Showing posts with label hadithi. Show all posts
Showing posts with label hadithi. Show all posts

Thursday, March 14, 2013

TUSISAHAU HADITHI ZETU TULIZOSIMULIWA PIA TULIZOSOMA:- LEO...MWANAMKE MWIZI!!!

Palikuwa na kijana moja aliyekuwa analala kwenye bwaru, hakuwa na mke. Siku moja aliondoka kwenda kutafuta mwanamke. Alifika katika mji wa watu, na katika mji ule palikuwepo wasichana watatu. Msichana moja mchawi, msichana mwingine mwongo na msichana mwingine mwizi. Basi, yule kijana akafikiri afadhali aoea nayeiba. Aliogopa mwanamke mchawi ataenda kumwua. Kadhalika, alifikiri Moyoni mwake: Kama nikioa mwanamke mwongo kutakuwa na mashauri kila siku. Akasema , afadhali nioe ayeiba nitaweza kumlimia.

Kweli akaoa mwanamke anayeiba, akaja naye nyumbani kwake. Akakaa naye. Siku moja mwanamume yule akachinja mbuzi, akakatakata maini na utumbo akampa mkewe apike. Basi, mwanamke yule akachukua ulezi akaanza kusaga kwenye jiwe. Mwanamume akaondoka akaenda kuoga maji mtoni. Mwanamke yule akaacha kusaga, akaingia nyumbani mwake pale alipokuwa amepika kitoweo, akachukua mwiko akaipua finyango moja akatoka nacho akazunguka nyuma ya nyumba akaanza kula. Mume wake alipotoka mtoni, baada ya kuona mke wake hayupo, naye akachukua finyango moja akazunguka upande wa pili akaanza kula. Mke wake alipomwona akasema :- Wa kukasirika hayupo , sote tunaiba.
MUWE NA  SIKU NJEMA SANA WOTE MTAKAOPITA HAPA. HADITHI NYINGINE ITAKUJA WIKI IJAYO PANAPO MAJALIWA....

Wednesday, January 30, 2013

LEO TUANGALIA HADITHI: MWENDO WA KINYONGA!!!

Hapo mwanzo, yasemekana kuwa Kinyonga alikuwa na mwendo wa haraka na hata kukimbia kwa kasi kama wanyama wengine. Hakuwa na mwendo wa kusuasua kama tumwonavyo siku hizi. Je, ni kitu gani kilichomfanya Kinyonga awe hivi alivyo?
Siku moja, lilipogwa la mgambo la kuwataka wanyama wote wakusanyike pamoja ili kuwe na mashindano ya kukimbia, wapate kujua ni mnyama gani hodari wa kuchanganya miguu kushinda wengine. Taratibu zilifanyika ili kuweka mambo yote sawa. Siku ya siku ilipowadia, mashindano ya kukimbia yakaanza: Msimamizi wa mashindano alianza kuhesabu: Moja, mbili, tatu! Loo, vumbi likaanza kutimka kutokana na kishindo cha mbio za wanyama wale. Kwa vile mbio zilikuwa za kasi sana, baadhi ya wanyama walioweka vitu mfukono mwao, vikaanza kudondoka, kimoja baada ya kingine. Kinyonga kutokana na ukali wa macho yake, akaviona vitu hivyo. Kadiri mbio zilivyozidi kupamba moto, na ndivyo vitu viliendelea kudondoka. Hatimaye, Kinyonga akashindwa kujizuia. Vitu vile vilimtinga sana. Akabadili uelekeo. Akawapisha wanyama wengine na kujifanya kama vile anakwenda kujisaidia. Kumbe, anarudi nyumba na kuanza kuokota vitu vilivyodondoshwa na wanyama wenzake. Kwa kuwa vitu vile vilikuwa vingi na vilidondoka ovyo ovyo bila mapangilio wowote, Kinyonga alianza kwenda polepole, kwa maringo na makini, ili aweze kuokota vizuri vitu vyote kisiachwe hata kitu kimoja. Alifanya hivyo sio kwa ajili ya kuwarejeshea wale waliopoteza, la hasha, bali kuweka kibindoni, ili vimfae mwenyewe maishani.
"Tamaa mbele, mauti nyuma." Sasa basi, kutokana na tamaa hiyo, alikiona cha mtema kuni. Jamaa tangu siku ile, hadi leo hii, hakuweza tena kutembea haraka wala kukimbia. Akawa "amejitaiti" mwenyewe. Halafu, akawa anabadilika badilika rangi kufuatana na mazingira ya sehemu anayokuwepo ili asije akaonwa na wenye mali zao. Vile vile, anazungusha zungusha macho huku na huko kana alivyofanya siku ili "alipookota" vitu vilinyodondoshwa na wanyama wenzake.
Na Kat.V.A. Ndunguru kutoka gazeti la Mlezi.
Je hadithi hii wewe msomaji inakufundisha nini?

Monday, August 27, 2012

BARANI AFRIKA:- UTAMADUNI WA KUSIMULIA HADITHI BADO NI MUHIMU!!!

Hadithi kama tujuavyo ni njia ya maridhiano isiyo na gharama na ya kudumisha utamaduni.

Wengi wetu tunakumbuka nyakati ambazo wazazi au mababu na mabibi zetu walipokuwa wakitusimulia hadithi za kufurahisha zilizotokea zamani. Nilipoiona picha hii nimekumbumbuka sana zamani nilipokuwa mdogo wakati wa jioni wote mnakusanyika na kusikiliza hadithi na hapo hapo mnamenya karanga au kupukuchua mahindi na hapohapo mnaota moto.....

Monday, July 23, 2012

Tuendelee na ile yetu …….HADITHI HADITHI…..HAPA NI HADITHI YA MVUVI NA SAMAKI WA DHAHABU!!!



