Sisi sote hukasirika mara kwa mara. Hasira ni sehemu ya hisia zetu kama vile ilivyo upendo, tumaini, wasiwasi, huzuni na woga. Hasira ilivyodhibitiwa inaweza kuonyeshwa kwa njia inayofaa na inaweza kuwa na faida. Kwa mfano, hasira inaweza kuwa na faida ikiwa itamfanya mtu aazimie kushinda vizuizi au matatizo fulani.
Kwa kawaida, mtu huudhika anapotendewa isivyo haki. Kutukanwa, au kukosewa heshima kunaweza pia kumuudhi mtu. Pia, mtu anaweza kuwa na hasira anapoona jambo fulani kuwa tishio kwa mamlaka au sifa yake.
Bila shaka, watu hukasirika na mambo tofauti ikitegemea umri, jinsia, na hata utamaduni wao. Isitoshe, watu hutenda kwa njia tofauti tofauti wanapopandwa na hasira. Watu fulani hawakasiriki upesi, nao husahau haraka wanapokosewa, lakini wengine hukasirika kwa haraka na huenda wakaendelea kuwa na hasira kwa siku nyingi, majuma , miezi au hata miaka.
Binadamu tumezungukwa na mambo yanayoweza kuchochea hasira. Zaidi ya hilo, siku hizi watu wanachokozeka kwa urahisi zaidi, Kwa nini imekuwa hivi? Sababu moja ni kwamba kuna mtazamo wa ubinafsi yaani umimi ambao umeenea mno.
Kwa kweli, watu wenye ubinafsi wasipopata kile wakitakacho, mara nyingi wao hukasirika. Kuna sababu nyingi kwa nini mwelekeo wa watu kulipuka kwa hasira unaongezeka, ambazo wewe msomaji na mimi twaweza kusaidiana kuzifikiria...
Na kama tunavyoelewa hasira imekuwa ni adui kwa watu wengi sana kwasababu imekwisha leta madhara makubwa sana kwa wengi
Binadamu anadaiwa kuwa ni kiumbe ambaye anakabiliwa na tishio la kuangamia kwa hasira kwasababu ya maendeleo anayoyafikia
Hivi ni kweli kwamba kadiri maendeleo yanavyoongezeka ndivyo uwezekano wa binadamu kuwa na hasira unaongezeka pia?.Kama ni kweli ipo hivi, kwa binadamu ni kitisho kwa usalama wake mwenyewe
Kuna haja ya kuwa na elimu na semina kwa wingi ili kuweza kumuokoa binadamu na kitisho cha hasira
