Showing posts with label uhuru. Show all posts
Showing posts with label uhuru. Show all posts

Sunday, December 9, 2012

JUMAPILI YA LEO NI JUMAPILI AMBAYO IMEANGUKIA SIKU AMBAYO TULIPATA UHURU 9/12/1961...


Nami nimea si wimbo huu wa maombi unafaa sana kwa siku ya leo. NACHUKUA NAFASI HII NA KUWATAKIENI WOTE JUMAPILI NJEMA NA PIA SIKU HII KWA UJUMLA

Wednesday, May 16, 2012

Wanafunzi wanasomea vibanda vya nyasi!!

Ni ile JUMATANO YA KIPENGELE CHA MARUDIO NA LEO NIMEONA TUTEMBELEE WILAYANI NAMTUMBO.ELIMU NIMEIPATA HABARI HII  Albano Midelo Haya KARIBUNI. 



 Wanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi
 SelousWilayani Namtumbo wakiwa darasani.

WANAFUNZI wa shule tatu za msingi zaidi ya 500 katika kata ya Rwinga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wanasomea kwenye madarasa yaliojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi.
Uchunguzi uliofanywa katika shule tatu kati ya saba zilizopo kwenye kata hiyo ambayo ipo mjini Namtumbo umebaini kuwa katika shule ya msingi Rwinga wanafunzi 296 wanasomea kwenye vibanda vya miti vilivyoezekwa kwa nyasi.
.
Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo Onesmo Mbawala alisema idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo wanasomea katika vibanda vya nyasi kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu wa vyumba 12 vya kusomea ambapo vyumba vilivyopo ni vinne tu na kwamba shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975 ina jumla ya wanafunzi 592.
Katika shule ya msingi Selous jumla ya wanafunzi 108 wa madarasa ya tano na sita wanasoma kwenye vibanda vya nyasi hali ambayo walimu wanasema inachangia kushusha taaluma kwa wanafunzi.
Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo Sheweji Simba alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 ina jumla ya wanafunzi 477 huku ikiwa na vyumba vinne tu vya madarasa kati ya mahitaji ya vyumba nane hali ambayo imesababisha baadhi ya wanafunzi kusomea kwenye vibanda vya nyasi .
Katika shule ya msingi Mkapa ambayo imepewa jina la aliyewahi kuwa kiongozi mkuu wa nchi Rais mstaafu Benjamin Mkapa pia kuna wanafunzi wanaosomea kwenye vibanda viwili vya nyasi kwa kuwa shule hiyo ina vyumba vinne tu kati ya mahitaji ya vyumba nane.
Mkuu wa shule hiyo Hans Mwailima alisema shule hiyo yenye wanafunzi 306 madarasa matatu yanasomea katika chumba kimoja ambapo kuanzia darasa la tatu hadi la sita wanasomea kwenye vibanda vya nyasi kwa zamu .
“Unajua wanafunzi wana tabia ya kutaniana hivyo endapo darasa moja wakisoma kwenye vibanda vya nyasi kila siku wenzao wanawatania hivyo kukata tamaa na wengine kuwa watoro hivyo tumeamua wote wawe wanasoma kwenye vibanda vya nyasi kwa zamu ili kujenga mvuto wa mazingira ya kusomea’’,alisema.

Wanafunzi wa shule ya msingi Mkapa Wilayani
Namtumbo wakiwa darasani na mwalimu wao.

Mratibu elimu kata ya Rwinga Thomas Komba amekiri shule tatu kati ya saba katika kata yake ambazo ni Rwinga,Mkapa na Selous wanafunzi kusomea katika vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi na kusisitiza kuwa shule za Minazini,Kidagulo,Migelegele na Mandepwende ndizo shule pekee katika kata hiyo ambazo hazina vyumba vya madarasa vilivyoezekwa kwa nyasi.