Ilipoishia ”Usiwe na hofu, baba kizee enenda kwa amani sasa.” Baba Kizee alirejea kwa mkewe mzuri. Lo! Akaona nini? Jumba zuri na barazani mkewe amesimama , amevaa vazi la maridadi la nyoya jema. Na kichwani kavaa kilemba kilichotariziwa vilivyo na vito vyema vikimning´nia shingoni. Na pete za dhahabu zilipamba vidole vyake na viatu vyororo vyekundu vikimkubali miguuni….NA SASA INAENDELEA…………
Na mbele yake watumishi wakimhangaikia, huku akiwavuta nywele zao na kuwacharaza bakora. Baba kizee akamsaili mkewe mzuri “Je, waonaje sasa mke wangu sasa roho imeridhia kibibi? Mkewe akamjibu kwa jeuri , na kumpeleka mazizini kufanya kazi za suluba huko.
Wiki moja ilipita iklifuatwa na nyingine. Na mkewe mzuri akiwa haridhiki kupita siku zote. Akamwamuru baba kizee aende tena baharini. “Enenda tena baharini ukamkabili samaki mkuu mwambie sitaki kuwa mwanamke wa basaba bora bali malkia mwenye enzi!”
Baba kizee akaona vi mno akadahili kwa nguvu. ”Nini tena, ew mwanamke! La hasha umechanganyikiwa! Kumbuka ya kuwa wanena na kutenda. Kama mke wa mvuvi utaifanya milki nzima ilemewe na kicheko!”
Mke wa mvuvi akazidi kisirani akamvuta masikio mumewe na kusema ”unathubutuje kubishana . Ewe kisonoko na mimi mwanamke wa nasaba  bora? Elekea hivi sasa baharini nakuamuru! Kama hutaki, nitakuburura hadi huko!” Baba kizee alijizoazoa na kwenda tena baharini. Bahari ile ya maji ya mbingu ikawa nyeusi tii, tena inatisha.
Akapaza sauti yake, akaita na samaki wa dhahabu akaja akiogolea. ”Ni nini tena kinachokukera. Ewe baba kizee, hebu niambie!” Kwa mwinamo wa hadhi baba kizee alijibu sawia ”ujaliwe neema Ewe Bwana wa Samaki! Mke wangu mzuri amecharuka tena safari hii ajipa wazo hatakuwa tena mwana wa nasaba bora. Yu ataka kuwa Malkia mwenye enzi.” Naye samaki wa dhahabu akajibu ”Usijali, ewe baba kizee rejea nyumbani kwa amani nawe utamkuta mkeo mzuri yu malkia!”
Baba kizee alirejea kwa mkewe mzuri na nini alikiona? Jumba lla kifalme, likimilikiwa na mwanamke wa hila akiwa ametamakani mezani. Wakuu na mabwana wakimngojelea, wakimnywesha mvinyo kwenye chombo cha dhahabu huku akividonadona vipande vinono vya nyama. Huku walinzi wenye macho makali wakimlinda pande zote wakiwa wamejihami kwa vishoka mikononi. Baba kizee akatupa jicho huku na huko. Jicho likamfeli, akagwaya! Alijiinamia hadhi ardhini mbele yake na kuweza kutoa maneno haya ”Heshima kwako na kicho Ewe malkia habe niambie sasa ikiwa moyo wako umeridhika?” Mkewe hakumthamini hata kwa mtupo wa jicho bali aliamuru watu wake kumuondolea mbali. Ndipo waungwana na wa nasaba bora wakamwelemea mbiombio wakamkwida shingoni. Na kumbeba hangahanga na mabawabu wa mlangoni wakamsindikiza nje kwa vishoka vyao.
Na halaiki yote kwa jumla yao wakajisheheni kwa kicheko. ”Hiyo ndiyo tosha yako ewe kizee mtovu wa busara! Na hilo liwe funzo lako kujijua wewe u nani siku za hapo baadaye! Na hivyo wiki ikayoyoma na nyingine ikafuata. Mama kizee akazidi utakavu, akatuma wajumbe wake kumkamata baba kizee. Walimpata, wakamleta mbele ya Malkia. Naye mke mzuri akanena kwa mumewe ”Enenda tena ukasujudu kwa samaki mkuu. Sitaki tena kuwa Malkia mwenye enzi, bali nataka kutamalaki maziwa yote na bahari na katika vina vya bahari. Nitaweka ngome yangu na huyo samaki wa dhabu atanitumikia mimi. Huku nikimtuma kotekote!” Baba kizee hakuthubutu kupinga kauli ya mkewe hivyo akaenda tena baharini na tazama! Tufani kuu ilitokea mawimbi makuu yaliinuka kumlaki, tetemeko tupu, muondoko wa ghasia, muungurumo mkuu hata hivyo baba alipaza sauti na kuita. Na samaki wa dhahabu akaja akiogelea ”kulikonit ena baba kizee njoo unieleze!” Kwa mwinamo wa hadhi baba kizee akajibu sawia ”Na ujaliwe neema Ewe Mkuu wa Samaki! Nimfanyeje huyu mwanamke? Huyu ajuza mjinga, hataki tena kuwa Malkia pia anataka kutawala maziwa na bahari. Anataka kuweka ngome zake katika vilindi vya bahari, na kukufanya wewe mwenyewe umtumikie. Na kukutuma wewe huk ona huko.” Samaki wa dhahabu alitulia tuli pasi na jibu na badala yake alipiga mkia wake majini akajerea kwenye maji makuu. Baba kizee alisimama ukingoni, akisubiri . Alisubiri kwa muda mrefu, lakini halikuja jibu. Hatimaye akarejea kwa mkewe mzuri, na tazama! Akamkuta amekaa mekoni kwenye kibanda kikongwe cha udongo na miti na mble yake kukiwa na kibeseni kilichoraruka hadi katikati. HADITHI IMEKWISHA..
Je Hadithi hii inatufunza nini? 

Thursday, March 29, 2012

POROJO YA LEO !!!

Bwana mmoja karudi nyumbani toka kazini amechoka ile mbaya, akaingia ndani na kujitupa kochini ili aangalie TV. Akamwambia mkewe:-
- Niletee bia, karibu inaanza .
-Mkewe akapumua na akampa bia.
- Baada ya dakika kumi na tano akasema :-
-Nipe bia nyingie maana karibu inaanza.
Mke wake akamwangalia kwa kuchoka choka lakini akampa bia nyingine:
Alipokuwa amemaliza ile bia baada ya dakika kadha akasema:-
- Nipe bia nyingie, kwani itaanza dakika yoyote ile.
-Mkewe akachukia na kumpigia kelele, akasema.
- Yaani huna kazi nyingine ya kufanya jioni hii, zaidi ya kukaa na kuangalia TV na kunywa bia?
Wewe huna lolote isipokuwa ni mvivu, mwanaharamu mkubwa.......
Yule bwana akapumua na kusema:-
-Sasa imeanza.......
Je wewe pia unajiuliza kama mimi ni nini kilichoanza?

Monday, October 3, 2011

TUIANZE JUMATATU HII YA KWANZA YA MWEZI NA HADITHI:- JINSI SUNGURA ALIVYOPATA MAJI


Hapa zamani za kale, kulikuwa na shida Kubwa sana ya maji katika nchi zote. Kwa bahati, likabakia ziwa moja tu. Wanyama wengi wa kila aina walipata maji yao kwenye ziwa hilo. Wanyama wakubwa kama vile Tembo, Simba na Chui; waliwanyanyasa sana wanyama wadogo waliofika kunywa maji kwenye ziwa hilo. Wakawa Hawana raha. Walipata maji kwa shida sana baada ya manyanyaso makali.

Sungura alipoona hivyo, alianza kukuna kichwa akifikiri jinsi ya kuepukana na adha hiyo. Akapata njia. Alitengeneza ngoma na kucheza kwa siri nyumbani kwake. Wanyama wengine waliposikia sauti ya ngoma ile ilivyosikika vizuri, wakavutika nayo. Wa kwanza kuvutika, walikuwa wanyama wakubwa. Wakamwendea Sungura ili wapate kuiona ile ngoma inayotoa sauti nzuri. Sungura akawaambia: “Mimi napiga ngoma hiyo na kucheza pake yangu kwa siri. Ninyi mkitaka kuiona, naomba mje moja moja, nami nitawaonyesha.” Hiyo ilikuwa mbinu yake tu kutaka kujua nani atakuwa wa kwanza na wa mwisho kuja kwake ili apate kuwatenda vibaya.


Tembo alikuwa wa kwanza kwenda kwa Sungura. Akamwambia: “Ingia nyumbani mwangu”. Tambo bila kukawia akaingia ndani. Loo, maskini Tembo! Sungura akafunga mango kwa Nguvu, mara akachoma nyumba yote. Tembo akafa.

Akaja Chui, bila kufahamu kilichotekea kwa Tembo. Yeye akapelekwa kwenye mlima wa mawe wenye mtelemko mkali. Sungura akamwambia: “Hapa wanapatikana wanyama wengi sana. Unisaidie kuwinda ili upate kula karamu kabla ya kucheza ngoma. Wanyama wanapatikana kwa urahisi sana ukifuata taratibu nitakayokuelekeza. Nayo ni hii: Ufumbe macho mpaka mnyama anapoanza kukupita. Kisha, ufumbue macho na umfuate kwa nyuma. Ndipo utakapofaulu kumkamata”.

Chui akakubali. Sungura akapanda mlimani kuporomosha jiwe kubwa. Likaja moja kwa moja kutoka juu na kumponda Chui aliyefumba macho kungoja mnyama. Sungura akamchukua Chui na kumchuna ngozi. Zamu ya Simba ilifika, akamwmbia: “Ngoma hii kila atazamaye, lazima achunwe ngozi kama walivyofanya wenzako. Tazama, ngozi hii ni ya nani? Si ya Chui?” Simba akakubali. Akachunwa kwa tamaa ya kutazama ngoma, akafa. Sungura Akava ngozi hizo kwa zamu ili kwenda ziwani kuwatishia wanyama wadogo. Sungura akatawala maji yale, wakati Wote wa shida, kutokana na werevu wake.

Fundisho
Hadithi hii inawahusu wanyama. Kadiri ya maelezo, unaweza kufikiri kuwa wanyama waliouawa hawakuwa na akili. Hiyo ni hadithi. Na kila hadithi inalo jambo la kujifunza. Kwa mfano:-

Sentensi ya mwisho ya hadithi: “Sungura akatawala maji yale, wakati wote wa shida, kutokana na warevu wake. Werevu wa sungura ulikuwa kuwahujumu wenzake. Hujuma sio kitu kizuri maishani. Ni dhambi. Sisi tusiwe werevu wa kuwahujumu na kuwaonea wenzetu. Mamoja wakiwa wakubwa au wadogo.Katika jambo hilo, Yesu anasema: “Kila kitu mlichomte-ndea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi” (Mt.26:40)
Werevu wetu uwe katika kuwapenda wenzetu na kuwatendea mema.

Hadithi hii imeandikwa na Kat.V:A Ndunguru . Mimi katika pitapita zangu nilikuwa hapa Peramiho basi nikawa nimenunua mkate na nikafungiwa gazeti na baada ya mkate kwisha nikawa naangalia gazeti au kipande cha gazeti na kukutana na hadithi hii nikawasoma wanangu na nimeona niiweka hapa Nayni msome na mcheke kama sisi. Na gazeti lenyewe linaitwa MLEZI.

Halafu hadihi hii imenikumbusha nilipokuwa darasa la kwanza na pili tulikuwa tukiimba sana nyimbo na moja ya nyimbo ni kama hii. Sungura Sungura mjanja wee X2 Ingawa mdogo hushinda wakubwa X2 Akili akili zatoka wapiX2 Ingawa mdogo hushinda wakubwa……

Tuesday, September 13, 2011

KISA CHA KOMBA NA AKINA KOMBA!!!!!

