Showing posts with label maisha. Show all posts
Showing posts with label maisha. Show all posts

Friday, December 27, 2019

SALAMU/BARUA KUTOKA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO:- SHUKRANI KWA WOTE!!!

Habari zenu jamani!!
Zimebakia siku chache tu kuumaliza mwaka huu 2019 na kuingia katika mwaka mpya 2020. Hakika miaka inayoyoma na watu tunazidi kuzeeka. Ninachotaka kusema ni kwamba, blog ya MAISHA NA MAFANIKIO inapenda kuwashukuru wanablog wenzake wote, wasomaji wote na watembeleaji wote kwa ushirikiano mzuri tulioonyeshana.
Najua katika maisha watu wote hawawezi kuwa sawa yaani kimawazo. Lakini katika hizi blog zetu kwa asilimia kubwa imekuwa ni changamoto kwetu. Tumekuwa hatupendi kupoteana, mara mmoja wetu anapokuwa kimya kwa muda basi wengine tunakuwa hatuna raha tunachukua hatua ya kumtafuta. Hii yote inaonyesha ni jinsi gani ukaribu wa wanaBLOG sisi tu/ulivyo, hakika najivuna sana kwa uwepo wenu na kwa hili napenda kusema SISI SOTE NI NDUGU. NA PIA NAPENDA KUWATAKIENI WOTE KILA DOGO NA PIA KILA KUBWA MTENDALO LIWE JEMA. NA MWAKA 2020 UWE WENYE MAFANIKIO. KAMA KUNA KITU ULIAHIDI KUFANYA MWAKA HUU BASI JITAHIDI UFANYA KABLA HAUJAISHA. KWANI KUMBUKA HAKUNA KISICHOWEZEKANA. PAMOJA DAIMA. KAPULYA WENU!!!!

Tuesday, March 20, 2018

KUMBUKUMBU.....NIMEIPENDA HII PICHA NA NIMEONA IWE PCHA YA WIKI HII

UJUMBE:- JANA NI HISTORIA. KESHO NI MIUJIZA  NA LEO NI ZAWADI.
NAPENDA KUWATAKIENI SIKU YA LEO IWE NJEMA SANA, FURAHA NA AMANIPIA. KAPULYA WENU....

Thursday, February 1, 2018

USIMUHUKUMU MTU YEYOTE ...MAANA HUYAJUI MAISHA YAKE

```Daktari aliingia hospitalini kwa haraka sana baada ya kuitwa kwa shughuli ya Upasuaji wa haraka, alipokea simu haraka, na kuvaa nguo za kazi na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji.

Wakati akielekea kwenye chumba cha upasuaji alimkuta baba wa mtoto anazunguka huku na huku karibu na chumba hicho akimsubiria Daktari. 

Baada ya kumuona tu, baba mtoto akapayuka: “ Kwanini umechelewa kuja? Hufahamu kama maisha ya mtoto wangu yapo hatarini? Hivi unayajua majukumu yako?”

Yule Daktari alitabasamu na kumwambia: “ Samahani sana, Sikuwa karibu na Hospitali na nimejitahidi kuja kwa haraka sana baada ya kupokea simu kutoka hapa hospitalini….. Na kwa kuwa nimeshafika ningekuomba upunguze jazba na hasira ili nifanye shughuli yangu” “Punguza hasira?! 

Hivi ingekuwaje kama mwanao ndiye angekuwa chumba cha upasuaji sasa hivi, ungeweza kupunguza hasira? Kama mwanao ndiye angekuwa anakufa sasa hivi ungefanyaje?” Yule Baba aliongea kwa hasira sana.

Yule Daktari alitabasamu tena na kumjibu: “Daktari hawezi kurefusha maisha ya Binadamu. Nenda katulie na umuombee mwanao, sisi tutajitahidi kadri kwa uwezo tulionao kwa Baraka za Mwenyezi Mungu”

 “Kutoa Ushauri kwa vitu visivyo wahusu ni rahisi sana” Alinong’ona yule Baba mwenye mtoto.

Upasuaji ulifanyika kwa masaa kadhaa mara tu baada ya kumalizika Daktari alitoka akiwa ana furaha,  “Asante Mungu! Mtoto wako amepona!” Kama una swali lolote utamuuliza Nurse!!” Bila ya kumsubiri Baba Mwenye mtoto kujibu chochote aliondoka kwa haraka kwenye eneo la upasuaji. 

“ Kwa nini ni mkorofi sana huyu Daktari? Yaani hawezi hata kusubiri kidogo nimuulize maendeleo ya mwanangu” Baba wa mtoto alimjadili akiwa na nurse baada ya Daktar kuondoka.

Nurse akamjibu, huku akitokwa na machozi:
“Mtoto wake alifariki jana kwenye ajali ya gari, alikuwa katika mazishi ya mtoto wake wakati tunampigia simu aje Hospitali kwa ajili ya upasuaji wa mtoto wako. Amefanikiwa kuyaokoa maisha ya mtoto wako, kwa hiyo ameondoka kuwahi mazishi ya mtoto wake.”

HEKIMA:
1. “USIMHUKUMU MTU YEYOTE…. SABABU HUYAJUI MAISHA YAKE NA KIPI
     KILICHOMKUTA KWENYE MAISHA YAKE.

2. “TENDA WEMA KADRI UWEZAVYO BILA YA KUJALI HALI ULIYONAYO.```
Nimeitoa mtandaoni nimeiweka hapa kibarazani kwa vile imeniguse sana na pia iwe fundisho kwa wengi.

Saturday, September 2, 2017

UJUMBE WA LEO:- KILA AITAZAMAYE KESHO YAMPASA KWANZA AIMALIZE LEO:- ACHA NIKUDOKEZE JUU YA MAISHA YA LEO...

1.Ishi kwa UPENDO usio na Unafiki.
2.Ishi na FURAHA isiyo na mipaka.
3.Ishi kwa AMANI na kila Mtu.  
4.Usiweke MAMBO yako wazi kwa kila mtu kwani binadam hatufanani.
5.Jiheshimu kwani HESHIMA yako inatokana na jinsi ulivyo.
6.Kuwa MVUMILIVU katika kila jambo ili kufikia mafanikio.
7.Weka MSAMAHA mbele kwa kila anaekukosea na unaemkosea.
8.MISUKOSUKO ni sehemu ya maisha na ndio hatua ya kuvuka ili kufanikiwa katika MAISHA hivyo usikate tamaa.
9.Omba na kumshkuru MWENYEZI MUNGU kwa kila jambo kwani yeye ndiye anayekupa UHAI.
TUMALIZIE NA WIMBO HUU ....

Sunday, July 9, 2017

UJUMBE WA JUMAPILI YA LEO...KUTOKA KWA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO

Sisi binadamu daima tunafanya kazi kwa kutumaini siku ya kesho itakuwa  bora lakini wakati kesho inafika badala ya kufurahi, basi sisi tuanaanza kunafikiria kesho tena itakuwa bora?  Hebu tuwe na siku ya leo sio kila wakati kufikiria ubora  wa kesho. MAISHA NI MAFUPI UPATAPO WASAA FURAHIA....JUMAPILI NJEMA

Wednesday, June 28, 2017

KUMBUKUMBU : - UNAKUMBUKA HADITHI HII MANDAWA NA MANENGE....

Hapo  zamani palikuwa na mtu na mkewe, mtu huyo aliitwa Manenge na mkewe aliitwa Mandawa. Siku hizo chakula kizuri kilikuwa maziwa na nyama.
Lakini vyakula hivi vilipatikana kwa shida shida. Maziwa yaliweza kupatikana tu kama mtu alikuwa na ngòmbe. Na nyama  iliweza kupatikana tu kama mtu alipewa zawadi  na jamaa yake au alinunua. JE  ? UNAIKUMBUKA HADITHI HII?

Wednesday, May 24, 2017

UJUMBE WA WIKI HII: MAISHA HAYAMTAMBULISHI MTU KWA WATU....

Maisha hayamtambulishi mtu kwa watu atakaokukutana nao. Kuna wakati, maisha yaweza kukukutanisha na watu ambao uliwahitaji/unawahitaji kukutana nao ili wakupe msaada, ili wakuumize, ili wakuongoze, ili wakuache mpweke, ili wakupende na ili wakupe/wakutie nguvu katika hatua ya  kukuimarisha ili uwe mtu imara katika maisha yako.....TUPO PAMOJA!

Monday, May 15, 2017

WANAUME NAO HUNYANYASIKA KIJINSIA MAKAZINI TOFAUTI NA INAVYODHANIWA !

Kama uki google kwa picha ‘Unyanyasaji wa kijinsia makazini’ utashangaa, kwani takribani asilimia 90 ya mapicha picha utakayoyaona yanawaonyesha wanawake wakifanyiwa unyanyasaji wa kijinsia na wanaume.

Lakini ukweli ambao hausemwi ni kwamba wanawake ni wachokozi zaidi ya mara 9 kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo ya kazi. Najua kuna baadhi ya wanawake wanaweza kutokwa na povu lakini huo ndiyo ukweli wenyewe.

Kwa kawaida unyanyasaji wa kijinsia ni kitendo cha kumchokonoa mtu wa jinsia tofauti au hata jinsia moja kwa kumfanyia vitendo au ishara za kimapenzi kwa nia ya kumtega, kumshawishi au kumlazimisha kufanya naye mapenzi.