“Shule zangu tatu za Rwinga,Mkapa na Selous katika kata yangu zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa hali ni mbaya tunafanya jitihada za kuhamasisha jamii ili waweze kujitolea kufyatua tofali kuzichoma kwa kushirikiana na serikali ili kupata vyumba zaidi na kumaliza kero hii ya aibu’’,alisisitiza.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Kasimu Ntara alidai kuwa kuwa kuwepo kwa madarasa yaliojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi katika wilaya hiyo kunatokana na kuanzishwa shule nyingi za msingi .
“Mpango wa uboreshaji wa elimu ya msingi MEM nchini ulisababisha kuanzishwa kwa shule nyingi hivyo baada ya kuondoka kwa MMEM serikali imeshindwa kumudu ujenzi wa vyumba vya madarasa jitihada zinaendelea kufanyika kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa’’,alisisitiza.

TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO KWA JINGINE LA ZAMANI!!

Friday, December 9, 2011

SALAMU ZA KUSHUREKEA MIAKA 50 YA UHURU TANZANIA KUTOKA SWEDEN...

Familia hii haiko nyumba katika siku hii ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru. Ingawa mwanafamilia mmoja hayupo katika picha. MUNGU IBARIKI TANZANIA, WABARIKI VIONGOZI WAKE, HEKIMA UMOJA NA AMANI MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE IBARIKI TANZANIA ....

Wednesday, October 5, 2011

Sasa tunakaribia Miaka 50 ya uhuru na mfumo huu wa upishi?

Huyu ni kati ya wanake aliyekutwa katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma akipika ugali wa mahindi kwa mtindi wa wa kutumia mafiga matatu,kutumia kuni ambazo zinatoa moshi mwingi kwa mama huyu. Katika karne hii ya 21 ambayo inasisitiza maendeleo katika teknolojia Je? huu ni uungwana kweli? au Je una maoni gani katika hali hii? picha kutoka HAPA

Monday, September 26, 2011

MIAKA 50 YA UHURU TANZANIA!!!!

Mimi leo nataka tutumie maazimisho ya miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu kujadili swali lifuatalo :-
Baba wa Taifa hayati mwalimu Nyerere, aliamini na kuja na falsafa ya maendeleo iliyokuwa inasema ili tuendelee kama taifa tunahitaji mambo muhimu manne(4) watu, ardhi, siasa safi na Uongozi bora. Lakini pia akasisitiza ili hayo maendeleo yafikiwe tunahitaji kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
Kwa zama hii tuliyonayo pamoja na kuwa na hivyo vitu vinne kumeongezeka suala la UFAHAMU NA MAARIFA.
Swali katika ngazi ya familia na koo zetu za Kitanzania tunahitaji mambo gani ya msingi ili kuendelea.
Maana kwa hali ilivyo hasa kwa sisi watanzania tumebobea katika kulaumu, kulalamika na kulaani wakati hata siku moja kulaani na kulalamika hakujawahi kuwa suluhu ya kile unacholalamikia, kulaani na kulaumu.
UJUMBE HUU:- Nimetumiwa na kaka yangu pia msomaji wa MAISHA NA MAFANIKIO SALEHE MSANDA AMBAYE NI MKAZI WA NJOMBE. TUJADALI PAMOJA....

Thursday, September 1, 2011

Baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika​, je Tanzania inakuhitaj​i?

Mwaka 2011, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasherehekea miaka ya uhuru wa serikali ya Tanganyika, taifa lililomezwa April 26, 1964 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa hesabu za haraka haraka utaona miaka hamsini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaadhimishwa April 26, 2014. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una faida na kasoro zake, lakini leo nitajadili mada inayouliza kuwa “baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, je Tanzania inakuhitaji?”.

Magwiji na wataalamu wa falsafa ya imani duniani, wanatuaminisha kuwa hakuna nguvu inayozidi upendo, wakidadavua zaidi husema kuwa penye upendo uliopea Mungu yupo. Hata ukitafakari maisha ya mahusiano tunayoishi, huna budi kumpenda mtu kwanza kabla hujaenda mbele zaidi kumpa nafasi ya kuwa mwenzi wako wa ndoa, katika muktadha huo ni kawaida kumwona kijana mwanamke akitoka bara la Amerika kufunga ndoa na kijana mume toka Mwanza, vivyo hivyo haishangazi kuona vijana wakivuka bahari na mito, milima na mabonde kutoka bara moja kwenda bara jingine kutafuta mapenzi yanayojengwa na upendo.

