Showing posts with label elimu. Show all posts
Showing posts with label elimu. Show all posts

Tuesday, July 25, 2017

ELIMU:- WAZAZI TUNAFIKIRI WATOTO WANAPATA ELIMU KUMBE WANAFANYA MIRADI KUINGIZA FEDHA KWENYE MFUKO WA SHULE...

Tutafika kweli kwa mtindo huu? Nimekumbuka mbali sana wakati ule nasoma shule ya msingi, kubeba tofali, kulima mashamba, kukata nyasi, kusomba kuni nk. aise kwa kweli tumehinya sana miaka ile...

Wednesday, October 26, 2016

JE? UNAKUMBUKA KITABU HIKI CHENYE HADITHI YA JUMA NA ROZA?

 Tia maziwa
Tia sukari
Roza ana kiu 
kunywa chai Roza"
AU HII HADITHI YA MWANASESERE

Nimekikumbuka sana hiki kitabu wale wenye umri sawa nami watakuwa pia wanakumbuka ....hivi vitabu siku hizi havipi kabisa ...TUPO PAMOJA...

Thursday, September 8, 2016

ELIMU:- WIZARA YA ELIMU MPO...WANAFUNZI WANASOMA KATIKA WAKATI MGUMU NA WALIMU KUFUNDISHA KATIKA MAZING MAZINGIRA MAGUMU...

Hao ni wanafunzi ambao wanasoma katika wakati Mgumu na kwenye mazingira Magumu Je? Wizara ya Elimu inafikiriaje hili swala?. Ni jabu kwa nchi kama Tanzania ambayo ina umri zaidi ya  Miaka 50 sasa wanafunzi kusomea chini ya miti na walimu kufundisha katika mazingira magumu kama hayo.
Je unategemea wanafunzi hao wataelewa? na Je? hii ndio Elimu Bora au Bora Elimu? kama kawaida palipo na wengi pana Majibu au Mjadala haya  Wasomaji wenzangu karibuni tutafakari kwa pamoja na  ikiwezekana tuchukue hatua........Kapulya wenu....PAMOJA DAIMA

Thursday, June 16, 2016

LEO TUANGALIE METHALI ZETU ZA KISWAHILI....

1. Jirani mwema ni bora, kuliko rafiki.
2. Waarabu wa pemba hujuana kwa vilemba.
3. Usifungue duka ili kupenda kucheka.
4 Ukitaka kusaidiwa nawe, saidia mwenzako.
5. Palipo na moshi pana moto.
6. Kizuri kwako, kibaya kwa mwenzako.
7. Kaa na mwenye tabia njema, utashiriki ya heshima.
8. Baba na mtoto mwanaume, mama na mtoto mwanamke.
Kwa leo ni hizi ila nitaendelea kpekua nyingine  na kama nawe msomaji unazo mbili tatu  usisite kuendeleza orodha...WOTE MNAPENDWA!

Wednesday, May 18, 2016

CHEKA TARATIBU NDUGU YANGU...!!!

Mwalimu aliingia katika darasa moja huko Iringa Vijijini na kuuliza wanafunzi wake. "Nani atanipa jibu la wingi wa Chumvi?" Mwanafunzi mmoja kwa kujiamini akasimama na kujibu, "Fyuvi!" Duh, kasheshe  hiyo.....!

Monday, February 1, 2016

NI MWEZI MPYA: NA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO IMEONA TUANZA HUU MWEZI KIHIVI:- TUANGALIE MISEMO NA METHALI TOKA TANZANIA NA MAANA YAKE....!

1. Anayetembea huokota, anayekaa huvimba tumbo (Kikerewe)
Maana ya methali hii ni kwamba riziki hupatikana kwa kutafutwa siyo kwa kukaa tu na kusubiri. Methali hii hutumika kwa wale wasiojishughulisha na kwa wale wanaojishughulisha na kufanikiwa kwa kudhihirisha ukweli wa juhudi yao

2. Atembea na moto mgongoni (Kibena)
Maana ya methali hii ni kwamba kama wewe si mkarimu, basi ujitegemee mwenyewe kwa kila kitu popote pale utakapokwenda. Methali hii hutumika kama fundisho kwamba hakuna mtu anayeweza kutenda kila jambo bila msaada wa wenzake Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

3. Penye majani makavu mabichi hayawaki (Kizigua na kinguu)
Maana  yake nikuwa penye wazee ni heshima kwa watoto au vijana kuwaachia wazee wakate mashauri; ikiwa vijana watakata shauri mbele ya wazee ni utovu wa adabu. Hutumika kuwaonya watoto wawe na heshima mbele ya wazee hasa katika kusema.

