Friday, May 8, 2009

TUENDELEE KUANGALIE SURA YA KIJIJI CHA LIKUYU FUSI SEHEMU YA NNE= KUNYUMBA

Nimeona afadhali nimalizie kuhusu Likuyu Fusi leo.

Baada ya muda mateka hao walipewa ruhusa ya kuoana na kuzaa watoto. Watoto hao wote walikuwa mali ya Mtepa na waliitwa “Gama”. Wakati wote wa maisha yao walikuwa chini ya nyumba ya Mtepa hata baada ya kufa kwake. Kimila hawa wanaitwa “Gama wa Chikopa”. Mfano mwingine, yupo mzee Zawemba Gama, alipokufa aliacha mke Mzinati mwenye watoto wawili. Baada ya kuondoa tanga bibi Mzinati alipewa ruhusa ya kuolewa na mume mwingine. Akaolewa na Kajanja Komba. Kajanja hakutoa mahari ya kumwoa Mzinati badala yake alitoa mbuzi mmoja dume kwa ndugu wa Zawemba kuwaomba kuwa anataka kuishi na bibi Mzinati. Hivyo Kajanja aliruhusiwa kumchukua Mzinati kwa masharti kuwa watoto wote watakaozaliwa watakuwa mali ya “Gama”. Kajanja hakuwa na haki juu ya watoto, ingwa watoto hawa ilikuwa damu yake. Kutokana na tatizo hili, Kajanja Komba aliamua kuacha jina lake na badala yake akachukua jina Kajanja Gama ili awe na haki ya watoto aliowazaa na bibi Mzinati. Kimila hawa wanaitwa “Gama wa mali” Mfano wa tatu, mzee Yombayomba Nungu aliishi na Mtepa Gama kwa muda mrefu toka ujana wao. Kila ilipotokea shida walisaidiana kama ndugu kumbe ni marafiki tu. Wakati wa pombe watu walibonga “Yeo Gama” au “Yeo Nungu” Mzee Yombayomba aliona aliona jina Nungu halina heshima kama jina la Gama. Baada ya kufa Mtepa, Yombayomba Nungu aliingia nyumba ya Mtepa kwa makusudi ya kuwatunza watoto wa Mtepa. Hapakuwa na mtu aliyemzuia au kushangaa maana kila mmoja alifahamu uhusiano wa Mtepa na Yombayomba. Ili kuwaonyesha watu kuwa yeye Yombayomba hakuwa rafiki au jirani tu, bali alijifanya kuwa ndugu ya Mtepa, hivyo Yombayomba aliamua kuacha jina la “Nungu” na badala yake akajiita Yombayomba Gama. Kimila hawa wanaitwa “Gama wa Kugula”. Nduna Laurent alionya kuwa hakuna sababu ya kugombana na watu wa aina hiyo.

Iwapo mtu aliamua kujiita GAMA au TAWETE kwa manufaa yake ni bora kumwacha alivyo ingwa kama watu wengine wanajua yeye si Gama au Tawete. Alionya pia kuwa watu wa aina hiyo ni wabaya sana na ni lazima kuangalia katika kushirikiana nao. Mtu kama huyo huhesabiwa kama mgeni asiyeaminika maana anaweza kufanya kitendo kibaya kwa wenyeji ili yeye apate kutawala. Kufuatana na utaratibu wa Wangoni katika utawala wa jadi, Manduna na Majumbe wengi walitoka katika jamaa zenye asili ya Waswazi, Watonga, Wakalanga, Wasenga na Wasukuma. Manyapara walichaguliwa toka makabila mengine yaliyojulikana kwenye vita vya makabila. Hapa chini imeorodhesha ufafanuzi wa Nduna Laurenti kuhusu Wangoni wa Songea kwa ujumla.

Wangoni wenye asili ya WASWAZI: Gama, Tawete, Chongwe, Magagura, Mswani, Maseko, Nyumoyo, Tole, Jere, Mshanga, Masheula, Nkosi, Mlangeni na Malindisa.

Wangoni wenye asili ya WATONGA: Makukura, Silengi, Ntocheni, Sisa, Ntani, Ngairo, Nguo, Matinga, Nkuna, Gomo na Pili.

Wangoni wenye asili ya WAKALANGA: Mbano, Soko, Moyo, Zenda, Newa, Shonga, Shawa, Chiwambo, Hara, Mapara, Mteka na Nyati.

Wangoni wenye asili ya WASENGA: Miti, Mvula, Sakara, Lungu, Tembo, Njovu, Duwe, Nguruwe, Ngómbe, Mwanja na Mumba.

Wangoni wenye asili ya WASUKUMA: Chisi, Ntara, Mpepo, Satu, Zinyangu, Chawa na Mzila.

Wangoni wenye asili ya WANYAME: Nyanguru.
Wangoni wenye asili ya WANDENDEULE: Ngonyani, Mapunda, Ntini, Milinga, Nyoni, Henjewele, Ponera, Luhuwu, Nungu, Mango, Nyimbo, Humbaro, Kigombe, Wonde, Ndomba, Tindwa, Magingo na Luambano.

Wangoni wenye asili ya WAMATENGO: Nchimbi, Ndunguru, Komba, Nyoni, Kapinga, Kifaru, Pilika, Hyera, Mbele, Mkwera, Ndimbo, Mapunda, Ngongi, Mbunda, Kinyero, Nombo na Kumburu.

Wangoni wenye asili ya WAPANGWA: Mhagama, Kihwili, Nditi, Lugongo, Njombi, Mwingira, Kihaule, Mbawala, Njerekela, Komba, Kayombo, Mselewa, Nandumba, Luoga, Luena, Mbena, Mwagu, Mlimira, Sanga, Kokowo, Miloha, Kihuru, Chali, Mwinuka, Nyilili, Mkuwa, Mhonyo, Mkinga, Ngaponda, Goliama na Ng´wenya.

7 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Pengine itabidi uandike kakitabu kadogo kuhusu kijiji cha Likuyu Fusi kwani karibu una kila kitu na uwezo wa kukachapisha unao. Kachapishe na pia kaweke mtandaoni. Katawasaidia wengi!

Yasinta Ngonyani said...

Prof. Matondo! Asante sana lakini labda nitahitaji msaada wako. kwani kuandika kitabu si mchezo

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Dada, Yasinta. Ni kakitabu kadogo tu ka kurasa kama 30 hivi kanakoendana na picha mbalimbali za hapo Kijijini na viongozi wa zamani na wa sasa. Si kazi ngumu sana!

Yasinta Ngonyani said...

Sawa ntajitahidi lakini sikuahidi sana maana si unajua tena majukumu kuandika kitabu inabidi utulie au nakosea?

Anonymous said...

Hebu dada Yasinta nisaidie ,hawa kina Haule watakuwa ni wapangwa au wamatengo maana sijawaona kwenye list yako.

Yasinta Ngonyani said...

Usiye na jina je kuna tofauti gani kati ya Kihaule na Haule kwa sababu Kihaule ni asili ya WAPANGWA

Anonymous said...

Asante dada kwa kutunufaisha pia mimi sijakinai kunufaika ni hivi kuna uhusiano gani kati ya MKWERA,NKWELA,MHAGAMA na MWINUKA mm nasikia ni sawa hasa MWINUKA ,MHAGAMA na NKWELA