Na hii inaweza kufanywa na mtu mwenye madaraka mahali pa kazi dhidi ya walio chini yake au kati ya wafanyakazi wenyewe kwa wenyewe. Na tatizo hili dhidi ya wanaume limekuwa likikua siku hadi siku katika maeneo ya kazi hapa nchini ni vile tu halisemwi kama linavyosemwa pale muathirika anapokuwa ni wa jinsia ya kike.

Wanawake wamekuwa wakijificha kwenye kichaka cha kujiona kama vile wao ndiyo waathirika wakubwa wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia mahali pa kazi wakati wanaume kwa upande wao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya namna hiyo lakini wamebaki wakiumia ndani kwa ndani kwa sababu hawana pa kusemea.

Ni nani asiyejua kwamba wanawake licha ya kuvaa mavazi yenye kuacha sehemu ya miili yao ya faragha wazi lakini pia mikao yao isiyo ya staha inawaweka baadhi ya wanaume katika wakati mgumu na kushindwa kufanya kazi. Hilo linaweza likaonekana si tatizo, lakini je vipi kuhusu mazungumzo yenye kushawishi ngono yanayofanywa na wananawake au vitendo vya kuwashika wanaume sehemu zao za siri ili kupima maumbile yao, vitendo vya aina hii viitweje kama siyo unyanyasaji wa kijinsia. Je vitendo vya kuwatomasa tomasa wanaume kunakofanywa na baadhi ya wanawake pale wanapoelekezwa kazi au kufundishwa kazi fulani huo siyo unyanyasaji wa kijinsia?

Kuna baadhi ya mabosi wanawake wamekuwa wakiwataka kimapenzi wanaume walio chini yao kwa nguvu na kama wakikataa watakiona cha mtema kuni. Wapo baadhi ya vijana wa kiume wamegeuka kuwa watumwa wa ngono wa mabosi wao na hawathubutu kufanya fyoko maana hatma ya kazi yao imo mikononi mwa hao mabosi wanawake.

Kuna haja sasa ya wanaume kusema sasa basi imetosha na sisi tutafute jukwaa la kusemea madhila yetu maana wenzetu wamejiweka kwenye kundi la waathirika wa vitendo hivyo kumbe na wao wamegeuka Chui ndani ya ngozi ya kondoo.

Kwa hisani ya Mtambuzi
JF

Tuesday, May 9, 2017

BLOGG YA MAISHA NA MAFANIKIO IMEONA HII IWE PICHA YA WIKI...

Nimeiangalia hii picha na kumpongeza huyu mama watoto wanne  na yeye mwenyewe jumla ni watu watano kwa baiskeli moja ....Duh! maisha haya kaaazi kwelikweli...lakini hata  hivyo kilichonifanya niipende picha hii ni nyuso zao wanaonekana wenye furaha na amani pia.....UJUMBE:- UKIWA NA FURAHA PIA AMANI MAISHA HUWA RAHISI KUYAKABILI. KAPULYA WENU.

Friday, April 28, 2017

NENDA KAMPENDE MKE WAKO

Nimetumiwa na simulizi hii na rafiki binafsi imenigusa sana nikaona niiiweka hapa kama kawaida nisemavyo sipendi kunyimana elimu. KARIBUNI!

Kijana mmoja alikua akimpenda sana Mama yake, kwakua Mama yake almlea kwa shida sana tena kwa upendo wa hali ya juu kijana yule alilipa fadhila kwa kuhakikisha kua Mama yake hakosi kitu chochote.

Baada ya kuoa yeye alihama nyumbani kwao na kwenda kuishi mbali kidogo na Mama yake, lakini katika mji uleule. Pamoja na umbali huo lakini kila siku alienda kumsalimia Mama yake na wadodgo zake.

Alikua akiwapelekea zawadi na fedha za matumizi. Mara nyingi akitoka kazini alikua akitumia muda mwingi nyumbani kwao na wakati mwingine hata chakula cha usiku alikula kule na kurudi nyumbani akiwa maeshiba.

Hali hiyo iliendelea kwa muda na hata walipobarikiwa kupata mtoto bado aliendelea kuwapenda ndugu zake na kutumia muda mwingi wa ziada akiwa nyumbani kwao kuliko nyumbani kwake.

Ingawa hakua akimdharau mkewe wala kumnyanyasa lakini alimpenda Mama yake zaidi. Siku moja jioni akiwa ametoka kazini, alifika nyumbani kwa Mama yake.

Aligonga mlango na kwa bahati nzuri Mama yake alifungua mlango. Lakini wakati akitaka kuingia akiwa na kapu la zawadi mkononi Mama yake alimzuia na kumuambia kuwa hakuna kuingia.

Kijana alishangaa akidhani kua ni utani lakini Mama alikataa katakata na kumuambia. “Mwanangu najua unanipenda sana lakini sasa ni zamu ya mkeo. Wewe ushakua mkubwa umeoa unafamilia yako, nenda kampende mkeo”.

Kijana alishangaa kwani yote aliyokua akiyafanya ni kwakua Mama yake aliteseka kwaajili yake. “Najua unayafanya yote kwa upendo ila mkeo anahitaji upendo pia. Mimi ni Mama yako, ni mtu mzima, lakini yule mkeo, bado ni binti lakini mna mtoto mdogo.

Kama unavyonipenda mimi mama yako nenda kampende Mama wa watoto wako ili aweze kuwalea watoto wenu waje kuwa na upendo kama wewe. Upendo unaonionyesha nikwakua Baba yako alinionyesha upendo wa hali ya juu.

Baba yako alinipenda sana, akanionyesha upendo, moyo wangu ukawa na amani nikawa na kazi ya kuwalea nyinyo kwa furaha. Sasa na nyinyi mna furaha unanihudumia.

Lakini wewe muda mwingi unautumia hapa, mkeo unamuacha peke yake mpweke. Mwanamke akiwa mpweke anakua na kisirani, akishakua na kisirani anakua na hasira na akiwa na hasira basi hutafuta sehemu ya kuzipeleka na anaweza kuzipeleka kwa watoto.

Akizipeleka kwa watoto watalelewa vibaya na hawatakuja kuwa watoto wazuri kama wewe. Nakupenda lakaini sikutaki tena kwangu, nenda kampende mkeo, tengeneza familia yako, hii ni ya kwangu na nishaitengeneza.

Mwanangu unanipenda sana lakini ipo siku nitakufa kama Baba yako, usihuzunike lakini ipo siku hawa wadogo zako wakiume wataoa, hawatakua na muda tena na wewe. Hawa dada zako wataolewa na kuwa na familia zao.

Watakua bize na familia zao kiasi kwamba hamtaonana, hiyo haimaanishi kuwa hawatakua wanakupenda, hapana watakupenda lakini maisha ndiyo yalivyo. Kama ambavyo mimi nilikua na Kaka zangu na Dada zangu.

Kama ambavyo Baba yako alikua na Kaka zake na Dada zake waliokua wakipendana lakini sasa kila mmoja ana familia yake. Wewe utabaki na mkeo na wanao, hao ndiyo watakua familia yako kama ambavyo Baba yako alibaki na mimi na nyinyi.

Sasa kama hukumuonyesha upendo mkeo sasa hivi unafikiri utaishi naye vipi ndugu wakikutelekeza kwasababu ya majukumu yao. Nenda kampende mkeo, mpeleke zawadi.

Kwangu utakuja mara moja moja nikikuhitaji, utakuja ukisikia naumwa na utanitumia matumizi mwisho wa mwezi. Katengeneze familia yako, nenda kanitengenezee wajukuu wazuri, wenye upendo kama ulivyo wewe Baba yao.

Mama alimaliza na kabla kijana hajasema chochote alifunga mlango na kuingia ndani. Kijana alilazimika kurudi nyumbani, alimkuta mkewe kanyongonyea.

Alimkabidhi lile kapu la zawadi na kumuambia zawadi zako hizi. Mke aliruka kwa tabasamu akimshukuru mumewe kwa zawadi ile, kwani muda ulikua umepita bile kupeleka zawadi nyumbani wala kuwahi vile.

****MWANAUME; Wapende ndugu zako lakini jua mwisho wa siku mtu pekee ambaye mtazeeka pamoja ni Mke wako. Kama huamini hembu muangalie Baba yako kule kijijini vipi bado anaishi na shangazi yako?

Lakini hembu muambie Bibi na Babu yako, si wako wawili tu, tena mmewatafutia na mfanyakazi ili awasaidie. Ndiyo huyo mwanamke unayemnyanyasa leo anathamani kuliko huyo Dada yako anayemtukana mkeo kila siku na wewe unachekelea.

Friday, April 7, 2017

PICHA YA WIKI...SIO MCHEZO HARUSI MTINI

Napenda kuwatakieni wote Ijumaa njema sana wote mtakaopita hapa leo pia mwisho wa juma uwe mwema...ni wenu kapulya.

Tuesday, March 14, 2017

MAISHA:- BAADA YA KUISHI MIKA 60 SASA WAFUNGA NDOA

Mzee wa miaka 98 aoa bibi  wa miaka 88 baada ya kuishi pamoja muda wa miaka 60 huku wakichunguzana.
WAZO: NIMEPENDA UAMUZI WAO.

Tuesday, October 18, 2016

TUSIWE WATU WA KUSAHAU MARAFIKI MAANA SIKU MOJA UTAWAHITAJI

RAFIKI NI BORA KULIKO MWANASESERE
Nimekaa hapa huku nikiwa na mawazo mengi katika kichwa changu...najiuliza:-  Hivi ni lini nitapata fursa ya kukutana na baadhi ya marafiki zangu? Hii ingekuwa fursa murwa kwangu kukutana tena baada ya muda mrefu kupoteana na kusikia maisha yao, familia na  kuhusu kazi zao. Muhimu zaidi kwangu ingekuwa kupata fursa ya kuonana na wao pia kuongea mawili matatu kwa nia ya kubadilishana mawazo. Kwani  ni vyema sana kuwa na  marafiki wanaokujali na unaowajali katika shughuli za kila siku za kimaisha. Tukumbuke, baadhi yetu marafiki ni kama funguo ya maisha. Inawezekana kazi uliyo nayo , mke/mume uliyo nayo nk umepata kwa kupitia rafiki. Kwa hiyo, tusiwe watu wasio wajali marafiki hasa wale wa muda. Binafsi nimepoteza marafiki wengi sana wale wa kitambo...jambo ambalo natamani siku moja tuonane tena  katika utu uzima huu. Ndugu zanguni kama mna marafiki ambao hakuona umuhimu wao jaribu kuwatafuta . Katika maisha ni vizuri kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kukutana na watu mbalimbali na mwisho mkawa marafiki wa kupendana zaidi ya ndugu uliyezaliwa naye tumbo moja. Pia tuwe na tabia kuchukua fursa kukutana na marafiki ili kujenga na kudumisha urafiki wetu maana mwisho wa siku utakuwa faida. Ila isiwe tu pale kwenye shida ndiyo urafiki,  hapana...ni vyema kujuliana hali kila wakati huku tukitakiana maisha mema hasa pale tukosapo muda wa kukutana. Maana katika maisha hakuna asiyependa kukumbukwa. Nadhani wengi wengi wetu tumekwisha wahi jiuliza:- kama ungependa kusahaulika na marafiki/watu wa karibu wako? nadhani jibu unalo....

Thursday, October 13, 2016

JIPE MOYO KAMWE USIKATE TAMAA KWA MUNGU YOTE YANAWEZEKANA

"Nilikuwa naangalia mpira wa miguu katika uwanja wa shule. Nilipokaa, nilimuuliza kijana mmoja juu ya matokeo ya mchezo. Kwa tabasamu, alijibu "Wako mbele yetu 3-0"! Nikasema, Kweli!! Mbona huonekani kukata tamaa.
"Kukata tamaa? "Yule mvulana aliuliza kwa mshangao.... Kwanini nikate tamaa wakati bado refa hajapuliza kipenga cha mwisho? Nina imani na timu yangu na meneja wa timu; Nina hakika tutashinda! Na kweli, mchezo uliisha 5-4 timu ya kijana ikiwa mbele! Alinipungia mkono taratibu, na tabasamu zuri akiondoka uwanjani; nilishangaa,mdomo wazi, ujasiri mkuu kiasi hiki; nilipenda alivyojiamini ;  Nilipofika nyumbani usiku ule, swali lake lilizidi kuja kwangu zaidi.
"Kwanini niogope wakati refa hajapuliza kipenga cha mwisho?" Maisha ni kama mchezo. Kwanini ukate tamaa wakati Mwenyezi Mungu ndiye meneja wako? Kwanini ukate tamaa wakati kungalipo uhai ndani yako? Kwanini ukate tamaa wakati kipenga chako cha mwisho bado hakijapigwa? Ukweli ni kwamba watu wengi hujipulizia wenyewe vipenga vyao vya mwisho. Lakini madamu ungalipo uhai, hakuna kisichowezekana muda haujakuacha. 
Nusu kipindi si kipindi kizima na ratiba ya Mungu kwa mwanadamu si ratiba ya mwanadamu kwa Mungu.
Usijipulizie kipenga chako cha mwisho wewe mwenyewe.
UJUMBE- Maisha ni changamoto  ambapo pia ni kama mchezo...twapaswa kuwa jasiri na kujiamini.

Monday, August 29, 2016

NI JUMATATU YA MWISHO YA MWEZI HUU WA NANE(8) NA UJUMBE KUTOKA KWA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO NI HUU! KAMWE USISAHAU AINA HIZI TATU (3) ZA WATU MWAISHANI MWAKO...

1. Mtu ambaye ame/alikusaidia ulipokuwa na hali/wakati ngumu/mgumu

2. Mtu aliyekuacha ukiwa na wakati/hali ngumu/mgumu

3. Mtu aliyekuweka katika hali/wakati ngumu/mgumu.
NAWATAKIENI WOTE MLIOPITA HAPA JUMATATU NJEMA. TUPO PAMOJA!

Monday, July 11, 2016

MAISHA YETU: FAHAMU NJIA SAHIHI YA KUKOSOA ILI MTU ASICHUKIE

KAMA binadamu tulioumbwa na Mwenyezi Mungu kila mmoja wetu amekuwa na upungufu katika eneo fulani, hali inayofanya mtu mwingine kutoa kasoro. Sio mbaya kutoa kasoro hiyo ila kuna njia nzuri ya kumkosoa mtu ili asichukie.
Leo tutaangalia mifano mbalimbali katika maisha yetu tunayoweza kuitumia pale tunapotaka kumkosoa mtu yeyote aliyefanya jambo kwa makusudi au kwa kutokujua bila kumfanya ajisikie vibaya. Kwa kuanzia, tumuangalie mkurugenzi mmoja aliyekuwa na viwanda mbalimbali vya kutengeneza nguo. Lakini siku moja aliamua kufanya ziara ya ghafla katika kiwanda chake kimoja.
Alipofika kiwandani aliwakuta baadhi ya wafanyakazi wake wakivuta sigara karibu kabisa na kibao kinachokataza uvutaji sigara sehemu hiyo. Mkurugenzi huyo akakisogelea kibao hicho na kuwaonesha wafanyakazi hao huku akiwauliza, ‘hamjasoma hapa?’ Wafanyakazi wote wakataharuki, wakashindwa kujieleza. “Vijana ningefurahi kama mngevuta sigara nje ya eneo hili au niseme hata nje ya kiwanda.”
Wafanyakazi hao walielewa kwamba bosi wao anatambua kuwa wamevunja sheria, lakini walimfurahia kwa sababu hakuzungumza nao kwa ukali, bali alizungumza kwa upendo na kuwafanya wajisikie kwamba wao ni wa muhimu katika kiwanda kile. Hilo lilikuwa ni fundisho kubwa kwao, kwani tangu hapo hawakurudia kosa hilo tena. Hivyo unaposhughulika na watu mbalimbali jaribu kuwa na busara katika kuwaeleza jambo.
Mfano mwingine ni kwa ofisa mmoja aliyejulikana kwa jina la Robby. Alikuwa na biashara zake na kila siku alikuwa akitembelea mojawapo ya biashara hizo. Ilifika siku moja akaenda kwenye ghala lake la vinywaji na kumwona mteja amekaa anasubiri huduma, lakini kulikuwa hakuna mtu wa kumhudumia kwa kipindi hicho.
Aligundua kuwa kwa wakati huo, wafanyakazi wake hawakuwa tayari kumsikiliza mteja huyo, bali walikuwa wamekaa kaunta, wakicheka na kuzungumza habari zao zinazowahusu bila kujali kuwa eneo lile ni eneo la kazi. Robby hakuzungumza lolote, taratibu akanyata kando ya kaunta na kumhudumia mteja yule mwenyewe na kukabidhi pesa kwa wauzaji hao wakati alipokuwa anaondoka.
Hapo tunaona kwamba Robby alitumia njia ya busara ya kuishi na wafanyakazi wale. Angeweza kutumia ukali au kuchukua hatua ya kuwafuta kazi mara moja, lakini kwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye hekima na busara, aliamua kumhudumia mteja yule aliyemkuta na hilo lilikuwa fundisho kubwa kwa wafanyakazi wake.
Aliwapa somo kwa njia ya vitendo kwamba kazi si mahali pa mchezo, bali panahitaji kuheshimiwa na kumheshimu kila anayehitaji huduma. Vile vile tunaona kwamba viongozi wa umma mara nyingi wamekuwa wakipingwa kutokana na kutokuonekana katika majimbo yao.
Mara zote wanasongwa na kazi, wamekuwa katika hali ya ulinzi muda wote na wasaidizi wao ambao hawapendi watu wawabughudhi mabosi, kwa kuruhusu wageni wazungumze nao.
Lakini kuna mbunge mmoja ambaye mara zote amekuwa akiwaasa wafanyakazi wake kuwaruhusu watu wamuone. Amekuwa akisema kwamba sera zake zipo wazi kwa kila mmoja, lakini wasaidizi wake wamekuwa wagumu kumuelewa, na kuendelea kuwazuia wananchi wasiweze kumuona kwa urahisi ili waeleze matatizo yao yanayowakabili.Baada ya kuona somo hilo halieleweki kwa wasaidizi wake, mbunge huyo mwishoni alipata suluhu kwa kuamua kuondoa mlango wa ofisi yake.
Kitendo hicho kilitoa ujumbe kwa urahisi kwa wasaidizi wake, kwamba mbunge huyo yuko wazi na yuko tayari kumsikiliza kila mmoja. Hapo inamaanisha kwamba si lazima kila mara ukawa unazungumza na watu ambao hawakuelewi, wakati mwingine unaweza kuzungumza kwa vitendo, utaeleweka.
