Thursday, November 22, 2018

USIACHE KWENDA KANISANI

 


Mshiriki wa Kanisa, ambaye hapo nyuma amekuwa akihudhuria ibada kila juma,
 aliacha kwenda Kanisani. 
Baada ya wiki kadhaa kupita, Mchungaji aliamua kumtembelea nyumbani kwake.
Ilikuwa jioni ya baridi. Mchungaji alimkuta ndugu yule nyumbani peke yake akiwa
amekaa mbele ya jiko akiota moto
dhidi ya baridi. Akiwa anajaribu kutambua sababu ya  Mchungaji kumtembelea,
alimkaribisha na kumpatia kiti ili 
waote moto pamoja na kusubiri kitakachoendelea.
Mchungaji aliketi, lakini hakusema chochote, alikuwa kimya. Katikati ya ukimya ule,
aliutazama ule moto na mkaa 
uliokuwa ukiwaka jikoni. 
Baada ya dakika kadhaa, Mchungaji akachukua kibanio cha mkaa,
kwa makini akachukua kaa moja lililokuwa 
linawaka zaidi na akaliweka chini peke yake na kisha akakaa tena kwenye kiti chake kimyakimya.

Mwenyeji alitizama chote kilichokuwa kikiendelea akijaribu kujifunza kimyakimya.
Kadri lile kaa lililowekwa pembeni 
lilivyokuwa likiishiwa muwako wake, taratibu majivu yakaanza kulishika na hatimaye likazimika kabisa. 
Likawa baridi likazima kabisa.

Hakuna hata neno lililozungumzwa tangu waliposalimiana.
Mchungaji aliutazama ule mkaa ulozimika 
na akaona kwamba huu ni wakati sasa wa kuondoka.
Alisimama taratibu akauokota ule mkaa ulozimika na
 kuurudisha katikati ya makaa mengine yaliyokuwa yakiwaka moto.
Papohapo likashika moto likaanza kuwaka 
kama makaa mengine.
Mchungaji akaanza kuondoka. Alipofika mlangoni,
mwenyeji akiwa anabubujikwa na machozi shavuni, 
akasema "Mchungaji,
 ahsante sana kwa kunitembelea na hasa kwa hubiri lako hili la mkaa. 
Nimelielewa somo na kuanzia juma lijalo, nitaanza tena kuja kanisani"
**MWISHO WA SIMULIZI*

Nini tunajifunza hapa? Katika siku hizi za mwisho,
mwovu atatumia kila mbinu kuwafanya wanadamu 
wasihudhurie makanisani kwa kuwapatia sababu mbalimbali.
Lakini ushauri wangu, usiache kwenda kwenye ibada
kwa kisingizio kisicho na mashiko.
Kuwa Kanisani na kujichanganya na waamini wenzako kuna faida kubwa na 
kunatia joto la kiroho. Ukijitenga na washiriki wenzako,
utazimika kiroho na hatimaye utakufa kabisa kiroho.

Usiache kwenda kanisani kisa eti kule hawakujali,
usiache kwenda kanisani kisa eti Mchungaji/Askofu anapenda 
sadaka sana, usiache kwenda kanisani kisa huna sadaka,
usiache kwenda kanisani kisa uko katika hisia, 
usiache kwenda kanisani kisa unahofia kurudia nguo uliyovaa juma lililopita,
 usiache kwenda kanisani kisa 
unahofia kuna mtu mmekwazana kule,
usiache kwenda kanisani kisa hujisikii, usiache kwenda kanisani kisa 
wamekuudhi.
Ukiacha kwenda kanisani utazimika kama lile kaa moja,
ni kanisani ndiko MUNGU huachilia baraka ya kutufanya 
tuwe moto mkali, tunapojitenga na kanisa,
baridi ya dunia hii itatupiga na hatimaye tutazimika kabisa. 
Tafadhali usiache kwenda kanisani na Mungu akujalie upate hamasa mpya.

_*Nimeikuta simulizi hii mahali:
Pengine yaweza kutusaidia tuhudhurie ibada ikibidi mpaka katikati ya wiki.*_

No comments: