Showing posts with label mwanamke. Show all posts
Showing posts with label mwanamke. Show all posts

Monday, May 10, 2021

MKE ASIYE NA MUME, AKAMCHUMBIE NANI?

Niolewe na nani mie! Isingekuwa vigeni, mwanamke kuchumbia Ningepita mitaani, mume kujitafutia, Nisimuudhi Manani, ndio nimejizuia. Mke asiye na mume akamchumbie nani? Ndege maingainga, si jambo la kujitakia, Mume mwema natamani, vipi tajitafutia? Na mwanamume haini, sitaki kunichumbia, Mke asiye na mume akamchumbie nani? Nimetulia nyumbani, sina mume kunioa, Wanifuatao ndani, si wachumba wa kuoa, Hutaka kunirubuni, maasini kunitia, Mke asiye na mume akamchumbie nani? Ndege maingainga, si kosa langu sikia, Niliolewa zamani na mume mwenye udhia, Kanitia kilabuni, pombe kumchuuzia Mke asiye na mume akamchumbie nani? Mimi nikamuamini, huku machozi nalia, Mume hii kazi gani, alokataza jalia? Kheri tukate kuni, mimi nitakuuzia. Mke asiye na mume akamchumbie nani? Akapanda hasirani, na maneno akafyoa: Mke wee mke gani, dini lini ulijua! Alipozidisha kani, ndoaye nikajivua. Mke asiye na mume akamchumbie nani? Wako mabwana wa shani, ningependa kunioa, Hawamtii shetani, Munguamewaongoa, Nao wamomashakani, kwa mabibi walooa, Mke asiye na mume akamchumbie nani? Tu wema hatujuani, wake na waume pia, Twaingia mashakani, kwa wenzi waso murua, Namlilia Manani, mume mwema kunioa, Mke asiye na mume akamchumbie nani? Nawe muombe, ndoa yenu kutulia, Tusikuone mwakani, viragoumepania, Mke na mume nyumbani, mumche Mola Jalia. Mke asiye na mume akamchumbie nani? Shairi hili limetungwa na Sheikh Amri Abedi, nami limenivutia nikaona niliweke hapa ili tujifunze kwa pamoja

Monday, May 23, 2016

KWA NINI WANAWAKE WANATENDEWA MAMBO YA AJABU NA WANAUME?

Siku ya leo nimeamka na mawazo mengi sana katika kichwa changu....Nimewaza na kuwazoa bila kupata jibu nimeona ni bora tuwaze pamoja.  Mawazo yenyewe  ni haya.....
Hivi ni kwa nini wanawake wanatendewa mambo ya ajabu na wanaume?
Ni kwa nini wanawake wanaonekena wanyonge mbele ya wanaume...?
Ni kwa nini wanawake wanakuwa wategemezi kwa wanaume...?
Kuna tofauti gani kati ya mwanamke na mwanamume kiakili, kihisia, kimwili na kiroho?
Ni nini chanzo cha yote haya:- Ni maumbile? Mfumo dume?  Je? ni uvivu tu wa wanawake?  Au ni kushindwa kujitambua kwa mwanamke?

Tuesday, March 10, 2015

MWANAMKE UNATAKIWA KUJITAMBUA!

Leo au niseme wiki hii katika pita pita zangu nimekutana na hii mada kwa dada Adela Kavishe nikaona si mbaya isambae haya karibu uungane nami.... Kila mtu anaweza kuwa na majibu tofauti pale anapoulizwa uzuri wa mwanamke ni nini? kuna atakayesema uzuri wa mwanamke ni muonekano wake, yaani umbo lake zuri la kuvutia, sura yake, miguu nk, lakini pia yupo atakayesema uzuri wa mwanamke ni kuwa na tabia nzuri ama uzuri wa mwanamke ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii. Majibu yote yanaweza kuwa na mtazamo tofauti, lakini ukimfikiria mwanamke mzuri ni yule ambaye anajitambua na kufahamu umuhimu wake katika jamii, mwanamke mzuri ni zaidi ya urembo wa sura yake, ama muonekano wake kumbuka sura nzuri haiwezi kudumu milele, kwani kuna siku itachoka na kuzeeka, muonekano wa mwili na wenyewe hubadilika siku zinavyozidi kwenda hata kama ufanye nini lakini mabadiliko katika mwili ni sehemu ya maisha ya binadamu, ila mwanamke ambaye ni mzuri kutokana na tabia yake, yaani mzuri kutoka moyoni siku zote atabaki kuwa mzuri haijalishi mabadiliko ya muonekano wake. Mwanamke mzuri ni mwanamke anayemjua Mungu na anaishi akiwa na hofu ya Mungu, vilevile ni mvumilivu, mpole, na anayejua kuishi na watu mbalimbali wanaomzunguka katika maisha yake. Mwanamke mzuri sikuzote anajikubali katika hali yoyote iwe ni katika shida au raha, siyo muongo ni mkweli katika maisha yake na wakati wote anasimamia ukweli bila kuwa na hofu. Mwanamke mzuri hatakiwi kuwa na hasira ijapokuwa ni kitu ambaocho kipo katika maisha yetu. Inapotokea unajiona umekereka na una hasira sana ni vyema ukajua namna ya kuzuia hisia zako ili usikurupuke kuchukua maamuzi ambayo yataleta madhara katika maisha yako, kumbuka kutafakari kila jambo kabla ya kuchukua maamuzi, Katika maisha ya mahusiano unaambiwa mwanamke mzuri sikuzote huijenga familia yake, na vilevile mwanaume yeyote ambaye unamuona anamafanikio katika maisha yake basi ujue kuna mwanamke mzuri ambaye amechangia kuwepo maendeleo hayo. Mwanamke mzuri akipenda basi atakupenda kutoka moyoni lakini mwanamke mwenye tabia mbaya akikupenda utaona matokeo yake kwani migogoro itakuwa haishi hususani kama akiwa amekupenda kwasababu ya mali zako siku zikiiisha hawezi kuvumilia ila mwanamke mzuri atakuvumilia katika shida na raha. Mwanamke mzuri anamvutia mwanaume mzuri, ijapokuwa wakati mwingine mwanamke mzuri anaweza kukutana na mwanaume mwenye tabia mbaya, na akavumilia, ila inapofikia wakati mwanaume huyo akazidisha manyanyaso kwa mwanamke huyu basi inampelekea kukakata tamaa na mwisho kulivua pendo, ukipata mwanamke mzuri katika maisha yako usichezee bahati muheshimu sana, na maisha yenu yatakuwa na furaha milele. Mwanamke mzuri sikuzote anatafutwa na mwanaume aliye mzuri, na siyo yeye anamtafuta mwanaume.Mwanamke mzuri sikuzote anawaza mambo mazuri, ikiwa ni pamoja na mafanikio katika maisha kwa njia ya kujituma na kuwa mbunifu huku akifanya kazi kwa bidii kufikia malengo yake, Mwanamke mzuri siyo mbinafsi, atawasaidia na kuwashauri wanaohitaji msaada kutoka kwake kulingana na uwezo alionao mwanamke mzuri ana huruma na anafurahia mafanikio ya wenzake. Ili kuwa mwanamke mzuri unahitaji kujitambua na kuwa na hofu ya Mungu atakusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo unaweza kukutana nazo katika safari ya maisha. Unaambiwa hakuna binadamu aliyekamilika lakini hakuna linaloshindikana kwa Mungu hata pale tunapokosea tunapiga magoti nakuomba msamaha na Mungu anatusamehe mara saba sabini, kisha maisha yanaendelea jambo la msingi ni kutambua kosa na kuwa makini usirudie kosa. katika maisha furaha ni jambo la msingi sana na ili kuwa mzuri sikuzote ni vyema ukaitafuta furaha kwa kuishi vizuri na watu wanaokuzunguka, usiwe mtu mwenye visasi, hasira,majungu, ubinafsi, chuki, choyo na mambo mengine kama hayo Mwanamke mzuri unatakiwa kuwa na upendo kwa watu wote.UJUMBE NA ADELA KAVISHE.... HAPPY WOMEN'S DAY Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka nchini tarehe nane mwezi wa tatu. Mwaka huu kitaifa yanafanyika mkoani Morogoro yakiwa na Kauli Mbiu “Uwezashaji Wanawake, Tekeleza Sasa.” KILA LA KHERI!!

Wednesday, June 4, 2014


Siyo kila dalili ya mwanaume kupenda ni ya kweli…!

Nimeisoma habari hii na nimeona sijasoma tu ila nimejifunza kitu na nimeona niiweke hapa ili wasioisoma wasome pale mpatapo wasaa na kuweza kupata mawili matatu hasa kwa wale wanaotarajia kuwa katika mahusiano...Nimeipata  kwa mzee wa UTAMBUZI. Haya karibuni
----------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Kuna wakati ambapo, wanawake wanajikuta wakikabiliwa na swali la, je, mwanaume huyu ananipenda kweli? Hii hutokea pale anapokutana na mwanaume ambaye, huenda amevutiwa naye. Pengine mwanaume naye anaweza kuonesha kuvutiwa na mwanamke huyo.
Kwa hiyo, mwanamke hujiuliza kama akubali ombi la mwanaume huyo na kukubali kuzungumza naye au kuanzisha naye uhusiano, kama mwanaume atakuwa amezungumza naye kuhusu jambo hilo. ni kweli kwamba, kuna ugumu kwa mwanamke kujua hasa ni kwa namna gani anaweza kujua kwamba, huyo mwanaume amempenda kweli au hapana.
Kuna vitu vingi ambavyo vinaweza kuwa ni dalili ya kumpenda mwanamke, lakini wakati huo huo vinaweza visiwe.
 
1. Hebu tuchukulie kwamba, mwanaume ameonesha kuwa na tabia tunazoziita nzuri. Labda amekumbuka kirahisi jina la mwanamke, ameonesha kuwa msikilizaji mzuri, ameonesha kuwa anajali kuhusu kinachosemwa na mwanamke, na amekuwa anamuuliza maswali kwa dhati na utulivu. Hapa mwanamke anaweza kuamini kwamba, huyu mwanaume anampenda. Lakini ukweli huenda ukawa ni kinyume chake. Inawezekana huyo mwanaume ni muungwana tu, na anaonesha tabia hizo kutokana na uungwana wake na siyo kutokana na kumpenda kimapenzi mwanamke.

2. Kuna watu ambao wana upendo, wamekomaa kihisia na wanajua kuhusiana vizuri na watu. Hii haina maana kwamba, kumwonesha mtu tabia hizo, kuna maana ya kumpenda au kumpenda sana mwanamke. Dalili hizi ni nzuri na inawezekana zikawa zinaonesha mwanaume kumpenda mwanamke, lakini mwanamke asilichukulie jambo hilo kwa namna hiyo.
3. Mwanaume anaweza kuonesha kuwa na udadisi kuhusu mwanamke kwa maana kwamba, kutaka kujua mambo yake, kumfuatilia au kuulizauliza kuhusu habari za mwanamke. Hii haina maana kwamba mwanaume amempenda kimapenzi. Inawezekana mwanaume akawa amevutiwa kimapenzi na mwanamke ndiyo maana akaonesha tabia hizo, lakini siyo lazima iwe hivyo. Kumbuka kwamba, mwanaume anaweza kuvutiwa na mazungumzo ya mwanamke, akavutiwa hata na namna alivyo usoni, hivyo akapenda kuzungumza naye lakini siyo kwa sababu anampenda.
4. Kuna wanaume ambao wana wake au wapenzi, lakini wanajisikia vizuri kusikiliza wanawake wengine au kujua tu habari za wanawake wengine, bila kuwa na haja ya kuanzisha uhusiano nao. Mwanaume anapompa mwanamke ‘ofa’ hasa ya chakula cha mchana au usiku, ni dalili ya wazi ya kuvutiwa naye. Hapa kuna uhakika mkubwa zaidi, labda tu kama mazungumzo yanayotajwa kufanywa wakati huo wa chakula yanafahamika, na ni ya shughuli maalum. Kwa hiyo ‘ofa’ ya chakula ni dalili nzuri na yenye uhakika. Lakini kuna jambo ambalo ni muhimu kwa mwanamke kulifahamu katika hali kama hii. Kuna wakati mwanaume kumpa ‘ofa’ mwanamke kwa chakula cha mchana au jioni, kunaweza kusiwe na maana ya moja kwa moja kwamba, uhusiano utaundwa. Inawezekana katika kutoka outing huko, mwanaume akaghairi. Kwa wengine huchukua muda hadi kuamua kuhusu kuunda uhusiano au hapana.
5. Hata mwanaume kuamua kumpeleka mwanamke kwa familia yao na kumtambulisha kama rafiki yake, ni hatua yenye kuonesha kwamba, mwanaume ameamua kumpenda mwanamke huyo. Lakini wakati mwingine hii inaweza ikawa ni janja yake kutaka tu kumthibitishia mwanamke ili amhadae vizuri, na wala hakuna maana ya uhusiano wa kudumu.
6. Kuzungumza kwa pamoja kuhusu masuala ya baadaye ya kiuhusiano, kama vile, idadi ya watoto na mambo mengine ambayo mara nyingi huzungumzwa na watu ambao tayari wako kwenye uhusiano ni dalili ya mwanaume kuvutiwa mwanamke. Lakini tatizo la jambo hili ni kwamba, kuzungumza masuala ya baadaye inaweza kuwa ni njia ya mwanaume kutaka kujisikia au kujua jinsi inavyokuwa katika mambo hayo. Inaweza kuwa pia ni njia yake ya kutaka kupima wanawake wanavyosema kuhusu masuala hayo. Lakini inaweza ikawa mwanaume huyo anatafuta kujua misimamo ya mwanamke huyo ili hatimaye afanye uamuzi. Kwa hiyo, bado haioneshi kuwa amevutiwa na kuamua tayari.
 
Mara nyingi wanawake hudanganywa na dalili fulani zinazooneshwa na wanaume wakati wanapoanza kuzoeana nao. Dalili hizi huwafanya kuamini kwamba, wanaume hao wamewapenda tayari, wakati siyo kweli. Kwa kuangalia baadhi ya dalili hizo kama nilivyozitaja, mwanamke anaweza kuwa makini wakati anapoanzisha uhusiano, ili asikurupuke na kujikuta amedanganyika. Ni kweli, kuna wakati ni dalili zinasema kweli, lakini kuna wakai zinadanganya kuhusu kupenda au kupendwa.
 
 

Sunday, March 2, 2014

KATIKA JUMAPILI HII YA KWANZA YA MWEZI HUU WA TATU TUANGALIA HILI, MKE:- FURAHA YA MUME WAKE!

Kitabu cha Mithali kinaeleza jinsi mwanamke mkamilifu alivyo, mwanamke aliye furaha na fahari ya mume wake. Mwanamke huyu anafanya kazi zake kwa bidii, ana hekima, ni mwaminifu na hutunza kwa uaminifu watu na vitu vya nyumbani. (Mit. 31:10-31)

Friday, June 14, 2013

UJUMBE WA IJUMAA YA LEO:- NYUSO ZA MWANAMKE!!!

Unajua ya kwamba:- Mwanamke kama dutu la udongo wa mfinyanzi huumbwa na kuumbuliwa na jamii kwa namna mbalimbali. Kama kinyonga, uso wake unabeba rangi tofauti kulingana na mikondo ya maisha na mapigo ya wakati. Itakuwaje mwanamke awe wa kuozwa kama mwenye ugaga wa hisia za kujichagulia mwenyewe; au awe wa kuuzwa kama pakacha la maembe katika soko la umma? Uso wa mwanamke ni njia mbilimbili; ikiwa hazai analea, asipokuwa akirimbesha anarembeshwa, kama hatumbuizwa, ikiwa hajengi anabomoa; na kila mtu anamtazama na kumtarajia aonyeshe  uongofu wa malaika kama kwamba yeye si mtu. Haya yanapokolea ndipo mwanamke anaonyesha nyuso zake.....NAWATAKIENI WOTE IJUMAA NJEMA SANA..KAPULYA

Sunday, June 9, 2013

NI DOMINIKA/JUMAPILI YA 10 YA MWAKA C...NA TUANGALIE/TUSOME HESHIMA YA MWANAMKE NA WITO WAKE!!!

"Mwanamke kama Mama na mlezi wa kwanza wa mwanadamu ana haki ya pekee kabla ya mwanamume. Umama kwa upande wa utu na maadili unaonyesha uwezo wa mwanamke wa kuumba ulivyo muhimu sana ambao unadhihirisha wito wa pekee na ni changamoto ya pekee inayomchochea mwanamume na ubaba wake"
"Heshima ya mwanamke hutegemea utaratibu wa upendo, nao ni hasa utaratibu wa haki na wa kupendana..."
"Hongera kwa mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!" Yesu akajibi, "Barabara; lakini heru yake zaidi yule aliyelisikia neno la Mungu na kulishika"

Thursday, March 14, 2013

TUSISAHAU HADITHI ZETU TULIZOSIMULIWA PIA TULIZOSOMA:- LEO...MWANAMKE MWIZI!!!

Palikuwa na kijana moja aliyekuwa analala kwenye bwaru, hakuwa na mke. Siku moja aliondoka kwenda kutafuta mwanamke. Alifika katika mji wa watu, na katika mji ule palikuwepo wasichana watatu. Msichana moja mchawi, msichana mwingine mwongo na msichana mwingine mwizi. Basi, yule kijana akafikiri afadhali aoea nayeiba. Aliogopa mwanamke mchawi ataenda kumwua. Kadhalika, alifikiri Moyoni mwake: Kama nikioa mwanamke mwongo kutakuwa na mashauri kila siku. Akasema , afadhali nioe ayeiba nitaweza kumlimia.

Kweli akaoa mwanamke anayeiba, akaja naye nyumbani kwake. Akakaa naye. Siku moja mwanamume yule akachinja mbuzi, akakatakata maini na utumbo akampa mkewe apike. Basi, mwanamke yule akachukua ulezi akaanza kusaga kwenye jiwe. Mwanamume akaondoka akaenda kuoga maji mtoni. Mwanamke yule akaacha kusaga, akaingia nyumbani mwake pale alipokuwa amepika kitoweo, akachukua mwiko akaipua finyango moja akatoka nacho akazunguka nyuma ya nyumba akaanza kula. Mume wake alipotoka mtoni, baada ya kuona mke wake hayupo, naye akachukua finyango moja akazunguka upande wa pili akaanza kula. Mke wake alipomwona akasema :- Wa kukasirika hayupo , sote tunaiba.
MUWE NA  SIKU NJEMA SANA WOTE MTAKAOPITA HAPA. HADITHI NYINGINE ITAKUJA WIKI IJAYO PANAPO MAJALIWA....

Tuesday, February 12, 2013

Wanawake wenye sura hii hawawezi kumuuwa nyoka akafa….!

Sura hiyo hapo ni ya mwanamke. Bila shaka umeshwahi kukutana na sura kama hii katika maisha yako. Kama hujawahi kukutana nayo huenda kuna siku utakutana nayo. Jaribu kuzingatia mdomo, meno, macho na paji la uso. Zingatia baadaye, sura nzima kwa ujumla.
Mwanamke mwenye sura kama hii ana tabia zifuatazo:
Ni mwanamke mcheshi na anayependa kujichakesha. ni mwanamke ambaye ana uwezo na ufahamu mkubwa kiakili. Anajua sana kujiuliza maswali kabla hajafanya jambo lolote kuhusiana na namna anavyohusiana na watu wengine. Ni mwanamke mvumilivu na mwenye subira kubwa kwa wengine, hasa wanaomhusu.
Nikisema ni mvumilivu na mwenye subira, nina maana kwamba, anapokerwa na mpenzi, ndugu au rafiki, huchukua muda kufanya uamuzi, hakurupuki tu. Hujiuliza maswali ya hekima kabla hajafanya jambo. Lakini ni mwanamke ambaye hawezi kuuwa nyoka akafa. Ina maana kwamba, akitendewa ubaya leo, ataendelea kuukumbuka kwa muda mrefu sana. Hatalipa kisasi, lakini itakuwa ngumu kwake kusahau.
Mwanamke mwenye sura kama hiyo, hakawii kubadilika. Anaweza kuonekana amekata tamaa kabisa katika jambo au mambo fulani, lakini akitiwa nguvu kidogo anabadilika kabisa na kujipa nguvu ya kuweza na akaweza hasa. Mwanamke mwenye sura hii ana juhudi ya kujenga maisha yake kwa kiwango chenye kushangaza. Anapoamua kufanya hivyo, hufanya kweli na hana mzaha na kile anachofanya.
Ni rahisi kwa mwanamke mwenye sura hii kuvunjwa nguvu, lakini sifa moja kubwa kwake itakuwa ni ile hali ya kujiambia kwamba, ana maisha yake. Lakini kuna bahati mbaya kwamba, wanawake wenye sura kama hii, huwa wanaingia kwenye uhusiano wenye mashaka kirahisi. Wanatokea kupenda kama vipofu na kushikwa kirahisi na wanaume ambao wameingia nao katika uhusiano. Huwa wanasaidia sana kama wamempenda mtu na kusaidia huku hufikia hatua ya utumwa na siyo upendo.
Wenye sura hii wanavyoonekana sivyo wanavyojibu kwenye ombi la tendo la ndoa. Wanaweza kuonekana kama wako tayari kushiriki tendo la ndoa kwa kuonesha dalili zote muhimu, lakini majibu yakaja tofauti kabisa, hadi mwanaume akashangaa.
Hii inatokana na ucheshi wao, kuwa huru katika kujadili mambo na kuchelea kuwakera wengine. Kwa hali hiyo, huwa wanajenga uadui na wanaume au watu wengine ambao hushindwa kuwaelewa. Uzuri wao mwingine ni kujiamini, kusimama kama wao. Kama nilivyosema, mara nyingi hujihesabu kama wao na sio kama watu wengine. Mara nyingi sana ni watu wasiojali sana wengine wanasema kitu gani juu yao.

Chanzo:- Utambuzi na kujitambua.

Thursday, June 14, 2012

HUU KWELI NI UUGWANA? AU AKINA MAMA TUNA MOYO WA KIKATILI HIVI KWELI?


Nimesoma habari hii na kuona picha hii nimepatwa na maumivu yasiyosemekana. Na nikaanza kuwafikiria  watu wanaofanya kila mbinu ili kupata watoto/mtoto halafu wengine wanatupa. Yaani nimeguswa na habari hii si kawaida. Nikaanza kuwa kubeba mimba miezi 9 maumivu yote ya kujifungua halafu anamtupa mtoto. Kama haku/hawataka watoto/mtoto kwa nini kutafuta mtoto? Mbona kuna vizuizi? Malaika kama huyo hana kosa... nashindwa kuendelea kuandika. Soma hapa chini...
----------------------------------------------------------------------------------------------------------
Wewe na mie tuchunguze vizuri photo hiyo, ni dampo la takataka eneo moja huko Mtwara,lakini ukichunguza sana utaona ni uchafu uliyokuwa pamoja na binadamu,binadamu aliyezaliwa na mwanamke.
Ni kitoto kichanga kilichozaliwa na mama huko Mtwara na kukitupa kwenye lindi la mikusanyiko ya kila aina ya uchafu,Hivyo wimbo wa nani kama mama una maana yoyote kwa akina mama wenye moyo wa ukatili kama huyo? .je ni kitu gani kilicho msibu mama huyo hadi kufikia kufanya kitendo hicho kiovu.( Source Mitandao ya Kijamii ) Picha na habari nimeipatahapa

Wednesday, February 8, 2012

Ni nani anayechangia kuvunja ndoa mke au mume?

Habari hii imenisikitisha sana na imeniuma sana nikiwa kama mwanamke. Na nimeshindwa kuvumilia kutoisambaza hebu soma mwenyewe. nimeipata hapa.

Ndugu mpendwa, nakusalimu kwa amani na upendo.

Mimi ni mmoja wa wapenzi wa blog yako, na huwa sikosi kuifungua karibu kila siku, na nikiikosa ninakuwa sina raha, na raha yangu huzidi zaidi pale ninapoona umeandika kitu , hasa kwenye visa vyako, vimekuwa kama kitu ambacho nikikikosa siwezi kuishi…umenipa limbwata la visa vyako…lol
Nimesikitika sana kuwa huna vitendea kazi au sehemu ya kujishikiza, ili uweze kutupa visa hivi ikiwezekana kia siku, maana hasa sisi tunaoishi nje, tunatamani kusoma habari za Kiswahili na hasa visa vyenye ukweli ndani yake, kama vya kwako, ambavyo ukivisoma ni sawa na mtu anayeangalia movie. Na kwanini usiweke matangazo,…mbona wenye mitandao wenine wanaweka, na utakuta mitandao yao haina mengine zaidi …sana-sana ni picha, udaku au umbeya.Mimi leo nimeamua kukuandikia jambo moja linaloninyima raha,…kama halitifaa kuliweka hewani nirudishie, na kama litafaa lipitie vyema, kama nimekosea Kiswahili nirekebishe maana tumeloea Ulaya hata lugha sasa inatupiga chenga. Kwa ujumla nimekuwa nikipitia mitandao mingi, na mingi imekuwa haielezi ukweli kuhusu mwanamke na mwanaume, hasa NDOA, Naizungumzia ndoa, kwani mimi nipo ndani ya ndoa, nana bahati ya kuishi kwetu bongo kwenye manyayaso ya hali ya juu ya ndugu na mama mkwe na pia kuja kuishi Ulaya, ambapo maisha yetu sio mabaya, tunakula ….Sasa ubaya upo wapi, najua wengi mtauliza, nakuwaza, Ubaya upo ndani ya ndoa yenyewe, ubaya upo kwenye kusikilizana, ubaya upo kwenye maisha ya mke na mume, mimi huku ni kama mfanyaakzi wa nyumbani, ninaweza kusema mimi ni mmoja wa wahanga wa ndoa,ingawaje nipo dunia ya sasa, ninaishi Ulaya na mume wangu, lakini maisha ninayoishi na mume wangu ni kama tupo ile dunia ya mababu zetu ambayo mke hana usemi. Mke ni kama bidhaa, yote nimevumilia sikujali kuwa nipo Ulaya, na kama ningeliamua kufanya lolote ningeliweza, lakini bado naiheshimu ndoa yangu. Mimi hapa nipo kama mshumaa tu, siku yoyote unaweza ukazima, na ni bora niyasema haya ili watu wajifunze na waysikie, mwanga wa mshumaa huu usiishie kwangu tu, uwamulikie na wengine wanaoteseka kama mimi.
Najua wengi mtanilaumu kuwa natoa siri yangu ya ndoa, lakini nimeona ni heri kufanya hivyo, ili iwe chachu kwa wale wanaume wengine wenye tabia kama hizi waweze kubadilika, ila kwa mume wanu imeshindikana, imekuwa kama mbuzi kupigiwa gitaa. Hapa nilipo umri umeshapevuka, siwezi kusema niachane naye, nikatafute mume mwingine, nani atanioa mimi wakati sura imeshachujuka. Sitaweza kuwatelekeza watoto wangu kwa kuabdili wanaume, hapana, ila nahitaji mawazo yenu, ….Kwanini naandika haya : Nimeamua kuyaaandika kwasababu kuna mtu aliuliza swali, je kati ya wanandoa wawili mke na mume ni nani anayechania kuvunja ndoa. Ndio sisi wanawake tunakuwa na kitu kinachoitwa kitchen party, je inatusaidiaje kudumisha ndoa zetu, huyu mtu aliuliza hivyo, nikashindwa kumuelewa kwani ndoa ni watu wawili, kama mke atajitahidi sana na mume bado haelewi hiyo ndoa, au hayo mafunzo ya kitchen party yatasaidia nini.
Nimefikiri sana, na kufanyia utafiti ukianzia kwangu mwenyewe na kugundua kuwa kati ya mwanaume na mwanamke anayechangia kwa kiasi kikubwa kubomoa ndoa,ni mwanaume ila nchi za kwetu,hasa nchi za dunia ya tatu(maskini,afrika)wanamwangalia mwanamke kama ndiye chanzo cha kuvunjika ndoa, hasa wakisema, eti wanawake wengi haweze kumtuliza mume, hawajitahidi kumshawishi mume atulie nyumbani na ndio maana wanatafuta nyumba ndogo n.k swali hapa ina maana mke pekee ndiye anatakiwa kufanya jitihada hizo?
Hebu tuziangalie jitihada za mwanamke hasa wa Kiafrika, na tujiulize mwanamume anataka jitihadi gani zaidi ya hizo, kwani,mwanamke wa kiafrika,anamoyo ule wa kuvumilia,maudhi pamoja na manyanyaso ya kila aina,anayofanyiwa na mume wk.Mfano,kupigwa, kuishi na mwanamume mlevi, kumvumilia mwanamume hata akichelewa kazini kwa visingizio mbali mbali,kuletewa watoto wa nje,au hata kuletewa nyumba ndogo au vimada nk.Lakini yote hayo,anayabeba ndani ya moyo wake,na anaona kuwa ni aibu ya ukoo,yeye kurudi kwao,kwa kisa,ameshindwa kuvumilia ndoa.Wanawake wengine,hadi wanapata vilema vya maisha,kwenye ndoa zao na bado wapo kwenye ndoa wanavumilia na kuendelea na maisha kama kawaida.Wengine,wanawafumania waume zao,lakini,wanabakia na siri na kuwatetea waume wao,kuwa hakufanya jambo lolote baya na vitu kama hivyo, je uvu,milivu gani kama huo, upendo gani kama huo, uvuto upi mnaoutaka, kucheza sebene peke yake.Hebu chukulia upande wa pili kwa mwanaume mfano mwanaume,akufumanie,itakuwaje, wewe uchelewe kurudi nyumbani itakuwaje, ….ukosee kufanya jambo fulani, na mengine mengi, mwanamke atakiona cha mtema kuni.
Kwa ujumla Ndoa,inaumiza sana kwa wanawake.Na vidonda vya ndoa au majeraha ya ndoa,ni mengi sana kwa mwanamke na hayaponyeki, kwani kila siku yanatoneshwa…Kwa ujumla mwanamke wa Kiafrika anastahili kupewa heko, na hili nimejifunza nilipokuja kuishi huku Ulaya. Huku Ulaya mwanamke ana haki zake, hayanyanyaswi ovyo,na ole wako mwanamume umnyanyase mkeo halafu alifikishe hilo swala kwenye vyombo vya sheria….sio kwamba nawasifia kwa hili, lakini kwa kiasi kikubwa limemkomboa mwanamke na kujiona kumbe na yeye ni kimumbe kama mwanaume.Mimi nimeishi maisha hayo ya taabu hata vile nipo Ulaya, nimekuwa nikiishi na mume wanu na kumfanyaia yote kama vile nipo nyumbani, lakini ….nasema lakini ni ule usemi usemao penye miti mingi hakuna wajenzi…imefikia mume wangu hawajabiki kwenye swala muhimu la ndoa yake, swala ambalo wengi wanatulaumu kuwa sisi sio wabunifu, hatujui mapenzi, lakini utajuaje kucheza mpira kama hujaingia uwanjani…hayo ni visingizio vyao na kusema ukweli kama hilo wao ndio wakulaumiwa, kwani walitakiwa kushirikiana na mkewe wakafundishana na kuelekezana sio kukimbilia vimada.
Uvumilivu una mwisho wake, na majeraha yakizidi sana mwisho wake yanaweza kugeuka kuwa kansa, ndio maana nimeandika hilo swala kwako, uliweke hadharani watu walijadili na wanaume wasema ukweli wao, ili sisi wanawake tujue ni nini hasa waanume wanakihitaji kutoka kwetu, ili tuwatimizie,… ili tukiwafanyia hivyo waweze kutulia majumbani kwao, ili mwisho wa siku ndoa ziwe na amani.Humutaamini kuwa wengine tunamaliza miezi zaidi ya mitatu hatuwajui waume zetu, waume zetu huku Ulaya wanasingizia kuwa wanachoka kwenye kubeba maboksi, je ni kweli hili au ni kisngizio cha mume wangu tu, au na wenzangu wanafanyiwa hivyo hivyo, …je huko wanaposhinda na hata kulala na machangudoa hawachoki, au wanatufanya sisi ni wajinga tu hatjui nini wanachokifanya, je hii ni ndoa kweli, je na sisi tukiamua kutoka nje ya ndoa waatsemaje, na kwa hilo ni nani atalaumiwa, lakini tunaogopa kuja kuwaacha watoto wetu mayatima kwa kuugua magonjwa mabaya.Samahani sana kama nitakuwa nimewakwaza wengine kwa hayo niliyoyaongea lakini kama ilivyo kawaida ukweli huuma, …
Mimi mwenye majeraha ya ndoa Mama Wawili.