Kwa kawaida unapobadilisha maneno mawili au matatu inaweza kuleta tofauti kati ya kushindwa na mafanikio katika kuwabadilisha watu wasiweze kuwa na uchungu. Unapotumia njia ya busara katika kumrekebisha mtu aliyekosa, inamfanya mtu yule asiyekuwa na uvumilivu katika kuwasahihisha wengine kwa kuwakosoa katika njia ya uwazi, kujifunza kitu.
Mfano mwingine upo kwa familia mmoja, iliyokuwa inakarabati nyumba yao, kwa kutumia mafundi ujenzi, familia hiyo ilifikia mahala ikaamua kuwashawishi mafundi kufanya usafi mara tu wamalizapo kazi yao.
Kwa siku za mwanzoni mwa ujenzi huo, mama mwenye nyumba alipokuwa akirudi nyumbani baada ya kazi, alibaini kuwa eneo la nyumbani kwake lilikuwa chafu, lenye kuonekana vipande vya mbao na uchafu mwingine. Mama huyo hakutaka kuzungumza na mafundi hao, kwa sababu walikuwa wamefanya kazi nzuri.
Kwa hiyo baada ya mafundi hao, kuondoka, yeye na watoto wake waliokota vipande hivyo vya mbao na kusafisha eneo hilo la ujenzi. Siku iliyofuata alimwita kiongozi wa mafundi waliokuwa wakijenga na kumwambia kuwa, “Nimefurahishwa na jinsi mlivyoacha eneo hili jana usiku, lilikuwa zuri na safi, na halikuweza kuleta usumbufu kwa jirani.” Tangu siku ile na kuendelea, wafanyakazi wale baada ya kazi walikuwa wakikusanya takataka zote na kuacha eneo lile safi. Na kiongozi yule alikuwa akihakikisha kama wafanyakazi wake wameacha eneo walilofanyia kazi likiwa safi.
IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI IMECHAPISHWA: 25 JUNI 2016

Friday, June 3, 2016

LEO TUNAADHIMISHA KUMBUKUMBU YA KUZALIWA KWA KIJANA WETU ERIK KUTIMIZA MIAKA 16...HONGERA SANA KIJANA WETU.... !

  Kaka Erik Nyumbani Ruhuwiko-songea 2015
Ndugu wapendwa natumai Ijumaaa hii itakuwa njema.Mungu azidi kuwabariki/kutubarika  katika yote.Hapa kwetu Ijumaa hii ni njema kabisaa. Leo tunaungana na kijana wetu mpendwa kwa kumbukumbu yake ya siku ya kuzaliwa Siku kama ya leo Mungu alitubariki na kutujaalia mtoto wa kiume kaka Erik. Mungu anaendelea kumtunza vyema katika yote. Mungu yu mwema sana, sifa na utukufu viwe kwakwe. Tunamweka kijana huyu mikononi mwake Baba wa Mbinguni katika yote. Aendelee kuwa Baraka kwetu kama wazazi,walezi, Ndugu,Jammaa,Marafiki na Jamii yote. 
Ngoja tu tuweka na wimbo ambao kaka Erik alianza kusikiliza kwa kujifunza kiswahili ingawa nilipata swali moja kwa nini wanasema Kenya na sio Tanzania mama? na wimbo wenyewe ni huu JAMBO BWANA

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA ERIK.

Friday, April 8, 2016

PALE TUNAPOYACHUKULIA MAISHA KIRAHISIRAHISI

Kama utayachukulia maisha kuwa ni dharura ni wazi utakuwa unakasirishwa hata na vitu vidogovidogo. Unapohisi kwamba, unaelekea kwenye kukasirika, unapaswa kujiambia au kujikumbusha kwamba, maisha siyo dharura. Kuyachukulia maisha kuwa siyo dharura ni pamoja na kujua kwamba, migogoro ya kimaisha ni jambo la kawaida na haiwezi kuepukika. Kujua kwamba, kukasirika hata siku moja hakuwezi kutatua matatizo yetu, badala yake hutuingiza kwenye matatizo makubwa zaidi kimwili na kiakili.
CHANZO:- KITABU CHA MAISHA NA MAFANIKIO

Sunday, March 27, 2016

KUTOKA MAISHA NA MAFANIKIO TWAWATAKIENI WOTE PASAKA NJEMA SANA

Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye alitoa uhai wake kwa ajili yetu, imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ua hao ndugu. Yoh. 3:16.
Pasaka njema na jumapili njema sana !!!

