Friday, December 10, 2010

KUMBUKUMBU+MAISHA

miti ya miembe
Najua hii habari/makala nilishawahi kuiweka lakini leo nimeamka na bado namfikiria/namkumbuka rafiki yangu Claire Mputa yaani kokote ulipo Claire jaribu kunitafuta nitafurahi kuwasiliana nawe tena.Haya ebu jikumbushe tena habari hii.
Nakumbuka ilikuwa mwaka 1983 nilikuwa naishi Lundo (Nyasa) wakati huo. Siku moja mchana nilikuwa naosha vyombo. Nilikuwa nasugua sufuria na vyungu hii ilikuwa kazi yangu. Kama mjuavyo Nyasa ni kula samaki sana. Kuna mtu alitupa miiba ya samaki ovyo na kwa mimi kutojua ni sehemu ile ile niliyokuwa nikiosha vyombo. Kwa bahati mbaya nilipiga magoti bila kujua napiga magoti kwenye miiba. Mmh kazi kwelikweli.

Baada ya siku goti lilianza kuvimba, nilichofanya tangu siku ile ya kwanza sikumwambia mtu nini kimenipata. Sababu kubwa ni kwamba ningeambiwa nibaki nyumbani. Sio kwenda shule ni mgonjwa. Na goti lilizidi kuvimba, lakini nilijikakamua na kuvumilia na maumivu yote. Kisa nilikuwa sitaki kubaki nyumbani bila kuhudhuria masomo.

Lakini siku moja wakati nipo shule nilikosa raha sana kwa maumivu. Rafiki yngu mmoja aitwae Claire Mputa aliona goti langu limevimba sana. Akanishauri niende hospitali naye atanisindikiza. Hata hivyo nilikataa kisa ni kile kile kuogopa kukosa masomo yatanipita. Lakini Claire aliweza kunishauri.

Ilichukua muda mrefu kufika hospitali kwani sasa goti lilikuwa limevimba mno na nilikuwa nachechemea na pia lilikuwa linauma sana, kwani kidonda kilianza kutunga usaa (infection). Kwa hiyo tulikuwa tunatembea polepole sana. Na hapo hatukuwa sisi tu kulikuwa na wanafunzi wengine pia waliokuwa wagonjwa wao walitangulia . Baada ya muda, yaani tulikuwa tunakaribia kufika hospitali tukawakuta wale wanafunzi wenzetu waliotangulia wamechepuka maporini ambako kulikuwa na miembe mingi iliyoshonana. Claire akaniambia; Yasinta twende tukaangalie wanafanya nini? Basi tukaenda kuangalia wote mie na Claire, tulipofika, tukawakuta wanafanya ule mchezo unaofanywa na wanandoa (ngono). Tulishangaa sana na kuondoka, kumbe wao walikuwa si wagonjwa walitaka tu kukwepa masomo na kwenda kufanya ule uchafu. Yaani ilikuwa kinyume kabisa na mimi, na sikutarajia kama wanafunzi kwa umri ule tuliokuwa nao wangeweza kufanya yale tuliowakuta wakiyafanya.

Haya, tulipofika hospital kama kawaida kukaa foleni. Mara ikaja zamu yangu Claire Mputa akanishika mkono na kunisindikiza ndani ya chumba ambacho kilikuwa maalum kwa mambo ya vidonda. Nakumbuka yule daktari alikuwa mzee kidogo, aliitwa Kataulaki. Alinitisha alipochukua mkisu mkubwa nilifikiri anataka kuukata mguu wangu. Lakini hakufanya hivyo alinitibu na mimi na Claire Mputa tukarudi tena shuleni.

Kikubwa ninachotaka kusema hapa ni kwamba kama Claire asingenishauri kwenda hospitali basi leo hii nisingekuwa na mguu wa kushoto. Na pia nisingeyaona yale nilioyaona kule miembeni, kwani yalinifunza kwa kiasi fulani. Napenda kuchukuwa nafasi hii kuwashukuru rafiki yangu Claire Mputa na pia yule Daktari Kataulaki
Napenda kuwaambia ahsanteni sana. IJUMAA NJEMA TUTAONANA TENA WAKATI MWINGINE!!!!!

