Sunday, December 6, 2009

KUELEKEA MIAKA 48 YA UHURU: TANZANIA YETU NA ELIMU ZA CHINI YA MITI

Nimevutiwa sana habari iliyowekwa na Profesa Mbele kwenye kibaraza chake akizungumzia juu ya mustakabali wa elimu huko nyumbani Tanzania, bofya hapa umsome .

Hakika habari hiyo imenikumbusha mbali sana yaani simulizi nilizopata toka kwa baba na mama yangu. Maana wao pia wamepata elimu ya aina hii, nakumbuka wakati fulani nilipokuwa mdogo nikisoma shule ya msingi wakati huo mama yangu alinisimulia kuwa wakati alipokuwa akisoma shule ya msingi alikuwa anatembea masaa yasiyopungua matano kutoka nyumbani kwao mpaka shuleni.

Baba naye alinisimulia kuwa yeye alipata elimu yake chini ya mti wa mkorosho na huku akiwa amevaa LUBEGA YA KANIKI (kufunga nguo nyeusi shingoni) lakini hata hivyo alimudu kupata elimu bora mpaka akawa mwalimu.

Kumbuka kwamba walikuwa wanazungumzia mambo ya miaka ya 60 wakati huo tukiwa ndio nchi yetu imejipatia uhuru na kuanza kujitawala. Wakati huo wananchi waalikuwa na mwamko wa Elimu huku wakichagizwa na serikali yao walimudu kusoma hata chini ya miti kwani kulikuwa na kampeni maalum iliyoanzishwa na serikali ya awamu ya kwanza ya kuhakikisha kuwa kila mtu anapata elimu ikiwa ni pamoja na elimu ya watu wazima. Wakati huo Serikali ilikuwa imetangaza vita ya kuwashinda maadui watatu ambao ni Ujinga , Maradhi na Umasikini, na tuliambiwa kuwa hauwezi kuwashinda maadui wawili yaani maradhi na umasikini iwapo hatutafuta ujinga, na ili tufute ujinga ilikuwa ni lazima watu wapate elimu, kwa hiyo swala halikuwa ni madarasa mazuri yaliyonakishiwa bali ilikuwa ni elimu kwanza, hata ikibidi chini ya miti ilimradi watu wapate elimu, halafu baada ya hapo hao maadui wengine yaani umasikini na maradhi itakuwa ni rahisi kuyashinda.

Wiki ijayo tunashereheka miaka 48 tangu tujitawale. Hii ina maana kwamba kama ni mtoto alizaliwa wakati huo tunapata uhuru, basi atakuwa ni mtu mzima ambaye amekwishajitambua na kumudu kujitafutia kipato na kujitegemea. Hapa nazungumzia mtu mzima ambaye amezaliwa akiwa na hana dosari ya kimaumbile yaani sio mlemavu, maana kama angekuwa ni mlemavu tungesema kuwa atakuwa anahitaji uangalizi ili amudu kusimama mwenyewe. Nchi yetu inayo utajiri wa asili kwa maana ya kuwa na ardhi yenye rutuba, madini,uoto wa asili, Misitu, na mbuga za wanyama. Hebu tujiulize hapa, hivi kama utajiri huo tulio nao ungetumika kwa busara hivi kweli tungekuwa na watoto wanaosomea chini ya miti leo hii hata baada ta miaka 48 ya uhuru?

Hii ni sawa na kijana aliyezaliwa miaka 48 iliyopita akiwa na siha nzuri, halafu akakuta baba yake amemuachia utajiri wa kila aina lakini akabaki kulia umasikini na kuishia kuombaomba.Ni aibu iliyoje nchi yetu hata baada ya miaka 48 ya uhuru bado tunaombaomba na kulia eti sisi ni masikini wakati Wenzetu wanakimbilia katika nchi yetu na kujichotea utajiri na kuhamishia kwao utadhani shamba la bibi.

Raisi wetu haishi safari za nje na hata alipoulizwa wakati fulani sababu ya yeye kusafiri mara kwa mara nje ya nchi, alidai kuwa kama ni kuomba misaada katika nchi hizo anazotembelea hawezi kumtuma waziri wake au mtu mwingine kwa sababu hawawezi kupewa kile watakachoomba, isipokuwa yeye.

Yaani mpaka leo hii Raisi wetu anajisifu kwa kuomba tena wazi wazi, wakati hilo ni jambo lenye kutia aibu. Wazungu ni watu wa ajabu sana, wakati unapowaomba misaada wataongea na wewe kwa bashasha na kwa akili ndogo utadhani wanakujali sana lakini amini kwamba ukiondoka huku nyuma wanakung’ong’a na kukudharau sana. Na usidhani huo utakaopewa ni msaada wa bure, ni lazima tu utaulipa kwa namna yoyote.

