Kila jamii ina visa asili, yaani imani ambazo zinaonekana kama kweli, wakati hazina ushahidi wa aina yoyote kuwa zina ukweli. Lakini, kila kisa asili, kina chimbuko lake. Chimbuko hilo husema kuhusu ambavyo jamii hiyo imekuwa ikiyatafsiri mambo.
Moja ya visa asili katika jamii yetu na jamii nyingine duniani ni kwamba, mwanamke anapoolewa na mwanamume na wakaishi kwa muda mrefu, hatimaye watu hao hutokea wakafanana sura.
Lakini, je kuina ukweli wowote katika jambo hili? Jibu ni kwamba, kuna ukweli ambao hata hivyo unahitaji maelezo zaidi ya yale ambayo tumeyazoea, yasiyo na uchambuzi.
Ni kweli, kuna wanawake ambao wanafanana sura na wanaume ambao wako nao kwenye ndoa.
Hata hivyo, suala la kuishi kwa muda mrefu halina ukweli. Kufanana kwa mke na mume huweza kujitokeza hata kabla hawajaoana.
Si watu wengi ambao wanajua kwamba, baba anapokuwa anampiga mama, yaani mkewe, watoto wanapoona vipigo hivyo, huathirika na wanakuja kutumia uzoefu huo ukubwani. Kama mume anampiga mkewe mara kwa mara kwa mfano, watoto wa kiume kwenye familia hii, wako kwenye uwezekano mkubwa sana wa kuja kuwapiga wake zao.
Tafiti nyingi zinaonesha kwamba, wanaume ambao huwapiga wake zao, wanane kati ya kila kumi walishuhudia baba zao au walezi wao wa kiume wakiwapiga wake zao.
Lakini, pia inaonesha kwamba, wale watoto wa kike ambao waliona mama zao wakipigwa na baba zao, wako kwenye nafasi kubwa ya kuja kuolewa na wanaume ambao nao wanapiga.
Kinachotokea ni kwamba, watoto hawa wa kike, ukubwani hutafuta wanaume ambao wana tabia kama za baba zao, wakiamini bila wenyewe kujua kwamba, wakiwapata wanaume hao watalipiza namna mama zao walivyofanyiwa na baba zao.
Bahati mbaya, badala ya kulipiza, hujikuta wanashindwa kutoka kwenye uhusiano huo wa mateso kwa visingizio mbalimbali. Hii hata hivyo, haina maana kwamba, wanawake wote wanaoteswa kwenye uhusiano wanaendelea kukaa humo kwa sababu hii. Wengine hukaa humo kutokana na utegemezi wa kihisia au kutokana na kutojiamini na hata sababu za kijamii, zikiwemo imani za dini.
Hata hivyo, wataalamu wamegundua kwamba, suala sasa siyo baba kumpiga mama peke yake, bali uhusiano kati ya mtoto wa kike na baba yake. Inaelezwa kwenye tafiti kadhaa kwamba, kama mtoto wa kike anaelewana vizuri sana na baba yake, kuna uwezekano mkubwa kwamba, mtoto huyo atakuja kuolewa na mtu ambaye anafanana na baba huyo.
Awali, tafiti zilipoonesha uwezekano huo, ilionekana kama porojo, lakini hivi karibuni jambo hilo limethibitishwa na vyombo vingi vya kiutafiti.
Hii imefanyika baada ya vyombo hivyo kuwatumia wanawake wengi katika kujaribu kuthibitisha jambo hilo.
Taarifa za kitafiti ambazo zimeripotiwa kwenye jarida la Evolution and Human Behavior, zinaonesha kwamba, mtoto wa kike ambaye ana uelewano wa karibu sana na baba yake utotoni, akija kuwa mkubwa, bila kujua atakuja kuvutwa na mtu ambaye anafanana sura na huyo baba yake.
Baadhi ya watafiti wanasema, labda hapo ndipo mahali ambapo panachimbuka ile imani kwamba, mtu na mkewe wakiishi kwa muda mrefu huja kufanana.
Pengine siyo suala la muda mrefu, bali zaidi ni kwamba, mwanamke ambaye anafanana na mumewe ni mwanamke ambaye alipokuwa mdogo alipendwa au kuelewana sana na baba yake.
Watafiti wengi waliofanyia kazi suala hili wanasema wamegundua kwamba, mtoto wa kike ambaye hakuwa na uelewano mzuri na baba yake, kwa kawaida havutwi kabisa na wanaume ambao wana sura kama ya baba yake.
Labda hii inaweza pia kuelezea ni kwa nini baadhi ya wanawake wazuri sana huolewa na wanaume ambao ni wabaya wa sura (kama jamii inavyowahukumu). Ni kwamba, inawezekana baba yake msichana alikuwa na sura nzuri na hawakuwa na uhusiano mzuri. Ni wazi, mwanamume mwenye sura ya aina ya baba yake hatamvuta. Lakini, hapa inategemea uzuri huo ulikuwaje, kwa sababu anachofuata msichana siyo uzuri au ubaya wa sura, bali sura inayofanana na ya baba yake au isiyofanana na ya baba yake.