6 comments:

emu-three said...

Dada Yasinta pole sana, na kusema usingeyaona yale ya kule miembeni, mmmmh, kwako wewe ni sawa unaonekana ulikomaa kiakili...na ulikuwa na ujasiri wa kujifunza kuwa ni `mabaya' kwa kizazi chetu hiki kinachokua, wangeona , ingekuwa chachu ya kufanya `mabaya'...WANGEIGA, situnaona haya kanda zinatouzwa mitaani, vijana wanaiga na matokeo yake ni nini...inatisha!

Upepo Mwanana said...

Ni kweli hii habari nilishaisoma siku za nyuma, lakini mmmmmmh!

Simon Kitururu said...

Nimekwazika na sentensi iishiayo na: `....kumbe wao walikuwa si wagonjwa walitaka tu kukwepa masomo na kwenda kufanya ule uchafu.´´.

Nakwazika sana na hasa WAZAZI ambao katika kuwafunda watoto wao huita tendo la ndoa UCHAFU ,...

...kwa kuwa naamini KISAIKOLOJIA wanaofundwa CHAKULA CHA USIKU kuwa ni uchafu huathirika kikufaidi kula tunda la asili mpaka UTU UZIMANI.

Na UKIFANIKIWA KUOA mmoja wapo kabla hujamuonja maswala NA kustukia utoaji wake nundu nyama na kuhisi mapema achukuliavyo shughuli na nini kiko nyuma ya ubahiri wa mgao wa tamutamu ...


...hasa kama kabla ya kuamua chukua MTU wotewote uliwahi kuonjeshwa shughuli hizi na KIMWANA ambaye shughuli hii haichukulii ni MATUSI wala UCHAFU na anaiingilia kiushupavu kama KIBANGA AMPIGA MKOLONI kichwakichwa kuwakilisha RAHA yake kwa nguvu zote na uhuru wote kinguvukazi akiichukulia ni KITU SAFI SANA kiumurua,....

.... unaweza kujikuta ULIYEOA ambaye anabaniabania kutoa yote kwa kuwa KICHWANI ana STIGMA ya kuwa ni kitu kichafu hakunogei sana na NAKUSHAURI msiajiri HAUSIGELI kwa kuwa anaweza akasababisha uanze kumuangaliaangalia kwa jicho la MAHABA halafu ukaua NDOA na kushindwa kuelezea ni kwa kuwa tu mkewako hakukandi mdadi vizuri na ukiwa likizo na muda mwingi unaadha kupata muda wakutafakari jinsi utamu zilipendwa unavyoumisi kwa jinsi hunogewi na MKEO.:-(

Nawaza tu kwa SAUTI!:-(

Ijumaa na WIKIENDI NJEMA Da Yasinta!

Alindwa Bandio said...

kweli ya kale ni mali na kwa kujikumbusha twajua wapi tulipotoka na tujipange vipi kufikisha malengo. ashukuriwe sana aliyegundua historia

Rachel Siwa said...

dada yasinta goti lilikupelekea kuona watoto wakifanya kibaba na mama!hahhaha!walimaliza masomo au mimba ndiyo vyeti vyao!.

Jacob Malihoja said...

Mhh hii stori najua kila mtu imemkumbusha mengi ya utotoni ... kwa ujumla utoto una mengi..na yote haya yanatokana na malezi ya wazazi na jamii kwa jumla .. inafanya nini.. inasema nini .. mbele ya watoto.. hayo mambo mliyoyaona kwa watoto wenzenu yapo na yataendelea kuwepo... kuna jambo la ziada linatakiwa hapo maana kwa siku hizi ndio kabisa ... watoto wamechanganyikiwa zaidi... lakini pia kuna watoto wengi kama ilivyokuwa kwa Yasinta .. wanayaona ya wenzao .. ila nao wanasubiri hadi watakapokuwa wakubwa inakuwa ni stori ...!