DADA YASINTA!
LEO NI KUPE KILE KISA CHA RAFIKI YANGU AITWAE FULKO KOMBA NA WATANI WAKE AKINA NJAIDI NA MASASI HAWA KAMA MAJINA YAO WOTE NI WATOKA KUSINI MWA TANZANIA MASASI NA RUVUMA HAWA NI WATANI WA JADI HALISI,.BASI SIKU MOJA HUKO ZAMCARGO KURASINI SASA MJI HUU UMEVUNJWA NA KUPISHA MRADI WA UPANUZI WA BANDARI. ILIKUWA SIKUKUU YA KRISMASI, KWA KAWAIDA HAWA AKINA KOMBA WALIKUWA NA KIKUNDI CHAO CHA NGOMA YA HUKO NYUMBANI SONGEA. HAWA WANATOKA PALE NJIA PANDA YA SONGEA NA PERAMIO KAMA UNAKWENDA CHIPOLE. JINA LIMENITOKA KIDOGO NIKIKUMBUKA NITAKUTAJIA .,BASI KILA MWISHO WA MWAKA AU KRISMASI HUWA WANAPIGA NGOMA ZAO NA WANAKESHA .BASI ...BWANA ..MWAKA HUO MKESHA ULIKUWA NA MVUA NYINGI KIASI KUWA MPAKA SAA TISA USIKU
WATU WALIKUWA WAMELALA, ILA KWA HAWA JAMAA WA MASASI KULIKUWA NA KIGROSARI NA KULE KURASINI KULIKUWA NA SIFA YA KUUZA MAFUTA YA MAGENDO YAANI PETROLI AU HATA MAFUTA YOYOTE HATA YA KULA ILIKUWA NI DILI. VIJANA WA KILEO NDIYI LUGHA YAO, BASI HAPO KWA MASASI WALIKUWA WALEVI WOTE NDIYO KISEBULE CHAO HATA USIKU WE GONGA TU NATAKA BIA UNAFUNGULIWA.
NA UNAPEWA UNACHOTAKA KWANI SIKU DILI IKIKUBALI BASI HAPATOSHI. KWAHIYO SIKU HIYO WATU WALIKUNYWA MPAKA MANANE. NA UJUWAVYO MLEVI ANAPOKUWA AMEPATA MARA ATOKE KWENDA HUKO MARA KULE BASI NJAIDI ALIKWENDA KUFUATA SIGARA PALE ZILIISHA , ALIPOTOKA MBELE KIDOGO ALIKUTA MNAZI, NA KUKUTA KINYAMA KOMBA ,, KINAPUMUA KWA MBALI ... KIMELALA ..BASI ALIRUDI NDANI NA KUWAAMBIA KUWA JAMANIEEE KOMBA KALALA PALE ,KOMBAAA,,,, NDIYO KOMBAA ANAUMWA AU ,,,JAMAA AKAJIBU SIJUWIII...TWENDE .. WAKAENDA KUMWONA WAKAKUTA KALE KANYAMA ..BASI MMOJA WAPO AKAWAAMBIA WALE WENZAKE KWAVILE HUYO KOMBA NA NDUGU ZAKE WAPO KARIBU BASI TWENDE ZETU TUKAWAAMSHE WAMPATIE MSAADA ,AU SIYO JAMANI.EEE WAKA JIBU ,,SAWAAA BASI WOTE WALE VIJANA WA MASASI WAYAO WAKAENDA KWA WANGONI ,,,NGOO NGOOO HODI ...MLANGO,,, NANI WEE ... AKASEMA ALOO KOMBA, FUNGU ...NDUGU YENU KOMBA KALALA PALE HAJIWEZI ,,,AKAULIZA KOMBAAA... NDIYO
YUPO WAPI ,,,PALE KWENYE MNAZI ,,,,,YEYE BILA KUHOJI ZAIDI AKAENDA KUMWAMSHA FULKO, NA NDUGU YAKE BOSCO WAO NAE AKAMFUATA THEO ILA KWAKUWA ENEO LILE WALIKUWA FAMILIA ILE WANAKAA PAMOJA WAKASEMA BASI TUKAMWAMSHE MUJESHI ,,KAKA YAO ,HUYU ALIKUWA MWANAJESHI ,BASI WOTE TIMU MZIMA WALIONGOZANA NA WALE VIJANA MPAKA PALE ALIPOLALA KOMBA ,..YUPO WAPI???? ...SWALI .. HUYU HAPA,,,, WAKAONYESHWA KOMBA MNYAMA, NDIYO HUYU?? ..NDIYO ,,,,,,HUYU NDIYO ,,,,,,,,,,,,
KWANI HUYU ANAITWA NANI??? WOTE WAKAJIBU KOMBA .........BASI NDIYO HUYO NDUGU YENU ,,,,,,,,,,WALE WAYAO WAKAONDOKA NA KUIACHA TIMU MZIMA YA WANGONI NA MAJINA YAO YA WANYAMA NA NDUGU YAO KOMBA MLEVI WA TEMBO,...... KUMBE KOMBA ANAKAWAIDA YA KUPANDA JUU YA MMNAZI NA KULINYWA TEMBO LA MNAZI HIVYO NAE SIKU ILE ALIBAHATIKA KUPATA POMBE YA MNAZI AKASHEREHEKEA VIZURI SIKUKUU YA MWAKA MPYA NA KUWAFANYA NDUGU ZAKE AKINA KOMBA WAACHE VITANDA VYAO NA KWENDA KUMWANGALIA NA KWAMAWAZO YA WANGONI KWANI WALIPOSIKIA KOMBA KALA WALIJUA KUWA NDUGU YAO KOMBA
AMEPIGWA BILA KUCHUNGUZA NI KOMBA GANI ??? HUYO ,
HIVYO NDICHO KISA CHA KOMBA NA AKINA KOMBA
NA IPO SIKU ITATOKEA KISA KAMA HICHO CHA NYANI NA AKINA NGONYANI................KWANI HAKUNA MAJINA YOTE YALIISHA ,,,,,,,,,,,, KOMBA, NYOKA , NDANDALA, MAPUNDA.,,,N.K POLENI WATANI ZANGU WA PALE LIPOKELA KITAI , NTYAN"GIMBOLE, LIPUMBA MATILI, HALALI PALE KIGONSERA , NGOMBO AU MBAMBABAY POLE KILOSA AKINA NCHIMBI ,MBUNDA KULE UMATENGONI
ASANTE MIMI MYAO SIYO MUYAO MAANA KWETU PALE NI MUHOGO UNAITWA MAYAO YAKIWA MENGI
HUU NI UTANI WA MAKABILA MAJINA NILIYO TUMIA NI YA KWELI YAWATANI ZANGU ILA HAIKUWA HIVYO NA WALE WA MASASI NI BINAMU ZANGU KWELI WANAITWA MAJINA HAYO.

-------------------------------------------------------------------------------------------------

KISA HIKI NIMETUMIWA NA MSOMAJI WA MAISHA NA MAFANIKIO KWA JINA LA ISSACK CHE JIAH KWA VILE ALIONA JINA LANGU NI NGONYANI AKAPENDA "KUNITANIA" NAMI HUWA SIPENDI KUFAIDI MAMBO KAMA HAYA PEKE YANGU NIKAONA NIWEKE HAPA ILI NANYI WENZANGU MFAIDI.

Wednesday, March 9, 2011

HII NI KAZI YA NANI??

Naona ni siku nyingi hatujasimuliana hadithi na leo nimeona ni wakati mzuri niwasimulia kahadithi haka:-Hadithi, hadithi….


Mmhh! ngoja kwanza nikune kichwa!!


Hii ni hadithi kuhusu watu wanne waitwao Kila mtu, Mtu, Mtu na Hakuna mtu. Kulikuwa na kazi muhimu kufanywa na kila mtu alikuwa na uhakika kila mtu angeweza kufanya kazi hiyo. Kila mtu angefanya kazi hiyo, lakini Hakuna mtu alifanya hivyo. Mtu alipata hasira kuhusu hili, kwasababu ilikuwa ni kazi ya kila mtu. Kila mtu aliwaza kuwa Kila mtu anaweza kufanya hivyo lakini Hakuna mtu aliyetambua kwamba kila mtu asingefanya hivyo. Na mwisho iliishia Kila mtu kumlaumu Mtu wakati Hakuna mtu aliyefanya chochote ambacho Kila mtu angeweza kufanya. ……mwisho wa hadithi!!!!

Thursday, February 18, 2010

HADITHI YA MWANA MPOTEVU

Hiii hadithi inanikumbusha mambo mengi sana sijui wenzangu mnasemaje?

Kulikuwa na baba mmoja aliyekuwa na watoto wawili wa kiume. Siku moja yule wa mwisho akamwambia baba yake : baba mimi sasa ni mkubwa naomba haki yangu nataka kuondoka kwenda mbali kutafuta maisha. Baba yake akampa pesa nyingi tu. Akaondoka akaenda zake na pesa zote.

Muda si mrefu akapata marafiki wengi tu. akawa anakula na kunywa nao pamoja na yeye ndiye aliyekuwa analipa kila kitu.

Lakini muda si mrefu pesa zote zikamwishia. Akawa hana kitu cha kula. Marafiki zake wote hawakumpa wala kumsaidia chochote isipokuwa walimtupa barabarani.

Siku moja akaondoka akaenda kwa mkulima mmoja na kusema ya kwamba anaomba chakula, aina yoyote ile, na halafu atafanya kazi kwake. Mkulima akamhurumia akampa chakula na akamwambia kazi yake ni kuchunga nguruwe wake.

Hata hiyo kijana bado alikuwa ana njaa. Akaanza kuwaza: kwa nini napata taabu hapa wakati baba yangu ana chakula kingi tu. Narudi nyumbani kwa baba tena. Nataka kufanya kazi kwa baba kuliko hapa.

Mara akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Na kusema baba, naomba radhi nimekosa. Ilibidi nisirudi na wala usinipokee tena hapa nyumbani kwako. Lakini baba kwa uchungu wa furaha akamkumbatia na kumpokea. Kwa furaha kubwa baba akamfanyia kijana wake sherehe kubwa kwa kufurahia kwa sababu kijana wake alikuwa amerudi tena kwake.

Kaka mtu akawa anarudi toka kazini(shambani) akakutana na babake asemaye. Mdogo wako amerudi tena nyumbani njoo tumsherehekee. Alipotea sasa amerudi tena.

Swali: Je? Hadithihii wewe inakufundisha nini?
Na je? ungekuwa wewe ni yule kaka mkubwa ungefanyaje?

Hebu sikiliza hapa lugha ya mwenzetu wasukuma mimi nimeipenda kwani nimeelewa neno moja moja hata hivyo najivunia lugha zetu za asili zinasikika.


Au kama hujaelewa hapo basi sikiliza hapa lugha yetu ya kiswahili

Tuesday, February 9, 2010

Kibanga Ampiga Mkoloni



Nasoma kitabu cha Tujifunze Lugha Yetu
Wapendwa

Jana niliposti hapa kijiweni http://ruhuwiko.blogspot.com/2010/02/kibanga-ampiga-mkoloni.html juu ya kisanga cha Kibanga kumbonda mkoloni. Awali nilitaka tu kuwakumbusha wanakijiwe juu ya stori hii lakini cha kushangaza Mt. Simon http://simon-kitururu.blogspot.com/na Chacha Ng’wanambiti! wamekuja na hoja nyingine ambazo haziwezi kupita bila kujadiliwa.

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...
kwa kung'ang'ania bakora mkoloni ana nguvu na jeuri!Je si kuna wakati tunag'ang'ania mambo hata yasofaa huku tukijiona tuna maguvu na jeuri ya kufanya tutakavo hata kama tunaumiza wengine? :-(
February 9, 2010 12:04 AM

SIMON KITURURU said...
Nimeipenda sana staili ya ngwala a.k.a kubwengana ya Mheshimiwa mpole Kibanga.Lakini bado :``Siku hizi kijiji cha Kwachaga kina maendele mazuri ya kilimo na mifugo. Maendeleo yote yamepatikana kwa sababu ya uongozi bora wa Serikali ya wananchi.´´- inanitamanisha nitamani kwenda huko KWACHANGA kwa kuwa BADO najiuliza zaidi kuwa;- hivi huko KWACHANGA ni Tanzania? Kwa maana nahisi viongozi wao wangeifaa kweli SERIKALI ya Tanzania baada ya Watanzania kumuondoa TANZANIA Mkoloni.:-(Ngojea niwashangilie washindi,Kibanga OYEEE! Ukoloni mamboleo OYEE!Nawaza tu!:-(
February 9, 2010 12:55 AM

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...
na kwa mtindo wa ushangiliaji wa mt. simon akiwa na glass ya komoni a.k.a ze bia mkoni, nina wasiwasi kama viongozi wetu watazinduka na kuuona ukweli wa kuwa twaweza kujiletea maendeleo wenyewe bila wakoloni:-(katika dunia ya sasa Kibanga angeweza kuonekana kichaa! je unadhani twahitaji vichaa wengi wa kuwazindua viongozi wetu kama alivozinduliwa waziri mkuu wa Italia?Samahani jamani, labda naanza kurukwa na akili :-( Lakini kama ndivo msinambie miye ndo niende kuwazindua hao walolala :-(
February 9, 2010 6:52 AM

SIMON KITURURU said...
@Kadinali Chacha Ng'wanambiti: Unauhakika Kibanga alivyompiga Mkoloni ni kweli Mkoloni aliondoka na Ukoloni wake?Si wajua kuwa jambo kubwa litofautishalo ukoloni na kwenda haja msalani a.k.a CHOONI ni kwamba UKOLONI hauhitaji Mkoloni awepo katika KOLONI kama Haja ihitajivyo ajisaidiaye chooni awe CHOONI?
February 9, 2010 10:49 AM

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...
@Mt. Simon: ni kweli kabisa mkoloni hakuondoka na ukoloni wake kwa kuwa kuna bado vijeba ambavyo ukiviangalia saaaaaana utastukia kuwa ni vikolini katika nguo za rangi ya kijani/njano :-(na kuhusu choo nadhani silazima mtu aende chooni kwani katika baadhi ya makabila kama la kwangu wawezakuta msitu wa jirani umesheheni uyoga kwa kuwa kuna mbolea-kinyesi cha mtu :-( na waweza ukakuta karibu na palipo na mzigo wa kinyesi aidha kuna kuna aidha jiwe ama nyasi badala ya ukoloni wa toilet paper :-(lakini, ni wangapi kati yetu tumefikiria kuhusu ujenzi wa choo au kujisitiri vichakani katika staili ya kumfukuza mkoloni mawazoni?Una hakika wewe si mkoloni ndani ya Utakatifu? :-(


Je WADAU, ni mafunzo gani tunayoweza kutohoa katika hadithi hii? Je ni kweli viongozi wa kijiji cha kibanga wanaweza kuwa suluhisho la ombwe la uongozi katika Tanzania yetu ya leo?

Saturday, September 12, 2009

HADITHI YA DOA JEUPE

Nadhani wengi tumewahi kuisikia hadithi hii kama hujawahi basi soma hapa na ufurahi au usikitike.

Hapo zamani, alikuwwepo mfalme ambaye hakupenda kabisa watoto wa kike. Akamwonya vikali mkewe kuwa akizaa mtoto wakike, atamuua.

Mke wake alijaribu kumsihi kuhusu swala hilo, kwa kumueleza kwamba watoto, wawe wa kike au wa kiume ni riziki ya Mungu. Vile vile mtoto wa kike, atamsaidia sana mama yake kwa mambo mengi, hasa shughulu za kika siku za nyumbani. Lakini, yote aliyozungumza mkewe, ilikuwa kama kuzungumza na kiziwi.

Wakati huo, mke wa mfalme, alikuwa na mimba, na siku zilikuwa zimewadia kuzaa. Mfalme, akasisitiza kuwa huyo mtoto ambaye yu njiani kuzaliwa ataishi iwapo atakuwa wa kiume. Mkewe akazaa mtoto, mtoto wa kike. Mfalme bila huruma akamuua yule mtoto.

Mkewe akabeba mimba tena, mara ya pili, vile vile akazaa mtoto wa kike. Mambo yakawa yale yale, mtoto akauliwa.

Mimba ya tatu, mfalme alikuwa safarini. Safari hiyo, ilichukua muda mrefu sana. Huku nyuma mkewe akajifungua mtoto wa kike tena. Kwa kuhofia mumewe kumuua yule mtoto, akaamua afanye kila aliwezalo yule mtoto aishi, kwa maana mumewe alikiwa hayupo. Alimchukua porini asijue la kufanya, akahangaika huku na huku. Hatimaye njiani, akajigonga na jiwe. Jiwe hilo halikuwa la kawaida, lakini yeye hakufahamu. Ghafla, baada ya kujikwatua kwnye ilele jiwe, mbele yake alisimama bibi kizee. Akamuuliza zote mkw wa mfalme kama ana matatizo. Bila kusita, yule mke wa mfalme akamueleza yote yaliyotokea kwa mimba zake za awali na akamueleza pia, alikusudia kumfanya nini huyu mtoto wa tatu aliyekuwa mikononi mwake. Isipokuwa hakufahamu afanye nini, na nani atamsaidia.

Baada ya yule bibi kizee kusikia hayo, akaamua kumsaidia mke wa mfalme, akamwambia:”Nitakusaidia, unaweza kuniachia mimi mtoto huyu. Nitamtunza, lakini ni lazima tupeane ahadi. Utakuwa unakuja kumuangalia wakati mume wako yupo safarini. Hata kama hatosafiri kwa muda mrefu, subiri mpaka asafiri, ni lazima uweke hiyo ahadi. Ikiwa mtoto wako ataugua, nitakuja kwenye ndoto zako. Kwa sababu ya doa jeupe kwenye goti lake, tutamwita Doa Jeupe.”

Wakakubaliana na kuwekeana ahadi. Mtoto akachukuliwa na bbi kizee, mke wa mfalme akaanza rahaa safari ya kurudi nyumbani. Njiani akawaza kwa furaha:- “Hatimaye, nimepata mtoto ambaye ataishi. Niliamini kuwa nitakufa bila ya furaha kama hiyo!”

Mfalme, baada ya siku kadhaa, alirejea toka safarini, kitu cha kwanza, akamwuuliza mkewe kuhusu hali yake. Mkewe akajibu: “Nilizaa mtoto ulipokuwa safarini, lakini aliktoka kabla ya wakati wake kwa hiyo hakuishi nikamzika.” Mfalme akampa pole mkewe kwa masikitiko ya kupoteza mtoto.

Wiki, miezi ikapita mkwewe akaomba sana mume wake asafiri tena, ili akamwone mtoto wake anaendelea vipi. Lakini mfalme, hakusafiri.

Siku moja, mfalme akachukua bundiuki yake akamuaga mkewa kwamba anakwenda mawindoni, siku nzima. Hata hivyo mkewe asingeweza kufanya lolote maana ulikuwa ni muda mfupi kwake. Mfalme akajitayarisha na kuondoka. Njianai kuelekea mawindoni, mfalme akakutana na Doa Jeupe. Kwa uzuri wake alivyoumbika, ingawa alikuwa bado msichana mdogo,mfalme akamfuata alipokuwa akielekea, mpaka kufika kwenye nyumba ya yule bibi kizee na akamwona Doa Jeupe anaingia ndani Akabisha hodi, hapo nyumbani kwa bibi kizee. Mfalme akamwuuliza bibi kizee:- “Huyu mtoto wa nani?” Akajibu: “ Huyu mtoto ni wangu wa kuzaa mwenyewe!” Mfalme akauliza tena: “Anaitwa nani?” “Doa Jeupe;” akajibu bibi kizee. Mfalme akajaribu sana kuzungumza na yule msichana, lakini Doa Jeupe akabaki akimwangalia bila kusema lolote! Mfalme mwishowe akasema : “nataka kumwoa huyu mtoto wako!” Bibi kizaa kwa heshima, akajibu: “ Unavyotaka mtukufu.”

Aliporejea nyumbani, akamweleza mkewe kwamba amekutana na msichana mzuri asiye mfano na angependelea kumwoa akifikia umri wa kuolewe.