Saturday, January 21, 2012

MWANAMKE NA NYUSO ZAKE!!!

NIMEIPENDA NUKUU HII EBU SOMA!! "Mwanamke kama dutu la udongo wa mfinyanzi huubwa na kuumbuliwa na jamii kwa namna mbalimbali. Kama kinyonga, uso wake unabeba rangi tofauti kulingana na mikondo ya maisha na mapigo ya wakati. Itakuwaje mwanamke awe wa wa kuuzwa kama mwenye ugaga wa hisia za kujichagulia mwenyewe; au awe wa kuuzwa kama pakacha la maemba katika soko la umma? Uso wa mwanamke ni njia mbilimbili; ikiwa hazai analea, isipokuwa akirembesha anarembeshwa, kama hatumbuizi anatumbuizwa, ikiwa hajengi anabomoa; na kila mtu anamtazama na kumtarajia aonyehe uongofu wa malaika kama kwamba yeye si mtu. Haya yanapokolea ndipo mwanamke anaonyesha nyuso zake." kutoka kwenye kitabu kiitwacho NYUSO ZA MWANAMKE.

Wednesday, December 7, 2011

KWELI MAMA NI NGUZO YA FAMILIA/JAMII INATAKIWA KUBADILIKA ILIKUWASAIDIA AKINA MAMA!!


Duh! kaazi kwelikweli najiuliza mpaka sasa kesho kutwa ni miaka 50 ya UHURU lakini...MWANAMKE KWELI NI MWANAMKE..
Picha inamuonesha mama mmoja kutoka katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma akikabiliwa na majukumu mazito kama anavyoonekana katika picha hii.Ingawa mama huyu anakabiliwa na changamoto mbalimbali bado anaonekana mwenye furaha.

Monday, October 10, 2011

MALI NA FEDHA NI KITU GANI KWA MWANAMKE?

Kuna jambo moja leo nataka kulizungumzia, nalo sio jingine bali ni hili la wanaume kutokujua hasa sisi wanawake tunawapendea nini katika ndoa au mahusiano.
Katika maisha yangu ya ndoa nimekuja kugundua mambo mengi sana ambayo huenda wanaume wengi hawayafahamu juu yetu sisi wanawake.

Kuna ujinga mkubwa sana ambao huwa unawasumbua wanaume. Wanaume wengi, sijui ni kutokana na malezi huwa wanadhani kwamba sisi wanawake tunahitaji fedha na mali ili kufurahia maisha ya ndoa au mahusiano.

Na dhana hii ambayo mimi naiona kama ni potofu, huwafanya wanaume kuamini kwamba wakiwa na fedha watakuwa wamemaliza matatizo yote ya mwanamke, na hivyo kuwa na ndoa au mahusiano yenye amani na utulivu.

Na kwa kuwa wanaamini hivyo, basi wakiishiwa ndani hapakaliki, wanahangaika kutafuta fedha ili kuzihami ndoa zao au mahusiano yao na wapenzi wao, kwani wanaamini kuwa bila fedha kutakuwa hakuna upendo tena kutoka kwa wake zao aua wapenzi wao.
Katika kipindi hicho cha ufukara ndipo mwanaume atakuwa karibu zaidi na mke au mpenzi wake kwa hofu ya kuogopa kuachwa, lakini baadae akizipata anakuwa hana muda na (bize)unajitokeza kwani wanakuwa na imani kuwa fedha ipo kwa hiyo uwezekano wa kuachwa na wake au wapenzi wao nao unakuwa haupo.

Sikatai wanaume kutafuta fedha kwa bidii ili kuondokana na umasikini na kuweza kijikimu kifamilia, lakini inapokuja kuonekana kuwa sisi wanawake tunawapenda wanaume kutokana na kuwa na fedha, hilo nalipinga kabisa.
Tuachane na zile dhana zilizojengeka siku hizi kuwa, wanawake wa siku hizi eti wanafuata pesa tu (after money) na wanathamini sana wanaume wenye fedha. Hilo inawezekana lipo lakini hebu tujiulize, hivi mwanamke anayempenda mwanaume kwa ajili ya fedha, hata akiolewa, unadhani atakuwa na amani kweli?

Kama mwanaume huyo atakuwa (bize) hana muda na shughuli zake, halafu anadai kuwa ana amani, basi labda atakuwa anaipata mahali pengine na sio kwa mume huyo, na hiyo ni hatari sana.
Kuna haja ya wanaume kujiangalia mienendo yao, je wanakuwa na muda na wake au wapenzi wao? Na wanatenga muda maalum wa kuzungumzia matatizo ya familia yao na kutafuta suluhu kwa pamoja?

Kuna haja ya wanaume kujikagua na kuangalia upya mahusiano na wake au wapenzi wao yakoje kabla mambo hayajaharibika

Thursday, September 22, 2011

WAZO LA LEO :- USIKIVU WA WANAUME NA WANAWAKE KATIKA MAISHA YA NDOA/ULIJUA KWAMBA...

...Kama unataka kupata usikivu wa mwanamme kitu muhimu ni kumgusa? na pia ulijua kama unataka usikivu wa mwanamke basi mnongóneze!!! TUTAKUTANA/ONANA TENA KESHO!!!!

Tuesday, October 19, 2010

Ataka talaka kwa nguvu ili aolewe na mwenye pesa


Mwanamke mmoja alitoa kioja baada ya kudai talaka kinguvu huku jamii iliyomzunguka ikimshangaa kwa kilichosemekana kuwa amepata mwanaume mwenye fedha.

Mwanamke huyo, alipokuja kwa wifi yake,kumueleza akamwambie kaka yake ampe talaka kwa kuwa alichoshwa na tabia zake,na kumuamuru akiwa hajampa talaka hiyo ataondoka hata kama hajapewa talaka.

“Mimi namuomba talaka kaka yako hataki kunipa ana maana gani? mimi simuhitaji tena nimechoshwa na dhiki mimi, anipe karatasi langu niondoke nyumbani kwake” na asiponipa naenda bakwata lazima aitoe” alifoka dada huyo kwa sauti bila hata aibu

Wifi huyo alijaribu kumuuliza alikosewa nini na kaka yake huyo, na swali hilo hakutaka kulijibu na kumueleza kuwa yeye anachohitaji ni talaka hahitaji maswali,

Hata hivyo mwanamke huyo ilifahamika na ndugu zake kuwa,alikuwa akitaka kuolewa na mwanaume mwingine ambaye alimuona atambadilisha kimaisha kwa kuwa ndugu zake hao alidai mwanaume huyo alikuwa na fedha zaidi ya mume wake wa sasa. Habari hii nimeipata Simon wa samvande

Friday, October 15, 2010

NI MIAKA MITANO LEO TANGU BIBI NA BWANA KALUSE WAFUNGE PINGU ZA MAISHA!!

Kaka Shabani Kaluse,Mkewe na Mvulana wao Abraham
Katika ndoa inatakiwa uvumilivu, upendo, maelewano nk. Familia hii leo imefikisha miaka mitano ya ndoa yao na matunda pia tunayaona, si mengine tena bali ni mtoto Abraham. Binafsi napenda kutoa HONGERA nyingi sana kwa siku yenu hii ya ndoa na pia nawatakieni kila la kheri mzidi kupendana na kuishi mpaka vikongwe kabisa na muwe na wajukuu wengiiii. Hakika nafurahi sana kuwa KAPULYA maana unajua mangi mengi kuuliza si ujinga bali ni kujua mengiiiii. Picha nimetumiwa na familia yenyewe zaidi ingia hapa mzee wa utambuzi. HONGERENI SANA KWA KUTIMIZA MIAKA MITANO YA NDOA!!!!!!!!!!!!!!!!!!



Wednesday, October 6, 2010

WANANDOA NA KAULI HIZI: HATA VIKOMBE KABATINI HUGONGANA, ITAKUWA SIE?

Ndugu wasomaji, Habari hii nilishawahi kuivuka hapa MAISHA NA MAFANIKIO. Binafsi imenivutia sana na nimeona tuirudie tena kwani KURUDIA KITU ni KUJIFUNZA ZAIDI. KARIBUNI UNGANENI NAMI.
------------------------------------------------------------------------------------------------

Je unadhani au kuamini kwamba kuna ndoa ambazo wanandoa wake hawagombani kabisa? Kama unaamini hivyo, basi unajidanganya na labda unaishi katika dunia ya peke yako.

Ni jambo lenye ukweli wa kutosha kabisa kwamba wanandoa wote duniani hutokea kugombana, lakini kugombana huko hutokana na migongano au mizozo ya muda tu ambayo huweza kutatuliwa na pande mbili kama wakiamua kufanya hivyo.

Wewe unayesoma hapa, napenda kukuambia ukweli kwamba usiogope migogoro ya ndoa, kwani hicho ni kitu ambacho kamwe huwezi kukiepuka. Kuna msemo mmoja unatumika sana huko nyumbani usemao, " hata vikombe kabatini hugongana itakuwa wana ndoa?" Hii ina maana gani, ina maana kwamba haiwezekani watu kuishi pamoja halafu msiwe mnatofautiana, na kama ukiona hivyo, jua kwamba hiyo ndoa si salama kwani siku yoyote bomu litapasuka na madhara yake yatakuwa ni makubwa kuliko kawaida.

Kuna watu ambao hata kama wamekosewa na wenzi wao hunyamaza kimya na kumeza hasira zao, wengine huogopa kuwakabili wenzi wao na kuzungumzia jambo linalowakera kwa kuhofia kuonekana kama wana kasoro au ghubu. Jambo hili ni hatari sana.

Kumkabili mwenzi wako na kumwambia hisia zako kama amekukosea au amekwenda kinyume na matarajio yako ni jambao la maana sana katika kudumisha uhusiano. Lakini naomba nitahadharishe kwamba, ni vyema kufanya hivyo bila kumshusha, kubeza au kusimanga kwani hiyo sio dalili nzuri ya upendo.

Inashauriwa kwamba wanandoa au wapenzi wanapokwaruzana inabidi wajadili tofauti zao bila kusigishana, kila mmoja akitaka kuwa mshindi, hiyo haitasaidia kuimarisha ndoa bali itaongeza tatizo. Ni vyema upande unaohusika na tatizo, uwajibike na kuomba radhi kwa ustawi wa ndoa, huo ndio ukomavu.

Kutojadili mgogoro kwa wanandoa na kuupatia ufumbuzi wa tatizo huwafanya wandoa kuwa mbali kihisia, na athari zake ni kuwakuta wanandoa wakiwa wageni wa kila mmoja kwa mwenzake, yaani hakuna mawasiliano, kila mtu na lwake.

Jambo la msingi kwa wanandoa ni kujadili tofauti zao pindi linapojitokeza jambo linalomkera mmoja wa wanandoa, kwani hakuna jambo linaloweza kujitatua lenyewe bila kutatuliwa na wandoa husika. Kuacha jambo lolote bila kulitafutia suluhu ni sawa na kutega bomu, ambapo siku likilipuka madhara yake ni makubwa sana.

Unaweza kukuta mwanandoa anakereka na mambo madogo madogo ya mwenzi wake lakini hasemi, ingawa yanamkera kupita kiasi akitegemea huyo mwenzi wake atajua na kuacha, thubutu…..inapotokea siku yeye amekosa jambo dogo tu na huyo mwenzi wake akamsema, basi atatumia fursa hiyo kuanza kujibu mapigo kwa kueleza yale yanayomkera kutoka kwa mwenzi wake, na hapo itakuwa kila mtu anavutia kwake kama mwamba ngoma………na aamini nawaambia kuwa kamwe hawezi kupatikana mshindi katika jambo hilo, kwani mjadala huo unaweza kutoka nje ya mada kila mmoja akijitahidi kutafuta makosa ya mwenzi wake hata yale yaliyotokea wakati wa uchumba wenu ili mradi vurugu tupu.

Inatakiwa wanandoa wajadili kila jambo linalojitokeza hadi kulipatia suluhu, vinginevyo ni kuichimbia ndoa yenu kaburi la mapema. Wakati mwingine unaweza kukuta mwanamke analalamika juu ya kutoridhishwa kwake na matumizi ya mumewe, na hapo mume naye ataanza kukumbusha juu ya matumizi yasiyo ya lazima yaliyofanywa na mke huko nyuma. Mke naye hataridhika atakumbushia jambo lingine na lingine hadi hata mada iliyokuwa ikijadiliwa inasahaulika.

Jambo lingine ni kujumuisha mambo, matumizi ya maneno kama, mara nyingi, kila wakati au mara kwa mara si mazuri sana. Unaweza kukuta mtu mwenzi wake amekosea jambo halafu mwenzie anamwambia “Kila mara huwa unafanya hivi” au mara nyingi huwa unafanya hivyo…..Hii ni hatari kwa ustawi wa wanandoa, kwani kwa kujumuisha ni sawa na kumwambia mwenzi wako kuwa kila mara yeye ndiye mkosaji.

Kwa haya niliyoyaeleza hapa sina maana kwamba huu ndio muarobaini pekee wa kuimarisha mahusiano kwa wanandoa, bali ni moja ya mambo muhimu kati ya mengi ambayo yakizingatiwa na wanandoa wote basi ndoa yao itakuwa imara Tujadili pamoja………..

Na hapa yalikuwa maoni ya baadhi ya wasomaji......

James Adolwa said...
Kweli unavyosema kuwa maranyingi mzozo ukidhihirika ni kwasababu kuna kero lililo fichika ama kufunikiwa. Swala lingine ambalo watu wanatakikana kuzingatia....wacha nitumie kiingereza kidogo....One needs to consider what one keeps steaming under the lid of the cooking pot. If you spend your time and energy focusing on the weaknesses or faults of another then all that you will see in the other person are weaknesses and faults...and you will end up cooking up a foul tasting broth that will spill over and put out the flame of your relationship.

Instead try and focus on the strengths and virtues of your partner and in the end you will find that you keep seeing more and more good things. This is not to say that all the experiences will be pleasant but rather all the bitter, sweet, sour and salty experiences work out together such that the sum total ; the big picture, the essence of the whole experience works out to be a pleasant experience for both. I am no expert but these are the thoughts that flowed from my soul.

October 12, 2009 8:34 PM
Ramson said...
Dada yangu hapo umenena, kaka James, naona imebidi kuandikwa kwa kiingereza ili kuweka msisistizo....kaaaazi kweli kweli.

Dada Yasinta hili ni darasa tosha kwa wale wanandoa ambao hawakubahatika kujifunza namna ya kutatua migogogro ya ndani katika uwanja ulio sawa. Unajua wazee wetu walipokuwa wakituambia kuwa ndoa ni kuvumiliana wengi walitafsiri vibaya, walijua kuwa ni kumeza hasira zetu pindi tunapokosewa na hii ilitumiwa vibaya zaidi na wanawake, lakini siwalaumu bali mfumo dume ndio uliowafundisha.......
Inaposemwa kuwa ndoa ni kuvumiliana maana yake ni kujadiliana kwa uwazi pale tatizo au kunapozuka kutoelewana juu ya jambo fulani na uzingativu uwekwe kwenye kutatua tatizo sio kubishana kwa ajili ya kumtafuta mkosaji. Tumelelewa katika familia tofauti, kuna baadhi ya wanume wamefundishwa kuwa hawapaswi kuwaomba wake zao radhi hata kama wamekosa,,,,,inabidi mke awe makini kama akishajua kuwa mumewe ni wa aina hiyo.....