4. Siku hufanana laini hazilingani (Kiha)
Maana ya methali hii ni kuwa kila mtu anayo bahati yake, leo wewe kwsho mwingine. Methali hii hutumika wakati wa kufariji mtu aliyepatwa na maafa.

5. Kichwa cha msitu (Kipare)
Maana yeke, kichwani mwa mtu kuna siri nyingi kama ulivyo msitu mkubwa. Methali hii hutumika wakati wa kuwambia watu kuwa hata kama ukifanya nini, huwezi kuzifahamu siri za mtu. Ni yeye peke yake anayeweza kuzifahamu siri zake mwenyewe. Huweza pia kutumika kwa kuwaonya watu wasiwadharau wengine wanapokuwa kimua kwani huenda wanafikiri mengi kichwani mwao.

6. Kushindwa na kufa ni mapacha (Kimasai)
Ushujaa huheshimiwa sana katika jamii kwa sababu unadumisha ulinzi wa nchi. Ushujaa na ujasiri vikipunguka maadui wa kila aina na dhiki kadha wa kadha husumbua jamii. Mashujaa wakishindwa basi jamii hufadhaika kwani mipango yake yote huvurugika. Methali hii hutumika kama onyo na pia kwa kukaza ujasiri.

7. Leo ni ugali wa kumpigia mbwa kiko cha mkono (Kisukuma)
Maana yake ni kwamba leo tunakula nyama. Mara nyingi Wasukuma hawapendi kumchinja ng`ombe bila sababu maalum. Kwa hivi hutumia mboga za majani kama kitoweo, wapatapo nyama hugawana mikononi wakati wa kula kwa hiyo hutumia kiko cha mkono kumfunza mbwa anayekaribia. Hutumika wakati mtu anapotunukiwa kitu kizuri.

8. Maneno mengi huvunja nyumba (Kichaga)
Maneno mengi nyumbani huvuruga unyumba kwa sababu mwisho wa maneno hayo ni ugomvi uletao mafarakano. Methali hii inatumika kama onyo kwa jamaa, ikiwa kumbusha kwamba maneno mengi ndio chanzo cha kugombana na kukosana.

Naona kwa leo inatosha lakini kama nawe unayo Misemo/methali usisite kuongezea...elimu ni kugawana...TUPO PAMOJA

Thursday, January 7, 2016

USEMI WA LEO KUTOKA KWA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO....!

Elimu sio maandalizi ya maisha- Isipokuwa ELIMU ndiyo  MAISHA.
TUPO PAMOJA!

Tuesday, May 19, 2015

PICHA KUTOKA KITABU CHA DARASA 5 TUJIFUNZE LUGHA YETU! KWA DARASA LA NNE...

Na kitabu chenyewe kinaonekana hivi kwa nje....Picha ya kwanza ni  hadithi ya jogoo aliyesema, ya pili ni Sadiki na Sikiri, ya tatu nimesahau  sijui kuna anayekumbuka anisaidie?.ya nne ni Sizitaki mbichi hizi

Thursday, April 23, 2015

DUH KAAAZI KWELIKWELI HAPA SIJUI MWALIMU ATAJIBU NINI???

Nimeipenda hii  angalia mwal. jinsi jasho linavyomtoka kwa kutafuta jibu. Watoto huwa wakweli sana na hawaoni aibu kuuliza swali....KILA LA KHERI.

Monday, February 2, 2015

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO INAPENDA KUMPONGEZA KAKA SAMWEL MBOGO "SAM" KWA KUFANYA GRADUATION

Ilikuwa ijumaa tarehe 30/1/2015, Ndugu kaka yetu Samwel Mbogo wengi tunamfahamu kwa jina la kaka S au Sam. Alifanya graduation yake katika kanisa CENTERBURY CRISTIAN CHURCH CATHEDRAL university (CCCU  huko London. Amepata Master degree ya phychotherapy. Ni Arts Therapy. NAMI NAPENDA KUTANGULIA KUMPA HONGERA SANA . 

Thursday, January 29, 2015

TUSISAHAU METHELI ZETU:

1. Njaa ni adui, hata mchawi yaua.
2. Haki ya nyani kuona fahari kwa mkia wake
3. Heri yao wazee kujifunga kwa mshipi tumboni.
4. Yu mcheshi machoni moyoni kuna mengine.
5. Binadamu ujikaze, Mungu atakusaidia.
6. Ee mtoto utakutana na watu katili.
7. Yakiteguka mapaja choo hutoka ovyo.
8. Mtoto wa simba sharti naye awe simba.
9. Yu ndugu machoni
10. Fuata maji yanakokwenda.
Methali hizi nimezipata katika kitabu cha SIASA HAPO KALE  ni methali katika hadithi za kingoni. Ambazo zimetafsiriwa kwa kiswahili. Na kwa kingoni nimeweka kwenye blog ya vangoni.blogspot.com.

Thursday, August 21, 2014

KISWAHILI:- METHALI ZETU!!

1. Usimwamshe aliyelala, utalala wewe.
2. Usipoziba ufa utajenga ukuta.
3. Usitukane mkunga na uzazi bado.
4. Uso mzuri hauhitaji urembo.
5. Vikombe vikaka pamoja havina budi kugombana.
6. Waraka ni nusu ya kuonana.
7. Wagombanao ndio wapatanao.
8. Usiache mbachao kwa msala upitao.
9. Mchumia juani, hula kivulini.
10. Mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe.
Ni hizi tu kwa leo ila nawe kama una mojo, mbili tatu usisite kuweka hapa eilimu ni kugawana. Haya siku na kazi njema . Wenu Kapulya:-)

Wednesday, July 9, 2014

LEO TUANGALIE BAADHI YA MISEMO NA METHALI TOKA TANZANIA

1. Mtoto wa kwale hapotezi njia yake (Kibena)
2.  Mtoto wa nyoka hukua na sumu yake (Kisambaa)
3. Mtoza ushuru sokoni huvumilia (Kichaga)
4. Mtu hodari husifiwa na watu (Kizigua na kinguu)
5. Mtu si sikio (Kiiraqw)
6. Muwa mmoja haujazi mtungi (Kipare)
7. mvua ya vuli imeanza (Kinyakyusa)
8. Mwanamke ni kambalemamba huamshwa na mkuki  (Kikerewe)
9. Ukiona mishale nyanyo ziko nyuma (Kimasai)
10. Kucheka hakuna majira, chenya majira ni kilimo (Kiha)
11. Tumbo la nguruwe halipasuliwi mbele ya watoto (Kisukuma)
12. Wazee walimtoa nyoka katika pua ya mwene (Kifipa)
KAMA NAWE UNA CHA NYONGEA KARIBU SANA SI MNAJUA  TUPO PAMOJA.....JUMATANO NJEMA SANA KWA WOTE..PANAPO MAJALIWA .  KAPULYA

Thursday, July 3, 2014

BADO TUNA MWENDO MREFU......

Nimeyatamani hayo maembe mno...ila zaidi ni kwamba hawa watoto ilibidi wawe darasani lakini wapo barabarani kutafuta maisha. Hapo ni barabara ya Tunduru Namtumbo…kijiji baada ya Namwinyu!.....picha kwa idhini ya kaka Chacha. Basi niwatakieni siku njema wote najua tupo wengi tunaotamani haya maembe:-)

Monday, May 19, 2014

JUMATATU YA LEO TUANZE NA CHANGAMOTO HII KUHUSU NCHI ZETU ZA AFRIKA!!!!

SWALI:- Je? ni nchi gani/zipi  haina/hazini  herufi A katika bara la Afrika?
NAWATAKIA KILA LA KHERI. PAMOJA DAIMA!!!

Wednesday, May 14, 2014

NI MUDA MREFU SASA UMEPITA :- METHALI ZETU....

