Showing posts with label burudani nchi. Show all posts
Showing posts with label burudani nchi. Show all posts

Tuesday, December 9, 2008

MJI MKUU WA NCHI YETU

Kumbukumbu kutoka kitabu cha TUJIFUNZE LUGHA YETU! Kitabu cha darasa la nne. Wengi natumaini mnakumbuka, binafsi nimekumbuka na nimefurahi sana. Binafsi nimekumbuka na nimefurahi sana soma ufaidi au ukumbuke pia:-)


Kusala ni mtoto wa Songea. Anasoma shule ya Lilambo. Ana mjomba wake, anafanya kazi jiji la Dar es Salaam, ambao ni mji mkuu wa Tanzania. Ni karani wa bandari.

Wakati wa likizo, Kusala alikwenda Dar es Salaam kumsalimu mjomba wake. Alichukua sanduku lake la mbao na kifurushi cha chakula, akaenda mpaka mjini Songea. Kesho yake akaondoka kwa basi kwenda Dar es Salaam.

Basi hili lilipitia njia ya nNjombe. Jioni likafika Iringa. Hapa wakalala. Asubuhi yake wakaanza safari kwenda Morogoro kupitia Mikumi. Mikumi ni mbuga ya wanyama.

KUsala aliona wanyama wengi. Kutoka hapo walikwenda moja kwa moja mpaka Morogoro ambako walifika kama saa kumi jioni. Baada ya kupumzika kidogo waliondoka kuelekea Dar es Salaam.

Walipokaribia Dar es Salaam, Kusala aliona majengo makubwa upande wa kushoto. Alimwuuliza mwenzake aliyekuwa karibu naye, ”Yale ni majumba gani?” Mwenzake akamjibu, ”Yale ni majengo ya Chuo Kikuu. Ni mahali maarufu sana hapa nchini.” Kusala akauliza tena, ”Je? Wapo watoto ?” Akajibiwa, “La, wasommao pale si watoto. Ni watu wazima.” Akaendelea kuuliza, “Wanasomea mpaka madarasa gani?” Akajibiwa tena, “Hawana madarasa. Wanasomea shahada za elimu mbalimbali.”

Walipofika katikati ya mji, Kusala alishangaa sana kuona taa zenye rangi mbalimbali. Taa hizo zilitundikwa juu ya milingoti mirefu ya chuma. Aliona magari makubwa, mabasi mengi na motokaa ndogo nyingi. Alishangaa sana kuona magari mengi hivi. Wakati wote huu alikuwa na wasiwasi. Hakujua atakalofanya ikiwa hatamkuta mjomba wake kituoni. Basi lilipofika kituoni alifurahi sana kumwona mjomba wake amekuja kumpokea. Usiku ule Kusala alilala sana kwa ajili ya uchovu wa safari.

Asubuhi yake Jumapili, mjomba wake aliwachukua yeye na binamu yake, Njoli, akawatembeza mjini. Kwanza walitembelea kiwanje cha ndege. Kusala alishangaa kuona jinsi kiwanja kilivyo kikubwa. Aliona ndege kubwa zikitua, akauliza, “Mbona Songea hakuna ndege kubwa kama hizi?” Mjomba wake akamjibu, “Songea ni mji mdogo. Hauna kiwanja kikubwa cha kutua ndege kubwa kama hizi.”

Kutoka kiwanjani Kusala alipelekwa kutazama Jengo la Bunge. Mjomba wake alimweleza kuwa humo Wabunge hukutana na kupanga mipango ya Serikali na maendeleo ya nchi. Baada ya hapo walikwenda kwenye kivuko cha bahari kupitia Ikulu. Hapo Ikulu, Kusala aliona askari walinzi. Pia aliona mbuni, tausi na kudu. Kusala akauliza, “Askari hawa wanafanya nini?” Njoli akamjibu, “Wanalinda zamu. Hapa ndipo Ikulu.” Kusala akauliza tena, “Ikulu ni nini?” Mjomba wake akamwambia, “Ni makao rasmi ya Mtukufu Rais wetu.

Walipofika kwenye kivuko walikata tikiti wakaingia katika pantoni na kuvuka mpaka ngámbo. Huko walitembelea mtambo wa kusafisha mafuta. Mtambo huu husafisha na kutenganisha lami, dizeli, mafuta ya taa na petroli.

Waliporudi walikwenda bandarini. Mjomba wake akawaonyesha ghala kubwa na mshine za kuinulia mizigo. Pia waliona meli nyingi kubwa kwenye magudi. Zilikuwa zikipakua na kupakia bidhaa. Pia yalikuwapo madau pamoja na mitumbwa. Wavuvi hutumia madau na mitumbwa kuvulia samaki.

Kusaka vilevile alitembezwa kuona stesheni kubwa ya gari la moshi. Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kuona gari la moshi. Alishtuka aliposikia makelele na kuona moshi mwingi. Watu wengi walikuwa wakingojea gari liondoke.

Siku nyingine Kusala alipelekwa kuona viwanda. Aliona watu wengi wakifanya kazi. Kusala na Njoli waliona viwanda vya kutengeneza nguo, mablanketi, sufuria na madebe. Walipofika Ubongo, alistaajabu kuona watu wengi wamesimama msululu nje ya kiwanda cha kutengeneza nguo. Kusala akauliza, “Hawa wanafanya nini?” Mjomba wake akamjibu, “Watu hawa wanatafuta kazi. Ni wageni mjini. Wameshindwa kukaa vijijini” Kusala alihuzunika sana, akamwambia mjomba wake, “mimi napendelea kuishi kijijini kwetu. Vijijini hakuna haja ya kusimama msululu kutafuta kazi. Maana kazi za shamba ni nyingi. Nitakapomaliza masomo yangu nitaanza kulima na kufuga kuku. Mimi sipendi kukaa mjini bila kazi.”

Kutoka Ubungo walipitia Kariokoo. Hili ni soko kubwa la Dar es Salaam. Vyakula na matunda mengi huuzwa hapo. Biashara nyingi huendeshwa katika maduka makubwa karibu na soko hilo. Kusala alisikia muziki wa redio ukiwastarehesha wauzaji na wanunuzi.

Kwa kweli, Kusala aliona mambo mengi mageni. Aliona watu wakikimbilia mabasi. Wengine wakienda mbio kwa miguu. Siku ya mwisho alitembelea kiwanda cha kutengeneza nyama za makopo. Alipoondoka alimshukuru sana mjomba na ndugu zake. Alipofika Songea aliwaandikia barua ya kuwashukuru na kusema kuwa alifurahi sana kuona jiji la Dar es Salaam.