Anonymous said...
Darsa hilo Yasinta, safi sana, umemaliza yote hata cha kuongeza sina kwa leo labda kifupi sana wanasema katika maandiko matakatifu kwamba "upendo huvumilia, hauhesabu mabaya na kadhalika..." basi kama tafsiri sahihi ya upendo ikiwepo miongoni mwa wana ndoa basi mchezo umeisha, du ni hivi jioni hii nilikuwa nasikiliza kipindi cha maridhiano kupitia redio Maria Tanzania du, niliyoyasikia huko yanatisha kisa kusaka mtoto sijui ujiko kwa mwanaume! na kisa kingine kilikuwa wiki iliyopita ambapo mwanaume alienda kuazima dume ili limzalishie watoto, huko kote mwanamke alikuwa anashinikizwa lazima afanye mapenzi na hilo beberu!!

SIMON KITURURU said...
Bomba la somo hili Dada Yasinta!

Lakini sijui kwanini huu msemo wa kuwa Vikombe hugongana kabatini huwa na wasiwasi nao kwa kuwa nashindwa kuwa na uhakika kuwa kihalihalisi labda VIKOMBE hugonganishwa na HAVIGONGANI tu kienyeji ndani ya KABATI.


Anonymous said...
My sista unanikuna jamani hilo ni kweli my sista kwani kila mtu kalelea kivyake na malezi yake just meet with her /him ukubwani ni lazima kuwe na migongano ya hapa na pale nduguyo tu mwajibizana sembuse mtu baki ooh please Kaka Simon Kitururu kwani utakuta wewe ukisusa wenzio wanakula food yote lkn familia nyingine ukisusa watu hawali mpaka ujongee mezani,Kuna wengine hata hajui kumheshimu dadaake or kakaake yote ni malezi hp umeelewa brother from anaother mother meanz ya vikombe kugongana ni misemo ya mafumbo ya mababu zetu soo Open ya Eyes oky!!!!

chib said...
Big up Kitururu, huwa naupinga msemo huo wa vikombe kabatini kugongangana, ukweli kama kabati imetulia, vitagongana vipi, ni wale wenye mafujo tu ndio huvigonganisha, au kama unakaa Sumatra ambako matetemeko ya ardhi hayaishi, hapo ndio vitagonganishwa na tetemeko. Ypte kwa yote, somo hilo ni zuri kabisa kwa watu wote wenye ndoa na watarajiwa.

SIMON KITURURU said...
@Anony: nankunukuuu ``ooh please Kaka Simon Kitururu kwani utakuta wewe ukisusa wenzio wanakula food yote......''

Hapo si kunauwezekano kiwagonganishacho ni FUDI?:-)

Nimekuelewa lakini MKUU na pointi yako nimeipata.

@MKUU CHIB: Hapo kwa mtazamo wangu umemaliza NUKTA


Markus Mpangala said...
Ni MSARAGAMBO hapo

Yasinta Ngonyani said...
Nachukua nafasi hii kuwashukuruni wote kwa maoni yenu kwani huku ndio kujifunza. Maana kila mtu anajifunza toka kwa mwingine. Ila sifungi mjadala karibuni kujadili zaidi

Monday, September 27, 2010

LAITI KAMA NINGEKUFAHAMU KABLA.........HADITHI YA KUFIKIRIKA


Miaka mitano iliyopita nilikuwa natafuta mke wa kumuoa ambaye angekuwa na sifa nizitakazo. Nilikuwa natafuta msichana mzuri wa wastani maana sikutaka kuoa mke mzuri kupindukia asije niua bure kwa presha na jakamoyo. Nilikuwa natafuta binti atakanikubali kama nilivyo na mapungufu yangu na mimi niliahidi kumkubali na mapungufu yake ili mradi asiwe ni mwenye tamaa ya kupenda sana pesa na mfujaji.
Awe na staha na anayeweza kukabiliana na hali yoyote, niwe nacho, nisiwe nacho au kwa kifupi tupendane kwa shida na raha.

Pamoja na sifa nyingine ndogo ndogo, lakini muhimu ni upendo na amani vitawale nyumbani kwangu.
Hatimaye nilimpata Binti Yasinaty, na kukutana kwetu kulikuwa ni kama muujiza, nakumbuka siku hiyo nilipanda daladala nikielekea kazini na kwa bahati kiti nilichokalia kilikuwa ni cha mwisho upande wa dirishani. Wakati nakaa nikahisi kukalia kitu kigumu, nilipopapasa ilikuwa ni simu mpya kabisa tena ya bei mbaya kama sikosei wakati huo ilikuwa inauzwa shilingi laki nne kwa wakati huo, kumbuka kwamba hapa nazungumzia habari ya miaka mitano iliyopita.

Kwa bahati mbaya simu ile ilikuwa imezimwa, na nilipojaribu kuiwasha iliwaka na kuzima kuashiria kwamba betri yake iliisha chaji. Niliiweka mfukoni na kujiuliza kuwa ile simu ilikuwa ni ya nani, sikusikia mtu kulalamika kwamba amepoteza simu na niliogopa kuuliza maana nilichelea mtu kujitokeza na kusema kwamba ni yake ilihali sio ya kwake.

Nilifika ofisini na kuanza kazi, baadae nilimuita katibu muhtasi wangu na kumwomba anisaidie kutafuta chaji ya ile simu kwa kuwauliza wafanyakazi pale ofisini, nilikuwa na shauku ya kumfahamu mwenye simu ile ili nimrudishie, kwani nilikuwa namuoana dhahiri akisikitika kwa kupotelewa na simu yake, kwa jinsi ilivyoonekana ilikuwa bado ilikuwa ni mpya kabisa na ilikuwa haijatumika zaidi ya wiki.

Katibu wangu muhtasi hakufanikiwa kuipata ile chaja ya ile simu. Niliweka ile simu kwenye droo ya ofisini kwangu ili jioni nikitoka nipitie nayo kariakoo ninunue chaja yake.
Ilipofika jioni alikuja mchumba wangu ambaye tulitofautiana wiki iliyopita na kuamua kutengana naye. Sikutaka kuonana naye na nilimwambia katibu wangu muhtasi amwambie kuwa niko bize na sitaki afike tena pale ofisini kwangu.

Ukweli ni kwamba nilimpenda sana lakini kitendo chake cha kukuta mwanaume mwingine chumbani kwake tena akiwa amelala kitandani kwake halafu anajidai kunidanganya kuwa eti ni binamu yake hakikunifurahisha kabisa. Nakumbuka nilisafiri kikazi kwenda Mbeya, na ilikuwa nikae kule kwa wiki moja, lakini ilitokea dharura huku Makao makuu Dar ikabidi nirudi baada ya siku mbili tu na nilipofika kwa kuwa ilikuwa ni usiku kama saa mbili niliamua kupitia kwa mchumba wangu ambaye alikuwa akiishi Mwengeili kupata chakula cha jioni kabla sijaenda kwangu Maeneo ya Sinza. Nilipofika nilimkuta akiwa nje akipika, lakini aliponiona alishtuka sana akabaki kinywa wazi, hakunipokea alibaki ameduwaa, nikahisi kuna jambo. Nilimsalimia alijibu kwa wasiwasi nilipotaka kuingia ndani, alinizuia, na huku akiongea kwa sauti yenye kutetemeka aliniambia eti ndani kuna binamu yake kaja na amejipumzisha kitandani kwake, nilishtuka. Niliiingia ndani moja kwa moja na kumkuta kijana amelala kitandani nilipomuhoji kuwa yeye ni nani na anafanya nini pale akaniambia kuwa yuko pale kwa girlfriend wake na alitaka kujua eti mimi ni nani..Sikutaka kuzua ugomvi, nilimwambia kuwa pale ni kwa dada yangu na nilifika kumsalimia, nilimuomba radhi kwa kuingia bila hodi, ila nilimshauri aharakishe kulipa mahari ili tujue kuwa dada yetu anaye mtu, ili wakati mwingine tubishe hodi, niliongea kwa utani, yule kijana alimsifia sana mchumba wangu kuwa ni mzuri hasa na anajua kupenda, alibwabwaja mambo mengi na upuuzi wao wanaofanya nikiwa sipo, niliongea naye kwa utani mwingi na kuaga na kuondoka, lakini moyoni roho ilikuwa ikiniuma kweli. Nilikuwa nampa yule binti karibu kila kitu alichohitaji, lakini kumbe hakuridhika bado akawa na mwanaume mwingine.

