Inatosha mwanamume kumpa mkewe fedha na kila kitu bila kuzungumza naye na kusikiliza hisia zake? Inatosha mwananke kumpa mapenzi ya kila aina mumewe wawapo chumbani bila kusema hisia zake kwake na kuwa tayari kufunga njia za kujadili mambo yanayowahusu? Hebu soma mfano huo hapo chini kwani kuna uvumbuzi wa ni kwa nini tunaweza kuwa na kila kitu kimapato au kisura na kimaumbile, lakini wapenzi wetu wakatuacha.
Johnson amerudi nyumbani kutoka kwenya shughuli zake na kama kawaida yake, salaam yake ya kwanza kwa mkewe ni kuuliza, “Mbona viatu vimewekwa njiani.” Pengine siyo salaam tu, bali hilo litabaki kuwa tamshi au kauli pekee kwa muda mrefu ujao wa jioni ile. Baada ya hapo Johnson huingia chumbani ambako hukaa sana hadi chakula kinapoiva. Mkewe anajaribu kumuuliza jinsi kazi ilivyokuwa kwa siku ile. Johnson, baada ya kujivuta sana anajibu kwa kifupi, “safi tu”.
Mkewe anajaribu tena kutafuta njia ya kuwasiliana na mumewe. Anajaribu kumsimulia jinsi gari moja la mchanga lilivyotaka kumuuwa utingo wake hapo mtaani mchana ule. Johnson anasikiliza habari hiyo bila kuonyesha hali yoyote ya mabadiliko na wala hajibu wala angalau kusema,. “Hawa utingo nao wana hatari.” Haoni, hana sababu ya kujibu. Lakini bado anaamini na anadai kwamba huyo ni mkewe, tena wakati mwingine akisema ni mkewe mpendwa. Wengi wetu ni kama Johnson au tuna wanaume kama yeye.
Tunaweza kuwa na kila kitu kwa upande wetu. Mali, umaarufu mkubwa, kazi nzuri, watoto wazuri na vingine, lakini tukakosa hisia kwa wapenzi wetu. Tukakosa kuwa na uwezo wa kubaini haja ya kujali kuhusu hisia za tuwapendao au tunaodai kuwa tunawapenda. Kukosa uwezo wa kubaini hisia ni kushindwa kwetu kufungua njia na mawasiliano kwa wenzetu hao.
Mawasiliano katika ndoa ni nini? Inaweza ikaonekana kama vile swali hili ni rahisi kupatiwa jibu, lakini kwa kweli ni wanandoa wachache sana wanaoweza kutoa jibu sahihi la swali hili. Mawasiliano kwa wengi ni kuzungumza au kijibizana. Huenda hiyo ni kweli, lakini hata wanaogombana huzungumza na kujibizana pia. Mawasilino katika uhusiano kwa kifupi, lakini kwa ufasaha, yana maana ya wanandoa kuzungumza kila mmoja kwa uhuru na kwa uadilifu. Wanandoa au watu wengine wowote wanapowasiliana vizuri, huzungumza juu ya matatizo yao, furaha, huzuni na kile kinachoenda kwenye akili au mawazo ya kila mmoja-huzungumza hisia zao.
Huwa tunasema na kushauri kuhusu mawasiliano mazuri ndani ya ndoa. Huwa tunasisitiza sana kuhusu wapenzi kuwa makini wanapojaribu kusema au kuwasilisha hisia zao kwa wenzao. Lakini huenda ugumu uko kwenye kufahamu maana ya mawasiliano ndani ya ndoa, achilia mali mawasiliano mazuri.
Lakini bila shaka kutokana na fasili hiyo fupi, tunaweza kuwa na picha angalau ndogo kuhusu maana ya mawasiliano katika ndoa. Mawasiliano mazuri ina maana vitendo fulani ambavyo vikifanyika katika utaratibu fulani, ndoa kukomaa na kushika mizizi kwa kiwango cha juu sana cha uimara, na ambayo yasipofanyika, uwezekano ni kwa ndoa husika kuanguka.
Pengine mtu anaweza kuuliza, inakuwaje watu ambao tulikutana tukiwa hatujuani, tukavutiana kwa sababu mbalimbali hadi tukafikia uamuzi kwa furaha kwamba tunaweza kuishi pamoja, leo hii tushindwe kuzungumza kwa uhuru na uadilifu? Kwa nini wanandoa hushindwa kuwasiliana? Kuna sababu nyingi, lakini inayokusanya zote ni moja-wengi hatujui umuhimu wa mawasiliano na pengine hatuoni kuwasiliana kama sehemu muhimu kwenye maisha yetu ya kindoa.