Huku nyuma bibi kizee alipata ndoto usiku ule. Ndoto hiyo ilimuonyesha nyumba yake mwenyewe. Nje ya nyumba barazani, aliona alama za mihuu ambayo alifanana na ya mfalme. Kutokana na ndoto hiyo. Akafahamu kwamba mfalme atarudi tena kwa sababu ya Doa Jeupe.
Kwa hiyo akamwambia Doa Jeupe asubuhi yake: “Mwanangu, mimi nina safari ndogo nitakapokuwa sipo, na yule mfalme akija, usimruhusu ndani ya nyumba. Na ukikutana naye nje, usishawishike kumfuata!” Doa Jeupe, akaahidi atafanya alivyoelezwa. Asubuhi, bibi kizee akaondoka. Baadaye kidogo, mfalme akaja muangalia aliyetegemea kuwa mkewe wa maisha ya baadaye. Alibisha hodi, lakini hakuna aliyefungua. Ikabidi aondoke bila mafanikio yo yote. Hayo, yalitokea mara nyingi na ukafika wakati mfalme akakata tamaa kbisa. Hivyo akachukua uamuzi wa kutafuta msichana mwingine, awe mkewe wa pili. Haikuchukua muda akaoa mke wapili. Akamwelezea kuwa :- “Nimekuoa wewe , kwa sababu sikuweza kumpata Doa Jeupe!”

Mkewe mfalme wa pili, kazi yake ilikuwa mkata kuni. Katika mojawapo ya safari mwituni kufuata kuni, alikutana na msichana mzuri sana. Aliporudi nyumbani, akamweleza mume wake kwamba amemwona msichana aliyemzungumza. Mfalme kusikia hivyo, akapata ari na hamu kubwa ya kwenda kumtafuta tena Doa Jeupe. Kweli alipofika ile sehemu mkewe alipomuona, alikuta nyayo za miguu ya Doa Jeupe,zikielekea nyumbani kwa bibi kizee. Akaenda moja kwa moja mpaka mlangoni akabisha hodi. Hakuna aliyemfungulia. Kwa masikitiko, akarudi kwake. Akajaribu tene na tena, mambo hayakubadilika.

Bibi kizee akaanza kuingiwa na wasiwasi, kwa hivyo akamfuata mke wa kwanza wa mfalme. Akameleza nini mumewe anachotaka kufanya kuhusu Doa Jeupe. Mamaye Doa Jeupe, alishtuka sana aliposikia hayo: “Haiwezekani”! alisema. Wakaja na wazo zuri pamoja kwamba yeye bibi kizee na Doa Jeupe wahamie porini zaidi. Wakafanya hivyo siku hiyohiyo.

Mfalme akakata tamaa kabisa, hasa baada ya Doa Jeupe na bibi kizee kuhama walipokuwa wakiishi zamani. Kwa sababu hiyo, Doa Jeupe na bibi kizee waliishi kwa amani miaka mingi bila kubughudhiwa.

Doa Jeupe, akawa msichana mzuri wa ajabu. Siku moja , bibi kizee, ilibidi asafiri kwenda kuangalia ukoo wake. Hivyo akamuacha Doa Jeupe peke yake pale nyumbani. Nyumba yao mpya, ilikuwa karibu sana na mto. Ambapo ndipo walipokuwa wakioga, kufua na kuchota maji. Doa Jeupe, siku hiyo akaenda kuoga peke yake. Wakati huo huo mfalme alikuwa katika moja ya safari zake. Njiani ilimlazimu avuke mto huo huo ambao Doa Jeupe alikuwa akiutumia. Dakika chache baada ya Doa Jeupe kumaliza kuoga na kurudi nyumbani, mfalme naye, akafika sehemu ile ile. Wakati akisubiri mtumbwa wa kumvusha alikaa juu ya jiwe, miguuni kwake, aliona unywele umejisokota katika mguu mmoja wapo . Alishangaa sana maana hajawahi maishani mwake kuona unywele mzuri kama huo. Akaamuru waja wapo wafanyakazi wake wamtafute mwenye unywele huo.

Haikuwa kazi rahisi. Waliendelea kufanya hivyo kwa siku nyingi. Hatimaye wakampata msichana mwenye unywele ule, ambaye alikuwa ni Doa Jeupe! Alipokuwa akioga, unywele ulitoka. Wakamlete mbele ya mfalme. Afurahi kupita kiasi kumuona amekuwa msichana mzuri aliyeumbika vizuri ajabu. Hatimaye, mfalme akafikiri, kuwa amampata msichana ambaye atakuwa mke wa tatu. Hakuwa na hamu ya kuishi na wake zake wawili.

Bibi kizee kupata habari hizo, akafunga safari kurudi kuja kumtaharisha Doa Jeupe asimwoe yule mfalme ambaye ni babake! Akamweleza ukweli wa mkasa wote toka mwanzo mpaka mwisho. Akasisitiza kwa kumwambia; “Usisahau kuwa, mfalme anataka kukuoa kwa sababu wewe ni mwanamke.

Alipomaliza kusema hayo, bibi kizee akaondoka tena: Doa Jeupe alipata uchungu baada ya kuambiwa ukweli wa visa vya baba yake. Mfalme akarudi kumwomba Doa Jeupe amwoe. Doa Jeupe akamjibu: “Usisahau kuwa, mimi ni mwanamke, kama unavyofahamu wanawake hawana faida. Hufahamu kama wanawake ni hatari? Wanaweza kukuua?
Mfalme akahamaki: “Nani kakuambia upuuzi huo?”
Doa akamwambia: “Babu zangu ndio walioniambia, wewe uliyesafiri karibu ulimwengu wote, umeshawahi kuona mwanamke mzuri kama mimi? Nataka nikueleze kuwa, mimi nimetumwa hapa duniani kuangalia mazuri na mabaya niko tofauti na wanawake wengine!”

Mfalme hakuweza kuelewa lo lote. Akabaki akimuangalia tu. Doa Jeupe akaendelea: “Sikia! Mimi ni Doa Jeupe, yule ambaye miaka mingi iliyopita, ulimwona kama msichana mdogo. Ukasema akikua ungependelea kumwoa. Mimi ni binti wa mke wako wa kwanza. Wewe ambaye uliwaua dada zangu wawili wa kwanza na wa pili mara baada ya kuzaliwa, na kusema kuwa hawana faida kwako, unataka kunioa?

Lazima ufahamu kwamba mimi naishi dunuani leo, kwa sababu mama alinizaa ulipokuwa safarini, kuhofia kwamba na mimi yangenikuta yaliyowatokea dada zangu, akanificha kwa bibi kizee. Hivyo, siwezi kuoana na baba yangu!”

