangu, muunge mkono/msaidie mume wako! Muda mwingine atakuwa kama amechanganyikiwa kutokana na ugumu wa maisha, madeni na vinginevyo ingawa ataonekana yuko sawa ila akilini mwake anayo hofu na majonzi makuu...atahisi hutaweza kumthamini tena kwa vile mambo yamemuendea kombo. Huo ndio muda utakao kubidi kuwa nae bega kwa bega ukimfariji.



Mwanangu njia sahihi ya kumuonesha mume wako kua unampenda ni kumuheshimu, najua inaweza tokea ukabishana nae, ukakwaruzana nae ila mwisho wa siku mwache ajue kuwa heshima yako kwake iko pale pale.



Mwanangu, unakumbuka siku ile nilipomkalipia vibaya sana mama yako? Alifanya nini? Alibaki kimya kabisa. Unakumbuka pia siku ile mama yako alivyonijia juu? Nilifanya nini? Nilibaki kimya kabisa! Binti yangu jifunze kuwa kimya muda mwingine pale mume wako atakapokuwa na hasira. Mmoja kati yenu atakapokuwa na hasira na gadhabu nyingi mmoja lazima atulie kimya. Kama wote mtaanza kupandishiana hasira tatizo hapo ndio huibuka. Na matatizo ya ndoa ndio huanzia hapo.



Mwanangu, kitu cha kwanza kujua kuhusu mume wako ni chakula anachokipenda. Kama anapenda vyakula vya aina nyingi weka katika akili yako. Usiache mpaka aombe chakula siku zote muandalie.



Kuna siku mama yako alinidaka nikiwa nimemshika mwanamke mwingine mkono, hakuwa mchepuko wangu ila ni rafiki yangu niliyepotezana nae kitambo. Mama yako aliponiona hakuanzisha ugomvi na yule mwanamke. Aliondoka kimya kimya.



Nilikuwa na hofu kuu kurudi nyumbani, ningemwambia nini anielewe? Lakini niliporudi nyumbani hakunisema chochote. Aliniandalia chakula mezani kama kawaida. Ila nafsini nilijiona kama nina hatia. Nikaanza kumuomba msamaha.



Kuanzia siku ile sikukaa kumtazama mwanamke wa pembeni mara mbili. Nani anajua? Je kama mama yako angegombana na mimi siku ile, labda ningeondoka nyumbani nakuangukia katika mikono ya mwanamke yeyote tu barabarani akanipoze. Muda mwingine ukimya huleta ufumbuzi mkubwa kuliko ugomvi.



Sahau kuhusu riwaya za mapenzi ulizosoma ulipokuwa shuleni. Unakumbuka filamu za kihindi na za kimarekani? Unakumbuka filamu za kitanzania na Kinaijeria? Unakumbuka tamthiliya za kifilipino? Nyimbo za westlife unazikumbuka? Sahau kabisa hayo mambo mwanangu! Usitegemee vitu ulivyokua ukiviona huko vitakuwepo katika ndoa yako. Maisha halisi ni tofauti na hadithi za kufikirika.



Kitu cha mwisho nachotaka nikuambie... Unakumbuka jinsi ulivyozaliwa? Sijawahi kukwambia! Baada ya ndoa yetu mimi na mama yako mambo yalikuwa magumu. Na mama yako ilimlazimu afanye kazi mbili kusaidia  familia. Nami pia nilikuwa nikifanya hivyo.


Nilikuwa nikirudi nyumbani saa moja jioni na mama yako alikuwa akirudi saa mbili usiku akiwa amechoka. Lakini tulipoenda kulala hakuninyima chakula cha usiku kitandani. Na kwa jinsi hii ndipo ulipozaliwa. Usijenge tabia ya kumyima mumeo chakula chake akipendacho cha usiku. Maana kufanya hivyo sio kumkomoa bali ni kuiharibu ndoa yako kwa mikono yako mwenyewe.


Kuwa mke mwema, na utakuwa binti yangu nitakae jivunia mpaka naingia kaburini........



Kila ka kheri binti yangu.
CHANZO CHA HABARI HII NI HAPA

No comments: