Monday, July 11, 2016

MAISHA YETU: FAHAMU NJIA SAHIHI YA KUKOSOA ILI MTU ASICHUKIE

KAMA binadamu tulioumbwa na Mwenyezi Mungu kila mmoja wetu amekuwa na upungufu katika eneo fulani, hali inayofanya mtu mwingine kutoa kasoro. Sio mbaya kutoa kasoro hiyo ila kuna njia nzuri ya kumkosoa mtu ili asichukie.
Leo tutaangalia mifano mbalimbali katika maisha yetu tunayoweza kuitumia pale tunapotaka kumkosoa mtu yeyote aliyefanya jambo kwa makusudi au kwa kutokujua bila kumfanya ajisikie vibaya. Kwa kuanzia, tumuangalie mkurugenzi mmoja aliyekuwa na viwanda mbalimbali vya kutengeneza nguo. Lakini siku moja aliamua kufanya ziara ya ghafla katika kiwanda chake kimoja.
Alipofika kiwandani aliwakuta baadhi ya wafanyakazi wake wakivuta sigara karibu kabisa na kibao kinachokataza uvutaji sigara sehemu hiyo. Mkurugenzi huyo akakisogelea kibao hicho na kuwaonesha wafanyakazi hao huku akiwauliza, ‘hamjasoma hapa?’ Wafanyakazi wote wakataharuki, wakashindwa kujieleza. “Vijana ningefurahi kama mngevuta sigara nje ya eneo hili au niseme hata nje ya kiwanda.”
Wafanyakazi hao walielewa kwamba bosi wao anatambua kuwa wamevunja sheria, lakini walimfurahia kwa sababu hakuzungumza nao kwa ukali, bali alizungumza kwa upendo na kuwafanya wajisikie kwamba wao ni wa muhimu katika kiwanda kile. Hilo lilikuwa ni fundisho kubwa kwao, kwani tangu hapo hawakurudia kosa hilo tena. Hivyo unaposhughulika na watu mbalimbali jaribu kuwa na busara katika kuwaeleza jambo.
Mfano mwingine ni kwa ofisa mmoja aliyejulikana kwa jina la Robby. Alikuwa na biashara zake na kila siku alikuwa akitembelea mojawapo ya biashara hizo. Ilifika siku moja akaenda kwenye ghala lake la vinywaji na kumwona mteja amekaa anasubiri huduma, lakini kulikuwa hakuna mtu wa kumhudumia kwa kipindi hicho.
Aligundua kuwa kwa wakati huo, wafanyakazi wake hawakuwa tayari kumsikiliza mteja huyo, bali walikuwa wamekaa kaunta, wakicheka na kuzungumza habari zao zinazowahusu bila kujali kuwa eneo lile ni eneo la kazi. Robby hakuzungumza lolote, taratibu akanyata kando ya kaunta na kumhudumia mteja yule mwenyewe na kukabidhi pesa kwa wauzaji hao wakati alipokuwa anaondoka.
Hapo tunaona kwamba Robby alitumia njia ya busara ya kuishi na wafanyakazi wale. Angeweza kutumia ukali au kuchukua hatua ya kuwafuta kazi mara moja, lakini kwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye hekima na busara, aliamua kumhudumia mteja yule aliyemkuta na hilo lilikuwa fundisho kubwa kwa wafanyakazi wake.
Aliwapa somo kwa njia ya vitendo kwamba kazi si mahali pa mchezo, bali panahitaji kuheshimiwa na kumheshimu kila anayehitaji huduma. Vile vile tunaona kwamba viongozi wa umma mara nyingi wamekuwa wakipingwa kutokana na kutokuonekana katika majimbo yao.
Mara zote wanasongwa na kazi, wamekuwa katika hali ya ulinzi muda wote na wasaidizi wao ambao hawapendi watu wawabughudhi mabosi, kwa kuruhusu wageni wazungumze nao.
Lakini kuna mbunge mmoja ambaye mara zote amekuwa akiwaasa wafanyakazi wake kuwaruhusu watu wamuone. Amekuwa akisema kwamba sera zake zipo wazi kwa kila mmoja, lakini wasaidizi wake wamekuwa wagumu kumuelewa, na kuendelea kuwazuia wananchi wasiweze kumuona kwa urahisi ili waeleze matatizo yao yanayowakabili.Baada ya kuona somo hilo halieleweki kwa wasaidizi wake, mbunge huyo mwishoni alipata suluhu kwa kuamua kuondoa mlango wa ofisi yake.
Kitendo hicho kilitoa ujumbe kwa urahisi kwa wasaidizi wake, kwamba mbunge huyo yuko wazi na yuko tayari kumsikiliza kila mmoja. Hapo inamaanisha kwamba si lazima kila mara ukawa unazungumza na watu ambao hawakuelewi, wakati mwingine unaweza kuzungumza kwa vitendo, utaeleweka.
Kwa kawaida unapobadilisha maneno mawili au matatu inaweza kuleta tofauti kati ya kushindwa na mafanikio katika kuwabadilisha watu wasiweze kuwa na uchungu. Unapotumia njia ya busara katika kumrekebisha mtu aliyekosa, inamfanya mtu yule asiyekuwa na uvumilivu katika kuwasahihisha wengine kwa kuwakosoa katika njia ya uwazi, kujifunza kitu.
Mfano mwingine upo kwa familia mmoja, iliyokuwa inakarabati nyumba yao, kwa kutumia mafundi ujenzi, familia hiyo ilifikia mahala ikaamua kuwashawishi mafundi kufanya usafi mara tu wamalizapo kazi yao.
Kwa siku za mwanzoni mwa ujenzi huo, mama mwenye nyumba alipokuwa akirudi nyumbani baada ya kazi, alibaini kuwa eneo la nyumbani kwake lilikuwa chafu, lenye kuonekana vipande vya mbao na uchafu mwingine. Mama huyo hakutaka kuzungumza na mafundi hao, kwa sababu walikuwa wamefanya kazi nzuri.
Kwa hiyo baada ya mafundi hao, kuondoka, yeye na watoto wake waliokota vipande hivyo vya mbao na kusafisha eneo hilo la ujenzi. Siku iliyofuata alimwita kiongozi wa mafundi waliokuwa wakijenga na kumwambia kuwa, “Nimefurahishwa na jinsi mlivyoacha eneo hili jana usiku, lilikuwa zuri na safi, na halikuweza kuleta usumbufu kwa jirani.” Tangu siku ile na kuendelea, wafanyakazi wale baada ya kazi walikuwa wakikusanya takataka zote na kuacha eneo lile safi. Na kiongozi yule alikuwa akihakikisha kama wafanyakazi wake wameacha eneo walilofanyia kazi likiwa safi.
IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI IMECHAPISHWA: 25 JUNI 2016

No comments: