Showing posts with label udadisi. Show all posts
Showing posts with label udadisi. Show all posts

Monday, October 1, 2012

KUMBE KUNA:- KIMWAGA MDADISI!!!

Jumatatu ya leo nimeona turudi nyuma kidogo ...kumbe kuna KIMWAGA MDADISI  pia sio KAPULYA MDADIDI TU....Hadithi hii kutoka kitabu cha JIFUNZENI LUGHA YETU KITABU 5...KARIBUNI
------------------------------------------------------------------------------------------------------------

 KIMWAGA NA BABU YAKE
HAPA NI KITABU CHENYWE KWA MBELE
Hapo zamani palikuwa na mtoto mmoja akiitwa Kimwaga. Mtoto huyo alimpenda sana babu yake Lukindo. Kimwaga na babu yake waliishi katika kijiji cha Kwemasafi, Wilayani Korogwe. Jioni, baada ya jua kuzama, Kimwaga alikuwa akikoka moto kwenye kibanda chao cha mazungumzo. Babu yake alikuwa akipenda sana kuota moto na kuzungumza na mjukuu wake.
Siku moja jioni, Mzee Lukindo na Kimwaga walikuwa wakiota moto. Kimwaga alikuwa mtoto MDADISI sana. Alimsimulia babu yake habari moja iliyomshangaza. Alisema, "Babu, leo tulikuwa tukilima katika shamba letu la shule. Mimi niliinua jembe kwa nguvu ili nichimbue magugu. Jembe likagonga jiwe, nikaona cheche za moto zinamulika. Hivi babu moto ulitoka wapi?
Babu yake akamwuuliza, "Hivi mjukuu wangu hujui hadithi ya moto?" Kimwaga akamjibu, "Sijui. "Babu yake akamwambia, "Basi nikueleze kidogo. Hapo zamani za kale binadamu hawakuwa na moto. Waliishi katika mapango yenye giza. Walikula matunda na nyama mbichi. Maisha yao yalikuwa ya taabu sana.
"Kwa bahati, siku moja mzee mmoja akachukua mawe, akayagongagonga ili yavunjike apate jiwe la kuchimbia viazi mwitu. Alipoyagonga aliona yakitoa cheche za moto. Alifikiri sana. Halafu akaweka manyasi makavu karibu na yale mawe, na akaendelea kuyagongagonga. Mara yale manyasi yakawaka moto. Kumbe alikuwa amegundua moto kama ulivyoona wewe leo wakati ulipolima huko shuleni."
Kimwaga akamwambia babu, "Kumbe hata mimi nimegundua moto." Kisha akaendelea, "Babu, juzi tulipokuwa tunatoka shule tulinyeshewa na mvua, tukalowa. Tulipofika kwenye shamba moja tulijificha chini ya kibanda kimoja kidogo. Mwenzetu Kimweri akapekechapekecha vijiti viwili vikavu. Mara tukapata moto, tukautumia kwa kukaushia nguo zetu. Je, babu moto ule ulitoka wapi?"
Mzee Lukindo akasema, "Aaa, wewe Kimwaga unadadisi sana. Basi sijakueleza hadithi nyingine. Hapo zamani sana, kabla mimi sijazaliwa, palikuwa na mtoto mmoja mtundu sana. Siku moja alitaka kutoboa kigogo kikavu ili atengeneze kidude cha kuchezea. Akachukua kijiti akaanza kupekecha. Kile kigogo kikatoa unga mweusi. Akaendelea kupekecha kwa nguvu sana. Akaona moshi. Mwisho ule unga mweusi ukashika moto. Akachukua nyasi kavu na kuziweka karibu na ule unga. Nyasi zikawaka moto. Kumbe naye alikuwa amegundua moto."
Siku nyingine tena, Kimwaga akamweleza babu yake namna alivyomtazama buibui. Akamwuliza babu yake , "Je babu, ule uzi ambao buibui hujengea nyumba unatoka wapi?" Mzee Lukindo akajibu, "Buibui ni mdudu wa ajabu. Anapotaka kujenga nyumba yake hutoa maji kutoka tumboni mwake. Maji haya yanapotoka nje tu huganda, na anapokwenda huonekana uzi."
Babu yake Kimwaga alipomaliza kusimulia habari za buibui, Kimwaga alikuwa anasinzia kwa sababu siku ile alichelewa sana kwenda kulala. Mzee Lukindo akamwambia, "Sasa mjukuu wangu, nenda ukalale. Nitakueleza hadithi nyingine kesho," Kimwaga akaenda zake kulala.
JUMATATU NJEMA KWA WOTE...

