MAANDALIZI ya safari yangu kwa ajili ya kumpeleka mtoto wa dada yangu kujiunga na masomo ya sekondari Morogoro yalikwenda vizuri na asubuhi yake nilijona mtu mwenye bahati.
Tulifika mapema kwenye kituo kikuu cha mabasi, Ubungo na tulipokuwa tunaelekea kwenye basi moja ambalo tulitaka kukata tiketi, tuliwaona wasichana kadhaa walioonekana kuwa ni wanafunzi, ni kweli nao walikuwa wanakwenda katika shule hiyo. Alikuwepo mwanamume mmoja aliyevalia vizuri ambaye alijitambulisha kuwa mwalimu wa shule hiyo.
Mwalimu huyo, ambaye alikuwa na vitambulisho vya kazi aliwaambia wazazi waliokuwa wanawasindikiza watoto wao wasisumbuke kwani yeye ametumwa kwa ajili hiyo. Hivyo, wazazi, walezi na sisi wengine tuliotumwa tulimkabidhi mwalimu huyo watoto nasi tukarudi nyumbani.
Kwa haiba aliyokuwa nayo mwalimu yule, kwa umri wake na hata upole alioonyesha, alivyokuwa anazungumza taratibu na alivyotuaminishia usalama, haraka tulinong’onezana kuwa ni mlokole. Niliporudi nyumbani asubuhi ile niliwachekesha wazazi wake kwamba 'nimekbidhi binti yao kwa mwalimu mlokole'.
Hilo lilikuwa kosa kubwa. Utaratibu ule ulikuwa tofauti na fikra zake moyoni, alikuwa mbwa mwitu. Mwalimu huyo ambaye, nahifadhi jina lake, ndiye alikuja kutupa pigo kubwa kwa kumkatisha masomo binti yetu baada ya kumpa ujauzito. Tumefungua kesi kortini.
Pamoja na kuchukua hatua hizo, tumekuwa tukijiuliza nini ki kifanyike ili, siyo tu kwa sisi kupata haki kutokana na binti yetu kupewa ujauzito na mwalimu anayepaswa kuwa mlezi wake, bali pia kuwadhibiti walimu wengine wa kiume wenye tabia ya kuwarubuni wanafunzi wa kike na kuwapa mimba.
Hii ni kwa sababu tuliokumbwa na kero siyo sisi tu bali wazazi wengi, na kumekuwa na malalamiko kila kona unayopita, kuhusu wanafunzi wa kike kukatishwa masomo baada ya kugundulika wamepata ujauzito shuleni.
Japokuwa baadhi ya wasichana hupewa mimba shuleni na wanafunzi wenzao wa kiume, watu wa mitaani pamoja na wafanyakazi, ukweli ni kwamba wengi wao hukatishwa masomo kwa kupewa mimba na walimu wao.
Taarifa mbalimbali na uchunguzi uliofanywa katika maeneo mengi, walimu wanahusika kwa kiasi kikubwa. Walimu hao huwapata wanafunzi kwa urahisi kwa vishawishi kadha wa kadhaa vikiwemo vya kuongezewa alama, kupewa maswali ya ziada (twisheni) na kupangiwa kazi nyepesi.
Kuna ukweli pia kwamba baadhi ya wasichana hupata ujauzito kutokana na kutokuwa na maadili mazuri, papara au ulibukeni wa maisha lakini wengine hulazimika kujenga mahusiano ya kimapenzi na walimu wao kwa kufundishwa masomo ya ziada ili wafaulu mitihani yake.
Kwa mfano, hivi karibuni, tulisikia katika baadhi ya vyombo vya habari vikiripoti kuwa mwalimu mkuu wa shule moja iliyoko Kusini mwa Tanzania amepandishwa kizimbani akikabiliwa na shtaka la kumpa mimba mwanafunzi wake.
Katika tukio kama hili, kwa hali ya kawaida unaweza usiamini wala kupata picha inakuwaje, lakini ndiyo hali halisi ya maisha yalivyo katika ulimwengu wa sasa. Kama mzazi wa kiume anaweza kujenga uhusiano wa kimapenzi na mtoto aliyemzaa sembuse mwalimu?.
Ukichunguza kwa makini utagundua chanzo cha tatizo hili ni tamaa ya walimu na ukiukwaji mkubwa wa kanuni za maadili kazini. Walimu hupaswa kuwa walinzi wa wanafunzi na waongoza maadili kinyume cha hivyo ni utovu wa nidhamu.
Mapendekezo yangu.
Kwanza wazazi wote wenye wanafunzi wa kike wahakikishe wanafungua kesi dhidi ya wahusika ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Endapo binti atadai hajui, kwa lengo la kumficha mhusika, basi binti huyo ashitakiwe binafsi.
Pili, wazazi tusikubali vishawishi vya wavulana au walimu au watu wengine weyote walihusika kwamba wasishtakiwe ila waachiwe wawatunze mabinti na ujauzito walionao. Imebainika hufanya hivyo kwa muda tu, baada ya miezi michache huwapa talaka na huo unakuwa mwisho wao.
Tatu, napendekeza serikali iweke uzito kwa upande wa walimu kwamba watakaobainika kuhusishwa tu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi waachishwe kazi. Nina uhakika hakuna anayependa kuachishwa kazi hivyo wataachana na tamaa yao kwa wanafunzi.
Hatua hizo zinaweza kuchangia kupunguza kuwepo kwa matukio kama haya na walimu watajitahidi kuishi juu ya tuhuma za kimapenzi.
Nne, uwepo utaratibu wa kuwapima wanafunzi wa kike kila mara na kuwapa ushauri nasaha kwamba wajifunze na wazoee kusema "hapana" wanapofuatwa na walimu wao kimapenzi.
Tano, iko haja ya kuweka sheria kuzuia wanafunzi kufika kwa walimu kama hawana uhusiano wa kidugu. Shule za seminari na zinazoendeshwa na masista zimeweza, kwa nini ishindikane katika shule za serikali?
Sita ni kwamba chanzo kingine cha matukio ya mamba ni kushiriki starehe. Wazazi wawazuie watoto wao; wavulana kwa wasichana kujiingiza kupita kiasi kwenye burudani kwani ni nchimbuko kubwa la maasi ya maadili na mwishowe kupeana mimba.
Hii ilitoka mwananchi la tarehe 23/6/2009 na mwandishi Elizabeth Suleyman.