Tuesday, November 10, 2015

TUNAPOISHI MAISHA YA WENGINE NA KUSAHAU YETU!!!

Maisha ya binadamu hapa duniani yanaanzia pale ambapo natoka kwenye tumbo la mama yake, japokuwa inawezekana kabisa binadamu alianza kabla ya hapo lakini kwa hapa duniani tunaanza kumhesabu kuwepo pale ambapo anatoka kwenye tumbo la mama yake na ndio maana umri wake unaanza kuhesabika kuanzia siku hiyo.

Binadamu huyu anapokuja hapa duniani kwa njia ya kuzaliwa wenyeji wake wa kwanza kabisa ni wazazi wake na ndugu zake wa familia hiyo kwa maana ya kaka na dada zake kama watakuwepo, hawa wenyeji wake wa kwanza ndio ambao wanaanza kumuelekeza na kumuonesha namna ya kuishi hapa duniani, kwa bahati mbaya sana ni kwamba hawa wenyeji kama wana mitazamo mibaya kuhusu maisha na dunia kwa ujumla ndivyo ambavyo mgeni huyu nae atayachukulia maisha ya hapa duniani kwa namna hiyo hiyo kwasababu wenyeji wake wamemuelekeza hivyo na kwasababu yeye ni mgeni basi hatakuwa na namna ya kupingana nao kwakuwa hajui lolote kuhusu maisha haya na dunia kwa ujumla.

Kimsingi makala yangu hii itaegemea sana hapo ili kuweza kuelezea kile ambacho ninataka kukielezea leo, wenyeji wetu hawa mara nyingi kama sio zote wametuaminisha na kutufundiosha mambo mengi sana ambayo yanakuja au yamekuja kutuumiza kwenye maisha yetu, kwanza kabisa kuna mambo ya aina mbili katika maisha yetu hapa duniani, nitajitahidi kuelezea kwa lugha rahisi kabisa ili niweze kueleweka zaidi.
1: Mabaya
2: Mema
Japokuwa kimsingi mambo yote haya yanategemea namna mtu mwenyewe anavyoyachukulia au kutafsiri baya na jema lakini bado haiondoi ukweli kuwa yote hayo yapo, kwa bahati mbaya au nzuri karibia binadamu wote tunayafasiri mambo haya kwa namna inayofanana hivyo tunajikuta kama ni matatizo basi tunakuwa na yale ya kufanana.

Wataalam wa masuala ya malezi wanasema kuwa binadamu anapokuwa na umri wa kuanzia mwaka 0 hadi 6 pale ndipo anapokuwa anaanza kujifunza na kuelewa mambo kwa kiwango cha juu sana kwenye mawazo yake ya kina, binadamu tuna mawazo ya aina mbili, kuna yale ya kawaida na yale ya kina ambapo ndipo "uhalisia" wa maisha yetu unajengwa, hili nitalielezea siku nyingine kwa kina, sasa basi wakati mtoto huyu anaandika mambo haya kwenye ubongo wake ambao unakuwa ni "mweupe" au kwa lugha nyingine tunasema uko mtupu kabisa mtoto huyu au binadamu huyu mpya anakuwa anaanza kujenga kitu kinachoitwa tabia.

Wataalam wanasema kuwa atakaeweza kuja kufuta kile ambacho mtoto amejifunza kwenye umri huo ni yeye mwenyewe tena kwa juhudu hasa maana sio kazi ndogo, katika kipindi hiki ndipo wengi wetu tunaharibikiwa au kuharibiwa na ndio kiini cha karibu kila tatizo katika maisha yetu, hata namna unavyoiona dunia na kuichukulia na namna unavyoyachukulia mambo chanzo chake ni huku, lakini pia kuna kipindi kingine ambacho binadamu huyu anaweza kujifunza ambacho ni cha miaka 7-18, inadaiwa kipindi hiki hakina nguvu sana kama kile cha utotoni japokuwa hata hiki nachoi kinaweza kumfanya mtu kuwa na tabia fulani lakini mara nyingi wanasema wataalam hawa kuwa msingi wa haya yote ni kipindi kile cha umri wa mwaka 0 hadi 6.