Hakika upendo ni nadharia ambayo hakuna maelezo yanayotosha kuidadavua kwa kilele chake. Bila shaka yoyote upendo miongoni mwa Watanganyika na Wazanzibar ndio uliozaa taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mtazamo wangu, upendo ule uliozaa muungano hapa Tanzania miaka 47 iliyopita, naona umepoa kama sio kufifia na kuchuja. Makala hii haitojadili nani amefifisha upendo huu hapa Tanzania.

Nakumbuka siku ile, taifa lilipotangaziwa kuhusu afya ya baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kuwa hali yake sio nzuri, Watanzania tuendelee kumuombea, mwili ulinisisimka kwa hofu. Nikapata baridi na hofu kuu, maswali mengi yalinikaba hasa nikijiuliza, itakuwaje nchi yangu bila “a great man, father of the nation?”. Hakika Mwalimu Nyerere alikuwa “great man”. Hata viongozi waliomzunguka wao pia walikuwa “great people”. Watanganyika hawa “great people” kizazi chao shurti kiwe “great generation”.

Wahenga walipata kusema kuwa “macho ni dirisha la fikra na ujasiri alionao mtu”, ukweli huu nauona kila ninapowatazama machoni Watanganyika nami nawaona kuwa na “great people”. Ujasiri huu tulionao hausemwi sana siku hizi, hivyo ipo haja ya kufanya kampeni ya makusudi miongoni mwa vijana wa Kitanganyika, hivyo upatapo fursa ya kushikana mkono na rafiki yako, vema ukamtazama machoni kwa walau dakika moja, kisha umwambie “you are a great person” kwa vile kila Mtanganyika ni kizazi cha “great people” ambacho ndio kiliasisi taifa la Tanganyika linalotimiza miaka 50 ya Uhuru tarehe 9 Desemba mwaka 2011.

“Great people” wale wakiongozwa na “great man” Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere walifanikisha kujenga misingi ya Taifa la Tanganyika na kufanikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, kwa vile upendo baina yao ulipea, vivyo hivyo waliipenda nchi yao na watu wake. Ukweli ni kuwa Watanganyika ni "great people", japo utamaduni wa kuambiana ukweli huu haupo tena nchini Mwetu. Nasisitiza kuwa Watanganyika ni kizazi cha “great people” kwa vile Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliweza kuwakaripia viongozi wa mataifa yenye nguvu za uchumi kama Amerika na Uingereza haya Israel pale alipoona matendo ya mataifa hayo yanaathiri kwa makusudi ustawi wa nchi zenye uchumi mdogo, kwa Mwalimu, kigezo cha ubinadamu hakikuwa uchumi bali ubinadamu wenyewe.

Mwalimu Nyerere hakuishia kukemea mataifa makubwa pekee, bali alikemea pia viongozi wa ndani ya Tanganyika ambao nia zao binafsi zilikuwa zinakinzana na maendeleo ya nchi yetu. Mwalimu hakusita kuanika udhaifu, uchafu na tamaa za viongozi hao na akasisitiza kuwa watu hawa wasipewe uongozi kwa hawana nia thabiti ya kuweza ustawi wa jamii ya Mtanganyika. Bila shaka yoyote, msimamo huu wa Baba wa Taifa ndio ulikuwa msimamo wa serikali yake yote, ndio ulikuwa msimamo wa viongozi wengine wote, Mwalimu Nyerere amekuwa “father figure” kwa viongozi wengi wa Tanganyika kwa kuwa na maneno machache na matendo mengi, nakumbuka tulipata kuwa na wimbo wa kusifia matendo ya Baba wa Taifa kuwa “Raisi wetu hapendi kusema, raisi wetu Nyerere baba, anaonesha mfano kwa vitendo”.