Mfalme akakataa kata kata, kuamini aliyokuwa akisikia akauliza ; “ Unaweza kunihakikishia vipi, kuwa wewe ndio yule msichana niliyemuona miaka mingi iliyopita?” Doa Jeupe alkamwambia : “Muulize mke wako wa kwanza ambaye ni mama yangu naye, atahakikisha!”
Mkewe mfalme akaitwa na akaeleza yote yaliyotokea wakati mumewe yuko safarini. Mfalme akamwuuliza; “Ni kweli kwamba ulizaa mtoto wa kike ukamficha nisimwone?” Mkewe akakubali. Mfalme akaendelea kusema: “Unaweza kunihakikishia kuwa msichana mzuri hivi, ni binti yako?” Mkewe akasema: “Nilimwita Doa Jeupe, sababu alizaliwa na kovu jeupe kwenye goti lake!”

Kila mmoja akawa akimwangalia Doa Jeupe ambaye alikuwa akionyesha lile doa kwenye goti lake! Huo, ulikuwa ushahidi wa kutosha! Mama na mtoto kwa furaha ilioje, wakaangukiana na kukumbatiana, wakimwacha mfalme amejaa aibu tele.

HADITHI HII INAWAKUMBUSHA AKINA BABA WENYE UROHO WA WANAWAKE WA WENZAO, KWAMBA WANAWAKE WAMEZALIWA KAMA WASICHANA WADOGO. HIVYO WASITAMANI VYA WENZAO, VYAO WAKAVICHUKIA.
Hadithi kutoka kwenye kitabu cha HADITHI na via kutoka Tanzania.

Friday, November 21, 2008

HADITHI YA MWANA MPOTEVU

Hiii hadithi inanikumbusha mambo mengi sana sijui wenzangu mnasemaje?

Kulikuwa na baba mmoja aliyekuwa na watoto wawili wa kiume. Siku moja yule wa mwisho akamwambia baba yake : baba mimi sasa ni mkubwa naomba haki yangu nataka kuondoka kwenda mbali kutafuta maisha. Baba yake akampa pesa nyingi tu. Akaondoka akaenda zake na pesa zote.

Muda si mrefu akapata marafiki wengi tu. akawa anakula na kunywa nao pamoja na yeye ndiye aliyekuwa analipa kila kitu.

Lakini muda si mrefu pesa zote zikamwishia. Akawa hana kitu cha kula. Marafiki zake wote hawakumpa wala kumsaidia chochote isipokuwa walimtupa barabarani.

Siku moja akaondoka akaenda kwa mkulima mmoja na kusema ya kwamba anaomba chakula, aina yoyote ile, na halafu atafanya kazi kwake. Mkulima akamhurumia akampa chakula na akamwambia kazi yake ni kuchunga nguruwe wake.

Hata hiyo kijana bado alikuwa ana njaa. Akaanza kuwaza: kwa nini napata taabu hapa wakati baba yangu ana chakula kingi tu. Narudi nyumbani kwa baba tena. Nataka kufanya kazi kwa baba kuliko hapa.

Mara akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Na kusema baba, naomba radhi nimekosa. Ilibidi nisirudi na wala usinipokee tena hapa nyumbani kwako. Lakini baba kwa uchungu wa furaha akamkumbatia na kumpokea. Kwa furaha kubwa baba akamfanyia kijana wake sherehe kubwa kwa kufurahia kwa sababu kijana wake alikuwa amerudi tena kwake.

Kaka mtu akawa anarudi toka kazini(shambani) akakutana na babake asemaye. Mdogo wako amerudi tena nyumbani njoo tumsherehekee. Alipotea sasa amerudi tena.

Swali: Je? Hadithihii wewe inakufundisha nini?
Na je? ungekuwa wewe ni yule kaka mkubwa ungefanyaje?

Thursday, October 30, 2008

KILA MTU ANA NDOTO YAKE KATKA MAISHA

HAPA INAKUJA HADITHI YA JUMA.

Mzee Banzi Kijiwe hujipatia pesa kwa kumlazimisha Juma Kombora kuomba omba mitaani. Wakati mwingine Juma hugoma kuomba mitaani na huwambia Mzee Banzi kuwa anataka kwenda nyumbani kwao Morogoro. Mzee Banzi humpiga sana Juma anapokataa. Juma Kombora ana umri wa miaka kumi tu na pia ni mgeni katika mji wa Zanzibar. Maisha ya Juma ni ya kusikitisha sana na mara nyingi hulala na njaa kwa kuwa Mzee Banzi humwachia pesa kidogo sana.
Juma pamoja na watoto wengine wawili hulala mtaani chini ya usimamizi wa Mzee Banzi. Vijana hawa aliwaleta Mzee Banzi Zanzibar kutoka Morogoro kwa njia ua kuwalaghai wazazi wao.

Juma kabla ya kuja Zanzibar alikuwa anaishi Morogoro na mara nyingi alitumia muda mwingi kuchunga mifugo ya baba yake Mzee Kombora na kucheza mpira wa miguu katika nafasi ya ushambuliaji. Juma alikuwa na ndoto akiwa mkubwa atakuwa mchezaji hodari mwenye uwezo mkubwa wa kupiga chenga za maudhi kama Ronaldo. Lakini siku moja ghafla aliitwa na baba yake na kuambiwa kuwa ataenda Zanzibar na rafiki ya baba yake Mzee Banzi. Mama Juma alifurahi sana siku ya kumuaga Juma maana rafiki wa mume wake, Mzee Banzi, alimpa zawadi mama Juma ya kilo 25 za Maharage na kila 25 za mchele pamoja na vitenge doti mbili. Mzee Banzi na Juma waliondoka Morogoro kwa basi mpaka mjini Dar es Salaam halafu wakapanda boti ya kasi mpaka mjini Zanzibar. Juma alikuwa hajawahi kupanda boti maishani mwake kwa hiyo alifurahi sana kupata nafasi hiyo. Wazazi wa Juma wanaamwamini sana Mzee Banzi na walitegemea atamsaidia Juma kupata kazi nzuri kwenye hoteli za kitalii mjini Zanzibar. Juma hajui wapi atapata msaada amebakiwa na ndoto tu za kuwa huru.

Swali langu:- Kwa nini tunakuwa wapesi kuamini ndugu na marafiki kuwa watatusaidia?.