Kuna wakati tunadhani kimakosa, kwamba kuwasiliana kunaweza kutuharibia uhusiano wetu badala ya kujenga. Kwa hiyo, tunaamua kuzifutika hisia zetu, mawazo yetu na ushauri wetu vifuani mwetu. Mtu amepatikana na tatizo, anadhani akimwambia mwenzake atamvunja nguvu, atamtisha au atamfanya amlaumu au kumuona hana maana. Hivyo, anaamua kunyamaza. Inapokuja kufahamika, mwenzake hudhani alimficha kwa kutomjali, kutomwamini au kutompenda. Badala ya kutatua tatizo, hali hiyo inakuwa imezua tatizo jipya.
Lakini kuna ukweli ambao sisi kama binadamu, kila mmoja wetu ni lazima aukubali. Ukweli huu ni ule kwamba, ndani kabisa ya mioyo yetu huwa tunatamani kuzungumzia hisia zetu. Tungependa sana bila shaka kuonyesha undani wetu, yaani hisia zetu kwa wengine. Siyo jambo la nasibu tu kwamba wengi wetu tunajikuta tunataka au tuna rafiki wa karibu angalau mmoja kwenye maisha yetu. Hii ni kwa sababu tunataka mahali pa kuonyesha nafsi zetu halisi, yaani kusema tunavyohisi. Tungependa kuwa atatudharau au kutuona tuna mapungufu. Badala yake atashiriki nasi katika hisia hizo, ziwe mbaya au nzuri, za kutisha au kufurahisha na za aibu au za sifa.
Lakini siyo kwa sababu ya sisi kusikilizwa na kueleweka u , lakini pia tungependa kuwasikiliza wale ambao nao wanatusikiliza. Kusikia hisia zao za ndani na ukweli unaoenda kwenye mawazo au hisia zao. Ukiangalia sana kutokana na ukweli huo, utaona kwamba, moja ya sababu ya kuoa au kuolewa ni kuwasiliana. Sasa kama hadhi ya chini sana, ni kama vile hiyo ndoa haipo kabisa. Bila mawasiliano, ndoa inakuwa ni sawa na muungano wa watu wawili wanaoishi chini ya paa siyo watu wawili wanopendana.
Hebu tujiulize. Unawezaje kusema au kupima kwamba ndoa fulani haina mawasiliano? Suala hili linaonekana kama vile liko wazi sana, lakini kamwe siyo hivyo. Watu wengi kwenye ndoa wanakabiliwa na migogoro na kutoelewana kwingi, lakini kamwe hakuna ajuaye kati yao kwamba tatizo ni kukosa mawasiliano. Kukosa mawasilino kunaweza kuzaa hali ambayo ndiyo inayoonekana kuwa ndicho chanzo cha tatizo ndani ya ndoa, kukosa mawasiliano kwenyewe kukiwa kumejificha au kukiwa wazi, lakini kwa sababu hatujali kuwepo au kutokuwepo kwake tukashindwa kuona.
Wakati mwingine ni kweli kwamba tatizo lililopo siyo kukosa mawasiliano, lakini kwa sababu hakuna mawasiliano, tatizo hilo huwa kubwa na pengine kuzaa matatizo mengine ambayo hatimaye huwa magumu kusuluhishwa. Matatizo ambayo yangesuluhishwa hufikia mahali yakaiangusha ndoa sababu yamekosa kusemwa na kutafutiwa ufumbuzi. Yatasemwa wapi na saa ngapi, wakati hakuna mawasiliano.
Makala hii nimeichukua kutoka kwenye kitabu cha Maisha na Mafanikio kilichoandikwa na Hayati Munga Tehenan ambaye alikuwa ni Mwalimu mzuri wa maarifa ya Utambuzi akitoa elimu hiyo kupitia magazeti yake ya Jitambue, vitabu na semina zake nchini Tanzania kabla ya kufariki dunia.
5 comments:
da yasinta, kazi ipo. wacha nisome hii post tena na tena nijifunze mambo mengi.
mambo ya hatai Tehenenan. alipoondoka kwenye mwili (kufa) tulidhani tutakuwa yatima, kumbe ilikuwa ni nafasi kuubwa ya kujifunza.
utambuzi bwana!
nimeipenda hiyo...
Ni sawa kabisa maneno yako.
Nadhani utajifunza mengi sana kaka Fadhy.
Kamala ni kweli utambuzi bwana!
twenty 4 seven! hata mie nimeipenda.
Born 2 suffer! ahsante!
Post a Comment