Mwalimu Nyerere alikuwa na shamba lake kule Butiama, shamba la Mwalimu lilikuwa mfano kwa wanakijiji wenzake, ukubwa wa shamba hili la Mwalimu haukuwa nusu ya ardhi ya kijiji, bali alichukua sehemu kidogo ili kila mwanakijiji mwenye nia ya kufanya kilimo naye apate ardhi. Hapa utaona fahari ya Mwalimu Nyerere haikuwa kujilimbikizia mali, ndio maana uwepo wa Tanzania ulimhitaji sana Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Swali linabakia, je baadhi ya viongozi tulionao ambao kujilimbikizia ardhi na mali kwa njia za ufisadi na kuuza mali asili zetu, Tanzania inawahitaji?

Kwa vile utamaduni wa kuambiana kuwa “sisi ni great people”, imekuwa kawaida kuona Watanganyika wa leo tunaishi kama pimajoto -thermometer- ambayo inabadilisha kizio cha joto kadiri unavyoiweka kwenye nyuzi joto tofauti. Ni kawaida kwa pimajoto kusoma nyuzi joto za juu ukiiweka kwenye mazingira yenye joto la juu, pia ni kawaida sana ikiwa pimajoto itatolewa kwenye mazingira ya nyuzi joto la juu na kuwekwa kwenye barafu itasoma nyuzi joto sifuri ama chini ya sifuri. Mfano huu unamaanisha kuwa Pimajoto inaathiriwa na mazingira, hali inayotokea sana kwa Watanganyika wa leo bila kujali elimu zetu, vipato vyetu ama namna yoyote ya uelewa uliokolea, tumekuwa tunaathiriwa sana na mabadiliko ya agenda ama mazingira, kwa mfano bei za bidhaa zinapopandishwa kiholela tunalalamika lakini hatuchukui hatua kukemea na kukomesha hali hiyo, zaidi tumekuwa ni walalamikaji tuliojaa woga wa kuuliza kwa nini hali ipo hivi, nashangaa sana tumekuwa sio “great generation” tuliozaliwa na “great people” chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye agenda yake ilikuwa kukemea uoza huu.

Mwalimu Nyerere na Waasisi wa Taifa letu hawakuishi kama Pimajoto, fikra zao hazikubadilishwa na mazingira kama ilivyo Pimajoto bali wao ndio walipambana kubadilisha mazingira magumu waliyokuwa nayo wakati huo hawakukubali chochote kilichodhalilisha utu wao, kilichobeza ubinadamu wao ama kilichodidimiza ustawi wa Tanganyika ama Watanganyika. Kwa kutunza heshima na utu wa Mtanganyika walisisitiza sana elimu ya ujamaa na kujitegemea. Ukitazama wengi wa viongozi tulionao Tanganyika ya leo wengi wanaishi maisha ya Pimajoto, wanabadilika badilika ili kufanikisha nia zao binafsi zinazokinzana na mahitaji ya mustakabali wa Taifa letu Tanganyika, baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyija, Watanganyika tunaoishi maisha ya Pimajoto, Tanzania inatuhitaji?

Miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika imeshuhudia awamu nne za maraisi wa Tanganyika, huku awamu ya kwanza ikiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi, awamu ya tatu iliongozwa na Mzee Benjamini Mkapa na awamu hii ya nne usukani umeshika na Raisi Jakaya Kikwete. Katika awamu zote nne, serikali imepambana na changamoto mbali mbali za maendeleo, pia imetumia fursa nyingi za maendeleo ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi, kisisasa na ustawi wa jamii. Yatokanayo na jitihada hizi na changamoto zake sio muktadha wa makala hii.