Nimeona usipite muda zaidi bila kuzikumbuka METHALI  zetu basi ungana nami  katika hizi chache nilizozikumbuka leo:-

1. Aninyimaye mbaazi, kanipunguzua mashuzi
2. Biashara haigombi.
3. Chanda chema huvikwa pete.
4. Dua la kuku halimpati mwewe.
5. Fimbo ya mbali haiui nyoka.
6. Kikulacho ki nguoni mwako.
7. Kosa moja haliachi mke.
8. Lisilokuwepo moyoni halipo machoni.
9. Mapenzi ni kikohozi hayaweza kufichika.
10. Mficha uchi hazai.
BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO INAWATAKIENI WOTE SIKU NJEMA SANA NA WOTE MNAPENDWA:-)

Saturday, May 10, 2014

TAHADHARI :UGOMVI UNAATHIRI AFYA YAKO!!!


 
Wanaume wasio na ajira wako katika hatari ya kuathirika zaidi kutokana na ugomvi
 
Ugomvi wa mara kwa mara baina ya wapenzi, marafiki ama hata jamii unaongeza hatari ya kufa kwa watu wenye umri wa makamo. Haya ni kwa mujibu wa watafiti nchini Denmark.
Watafiti wamesema kuwa wanaume na wale ambao hawana kazi wako katika hatari Zaidi.
 
Utafiti huo katika jarida la 'Epidemiology and Community Health', unasema kuwa shughuli za kukidhi matakwa na mahitaji ya jamii pia zimehusishwa na idadi kubwa ya vifo vya mapema.
Pia kulingana na utafiti huo utu wa mtu na uwezo wa mtu binafsi kukabiliana na dhiki ilichangia katika matokeo ya utafiti huo.
Ingawa watafiti hao kutoka chuo kikuu cha Copenhagen waliweza kupata uhusiano uliopo kati ya vifo vya mapema na kugombana, na kuwa ugomvi uliongeza hatari ya vifo vya mapema mara tatu, hawakuweza kuelezea kikamilifu sababu haswa ya hali hiyo.
Utafiti wa hapo awali ulionyesha kuwa watu wenye wasiwasi mwingi na mahitaji mengi kutoka kwa wapenzi wao na watoto, pamoja na wale wanao gombana mara kwa mara na jamaa wao, wamo katika hatari kubwa zaidi ya kuugua magonjwa ya moyo na kiharusi.
Tafiti za hapo awali pia zaonyesha kuwa utangamano mwema na watu pamoja na marafiki wengi ina athari chanya katika afya, huku utu kwa kiasi kikubwa ukiamua jinsi mtu hupokea na kuguswa na hali za kijamii pamoja na mahusiano.

Wapendanao hawapaswi kugombana

Kumsumbua mpenzi wako pia kunahatarisha afya
Katika utafiti huu, watafiti walisema kuwa athari za kisaikolojia zinazosababishwa na dhiki, kama vile shinikizo la damu na ongezeko la athari ya magonjwa ya moyo, ndizo hasa zinaweza kueleza athari ya ongezeko la vifo vya mapema.
Utafiti umeonyesha kuwa wanaume wanapokabiliwa na hali za dhiki kwa kuongeza homoni inayokabiliana na hali ya dhiki na wasiwasi, jambo ambalo linazidisha athari ya kiafya.
Utafiti huo ulihusisha watu 9,875 wake kwa waume wenye umri wa kati ya miaka 36 na 52 na ulitumiwa kuchunguza uhusiano uliopo baina ya hali ngumu ya uhusiano wa kijamii na vifo vya mapema.
Wote walikuwa wameshiriki katika Utafiti ‘Denmark Longitudinal’ kuhusu Ajira, ukosefu wa ajira na afya , kuanzia mwaka wa 2000.
Utafiti uligundua kuwa wasiwasi wa mara kwa mara au mahitaji yanayotokana na wapenzi na watoto ulihusishwa na ongezeko la kufikia 50%- 100% la vifo vya mapema.
Ukosefu wa ajira ulionekana kuongeza athari hasi za uhusiano mgumu wa kijamii. Wale ambao hawako kazini wameonekana kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kifo kutokana na jambo lolote kinyume na wale walio na kazi.
wanaume pia wako katika hatari zaidi kutokana na mahitaji na wasiwasi unaotokana na wapenzi wao wa kike , huku wakiwa katika hatari kubwa zaidi ya kifo zaidi ya ile ambayo kwa kawaida imehusishwa na kuwa mwanamume.
Dakta Rikke Lund, wa kitengo cha afya ya umma katika chuo kikuu cha Copenhagen amesema kuwa wasiwasi na ugomvi ni sehemu ya maisha. Lakini akaongeza kuwa watu ambao wanakuwa na migogoro mara kwa mara wako katika hatari zaidi lakini wanaweza wakasaidiwa.
CHANZO: BBC.