Tunapokuwa tunalelewa katika kipindi hicho tunafundishwa kuyapenda zaidi mambo hasi au mabaya kuliko yale chanya au mazuri, unaweza kushangaa au kuanza kukataa, lakini usijali maana nitakueleza kwa mifano pia.
Mfano:-
Hebu chukulia umerudi nyumbani jioni halafu ukafika nyumbani kwako ukakuta taarifa kwamba jirani yako, yaani mliepanga nae nyumba amepita kwenye uchochoro huko njiani alipokuwa anakwenda kwenye shughuli zake na kuokota fuko la hela limejaa kweli kweli....

Baada ya kupata taarifa hii, kwanza utauliza ni kiasi gani na baada ya kupewa jumla ya fedha utapata wivu na baada ya kuona tu huna la kufanya utaishia kumpongeza alieokota na kusema "una bahati sana wewe", hautafikiria kama na wewe unaweza kuja kuokota fuko lile la hela na hata mtu akikuambia kuwa na wewe uwe unapita vichochoroni unaweza kukutana na fuko la hela unaweza kumchika sana mana hauamini kama inaweza kukutokea maana unajua na unaamini ni vigumu.

Lakini wewe huyo huyo siku nyingine ukirudi na ukakutana na taarifa kuwa kuna mpangaji mwenzako mwimngine ambae alipita kwenye barabara fulani kisha akakutana na vibaka na kumkaba kisha wakampora kila kitu, utaingiwa na huruma na utampa pole, baada ya hayo utaingiwa na hofu sana...

Hofu hiyo haitasababishwa na kitu kingine chochote isipokuwa utaamini kabisa na wewe kuna uwezekano mkubwa sana wa kuja kukutana na tukio kama alilokutana nalo mpamgaji mwenzako huyo, kama kuna mtu akikuambia usipite barabara ile aliyopita jirani yako maana kuna uwezekano wa kukutana na vibaka na kuporwa utaona ni ushauri wa maana sana na utaamini kabisa hili linawezekana kukutokea wewe.

Ndivyo ilivyo,wakati tunakua tuliaminishwa hivyo kuwa yale mabaya ndio yanaweza kututokea sisi lakini mazuri hayawezi kututokea sisi hao hao, aina hii ya imani au fikra imejengeka kwentu tangu tukiwa watoto wadogo na tumerithishwa kutoka kwa wazazi wentu na jamii yetu hivyoi kuikwepa ni kama haiwezekani mpaka utakapokuja kujifunza utambuzi na kujua matatizo haya.

Tatizo hili la kimalezi linakuja kuzaa tatizo lingine kubwa sana ambalo ndio msingi wa makala hii na tatizo hilo ni la kuja kuishi maisha ya wengine huku sisi tukiyaacha maisha yetu.

Je ni kwa namna gani hili linatokea? Hebu soma kisa hiki cha kweli kabisa halafu utanuelewa tu......

Niliwahi kupanga nyumba moja kipindi fulani huko nyuma na dada mmoja hivi ambae alikuwa na rafiki yake mmoja ambae alikuwa ameolewa, hebu tuchukulie kuwa huyu dada niliekuwa nimepanga nae nyumba moja alikuwa anaitwa Anna na huyu aliekuwa ameolewa alikuwa anaitwa Rebeca....

Anna alikuwa ni rafiki mkubwa sana wa Rebeca na walikuwa wanashaurina mengi sana, Anna alikuwa hajaolewa kama rafiki yake, huyu rafiki wa Anna alikuwa anaishi kwenye ndoa ya mateso sana maana mumewe alikuwa ni mfujaji wa hela na mlevi lakini pia alikuwa ni mtu wa kubadilisha wanawake sana,Rebeca alikuwa akipata kipigo karibu kila siku kutoka kwa mumewe na kila kitu alikuwa anamsimulia rafiki yake Anna

Anna alikuwa ni kama mfariji wa Rebeca kwenye mateso ya ndoa yake ile,baada ya muda Rebeca alianza kuugua maradhi ya moyo na pia alianza kupata matatizo ya miguu na baadae alianza kulazwa mara kwa mara,rafiki yake alijitahidi sana kwenda kumsalimia kila alipopata muda na baada ya mwaka mmoja wa kuugua Rebeca alifariki dunia akimuacha mumewe na mtoto mmoja wa miaka 6

