Showing posts with label kumbukumbu maisha. Show all posts
Showing posts with label kumbukumbu maisha. Show all posts

Tuesday, August 28, 2012

HAPA WENGI TUNAKUMBUKA MALEZI YA WATOTO!!


Katika malezi/makuzi watu tumetoka mbali, huyu binti hapa ananikumbusha mbali sana.Wazazi wanaondoka asubuhi huku wakitegeme binti mimi/huyu afanye kazi ya kuchota maji. Na hapo labda sio ndoo moja tu pipa zima. Na hapo hapo amtunze mdogo wake. Na labda kuchochea maharage pia. Hali hii kwa sasa hakuna kabisa maisha yamebadilika kabisa ndiyo kwanza utakuta mtoto anamtuma mzazi wake. Maisha siku hizi yamekuwa  watoto na TV, Komputa, simu nk. Hata kumwona mtoto siku hizi anasoma kitabu ni mara chache sana. Ndiyo maana  sisi tuliolelewa  katika malezi ya aina hii kama huyu binti inatupasa tuendeleza kwa kuwahimiza  watoto wetu waweze kufanya hivyo hata kama ni kidogo. Polepole ni mwendo...Hata hivyo najua hali hii ya watoto kusaidia kazi za nyumbani vijijini bado inaendelea. Binafsi niitazamapo picha hii najiona ni kama mimi...na naweza nikasema natamani niwe tena kama huyu binti...Je? umewahi kuifanya kazi hii? au labda kuchunga mbuzi na ngómbe kama watoto hawa hapa....


....na hapa ndipo watu wanapojifunza maisha  ni nini/ hawa ndiyo  wataweza kuyamudu maisha yoyote yale na pia kujua ugumu na uzuri wa maisha ....JUMANNE NJEMA!!!!

Monday, March 15, 2010

Pendo langu kwako wewe

Uketi chini mpenzi, ya moyoni nikwambie,
Daima nitakuenzi, uhai uniishie,
Hutoipata simanzi, nataka ufurahie,
Pendo langu kwako wewe, halipimwi kwa mizani.

Halipimwi kwa mizani, uzitowe wazidia,
Pendo linayo thamani, hakuna cha kufikia,
Hata kwa mizani gani, huwezi kulipimia,
Pendo langu kwako wewe, hutolikuta dukani.

Hutolikuta dukani, ati labda lauzwa,
Pendo li ndani moyoni, kwalo pendo nimemezwa,
Kwani halina kifani, kwa kitu likaigizwa,
Pendo langu kwako wewe, kwa mwingine hulikuti.

Kwa mwingine hulikuti, pendo akakupatia,
Nina pendo lenye dhati, ya moyo uloridhia,
Pendo liso na wakati, daima kufurahia,
Pendo langu kwako wewe, ling'aalo kama nyota.

Ling'aalo kama nyota, maishani kuwa nuru,
Pendo raha kulipata, kufaidi kwa uhuru,
Pendo chozi kunifuta, kwa nini nisishukuru,
Pendo langu kwako wewe, liishi zote dawamu.

Liishi zote dawamu, linipe raha ya moyo,
Pendo hili na lidumu, kwa furaha linipayo,
Pendo hili mbona tamu, kwa tamu niipatayo,
Pendo langu kwako wewe, kamwe halina mipaka.

Kamwe halina mipaka, pendo mali yako yote,
Kukupenda sitochoka, pendo ulimi na mate,
Juwa kwangu umefika, wala us'ende kokote,
Pendo langu kwako wewe, waache waone wivu.

Waache waone wivu, kwa pendo ninalokupa,
Sisi tule zetu mbivu, pendo lizidi nenepa,
Kwako niwe msikivu, sitowaza kukutupa,
Pendo langu kwako wewe, wacha lizidi shamiri.

Wacha lizidi shamiri, wacha pendo na ling'ae,
Kukupata ni fahari, wengine uwakatae,
Pendo kwako li mahiri, unifae nikufae,
Pendo langu kwako wewe, mbona linanipa raha.

Mbona linanipa raha, ni bahati sana mie,
Pendo lajaa furaha, wacha nilifurahie,
Kwa pendo nipate siha, nishibe na nichanue,
Pendo langu kwako wewe, ni mwisho wa mambo yote.


Nimelipenda shairi hili na nimeona sio vibaya kama nikiliweka hapa kuwakilisha ujumbe huu. Nimelipata toka kwa http://fadhilimshairi.blogspot.com/. Haya tufurahi pamoja.