Tuesday, May 6, 2014

UKOSAPO NENO JEMA, KHERI UJINYAMAZIE.

Nakuasa usikie, usemaji ni karama,
Maneno usirukie, sema mambo kwa kupima,
Utamkapo ujue, neno halirudi nyuma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Kheri ujinyamazie, ovu huleta khasama,
Majuto yasikujia, “Laiti nisingesema”,
Mtu baa azuae, Motowe utamchoma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Ni wengi wajiponzao, kwa zao mbovu kalima,
Heshima waitakao, waseme usemi mwema,
Wale waumbukanao, ni kwa ndimi kuparama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Watazame wakuao, dunia kuwatazama,
Ni wale wapimiao, kabla ya kuyasema,
Na kimya wanyamazao, wakosapo neno jema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Neno huenda likuwe,lizidi hata vilima,
Mambo mawi liyazue, akili zende mrama,
Au mema yatukie, liwapo neno la wema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Funzo walitufunzao, wazungupule wa zama
Zama za kale na leo, walokimcha Karima,
Yawe mema tusemao, tusije zusha zahama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Mola akubarikie, na ambaye akusoma,
Na furaha ututie, uwe ni diwani njema,
Mema utuhadithie, wana kwa watu wazima,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Shairi hili limetungwa na Mshairi maarufu Afrika Mashariki Bwana Amri Abedi, nami nimeona sio vibaya kulirejea ili tujifunze pamoja.................

Monday, February 3, 2014

MSAADA WA VITENDAWILI NA MAANA ZAKE!!

Nimetumiwa ujumbe huu lakini kwa bahati mbaya hivi vitandawili kwangu vimekuwa vigumu kidogo kwa hiyo naomba ndugu zangu tusaidiane maana palipona wengi hapaharibiki kitu..Natunguliza shukrani zangu za dhati kwenu. Na ujumbe wenyewe unasema hivi:- karibuni!!
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Dada Yasinta, habari za leo? Samahani naomba msaada wako kwa vitendawili vifuatavyo:
1) Wanastarehe darini.
2) Sina dada wala kaka, lakini baba wa huyu jamaa ni mtoto wa baba yangu.
3) Nguo ivaliwayo kila siku isiyoingiwa na chawa.
4) Ini la ng'ombe huliwa hata na walio mbali.
5) Chatembea na hakijapata kupumzika hata nukta moja.
6) Mvua kidogo ng'ombe kaoga kichwa.
7) Njoo hapa nije hapo.
8) Msitu ambao haulii hondohondo.
9) Aliwa, yuala, ala, aliwa.
10) Ajenga ingawa hana mikono.
JUMATATU IWE NJEMA KWA WOTE!

Tuesday, January 7, 2014

NI JUMANNE YA KWANZA YA MWAKA HUU 2014 NAMI NIMEONA TUIANZA KWA MTINDO HUU:- METHALI ZETU!!! UNAZIKUMBUKA HIZI?:-)

1. Asiyekuwepo machoni, na moyoni hayupo.
2. Bendera hufuata upepo.
3. Chururu- si ndo, ndo, ndo.
4. Dua tupu haliachi kuvuma.
5. Fuata nyuki ule asali.
6. Hakuna msiba usiokuwa na mwenziwe
7. Heri kufa macho kuliko kufa moyo.
8. Ikiwa hujui kufa, tazama kaburi,
9. Jogoo la shamba haliwiki mjini.
10. Kimya kingi kina mshindo mkuu.
SIKU YAKO IWE NJEMA SANA NAWE KAMA UNA METHALI UIKUMBUKAYO KARIBU KUISEMA/ANDIKA.