Showing posts with label mahitaji. Show all posts
Showing posts with label mahitaji. Show all posts

Tuesday, March 3, 2009

MWANAUME NA MWANAMKE MAHITAJI YAO.SEHEMU YA II

a) Usalama: Ndiyo hali ya kujisikia kuwa huna hofu yoyote au wasiwasi. Wakati ambapo hakuna kitu cha kutisha au cha kuvuruga akili. Najisikia salama hatari ikiwa mbali, maadui hawapo nami nimeshinda matatizo.
Yapo mambo mengi ambayo yanaweza kutuondolea usalama katika mioyo yetu. Ajali yaweza kutokea, vita, magonjwa yaweza kutupata; watu pia wanaweza kutudhuru, kuiba mali yetu na hata kuhatarisha maisha yetu. Hofu ipo ndani yetu kwa namna nyingi. Hofu ya mambo tusiyoyajua, hasa katika kutafuta kazi, au tukiwa ugenini, tubadilishapo mtindo wa maisha.

Ingawa yote hayo yapo, bado tunajua usalama. Kuna usalama wa mtoto kifuani kwa mama yake. Usalama wa mtoto ashikapo mkono wa baba yake. Usalama wa rafiki ambaye anajua kwamba kwa vyo vyote rafiki yake yuko tayari kumsaidia. Usalama wa mwanamke aliye na hakika juu ya mapendo ya mumewe. Usalama huu ndio msingi wa haja zetu na usalama unatakiwa hasa katika ndoa. Haja hiyo ya usalama ikitoshelezwa, amani kubwa na utulivu wa moyo hupatikana.

b)Kukubalika: Haja yetu ya pili yaitwa kukubalika. Ni haja ambayo wewe na mimi tunaijua sana. Ni ile hali ya kukubalika na watu kama tulivyo, kueleweka nao, kpokewa jinsi tulivyo na tunavyojitahidi kuwa. Kila mmoja wetu anahitaji sana mtu mwingine wa kumsindikiza, kufurahi na kuhuzunika pamoja naye. Mtu ambaye anajua matatizo na matakwa yetu; pia mwenye kuelewa tunayohofia.
Jaribu kufikiri kidogo maisha yangalikuwa ya namna gani kama hatingalikuwa na mtu ye yote wa kumkimbilia wakati wa shida, au mtu wa kutupongeza na kututia moyo.

Katika ndoa mwezi wako Mume/mke, anatazamia kupata hayo kutoka kwako. Mume wako ama mkeo anataka kuhakikishiwa kwamba kwa upande wako hatapata masharti yo yote ya kumkubali; hii ina maana kwamba unamkubali na kumpokea kwa furaha jinsi alivyo nawe unamjulisha jambo hili.

Hii haina maana kwamba huwezi kuona kasoro na udhaifu alio nao mwenzako. Maana yake ni kwamba unakuwa tayari kumwambia: “Najua ya kwamba wewe si mkamilifu, lakini nakupenda jinsi ulivyo, na pia nakubali ujue kuwa wala mimi si mtu mkamilifu. Hata hivyo nina hakika kuwa unanipenda”. Unapokuwepo ukubaliano wa namna hii kila mmoja huwa na imani kubwa na mwnziye na kujiamini pia.

c) Kuthaminika: Ndilo hitaji la tatu ndani mwetu. Je, tulieleweje hitaji hilo? Unaweza kupata mwanga kidogo juu ya jambo hili kama ukikumbuka jinsi unavyojisikia wakati umekwisha fanya kila juhudi na kujisumbua ili upate kumfurahisha mwingine. Halafu mtu huyu unayetaka kumfurahisha hajali wala hatambui kwamba umefanya kitu kwa ajili yake. Katika hali hii utajisikia kama umekosa kitu fulani, na kitu chenyewe ni kuthaminika.

d) Kujikamilisha binafsi: Hiki ndicho kilele cha mahitaji yote ya hisi. Ni ile hali ya kujisikia kitu cha maana. Kujisikia kwamba nimetumia vipaji vyangu vyote kikamilifu. Nimetumia nguvu zangu zote za mwili, akili na moyo, na kweli nimefaulu kuwafurahisha wengine. Kwa kufanya hivi najiona mtu zaidi.
Si lazima kufanya mambo makubwa. Kwa mwanamke yaweza kuwa kazi ya kudarizi au kuremba kwa ushanga, kupamba nyumba kwa namna ya pekee, kutengeneza nguo za watoto zitakazomletea sifa ya wengine. Kwa mwanamume yaweza kuwa kuchukua kozi kwa njia ya posta ili kupata kazi nzuri zaidi au mshahara mkubwa zaidi.

Katika kufanya mambo haya kila mmoja anahitaji mwenzake, mume au mke. Kwa sababu kule kujikamilisha binafsi, mara nyingi, huhitaji msaada wa mwenzio. Mapendo yake yatakudhihirishia vipaji fulani ambavyo hukuvijua kwanza, na mapendo haya haya yatakupa nguvu ya kuviendeleza. Kwa pamoja utaweza kujijenga. Kwa pamoja pia mtayatosheleza mahitaji haya yaliyomo ndani ya moyo wa kila mwanamume na kila mwanamke.

Mahitaji ya kiroho
Aina ya mwisho ya mahitaji ni yale ya kiroho. Je, nina maana gani kusema hivi? Ninataka kusema, kuhitaji kitu kilicho kikubwa zaidi kuliko vile vya kibinadamu. Ni kuhitaji heri iliyo kubwa zaidi ya ile ya kibinadamu, kuhitaji amani iliyo kuu kupita moyo wa binadamu, kuhitaji Mungu Mwenyewe.

Saturday, February 28, 2009

NGOJA LEO TUANGALIE:- MWANAUME NA MWANAMKE MAHITAJI YAO.

Katika maisha yetu ya kila siku, mara nyingi twasikia:- ”nahitaji nguo mpya” au ”nahitaji kutengeneza paa la nyumba yangu”. Au, “Nahitaji fedha”; “Nahitaji chakula”. Neno “hitaji” twalitumia hata katika mambo mengi. Baada ya kuumwa na mbu nahitaji kujikuna ili kupunguza kuwasha. Au ninapokuwa na hofu najisikia kama nahitaji mtu wa kunisaidia.

Aina mbalimbali za mahitaji:-
Sisi wanadamu tuna mahitaji ya aina nyingi. Mengine siyo makubwa. Mara mahitaji hayo yatimizwapo, tunapata furaha kwa muda mfupi na kuonekana tumetosheka. Mahitaji mengine ni muhimu na ya msingi katika maumbile yetu. Ni ya lazima kwa maisha yetu. Mahitaji haya tukiyapata, twasikia raha. Yasipotimizwa tunakuwa na udhaifu, huzuni na umaskini. Sio umaskini wa fedha bali wa afya, au ukosefu wa raha na amani.

Sasa tuone mahitaji yaliyo muhimu kwa sisi wanadamu wote. Mahitaji haya anayo kila mmoja – mwanamume na mwanamkw - ingawa kila mmoja anayadhihirisha kwa njia tofauti. Mahitaji haya yaweza kugawanyika katika sehemu tatu:- mahitaji ya kimwili, mahitaji ya kimoyo (hisi) na mahitaji ya kiroho.

Mahitaji ya Kimwili
Kwanza kabisa, kuna yale mahaitaji muhimu ya mwili:- kupumua hewa, kula, kunywa, kupumzika na mahali pa kukaa. Haya ni mambo muhimu na ni lazima mtu ayapate. Tunajua yanayompata mtu aliyekosa hewa. Ikiwa chembechembe za ubongo wake zinakosa hewa safi, anaweza kuanza kusikia kizunguzungu, baadaye kuzimia na kufa.

Tunajua pia kwamba ili tuishi ni lazima tule na tunywe. Ni watu wachache sana wawezao kustahimili njaa kwa muda wa siku 10. Usingizi na kupumzisha mwili ni jambo muhimu pia. Mwili wetu unahitaji kujenga nguvu mpya kwa njia ya mapumziko. Tunahitaji nguvu mpya kuendelea na shughuli zetu za kawaida.

Kati ya mahitaji haya ya mwili kuna lingine, nalo ni lile lililomo katika maumbile yetu, yaani katika utu ume au utu uke. Ndiyo haja ya kufanya mapenzi. Tunaelewa kwamba jambo hili ni la msingi katika maumbile yetu. Ni wazi kwamba haja hiyo hutaka kujidhihirisha. Mwanaume atafikiri kama mwanaume na atafanya kazi kama alivyo: atapenda kama mwanaume. Hali kadhalika mwanamke. Wakati mwingine hamu ya kumhitaji mwanaume au mwanamke inaonyeshwa katika tendo la kukaribiana; lakini hii si njia tu pekee ya kuonyesha mapenzi.
Mahitaji ya kiroho (Hisi)
Lipo kundi la pili la mahitaji tungeweza kuyaita mahitaji ya ndani, mahitaji ya moyoni. Mahitaji haya ni yale ya hisi. Watu waliojifunza elimu ya akili na moyo wa binadamu wanatambua kwamba kuna mambo manne ambayo kila mmoja wetu anahitaji:- Usalama – Kukubalika katika jumuiya – Kuthaminika – na Kujikamilisha binafsi: Tutaangalia kwa undani kila moja si muda mrefu:-
.