Monday, November 19, 2012

JUMATATU HII TUNANZE NA SWALI HILI? NINA KASORO GANI?

Jerome na Sesilia walikuwa wamemaliza miaka mitatu tangu waoane. Jerome alikuwa fundi wa saa. Alikuwa amejenga duka lake dogo nje ya nyumba yao. Kila siku, isipokuwa Jumapili, watu waliweza kumkuta hapo. Alipenda kuimba wakati akifanya kazi na kama hakuwa akiimba, basi redio ilikuwa ikicheza muziki kwa sauti kubwa na safi kwa wapita njia wote kusikia.

Watu waliwafahamu kama watu wawili wenye raha. kabla ya kufunga ndoa, Sesilia hakuwahi kuishi mjini. Miaka yake ya kwanza nyumbani mwao mpya ilimshangaza kwa vile alivyowaona watu wakiharakisha kwenda huku na kule. Katika kijiji chake alimokuwa, maisha yalikuwa tofauti sana na tena ya polepole zaidi. Lakini hapa kelele zilikuwa nyingi mno, milio ya honi hasa za watu wenye taksi, na sauti za watu wakiitana.

Lakini alikuwa anafurahi kuvumilia yote haya kwa ajili ya ndoa yake kwani alimpenda sana Jerome. Alijua ya kwamba Jerome alimpenda pia. Hakuongea sana juu ya jambo hilo, lakini Sesilia aliweza kuliona kwa namna alivyokuwa anamwangalia, katika utaratibu wa sauti yake na katika kumtunza kwake. Alizoea kuimba alipokuwa akifagia nyumba. Huko nje pia Jerome naye alikuwa akiimba na sauti zao kwa pamoja ziliwaambia watu waliopita karibu kwamba hiyo ilikuwa ndiyo nyumba yenye raha.

Siku moja, Sesilia akiwa sokoni, alisikia jambo lililomtia uchungu sana. Lucy, kutoka katika kijiji chake, alimwambia kwamba jioni iliyopita alikuwa amemwona Jerome akiingia katika nyumba ya wageni.

"Kwa nini lakini?" Sesilia aliwaza. "Bila shaka siyo kuwa na mwanamke mwingine" Ndiyo Lucy alikuwa na hakika alikuwa ndiye Jerome. Sesilia alijaribu kujisadikisha kwamba bila shaka haikuwa hivyo lakini hakuweza kufukuza wasiwasi mkubwa uliokuwepo moyoni mwake. Alifahamu kwamba watu wengi kati ya watu wake hawakuona kwamba ni jambo baya sana kwa mtu wa ndoa  kuwatembelea wanawake wengine. lakini aliamini ya kwamba ndoa yao ilikuwa tofauti na ndoa nyingine nyingi.

Aliamua kutosema neno lolote. Atasubiri na kufungua macho. Jerome alionekana kama hali yake ni ya kawaida lakini hapa na pale Sesilia alitambua badiliko katika mwenendo wake kwake. Ama, haya yalikuwa ni mawazo yake tu? hakuweza kusema.
Jioni moja, baada ya chakula cha jioni, Jerome alimwambia Sesilia kwamba alikuwa anakwenda kutembea. "Nimeketi kutengeneza saa kutwa kucha, na nisiponyosha miguu ninahofu nitasahau namna ya kutembea", alimwambia haya haku akifunga mlango wa duka lake.
Alipomfuata nyuma barabarani, Sesilia aliona aibu ya kufanya hivyo. Lakini ilimbidi kujua. Labda alikuwa anakwenda kwa wanawake. Walikuwa wanaelekea kwenye nyumba ambayo Lucy alikuwa amemwelezea. hata hivyo mtu aliyeweza kuwa na sababu nyingine za kutembea kwenye mtaa huu. Labda Jerome hakujali alikuwa anakwenda wapi.

Moyo wa Sesilia ulisimama alipomwona Jerome akiingia kwa mlango wa nyuma wa baa /nyumba ya wageni
maalumu ambayo waliishi wanawake. Kumbe, Lucy alikuwa amesema kweli. Akijawa na uchungu, huzuni na hasira, Sesilia alirudi nyumbani polepole. Alijiuliza: "Nina kasoro gani? kwanini Jerome ana haja ya kumwendea mwanamke mwingine? Kwa nini hakai nami? Nina kasoro gani?"
Sesilia hakuweza kujua kilichokuwemo akilini mwa Jerome. Hakuweza kujua kwamba Jerome alikuwa amezoea raha aliyokuwa nayo na kwamba sasa alitaka kuonja kitu kipya, alitaka kugundua mambo mapya na pia alitaka watu wapya wamtosheleze. Sesilia hakujua hayo lakini aliazimia atamfundisha Jerome asikose uaminifu tena----yaani hata naye Sesilia atapata mpenzi.
Je? Unafikiri nini kilimfanya Jerome afanye kama alivyofanya?


3 comments:

Justine Magotti said...

wamependeza sana nimependa hilo poziiiiiiiiiiiiiiiiii

ray njau said...

Duh;Ndoa na changamoto zake!!

Anonymous said...

Kwanini ndoa ni chungu namna hii, kwanini lakini yanatokea haya kwa maisha yangu hakika najutia kila hatua ninayo piga. Soijui kwanini