Showing posts with label kumbukumbu ya utotoni. Show all posts
Showing posts with label kumbukumbu ya utotoni. Show all posts

Tuesday, June 28, 2016

KUMBUKUMBU ISIYOSAULIKA...NIMEKUMBUKA MIAKA ILE NILIPOKUWA BINTI MDOGO NA KAZI YA KUTWANGA MIHOGO ILI KUPATA UNGA WA UGALI KULE NYUMBANI LUNDO/NYASA!

Ama kweli tumetoka mbali...nakumbuka shughuli hizi kama vile ilikuwa jana. Ila mama yangu huko aliko asterehe kwa amani. Ahsante mama kwa kunifunza hizi kazi, hata kama ilikuwa kwa mikwala:-) maana nakumbuka nilikuwa nachukua mihogo na vifaa vingine na kwenda kwa rafiki zangu Oliva,,, na huko sasa nikitoka saa nane  nyumbani kurudi saa kumbi na mbili. Kisa kucheza mipira wa kudaka(rede...redesta)...mmmmhhh we acha tu...je nawe unakumbuka shughuli  yoyote ile....

Monday, August 27, 2012

BARANI AFRIKA:- UTAMADUNI WA KUSIMULIA HADITHI BADO NI MUHIMU!!!

Hadithi kama tujuavyo ni njia ya maridhiano isiyo na gharama na ya kudumisha utamaduni.

Wengi wetu tunakumbuka nyakati ambazo wazazi au mababu na mabibi zetu walipokuwa wakitusimulia hadithi za kufurahisha zilizotokea zamani. Nilipoiona picha hii nimekumbumbuka sana zamani nilipokuwa mdogo wakati wa jioni wote mnakusanyika na kusikiliza hadithi na hapo hapo mnamenya karanga au kupukuchua mahindi na hapohapo mnaota moto.....

Thursday, September 15, 2011

KUMBUKUMBU NILIPOKUWA MDOGO/KACHIKI!!!

Mti wa mbura ukiwa na matunda yake bado mabichi





Leo nimekumbuka nilipokuwa kabinti kadogo (kachiki). Wakati huo nikiishi Lundo kando ya ziwa nyasa. Lundo kwa asili kuna miti mingiii sana ya mibuni/mbura, hii ni aina ya miti inayozaa matunda madogomadogo ya njano.

hapa zikiwa zimeiva tayari


Matunda haya huliwa kama yalivyo, pia nakumbuka tulikuwa tukiyatwanga kwenye kinu ili kupata urahisi wa kupata juice yake ambayo ni tamu haswa.
Pia hizi mbura zikikauka ni karanga tamu sana zipo ndani yake. Namna ya kuzipata hizo karanga hizo, ni kwamba:- unaweza kuzibangua kwa kutumia shoka, au jiwe (kienyeji).
Sasa siku moja mchana, kama sikosei hata shule nilikuwa sijaanza maana nilikuwa bado kachiki, lilinitokea tukio ambalo kamwe sitakuja kulisahau katika maisha yangu.
Naomba muungane nami katika simulizi ya mkasa huo, maana naona mnaanza kujiuliza ni nini kilimtokea binadamu huyu?
Ilikuwa hivi…….Nilikuwa na rafiki yangu aitwaye Puna Mahecha, huyu alikuwani shoga yangu hasa maana tulikuwa kama Kurwa na Doto. Basi Bwana, siku hiyo ya tukio, nakumbuka ilikuwa ni baada ya kuushindilia Ugali kwa Samaki na Matembele, tukatoka na shoga yangu kwenda kutafuta hizo Mbura. Sasa baada ya kukusanya Mbura zetu za kutosha, si mnajua mambo ya kitoto, tukaanzisha mchezo wa kulenga shabaha kwa kutumia zile Mbura ili kupima kama ni nani mwenye shabaha zaidi ya mwingine. Tukawa tunawekeana zamu………Puna-Yasinta, Puna -Yasinta nadhani tulifanya hivyo zaidi ya mara mia moja.
Ikafika zamu yangu tena, mara hii Puna akalenga bwana… Tapu……... Weee bwana wee kulichirizika damu.! Hapo ujanja wote ukaniishia na kilio kikawa kikubwa kweli. Bahati mbaya zaidi ilikuwa ni mkono wa kulia. Kwa hiyo sikuweza kula ugali kwa siku kadhaa kwa kutumia mkono huo. Sijui kama ningekuwa nimeanza shule ingekuwaje?...Nimekumbuka kisa hiki kwa vile nilikuwa nafanya kazi fulani nikajitonesha na kuhisi maumivu……….Mweh…hata baada ya miaka yote hii? Kweli michezo ya utotoni ina raha na hasara zake.Puna kama upo popote pale na unasoma simulizi hii nitafute rafiki yangu. Nitafurahi sana. Rafiki ni bora kuliko Mwanasesere.