Baada ya msiba Anna aliendelea na maisha yake kama kawaida lakini alikuwa akisema hana hamu ya kuolewa kwasababu ya mateso aliyokuwa anayasikia na machache kuyashuhudia aliyokuwa anayapata rafiki yake ambae kwa wakati huo ni marehemu, lakini haikupita muda mrefu rafiki yake ya kiume Anna ambae pale nyumbani alikuwa mwenyeji na nilifahamiana nae pia maana alikuwa akija pale mara kwa mara aliamua kumuoa Anna. Anna alionesha kusita sana lakini baadae aliamua kukubali na ndoa ilifungwa na baadae Anna alihamia kwa mumewe.....

Maisha yalianza lakini baada ya miezi minne mumewe Anna aliachishwa kazi baada ya kampuni aliyokuwa anafanyia kazi kufilisika, alirudi nyumbani na kuanza harakati za kutafuta kazi nyingine, lakini huyu jamaa alianza kulalamika tabia ya mkewe kutomuamini haswa pale anapokuwa amechelewa kwenye harakati zake za kutafuta kazi maana kuna wakati alikuwa analazimika kwenda mbali kidogo na pale walipokuwa wanaishi kutafuta kazi.

Mumewe Anna alikuwa anasema mkewe alikuwa hampi hata hela ya nauli alipokuwa anataka kwenda kuhangaika kutafuta kazi na alikuwa anasema kuwa mkewe huyu alikuwa anasema kuwa akimpa hela atakwenda kuzinywea pombe na kuwahinga wanawake, huyu jamaa alishangaa sana maana hajawahi kunywa pombe na alikuwa anajiuliza sana kitu gani kinachomfabnya mkewe kufikiria hivyo,pia anasema hakuwa mtu wa wanawake pia na alikuwa akishangaa sana sababu ya mkewe kuhisi hivyo.

Aliendelea kumpuuza na kuhangaikia kutafuta kazi na wakati akiwa hajapata alikuwa akifanya vibarua vya hapa na pale ili kupata hela ya matumizi madogo madogo ambayo hakuwa akiipata kutoka kwa mkewe japokuwa alikuwa akifanya kazi iliyokuwa inamuingizia kipato kikubwa sana tu.

Kuna wakati ulikuwa unaibuka ugomvi miubwa sana kati ya Anna na mumewe kwasababu Anna alikuwa kimtuhumu jumewe kuchelew maksudi kwasababu alikuwa akitumia muda na vijihela vya vibarua kuhonga wanawake ma kunywa pombe.jamaa alikuwa anakasirika na ulikuwa ukiibuka ugimvi mkubwa sana mara kwa mara, taratibu ndoa yao ikaanza kupata ufa mkubwa sana na ikafikia wakati kukawa na mikwaruzano kila siku huku Anna akimlaumu mumewe kwa kuwa na wanawake wengi.

Mumewe huyu alikuwa anafahamiana na kijana mmoja ambae alikuwa mara nyinbgi wakienda wote kutafuta kazi maana kijana yule alikuwa amemaliza masomo yake ya elimu ya juu, kijana huyu alikuwa anashangaa sana sababu ya mkewe huyu jamaa kumtuhumu mumewe kuwa na wanawake kwasababu hajawahi kusikia huyu jamaa [mumewe Anna] kuzungumzia wanawake wengine achilia mbali kuwa nao.

Ndoa ya Anna ilifikia tamati baada ya miaka miwili tu ya ndoa hiyo na waligawana kila kitu huku Anna akiwa anaondoka kwenye ndoa hiyo akiwa na mtoto mdogo........


Ukitazama kwa juu juu huwezi kuona kiini cha tatizo la ndoa ya Anna, lakini hapo utaona kuwa Anna alikuja kuyaishi maisha ya marehemu rafiki yake, hapa badala ya kuyachukulia maisha ya rafiki yake kama shule yeye aliyachukulia kuwa yake.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya kuyachukulia matukio yanayotokea maishani mwetu kama shule na kuyachukulia yetu, mtu anaevuka barabara kwa mfano, huku akijiona kama mtu ambae atagongwa na gari, huyo ana uwezekano mkubwa sana kugongwa na gari kwasababu atababaika kila akivuka barabara na kupoteza umakini kitu kitakachomfanya agongwe kirahisi sana.