Wednesday, March 23, 2016

SABABU 4 AMBAZO KAMWE HUPASWI KUACHA KWENDA HAJA NDOGO PALE MAUMBILE YANAPOTAKA UFANYE HIVYO…


ANAHITAJI KWENDA HAJA NDOGO
Wote tunajua kwamba pale tunapokuwa tumebanwa  kweli kweli na haja ndogo(mkojo).
Wakati mwingine huwa tunalazimika kwa muda mrefu kukaa bila kwenda haja ndogo na
hata mwishowe kuhisi kana kwamba kibofu kinataka kupasuka.
Wakati mwingine tunakuwa katika sehemu ambazo hakuna maliwato yaliyoko karibu na
wakati mwingine huwa tunakuwa na marafiki tukipiga soga kiasi kwamba hutuwia
vigumu kuacha kukatisha mazungumzo ili kukidhi hitaji hilo la kimaumbile, lakini pia
wakati mwingine huweza kuwa na foleni ndefu kwenda maliwato hasa katika maeneo ya
Mighahawa au maeneo ya jumuia.
Zipo sababu nyingi kwa nini wakati mwingine yatupasa kuvumilia/kutunza  mkojo kwa
muda mrefu iwezekanavyo kutokana na maeneo tuliyopo kutokuwa rafiki katika kukidhi
hitaji hilo la kimaumbile lakini ni vyema tukijua kwamba jambo hilo lina athari kubwa
kiafya kwetu.
Kwa nini inasisitizwa kwamba tunapokuwa na hitaji hilo la kimaumbile tutafute mahali pa
kujisitiri haraka iwezavyo. Ni kwamba kibofu cha mkojo ni chombo ambacho kinaweza
kubeba/kutunza hadi lita 0.5 za mkojo. Wakati kibofu kikiwa kimejaa kama theluthi mbili
ubongo huwa unapata hisia kwamba ni lazima ukojoe. Lakini kwa sababu mawasiliano
kati ya kibofu cha mkojo na ubongo ni sehemu ya mfumo wa neva involuntary, unaweza
kuamua ni muda gani unaweza kukojoa - hivyo kuna wengi ambao wanaweza kukaa na
mkoja kwa muda mrefu, lakini hata hivyo ni vyema tukijua kwamba jambo hilo ni hatari
kwa afya zetu.
Hizi hapa ni sababu nne(4) kwa nini hupaswi kukaa na mkojo kwa muda mrefu.
1. Unaweza kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo
Kama hukojoi kuna hatari bakteria kuwa wengi/kuzidi katika mkusanyiko wa mkojo huo 
watafiti wa (illusterad vetenskap) wanasema wakati unapokojoa bakteria wanatoka nje
ya vimelea(bomba la mkojo). Bakteria, mara nyingi koli bakteria kutoka kwenye utumbo
inaweza kusababisha magonjwa ya maambukizi kwenye njia ya mkojo ambayo inaweza
kukua na kuwa hatari kwa figo. Hii kwa upande mwingine inaweza kusababisha sumu
kwenye damu utafiti umegundua hivyo.
2. Kibofu cha mkojo chaweza kuvuja mara kwa mara.
Kama unatunza mkojo mara nyingi kibofu cha mkojo wako kitatanuka na kuwa kilegevu.
Hii inaweza kusababisha tatizo la udhaifu wa kibofu kuwa mtepetevu ambapo mkojo
unaweza kuwa unatoka wenyewe matone  matone  kila wakati na matone huishia
kwenye nguo ya ndani na hapo ndipo mtu hujikuta unanuka mkojo mara kwa mara.
3. Unaweza kusababsha uharibifu wa figo:-
Mkojo unaozalishwa katika figo wakati unapoutunza mkojo huo kwa muda  mrefu kiasi 
cha kibofu cha mkojo kukaza kwa kuzidiwa basi figo hufanya kazi ya kupeleka mkojo
katika njia ya bomba la mkojo kwa shinikizo (presha) na unapoendelea kuzuia ndipo
unaposababisha athari kiafya. Utafiti wa Illustrared Vetenskap umebainisha kwamba hali
hiyo inaweza kusababisha uharibifu wa figo.
4. Kibofu cha mkojo kinaweza kupasuka na tumbo lako kujaa mkojo.
Kibofu cha mkojo kinaweza kupasuka. Lakini ni nadra, kwa kawaida watu ambao
wamepata tatizo la kibofu cha mkojo au ulevi ambapo mwili waweza "kusahau" kukojoa.
Wakati kibofu cha mkojo kikipasuka mkojo hutawanyika katika tumbo na unaweza
kueneza maambukizi na pia huwa na maumivu makali sana na athari nyingine kiafya.
NIMEONA NIWASHIRIKISHE HABARI HII ILI TUWE MAKINI KWENDA DAIMA HAJA
NDOGO PALE TUNAPOHITAJI, ILI KUEPUKA HIZI HATARI.
CHANZO: NEWSNER VATENSKAP.