Wednesday, April 1, 2009

Hivi haya maswali hutokana na nini hasa?

Nimepita ktk kibaraza cha kwa kaka Ramadhani msangi http://www.uchambuzi.blogspot.com/nimeona maswali haya ni maswali mazuri na ni kweli hata mimi nimekuwa nimejiuliza "hivi haya maswali hutokana na nini hasa?" je mtu huwezi kuongea tu bila kuuliza maswali? (Pia yamenigusa kwani binafsi ni mtu wa maswali sana:-)

Limekuwa ni jambo la kawaida sana ambalo limeshazoeleka, kuwa unapokutana na washkaji zako mitaani wanakuuliza kwanini hiki, mara kwanini kile nakadhalika.

Chukulia mfano ulikuwa unafanya kazi, unapoacha au kuachishwa kazi, watu watakuuliza kwanini umeacha au kuachishwa kazi? Kama ulikuwa na demu, mchumba, mke au rafiki na ukaachana naye, watakuuliza kwanini uliachana naye.

Kama ulikuwa unatembea kwa gari na siku ukaamua kuzurura mitaani kwa mguu watakuuliza mbona huna gari leo, na maswali mengine kama hayo. Ninachojiuliza ni kuwa mbona uulizaji wa maswali haya huzingatia upande mmoja zaidi?

Mbona unapokuwa kazini hakuna anayekuuliza kwanini unafanya kazi? Mbona unapokuwa na huyo demu, mchumba, rafiki au mke, hawaulizi kwanini unaye? Mbona unapokuwa unaendesha gari hawakuulizi kwanini unaendesha gari au kwanini ulinunua gari?

Hivi aina hii ya maswali hutokana na nini hasa?

Tuesday, December 16, 2008

KAPULYA MDADISI+(YASINTA MDADISI) =MAISHA

Mwenzenu nimekuwa nimeitafuta hadithi hii muda mrefu sana kwani nakumbuka niliisoma shule ya msingi . Sababu kubwa ya kuitafuta ni kwamba watu wengi wamekuwa wakinipachika majini kutokana na udadisi wangu , wengine wananiita mdadisi, maswali magumu, dada mwenye nguvu, na wengine Kapulya ndio maana naiandika leo. Nadhani wengi tunaikumbuka sana hadithi hii:-

Mzee Mwembe alikuwa mwenye nguvu nyingi na hodari sana wa kufanya kazi za mikono. Aliishi katika kijiji cha mdulo, Wilaya ya Rungwe.

Siku moja baada ya shughuli nyingi za mchana kutwa, Mzee Mwembe alijipumzisha kivulini huku akibugia bwimbwi la mahindi. Karibu naye alikuwepo Kapulya, mtoto wake wa kiume wa kwanza. Kapulya alikuwa mdadisi sana alipenda sana kuuliza maswali. Baba yake alimpenda kwa kuwa maswali yake yalikuwa na busara. Alipomwona baba yake awtulia, kamwuliza, “Baba, babu zetu waliwezaje kuishi na kupata chakula chao bila majembe, mikuki, mapanga na miundu?” Tatizo hili lilikuwa likimsumbua sana kichwani mwake kwa sababu alikwisha sikia kwamba vifaa hivi havikuwepo siku za kale. Mzee Mwembe akachukua bilauri ya maji akayanywa na huku akimsikiliza sana mwanawe. Baada ya kukohoa mara mbili hivi akamweleza, akisema, “siku hizi tunasikia katika mikutano ya siasa maneno mengi sana. Kwa mfano, mawazo ya kujitegemea yanatufundisha tusiwe wanyonyaji au makupe. Katika kujitegemea yatupasa kufikiri na kuvumbua vitu vyetu wenyewe ili kuyafanya maisha yetu yawe rahisi. Hivi ndivyo wazee wetu wa zamani walivyoishi. Pengine utasema kuwa maisha yao yalikuwa magumu lakini wao waliyafurahia. Kila kitu walikipata kwa kukifanyia kazi. Mtu goigoi na mnyonge aliishi kwa taabu na dhiki. Hii yote ilisababishwa na uhaba wa vifaa bora vya kufanyia kazi. Hapakuwepo na majembe, miundu, wala mikuki iliyotengenezwa kwa chuma kama ilivyo sasa. Hata hivyo kila mtu mwanaume aliweza kujitegemea kwa kutumia vifaa vyake vya kumsaidia kuendeshea maisha yake. Ilibidi kutengeneza vifaa hivi kwa kutumia miti. Miti yenyewe ilikuwa ni ile iliyochaguliwa maalum kwa kazi hii. Miti iliyokuwa inafaa ilikuwa ni ile iliyoweza kudumu muda mrefu bila kuharibika.