Nilitoka na nilimkuta kajiinamia pale nje, sikumuaga nikaondoka zangu. Nilipofika nyumbani nilimtumia ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani nikimwambia kuwa kuanzia siku hiyo ilikuwa ni mwisho wa uhusiano wetu. Hakijibu na siku iliyofuata alipiga simu lakini sikupokea, alibadilisha namba na nilipopokea na kugundua kuwa ni yeye nilikata simu, baadae zilifuata ujumbe kadhaa wa simu yake ya kiganjani akitaka tuonane ili tuyamalize. Sikumjibu. Na ndio akaamua kuja ofisini.

Nilimpigia simu katibu muhtasi wangu na kumuamuru amwambie yule binti aondoke pale ofisini. Niliambiwa kuwa amekataa, nilimpigia simu dereva wangu na kumuuliza kama gari limeshatoka gereji, akanijibu kuwa gari litatoka baadae kidogo, nikamwambia akitoka gereji aende nalo nyumbani kisha kesho asubuhi anifuate. Gari langu liliharibika siku mbili zilizopita, hivyo nililazimika kupanda daladala au taxi kama nikiwa na dharura. Niliondoka pale ofisini nikimuacha akiongea na katibu wangu muhtasi na kuondoka zangu. Nilikodi taxi na wakati niko njiani nikakumbuka kuhusu ile simu, lakini niliisahau ofisini, kwa hiyo sikupitia kariakoo tena. Nilikwenda moja kwa moja hadi kwa rafiki yangu anayeishi maeneo ya Kijitonyama na kupoteza muda huko hadi usiku ndio nikarudi nyumbani.

Siku iliyofuata dereva alinifuata na kunipeleka ofisini, nilipofika nilimpa ile simu na kumtuma akanitafutie chaja ya ile simu. Baadae alirudi akiwa na chaja ya simu ile na kunikabidhi. Niliichaji na ilipojaa niliiwasha ziliingia ujumbe kadhaa kutoka kwa watu waliokuwa wakimtafuta mwenye simu ile, nilipozisoma niligundua mwenye simu ile alikuwa anaitwa Yasinaty, nilikata shauri nimpigie mmoja wa watu waliokuwa wametuma ujumbe ambaye alionekana kuwa ni mama yake. Nilipompigia simu na kuuliza kama anamjua mwenye simu kwanza alitaka kujua mimi ni nani na kwa nini simu ya mwanaye ninayo mimi. Nilimsimulia kila kitu na nilimuomba ampe mwanae namba yangu ya simu na kumuomba amwambie awasiliane na mimi ili nimpe simu yake. Yule mama alifurahi sana na kunishukuru sana, kumbe ile simu Yasinaty alitumiwa na kaka yake aishie Ughaibuni.

Mchana nilipigiwa simu na Yasinaty na tuliongea mengi na alionekana ni binti mchangamfu kweli, alinimbia kuwa anafanya kazi kwenye Hoteli moja ya kitalii maarufu iliyoko katikati ya jiji, nilimuahidi kumpitia kazini kwake jioni nikitoka ofisini.
Nilimpitia jioni na kama alivyonielekeza kuwa yuko reception nilimkuta pale akimalizia kazi na aliniomba nimsubiri kweye kijimgahawa kilichopo pale ndani, kwa kuwa mimi sio mnywaji wa pombe niliagiza juisi ili kumsubiri. Baadae alinipitia pale nilipokaa na kunimbia kuwa anatoka hivyo tukutane nje kwani anakwenda kubadili sare za kazini. Alitoka na kunikuta nje nikimsubiri, alipanda kwenye gari na nilimuomba dereva wangu atupeleke Hoteli nyingine ya kitalii maarufu pale hapa jijini ili tupate kahawa na Yasinaty. Tulifika pale tuliagiza vinywaji. Nilitumia wasaa ule kumtazama vizuri Yasinaty, alikuwa ni binti mrembo sana, na mchangamfu hasa, naamini alistahili kufanya kazi reception.

Nilimkabidhi simu yake na yakafuata maongezi mengine ya kujuana na simulizi za hapa na pale. Huo ndio ukawa mwanzo wa kujuana na Yasinaty, ambaye baadae alikuja kuwa mke wangu mpenzi.

Laiti kama ningekufahamu kabla Yasinaty………………….

Habari hii nimetumiwa na msomaji wa blog hii ya MAISHA ambaye anasheherekea ndoa yake kutimiza miaka mitano leo. Na nimeona si vibaya kama nikiweka hapa.

Monday, September 6, 2010

‘Housigeli’ anataka kuniharibia ndoa

Mama mkwe
habari yako. Nategemea mzima wa afya na hutasita kunisaidia kunipa ushauri unaonifaa. Mimi ni mwanamke mwenye watoto wawili. Tangu nimeolewa miaka sita iliyopita, nimekuwa na msichana wangu wa kazi mmoja ambaye nimempenda sana hasa kwa kuwalea vizuri watoto wangu na kuwa mwepesi wa kazi. Kutokana na kuishi vizuri na ‘housigeli’ huyu, amekuwa kama mtoto wa nyumbani na hata ndugu zangu na wa mume wangu wanampenda sana na wamemzoea kupita kiasi.
Tatizo hili la kuwazoea ndugu wa mume wangu sasa naona linataka kuharibu ndoa yangu kwani huyu msichana ameanza tabia mbaya na amemweleza mkwe wangu kuwa mimi situlii nyumbani na sina muda wa kumshughulikia mume wangu kwani kazi zote anafanya yeye, mimi kazi yangu kusafiri na kushinda kazini. Huyu mama mkwe wangu kusikia hayo, amekuja juu na sasa anamshinikiza mume wangu aniache eti nashindwa kuhudumia nyumba na badala yake amuoe ‘housigeli’. Mume wangu ameshtuka na amenieleza kila kitu hali iliyonikasirisha sana.
Sasa naomba ushauri wako kwani mama mkwe bado yupo kwangu, je, nifanyeje kabla hajaondoka kurudi kwake? Mama Kelvin Tabata, Dar es Salaam. Mama Kelvin pole sana kwani inaonekana huyo mama mkwe wako hajaelimika vya kutosha. Uzuri wa mwanamke haupimwi kwa kazi za nyumbani pekee, bali kuna mambo mengi na mkwe wako anapaswa kutambua kuwa wewe unafanya kazi hivyo huwezi kukaa nyumbani muda wote na ndiyo sababu ukatafuta msaidizi.
Lakini pia ni vyema ukiwa nyumbani ufanye kazi zilizopo ikiwamo kumpikia mumeo na kumhudumia ipasavyo. Usiwe na hasira za haraka kwa msichana wako wa kazi kwani inawezekana aliulizwa kimtego naye akajibu vizuri tu lakini mkweo akawasilisha kwa mumeo vibaya. Nadhani mumeo pia anapaswa amweleze mama yake kwa upole kuwa wewe unafanya kazi na huwezi kufanya kazi zote za nyumbani. Pia amweleze kuwa huyo msichana wa kazi kamwe hawezi kuwa mke wa mtoto wake.
Naamini mtoto wake akimwelimisha na akawa na msimamo, mama mkwe wako ataelewa au hata kama hataelewa, atashindwa kuendelea kusisitiza anachotaka. Ni vyema pia ukakaa na mshichana wako na kumhoji ilikuwaje hata wakazungumza hayo na mkweo na ukiona kama alichokonolewa basi mtahadharishe akae mbali na mama mkwe na asiwe mwepesi kueleza mambo ya ndani ya nyumba kwa mkweo.
Hata hivyo fanya uchunguzi wako kwa siri na ukiona msichana wako anapalilia ili aolewe yeye, basi ni vyema ukatafuta msichana mwingine wa kazi na huyo kumwondoa ili asije kuharibu ndoa yako. Haina haja kugombana na mtu yoyote kwani naamini huyo mkweo ataondoka na nyinyi mtaendelea na maisha yenu. Pia jifunze kuvumilia kwani wakwe wengine uelewa wao ni mdogo.

Habari hii nimeipata jamii forum na nimeona si vibaya kama nikiweka hapa Maisha na Mafanikio.