Kwa makala hii, miongoni mwa maswali ya kujiuliza ni:- je serikali ikiwa ni mzazi wa kila Mtanganyika, inawapokea Watanganyika na matatizo yao na kuwaongoza kutatua shida zao? Kwa maana jitihada zilizofanywa na awamu zote, miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika zimefanikiwa kiasi gani kutatua matatizo yanayokabili ustawi wa jamii ya Mtanganyika? Je, miaka 50 inatosha tu inaalika sherehe na karamu ya kujivunia uhuru ama ni fursa kwetu kutafakari wapi tulipojikwaa kama Taifa badala ya kulalamikia wapi tulipoangukia? Maana miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika haijatosha kutatua shida za msingi kama uhaba wa madawati mashuleni, uhaba wa madawa, vitendanishi tiba na watumishi hospitalini, kukosekana kwa nishati ya umeme ya uhakika na mambo mengine mengi.

Kwa bahati mbaya sana miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika , taifa letu linashuhudia matumishi ya ujuzi na utaalamu wa baadhi ya viongozi wenye tamaa, ulafi na ubinafsi vikitumika kuzidisha umaskini miongoni mwa jamii kubwa ya Watanzania, je, Tanzania itakapofikisha miaka 50, hapo tarehe 26 April 2014 itakuwa bado inahitaji viongozi wa namna hii?

Nihitimishe kwa kusema kuwa, kila tunapotazama tulipotoka, hasa baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, vema tukijua kuwa sisi Watanganyika ni “great people” mambo yaliyofanywa na waasisi wa Taifa letu ni mfano hai wa hiki ninachosema. Changamoto tuliyonayo leo hii ni kuishi maisha ya Pimajoto, ambayo ni kinyume na silika ya “great people” maana “great people” wote huwa wanabadilisha mazingara yao na kuyafanya kuwa bora zaidi kwa ustawi wa taifa lao na vizazi vijavyo. Serikali haina budi kusimamia sheria zake ili wajanja wachache wasitumie maarifa waliyoyapata kuihujumu serikali, badala yake wataalamu hawa watumike kusaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa, tukifuata njia hii ndiposa tutajibu hoja ya Miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika, je Tanzania inanitaji?
Imeandikwa na,
Barnabas Mbogo.
Nyamagana, Mwanza
.

Picha ya wiki:- Kuelekea miaka 50 ya Uhuru!!!!




Sijui itakuwa hivi mpaka lini? Maana sasa tunaelekea miaka 50 ya uhuru lakini hali ni ile ile......sijui mwenzangu mnasemaje??

Friday, November 26, 2010

Ijumaa njema!! UHURU, hivi ni lini mtu anakuwa huru???



Wimbo huu kila nikiusikiliza napatwa na furaha lakini pia napatwa na huzuni kiasi kwamba natokwa na machozi. Sijui wenzangu pia mnajisikia hivyoo:-( HATA HIVYO NAWATAKIENI MWISHO WA JUMA MWEMA !!!!!!!

Wednesday, December 9, 2009

TANZANIA BARA LEO INATIMIZA MIAKA 48 YA UHURU



Ni siku ya UHURU NA JAMHURI kwa taifa lote la watanzania kokote walipo.

Sunday, December 6, 2009

KUELEKEA MIAKA 48 YA UHURU: TANZANIA YETU NA ELIMU ZA CHINI YA MITI

Nimevutiwa sana habari iliyowekwa na Profesa Mbele kwenye kibaraza chake akizungumzia juu ya mustakabali wa elimu huko nyumbani Tanzania, bofya hapa umsome .

Hakika habari hiyo imenikumbusha mbali sana yaani simulizi nilizopata toka kwa baba na mama yangu. Maana wao pia wamepata elimu ya aina hii, nakumbuka wakati fulani nilipokuwa mdogo nikisoma shule ya msingi wakati huo mama yangu alinisimulia kuwa wakati alipokuwa akisoma shule ya msingi alikuwa anatembea masaa yasiyopungua matano kutoka nyumbani kwao mpaka shuleni.

Baba naye alinisimulia kuwa yeye alipata elimu yake chini ya mti wa mkorosho na huku akiwa amevaa LUBEGA YA KANIKI (kufunga nguo nyeusi shingoni) lakini hata hivyo alimudu kupata elimu bora mpaka akawa mwalimu.