Na ndio maana hata mheshimiwa Rais akasema kwamba akienda yeye ni rahisi kupewa kwa sababu yeye ndiye mwenye jibu la mwisho. Kwa mfano kama waziri wa Nishati na madini akienda kuomba misaada na akapewa sharti la kuipatia tenda kampuni maarufu ya nchi hiyo ili ije ichimbe madini au Gesi hapa nchini kwa mrahaba mdogo, itakuwa ni vigumu kwa waziri huyo kutoa jibu la moja kwa moja bila kushauriana na mheshimiwa rais, hivyo kutakuwana mlolongo wa safari za kwenda na kurudi mpaka kufikia makubaliano wakati akienda Raisi mwenyewe anakuwa na jibu moja tu, ndio au hapana.

Nchi yetu bado inayo kiwango kidogo cha ongezeko la watu, hii ina maana kwamba bado tunayo ardhi ya kutosha na kwa kuwa bado kuna mapori wananchi wamekuwa wakitawanyika huku na huko kujitafutua makazi na kutafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, lakini cha kushangaza serikali yetu bado imelala usingizi wa samaki aina ya pono bila kuharakisha usambazaji wa miundo mbinu katika maeneo mapya yanayokaliwa na watu. Ni aibu mpaka sasa serikali kusubiri ripoti za vyombo vya habari ili kupata taarifa kuwa ni mahali gani wananchi wanahitaji shule, barabara, zahanati na maji safi.

Na ndio maana wananchi wanaamua kujianzishia shule zao chini ya miti na kutafuta mwalimu ili watoto wao wapate elimu. Kuliko watoto kutembea masaa matatu kwenda shule na masaa matatu kurudi nyumbani . Zamani hatari kubwa iliyohofiwa na wazazi juu ya watoto wao wanapokwenda shule za mbali ilikuwa ni wanyama wakali na nyoka, lakini siku hizi mambo ni tofauti, kuna kubakwa kwa watoto wa kike au hata kuuawa na kukatwa viungo au kuchunwa ngozi.

Athari za watoto kusoma mbali ni nyingi sana lakini kubwa kabisa ni uchovu na njaa. Ni jambo lisilo na ubishi kuwa ni vigumu hata wanafunzi kumuelewa mwalimu kutokana na kusinzia. Maana hapo watakuwa wamechoka. Kwani mwendo mwingi waliutumia kutembea na wakifika shuleni ni kusinzia tu.

Kwa ujumla naweza kusema , mwalimu ni muhimu kuliko vyote.Lakini mazingira ni muhimu pia. Bila kusahau wanafunzi wenye afya na wenye shibe ili kumudu kusoma na kuelewa kile wanachofundishwa na waalimu wao.

6 comments:

Fadhy Mtanga said...

Mmh! Kumbe ni miaka 48 ya uhuru? Kazi ipo. Najua wanajitetea kuwa nchi ni changa. Hivi miaka 48 bado ni uchanga?

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

Yes Fadhy, ni changa bado! Si unaona inapokea maagizo toka kwa wakubwa na inatii kama ntoto?

Kazi ipo kweli kweli...lol

Bennet said...

Hiyo sehemu kuna diwani na mmbunge lakini wao wanakalia posho mbili mbili na kuwasahau wapiga kura

chib said...

Shughuli ipooo

Mzee wa Changamoto said...

Nilisema kuna wakati mtu UNASHIBA NJAA.
Ndio tunakoelekea huku

Anonymous said...

Habari zenu. Ilikuwa ngumu sana kwangu wakati mpenzi wangu aliniacha kwa mwanamke mwingine. Niliharibiwa kihisia, nilivunjika moyo na sikujua la kufanya ili kumrudisha. Nilihangaika kwa miezi mingi na niliendelea kutafuta msaada kutoka kila mahali hadi nilipopata kujua kuhusu DR DAWN. Niliwasiliana naye na kumweleza shida zangu. Alikuwa tayari kunisaidia na kunisisitiza nifuate taratibu ili aweze kurejesha penzi kati yangu na mtu wangu na pia kuhakikisha tunarudiana wote wawili. Nilipata mahitaji yote na ilifanya kazi hiyo. Baada ya saa 48, nilipata ujumbe kutoka kwa mpenzi wangu akiniuliza tarehe. Sasa tuko pamoja tena na shukrani zote kwa DR DAWN. Anaweza kukusaidia kumrudisha mpenzi wako,
Anaweza kukusaidia na uchawi wa ujauzito,

Anaweza kukusaidia kuponya aina yoyote ya ugonjwa.

ikiwa uko tayari kuamini na kubaki na matumaini. Watumie barua pepe tu kupitia: dawnacuna314@gmail.com
WhatsApp: +2349046229159