Matumizi ya vifaa hivi yalikuwa ya aina nyingi. Watu walitumia mikuki kwa kuwindia na kama kinga yao wakati wa safari. Majembe yalitumika kwa kazi ya kulimia na mashoka yalitumika kwa kupasulia kuni”

Kapulya alivutwa sana na maelezo hayo. Akabaki akimsikilza baba yake kwa makini sana. Mzee Mwembe hakukomea hapo, bali aliendelea kusimulia kwamba watu wa zamani walikuwa na tabia nzuri sana. Baadhi ya vitu vingi walivyogundua walivitoa vitumike kwa faida ya wote. Kwa njia hii maarifa ya uvumbuzi yaliendelezwa vizazi hadi vizazi. Kwa kutumia maarifa ya vizazi vilivyotangulia nasi pia tunaweza kuvumbua vitu vipya. Hivyo maisha ya binadamu huendelea kuwa bora na yenye manufaa.

Kapulya alipenda kujua pia jinsi watu wa kale walivyopata moto kwa kupikia vyakula vyao. Alikwisha sikia kuwa hawakuwa na mitambo ya kutengeneza vibiriti kama tuliyo nayo sasa. Hapo Mzee Mwembe hakutaka kmweleza kwa maneno tu. Akamwambia, “Chukua hicho kijiti kilicho hapo nyumba yako. Kichonge kidogo kwa kisu mpaka kipate uso uliosawazika.” Kapulya akafanya kama alivyoagizwa.

Kisha Mzee Mwembe aliendelea kusema. “Sasa tafuta kijiti kingine chenye unene wa kidole chako cha mkono. Halafu kikate kiwe na urefu wa kutosha. Baada ya Kapulya kukusanya vitu hivi Mzee Mwembe akamwelekeza atengeneze kijishimo karibu na ncha ya kile kijiti cha kwanza. Akafanya hivyo. Kisha baba yake akamwambia, “Sasa chukua kijiti chenye kishimo na kiweke juu ya majani makavu yaliyo laini.” Halafu baba yake alimwambia apekeche kile kijiti katika kile kishimo. Akafanya hivyo kwa nguvu sana. Basi akaona vumbi lenye moto sana likianguka juu ya yale majani makavu. Hapo aliona moshi ukitoka. Akazidi kupekecha kwa nguvu zaidi. Baba yake akamwambia, “Sasa chukua hayo majani yanayotoka moshi. Yapulize taratibu.” Akafanya hivyo na mara akaona moto ukiwaka Kapulya akawa amagundua njia ya kupatia moto. Uso wake uliwaka kwa furaha. Akaongeza majani. Halafu alichochea kuni ndogo ndogo na mwishowe akaongeza kuni kubwa. Akakata mahindi akayachoma.

Kwa njia hii ya kuuliza maswali na kwa tabia yake ya kujaribu kugundua vitu vipya Kapulya amejifunza mambo mbalimbali. Haoni haya kuuliza maswali kwa sababu anajua ya kuwa “kuuliza si ujinga.”

SWALI langu kwa ninyi mlionipachika hayo majina:- Je kweli nastahahili kuitwa hayo na kweli nipo sawa na Kapulya? Ni hilo tu.

Saturday, August 23, 2008

AGOSTI 23,2008 MIMI NDIVYO NILIVYO

Udadisi;- Watu wengi wamechoka na mimi kutokana na udadisi wangu, maswali yangu pia. Wanasema huwa hawapati jibu waulizapo swali/maswali. Badala ya kupata jibu, wanapata swali pia. kama vilw KWA NINI? Ni kweli huwa nafanya hivi, sio kwamba nataka kuwatesa wao hapana ila ndivyo nilivyo au niseme ndivyo nilivyozaliwa. Na nimekwisha zoea ila sasa wengi wanaona kero sana. Je ni tabia mbaya kufanya hivyo? Nisaidieni wasomaji.