Lakini mtu anaevuka barabara hukua akijua kuna kugongwa na kulichukulia hilo kama suala la kumfanya ajue kuwa akiwa makini hawezi kugongwa na kuchukulia matukio ya watu kugongwa na magari kama shule kwake huyu atakuwa na utulivu wa hali ya juu na utulivu huo utamsababishia umakini mkubwa na kumfanya asibabaike na kufanya uwezekano wa kugongwa na gari kuwa mdogo sana au kutokuwepo kabisa.

Anna aliona maisha ya Rebeca ni maisha yake pia na akayachukua kama yalivyo kwenda kuyaishi kwa mumewe ambae masikini ya Mungu wala hakuwa na tabia kama za shemeji yake Anna [mume wa Rebeca] Anna alimuona mumewe kama ni mume wa Rebeca na akawa na hamaki na kuhisi mabaya kila wakati kumhusu.

Matatizo haya leo na sisi tunayo,chochote ambacho kinaweza kumtokea mtu fulani na kikawa ni kibaya basi tunakibeba na kukifanya chetu na matokeo yake tunaishi maisha ya wengine huku yetu tukiyaacha kabisa.

Tunapokuwa tunatafuta kazi tunakuwa tunatafuta huku tayari tukiwa tumekosa kazi hizo kwasababu fulani alishatafuta akakosa.

Tunapokuwa tunatafuta wachumba tunatafuta wachumba wa aina fulani au wenye sifa fulani kwasababu kuna hiki na kile kilishawatokea akina fulani, hatutafuti wachumba ambao sisi tunawataka isipokuwa tunatafuta wachumba wanaotofautiana na wachumba wa akina fulani maana tumeyabeba maisha yao na kuyafanya yetu.

Tunapokuwa tunasoma ni hivyo hivyo, yaani sisi hatupo kabisa, tumefundishwa kuyapenda mambo hasi na yakiwatokea mambo hasi wenzetu basi tunaamua kuyabeba na kuyafanya yetu, lakini yale mazuri hatuyachukui na tunaamini sio yetu kabisa.....

Malezi yetu yanatuumiza sana, tunaishi kwa matukio, hatumuamini Mungu tena na tunaona fulani kafilisika tunaona na sisi tuko njiani kufilisika, tunaona fulani kaachika kwenye ndoa kwasababu za mateso na sisi tunaona tuko njiani kuachwa na tunaanza kujilinbda na kuwa na tabia za ajabu ajabu.....

Ifikie wakati tujifiunze kuwa sisi ili tufanye maisha yetu kuwa mazuri na yenye furaha....

Habari hii nimetumiwa na Peter Shirima [King] 0786256380. Baada ya kuisoma kwa makini nikaona si vibaya  nikiiweka hapa Maisha na Mafanikio  ili wote tupate elimu hii. AHSANTE PETER!!.

2 comments:

Anonymous said...

Asante sana kwa kushare nasi huu ujumbe ni wa mafundisho ya kufanyia kazi kwa kweli! kubeba maisha ya wengine si vizuri tunajitwika yasiyotuhusu na badala ya kufanya mambo yetu wenyewe, na kila tatizo lina aina yake ya suluhisho na si lazima suluhisho likawa la aina moja kama tulivyoona kwa anna mana angetulia na kuchunguza kumbe yeye suluhisho lake lilikuwa kumshauri mumewe arudi mapema nk. kulikoni kubeba maisha ya marehemu rafikiye akijua anatoka kwenye michepuko bila hata kutafiti kwa undani yeye kama yeye, Mungu atusaidie tunapoishi katika hii dunia ya leo. Siku njema.

Yasinta Ngonyani said...

Usiye na jina! Ahsante kwa mchango wako. Kwani kwa kupata mchango kama huu ndio nami nazidi kupata hamu/moyo wa kuzidi kuwa nanyi katika kublog.PAMOJA DAIMA!