Kumbuka kwamba walikuwa wanazungumzia mambo ya miaka ya 60 wakati huo tukiwa ndio nchi yetu imejipatia uhuru na kuanza kujitawala. Wakati huo wananchi waalikuwa na mwamko wa Elimu huku wakichagizwa na serikali yao walimudu kusoma hata chini ya miti kwani kulikuwa na kampeni maalum iliyoanzishwa na serikali ya awamu ya kwanza ya kuhakikisha kuwa kila mtu anapata elimu ikiwa ni pamoja na elimu ya watu wazima. Wakati huo Serikali ilikuwa imetangaza vita ya kuwashinda maadui watatu ambao ni Ujinga , Maradhi na Umasikini, na tuliambiwa kuwa hauwezi kuwashinda maadui wawili yaani maradhi na umasikini iwapo hatutafuta ujinga, na ili tufute ujinga ilikuwa ni lazima watu wapate elimu, kwa hiyo swala halikuwa ni madarasa mazuri yaliyonakishiwa bali ilikuwa ni elimu kwanza, hata ikibidi chini ya miti ilimradi watu wapate elimu, halafu baada ya hapo hao maadui wengine yaani umasikini na maradhi itakuwa ni rahisi kuyashinda.

Wiki ijayo tunashereheka miaka 48 tangu tujitawale. Hii ina maana kwamba kama ni mtoto alizaliwa wakati huo tunapata uhuru, basi atakuwa ni mtu mzima ambaye amekwishajitambua na kumudu kujitafutia kipato na kujitegemea. Hapa nazungumzia mtu mzima ambaye amezaliwa akiwa na hana dosari ya kimaumbile yaani sio mlemavu, maana kama angekuwa ni mlemavu tungesema kuwa atakuwa anahitaji uangalizi ili amudu kusimama mwenyewe. Nchi yetu inayo utajiri wa asili kwa maana ya kuwa na ardhi yenye rutuba, madini,uoto wa asili, Misitu, na mbuga za wanyama. Hebu tujiulize hapa, hivi kama utajiri huo tulio nao ungetumika kwa busara hivi kweli tungekuwa na watoto wanaosomea chini ya miti leo hii hata baada ta miaka 48 ya uhuru?

Hii ni sawa na kijana aliyezaliwa miaka 48 iliyopita akiwa na siha nzuri, halafu akakuta baba yake amemuachia utajiri wa kila aina lakini akabaki kulia umasikini na kuishia kuombaomba.Ni aibu iliyoje nchi yetu hata baada ya miaka 48 ya uhuru bado tunaombaomba na kulia eti sisi ni masikini wakati Wenzetu wanakimbilia katika nchi yetu na kujichotea utajiri na kuhamishia kwao utadhani shamba la bibi.

Raisi wetu haishi safari za nje na hata alipoulizwa wakati fulani sababu ya yeye kusafiri mara kwa mara nje ya nchi, alidai kuwa kama ni kuomba misaada katika nchi hizo anazotembelea hawezi kumtuma waziri wake au mtu mwingine kwa sababu hawawezi kupewa kile watakachoomba, isipokuwa yeye.

Yaani mpaka leo hii Raisi wetu anajisifu kwa kuomba tena wazi wazi, wakati hilo ni jambo lenye kutia aibu. Wazungu ni watu wa ajabu sana, wakati unapowaomba misaada wataongea na wewe kwa bashasha na kwa akili ndogo utadhani wanakujali sana lakini amini kwamba ukiondoka huku nyuma wanakung’ong’a na kukudharau sana. Na usidhani huo utakaopewa ni msaada wa bure, ni lazima tu utaulipa kwa namna yoyote.