Lakini, kama mtoto wa kike alielewana sana na baba yake ambaye ana sura mbaya kwa mujibu wa vipimo vya jamii, atajikuta akivutwa na wanaume wenye sura kama ya baba yake (mbaya) ambapo itakuwa rahisi kwake kuolewa na mmoja kati yao na siyo na wale wenye sura nzuri.
Hebu fikiria kuhusu mtoto wa kike ambaye anafanana na baba yake, halafu anaelewana sana na huyo baba.
Ina maana kwamba, atakuja kuolewa na mwanamume ambaye siyo tu kwamba, anafanana na baba yake, lakini pia ambaye anafanana naye (mwanamke). Kwa kuwa kuna idadi kubwa ya watoto wa kike wanaofanana sura na kuelewana na baba zao, ina maana ndoa za wanaofanana nazo ni nyingi. Lakini, je utafiti huu unataka kuwafundisha wale akina baba ambao jamii inawahukumu kwamba, wana sura mbaya, kutokuwa karibu na watoto wao wa kike ili kuwaepusha kuja kuolewa na wanaume wenye sura kama zao? Bila shaka hilo si lengo la utafiti huu.
Ukweli ni kwamba, kama msichana amempenda mwanamume, maana yake ameona kwake ni mzuri, tofauti na jamii inavyoona.
Kama jamii imepanga viwango vya uzuri na ubaya, ni suala la mtu kuviamini au kutoviamini viwango hivyo. Watafiti wote wanakubaliana jambo moja kwenye utafiti huu, kwamba huenda wanawake huchagua wenza kwa kigezo hiki cha maelewano yao yalivyokuwa na wazazi wao.
Ni kwamba, mwanamke anaweza kumwona mwanamume mwenye sura nzuri, ambayo pengine ni kinyume na ile ya baba yake (mbaya), na akajua kwamba ni sura nzuri.
Lakini, linapokuja suala la kuoa, akachagua sura mbaya ambayo ni ya baba yake. Ninaposema sura nzuri au mbaya, ninazungumzia jamii inavyoona, kwani ukweli ni kwamba, hakuna sura mbaya au nzuri, bali mtu mwenyewe anayetazama anavyoona.
Inaelezwa kwamba, suala ni yupi mzuri kwenye ubongo wa binadamu, halipangwi na wale tunaowaona, bali zaidi hupangwa na wale ambao tulikuwa na uhusiano nao wa dhati na mzuri sana tulipokuwa wadogo. Hapa, baba kwa mtoto wa kike ndivyo ilivyo.
Nimekutana na hii kwa kaka Shabani Kaluse. Na pia, makala hii iliwahi kuandikwa katika gazeti la Jitambue.
7 comments:
Hii mada imekaa vyema, ila natohoa kidoho kwa uoni wangu kuwa watu wakiona baadaye wanafanana!
Mimi nikajiuliza swali moja, je kuna mtu anaweza kunadikuwa yeye ana sura mbaya? kama wapo wanasema tu kimdomo, lakini kila mtu mara nyingi hujiona ana sura nzuri!
Kwa mantiki hiyo basi, mzuri kwako atakuwa sawa na sura yako. Kautafiti kangu ni kuwa, kutokana na kujiona wewe ni mzuri, basi utakayemuona analandana na sura yako atakuwa `mvuto kwako'!
Mkioana, watu watasema mumefanana! au sio
Hako nikautafiti kangu tu, na kawazo kangu tu!
Mmmh!
Nje ya topiki:
Ambiere Kaluthe umetutenga lakini siku hizi!:-(
Nyoka katoka pangoni.........Dada Yasinta ahsante kwa kutukumbusha mada hii ambayo niliiweka pale kwangu siku nyingi kidogo.
Ambiere Kitururu, nipo ndugu yangu majukumu na kutafuta elimu ukubwani kumenibana kaka. Najaribu kutengeneza ratiba itakayonifanya nirejee jukwaani kama zamani, naomba uvumilivu wenu.
Nahisi nina deni kwa kweli.......
@Ambiere Kaluse:
Hakuna taabu Mkuu unajua tunakumisi tu MKUU!
Tuko Pamoja !
Nimejifunza mambo mengi kupitia makala hii ambayo nilikua sijui undani wake.
Asante Da Yasinta na wadau wengine wa blog
MAKULILO
Aise ipo kazi hapa maana ukichunguza maandiko ya Munga Tehenan huwa anaeleza kuzini kisaikolojia(rejea kitabu chake cha MAISHA NA MAFANIKIO), kwahiyo huyu mtoto a.k.a kimwana akikumbuka tu upendo wa baba yake basi anahisi baba nanihiiii amem-love kweli kweli(kwa kutumia lisura la baba yake) mweeeeeeeeeeeeeee mcharukoooooo
mada imetulia dada yangu Yasinta yaani imenikumbusha kipindi nasoma chuo kikuu kulikuwepo na mhadhili wa Saikolojia wangu Dk. Kisanga yaani nilikuwa ntamani aendelee kutuhadhili hata kama kipindi chake kimeisha.
Post a Comment