Habari za leo ndugu zanguni leo nimeamka nikiwa na fikra nyingi sana juu ya jambo hili la malezi yetu ya utotoni yanvyoweza kuathiri ndoa...Naanza na mfano huu:- Patrick na Maria ni mke na mume, kila mmoja amelelewa malezi tofauti.
Patrick alisema tangu nakua au napata akili, nilizoea kumuona baba akirudi nyumbani muda wowote anaotaka na sijawahi kusikia ugomvi wowote toka kwa mama kuhusu kuchelewa huko.
Kwenye akili yangu, nikaamini kwamba, kumbe mwanamme anaweza kurudi muda wowote nyumbani hata kama ni usiku wa manane. Pia niliwahi kumsikia mzee mmoja akimwambia mzee mwenzake ambaye alikuwa anaomba amruhusu aondoke ili awahi nyumbani.... alimwambia hivi.... wewe ni mwanamme bwana, unawahi nyumbani kufanya nini? Au unaenda kupika? Maneno haya yalimuumiza sana mzee yule na mwisho aliamua kubaki wakaendelea kunywa pombe yao taratibu huku akimshukuru kwa ushauri wake mzuri.
Maneno haya yakazidi kumfanya Patrick aamini kwamba kumbe mwanamme hapaswi kurudi mapema nyumbani, alianza kuwaza na kujisemea kimoyomoyo, na mimi nikioa nitakuwa nafanya hivyohivyo kwani huo ndio uanaume.
Kwa upande wa pili, Maria mke wangu kakulia kwenye familia ya mzee Mapunda ambayo baba alikuwa anarudi mapema sana nyumbani, na binti Maria akaamini kwamba kumbe mwanamme anapaswa awahi kurudi nyumbani. Hajawahi kusikia ugomvi wowote kutoka kwa baba na mama yake.
Watu hawa wawili ambao wamekulia malezi tofauti wakaoana, wakawa mke na mume.
Siku za mwanzo bwana Patrick alikuwa anawahi kurudi nyumbani kama ilivyo ada ya mapenzi mapya. Ndoa ilikuwa na furaha kubwa sana
Baada ya miezi miwili kupita, mume akaanza kuchelewa kurudi nyumbani kitendohiki kilimuumiza sana bi Maria , akahisi mume wake kapata mchepuko ( mwanamke wa nje), ugomvi ukachukua mkondo wake, bi Maria akaanza kumnyima unyumba mume wake, akatumia tendo kama silaha ya kumwathibu mumewe, furaha iliyokuwepo kwenye ndoa hii ikayeyuka ghafla, paradiso iliyokuwepo ndani ya ndoa hii ikageuka na kuwa jehanamu, ikabaki historia, ikawa asubuhi ikawa jioni, maisha yakaendelea.
Mume akazidisha kuchelewa, hamu ya mapenzi ikampanda, akaamua kutafuta mwanamke wa pembeni ili apozee hamu zake.
Siku moja wanandoa hawa wakaamua kwenda kupata ushauri kwa mtaalamu wa masuala ya ndoa. Baada ya kuwasikiliza akawaeleza kwa kina namna jinsi malezi yao utotoni yalivyopelekea kuharibu ndoa yao. Akawapa mtihani wachague, wafuate malezi ya mke au mume? Kwa kuwa mume alikuwa akimpenda sana mkewe akashauri wafuate malezi ya mke ya yeye kuwahi nyumbani mapema.
Huwezi amini sasa hivi ndoa ya bi Maria na bwana Patrick ina amani na furaha maradufu ukilinganisha na wakati wanaoana.
Hebu na wewe jiulize kwenye ndoa yako, kwa nini huelewani na mwenzi wako?
2 comments:
Asante sana Kapulya kwa mafundisho ya ndoa. Ni ukweli usiopingika kuwa tofauti za malezi zinaathiri sana ndoa zetu. Ubarikiwe.
Usiye na jina nimefurahi kusoma maoni yako ya moyoni. Unajua na hii ni ndiyo maana utakuta wanaume wengine au wanawwake wanapenda sana kuwanyanyasa wenzi wao kwa vile waliona katika malezi ilikuwa hivyo.
Post a Comment