Na ndio maana hata mheshimiwa Rais akasema kwamba akienda yeye ni rahisi kupewa kwa sababu yeye ndiye mwenye jibu la mwisho. Kwa mfano kama waziri wa Nishati na madini akienda kuomba misaada na akapewa sharti la kuipatia tenda kampuni maarufu ya nchi hiyo ili ije ichimbe madini au Gesi hapa nchini kwa mrahaba mdogo, itakuwa ni vigumu kwa waziri huyo kutoa jibu la moja kwa moja bila kushauriana na mheshimiwa rais, hivyo kutakuwana mlolongo wa safari za kwenda na kurudi mpaka kufikia makubaliano wakati akienda Raisi mwenyewe anakuwa na jibu moja tu, ndio au hapana.

Nchi yetu bado inayo kiwango kidogo cha ongezeko la watu, hii ina maana kwamba bado tunayo ardhi ya kutosha na kwa kuwa bado kuna mapori wananchi wamekuwa wakitawanyika huku na huko kujitafutua makazi na kutafuta ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, lakini cha kushangaza serikali yetu bado imelala usingizi wa samaki aina ya pono bila kuharakisha usambazaji wa miundo mbinu katika maeneo mapya yanayokaliwa na watu. Ni aibu mpaka sasa serikali kusubiri ripoti za vyombo vya habari ili kupata taarifa kuwa ni mahali gani wananchi wanahitaji shule, barabara, zahanati na maji safi.

Na ndio maana wananchi wanaamua kujianzishia shule zao chini ya miti na kutafuta mwalimu ili watoto wao wapate elimu. Kuliko watoto kutembea masaa matatu kwenda shule na masaa matatu kurudi nyumbani . Zamani hatari kubwa iliyohofiwa na wazazi juu ya watoto wao wanapokwenda shule za mbali ilikuwa ni wanyama wakali na nyoka, lakini siku hizi mambo ni tofauti, kuna kubakwa kwa watoto wa kike au hata kuuawa na kukatwa viungo au kuchunwa ngozi.

Athari za watoto kusoma mbali ni nyingi sana lakini kubwa kabisa ni uchovu na njaa. Ni jambo lisilo na ubishi kuwa ni vigumu hata wanafunzi kumuelewa mwalimu kutokana na kusinzia. Maana hapo watakuwa wamechoka. Kwani mwendo mwingi waliutumia kutembea na wakifika shuleni ni kusinzia tu.

Kwa ujumla naweza kusema , mwalimu ni muhimu kuliko vyote.Lakini mazingira ni muhimu pia. Bila kusahau wanafunzi wenye afya na wenye shibe ili kumudu kusoma na kuelewa kile wanachofundishwa na waalimu wao.

Friday, October 17, 2008

RAMANI YA TANZANIA NA MBUGA ZAKE


Naipenda nchi yangu, Tanzania ni nchi yenye amani katika Afrika.

Wednesday, October 8, 2008

MAISHA NA MAZINGIRA

Leo mwenzenu nimeamka vibaya, Kwani nimekasirika sana. Kisa ni kwamba nimekuwa nimefikiri muda mrefu ni vipi watu wanaweza kufanya hivi. Yaani siku zote hizi nilikuwa nimefungwa kabisa. Leo ndo naamka na nimekasirika mno. Mazingira, nani alisema watu wanaruhusiwa kumiliki maji au niseme nusu ya bahari. Watu wageni wanatoka huko na mihela yao na kuja nchi za wengine na kuamua yeye anamiliki nusu bahari. Kwa mfano Jangwani Seabreeze Resort, mtu anatoka huko Pakistani na kujengelea fensi ile wenye nchi wasiwe huru kwa nini? Na kwa nini wengine wanakubali kulipa pesa nyingi kwa sehemu ambayo Mungu ameifanya ili watu wote wafurahie maisha. Lakini sasa ni wachache tu wanafurahia. Kwa kweli naumia sana kuona wananchi hawana uhuru kwa sababu ya mtu ana pesa na katoka huko PAKISTANI. WATANZANIA TUSIWE HURU KATIKA NCHI YETU. Bado sielewi kwa nini? Je? wenzangu mnaelewa?