Tuesday, March 26, 2019

LEO NIMETUMIWA ZAWADI HII NA RAFIKI YANGU

Baada ya kushukuru nimemlaumu sana kwa kunitamanisha.....ahsanten  kwa zawadi rafiki yangu umenikumbusha kwetu Lundo/nyasa

Saturday, March 23, 2019

ASIFIWE TUTAMKUMBUKA DAIMA!

AHSANTE KAKA JACOB MAHOLIJA KWA KUMBUKUMBU  HII NZURI  NIMEONA NIIWEKA HAPA KIBARAZANI KWA VILE LEO NI MIAKA  9 SASA  IMETIMIA  HAUPO NASI KIMWILI ILA KIROHO.
Leo ni arobaini ya Mpendwa wetu Asifiwe Ngonyani alama ya upole na upendo iliyofutika ghafla tarehe 23/3/2011 kama imefanyika ilivyopangwa.
Pamoja na kuwa mila zetu wengi zinatueleza kuwa arobaini ni kuhitimisha msiba lakini ukweli itachukua muda huzuni kufutika katika mioyo yetu, hasa kwa tuliopata bahati ya kumuona binti huyo. Tunakubali kwasababu kazi ya mungu haina makosa. Bali Asifiwe Tutamkumbuka.

                      ASIFIWE TUTAMKUMBUKA!

Marehemu Asifiwe akiwa na baba
Kwa upande wangu nikiwa na siku kadhaa mbali na Jiji la Dar es Salaam katika Vijiji ambako network ya mawasiliano ni mtihani kidogo hali yangu ya kifikra ilikuwa tata kidogo, nahisi ilikuwa ishara ya taarifa ya kusikitisha.. nilipokuwa katika vijiji vyenye mtandao, niko bize, baadae nikaona Misscall ya Yasinta. Sikuwa na hela ya kutosha kwenye simu siku iliyofuata Simu iliita nikiwanayo mkononi nikapokea.
Tofauti kabisa na nilivyozoea napompigia au anaponipigia, habari niliyoipata ilininyong’onyesha!, Kwa sauti ya unyonge Yasinta alisema “Jacob nilikuwa nakutafuta ulikuwa hupatikani, nilitaka nikupe taarifa Asifiwe Hatunaye Tena” kwanza nilijipa moyo huenda sikuwa kwenye simu ni mawazo tu .. lakini kwanini niwaze hivyo?....ikabidi nimuulize “Unasemaji Yasinta?” .. “Asifiewa Amefariki” alirudia kunithibitishia … hatukuongea sana .. nilimwambia tutaongea .. bado nikiwa nahisi labda ni mawazo tu .. nikamtumia msg kumuuliza tena, alinijibu “ni kweli Jacob, Asifiwe Ametuacha” tuliendelea kuchati kwa muda kidogo lakini dakiki zilivyozidi nilizidi kuishiwa nguvu.. nikakata mawasiliano..maana taarifa zilikuwa zinazidi kuniumiza!
Nilikuwa namfahamu Asifiwe baada ya kumtembelea Nyumbani Ruhuwiko miezi michache baada ya kurudi Kutoka kwenye matibabu ya moyo Dar es Salaam mwaka jana.
Ktika picha ya pamoja na Marehemu Asifiwe
Kwa waliowahi kukutana na binti huyu kama kaka Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti aliyewahi kumtembelea pale Hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo, Shaabani Kaluse ambaye pia Jumamosi ya terehe 18/03/2011 alipata bahati ya kumuaga Asifiwe, na wengine waliowahi kumuonawataungana nami kuwa binti huyu alikuwa mpole, mtulivu mwenye sura ya heshima na upendo.
“Nilijikuta nikimwambia kuwa sasa anatakiwa kurudi Shule, akiwa na tabasamu pana usoni mwake alinijibu kuwa yuko tayari kurudi shule na ndipo baba yake akaniomba nimsaidie kumtafutia shule nzuri atakayosoma binti huyu” alisema Shaabani Kaluse, ambaye naungana naye mia kwa mia.
Asifiwe alikuwa na kiu sana ya kusoma, kama ilivyokuwa kwa Kaluse nilipomtembelea, katika mazungumzo alionyesha sana kiu ya kusoma, nilimuahidi kumsaidia atakapukuwa ametulia vizuri na nikampa kitabu kinachoitwa “Mpenzi wa Kweli” nilichokiandika kwa ajili ya vijana hasa wanafunzi kikizungumzia maadili na umuhimu wa kupenda Elimu. Alikipenda sana!.
Nasikitika nilichelewa kupata taarifa, nasikitika sikushiriki wakati wa msiba ila wanablog 53 kwa niaba ya wote walipata kushiriki vizuri msiba huu mzito online, wengine walitumia simu .. wengine wakaandika kwenye blog zao .. Yasinta hakuwa peke yake wakati huu mgumu.
“Dada Naomba uamini kuwa msiba huu sio wakwako peke yako ni msiba wetu sote, yaani familia ya Mzee Ngonyani na ya Mzee Mkundi au pengine na Wanablog wote wa ndani na nje ya nchi.
Ni msiba wetu kwa sababu wengi wetu tulikufahamu wewe kupitia maandishi yako katika Blog ya Maisha na Mafanikio ambapo pia tukaifahamu familia yako na familia ya Mzee Ngonyani” alisema Koero mkundi katika blog yake.
Baada ya kuongea mambo mbali mbali namna ya kumsadia asifiwe, nilipata picha na Mzee Ngonyani.
Binafsi nilitarajia kuhudhuria arobaini ya Asifiwe, lakini nasikitika nimekuwa na wakati mgumu kimajukumu. Hata hivyo leo usiku mdogo wangu anasafiri kuelekea Sweden atanifikishia Salamu zangu kwa Yasinta. Lakini pia nitakapokuwa Songea hivi karibuni nitamtembelea Mzee Ngonyani kumpa pole.

Friday, March 22, 2019

Friday, March 15, 2019

ZILIPENDWA- MOROGORO JAZZ BAND ATT RTD DAR ES SALAAM


NAWATAKIENI MWISHO MWEMA WA JUMA .
UJUMBE WANGU WA LEO:- AMANI, UPENDO NA FURAHA NDIYO VIVWE NGUZO YETU. Kapulya wenu.

Wednesday, March 13, 2019

PALE UNAPOSUBIRI KUSIFIWA!


Unapofanya jambo lolote, fanya tu kama nafsi yako inakubali na inafurahia jambo hilo.
Usifanye jambo kwa kutegemea kusifiwa. Kumbuka usiposifiwa itakuuma sana, lakini ukisifiwa bila kutegemea sifa hiyo, utajisikia furaha sana.

Bila shaka utakubaliana na mimi kuwa Binadamu ni kiumbe anayependa kusifiwa, lakini ikitokea ukawa na kiu kubwa ya kupenda kusifiwa , basi inabidi ujiulize, ni wapi pana kasoro kwenye fikra zako.

Haiyumkini katika malezi yako hukuwahi kusifiwa kamwe na maisha yako yalitawaliwa na kulaumiwa kwingi na kukosolewa, hivyo ukajikuta ukihitaji kukamilishwa.

Haya burudika na shairi hili la Malenga wa Mvita.

UWATAPO HAKI YAKO

Namba nawe mlimwengu, pulikiza matamko
Nikweleze neno langu, uzinduwe bongo lako
Nayo nda M'ngu si yangu, na ayani haya yako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Simama uitete, usivikhofu vituko
Aliyo nayo mwendee, akupe kilicho chako
Akipinga mlemee, mwandame kulla endako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Amkani mulolala,na wenye sikio koko
Isiwe mato kulola,natutizame twendako
Tuwate na kuduwala,usingizi si mashiko
Uwatapo haki yako,utaingiya motoni


Teteya kwa kula hali, usiche misukosuko
Siche wingi wala mali,sabilisha roho yako
Unyonge usikubali, ukaonewa kwa chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni



Siche kifaru na ndovu, wangazidi nguvu zako
Wapempe kwa uwekevu, unusuru haki yako
Siandame wapumbavu,kilicho chako ni chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Cha mtu hakifitiki,kikafungiwa kiliko
Huzuka kikawa hiki,kazana utwae chako
Uwatapo yako haki,fahamu ni dhara kwako
Leo na kwa Mola wako,utaingiya motoni



Fumbuwa unyang'arize, uone duniya yako
Bure sijiangamize,kuangalia wendako
Utatupa upoteze,wende ambapo si pako
Uwatapo haki yako,utaingiya motoni


Kadhalika nako pia,huko ambako sikwako
Huwezi kujitetea,wala huwi na mashiko
Basi iwaze duniya,kwani ya kale hayako
Uwatapo haki yako ,utaingiya motoni


Kadi tamati shairi,sitii la ongezeko
Mwanati iwa tayari, utete haki yako
Unyonge usiukiri,Jifunge ufe kwa chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

Shairi hili limetungwa na Ahmad Nassir wa Malenga wa Mvita

Monday, March 4, 2019

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO IMETIMIZA MIAKA KUMI NA MOJA MWAKA HUU TAREHE 23/2/2019

Hapa ni mwenyewe mamaMaisha na Mfanikio AKA Kapulya
Blog ya Maisha na Mafanikio kama mchezo mwaka huu  yatimiza miaka kumi na  (11). Napenda kuchukua nafasi hii na kusema:- Hii yote ni kutokana na uwepo wenu ulioambatana na upendo pia ushirikiano mzuri mlio nao. Na kubwa zaidi ni kwa familia yangu kwa kuwa bega kwa bega nami. Pia napenda kusema kwa kupitia michango ya wasomaji na wanablog wenzangu nimeweza kijifunza mambo mengi sana. Na ndiyo kwa sababa hii napenda kusema:- AHSANTENI SANA KWA USHIRIKIANO WENU NASEMA TENA KWANI NAAMINI BILA NINYI, NISINGEFIKA HAPA NILIPO LEO. KWA KWELI NAAMINI KUWA SISI SOTE NI NDUGU NA NI WATOTO WA BABA MMOJA. UPENDO NA UMOJA WETU UDUMU DAIMA NA PIA MILELE!!!!!......Halafu la kufurahisha siku niliyoanza kublog ilikuwa ni JUMAMOSI na mwaka huu pia  ni JUMAMOSI... HAYA NIWATAKIENIAMANI NA FURAHA  KWA WOTE MTAKAOPITA HAPA NA WENGINE WOTE.