Wednesday, May 6, 2009

TUENDELEE KUANGALIE SURA YA KIJIJI CHA LIKUYU FUSI SEHEMU YATATU = KUNYUMBA

Inaendelea toka sehemu ya kwanza ya Kijiji cha Likuyu Fusi.

Mazao haya yote ni kwa ajili ya chakula chao na kuuza ziada. Baadhi ya wananchi wanalima tumbaku, kwa ajili ya kupata fedha kidogo za matumizi. Wakati wa kiangazi wananchi hulima mboga za aina mbalimbali, kama mchicha, mabogo, nyanya, lipwani, bamia na siku za karibuni wameingiza aina ya mboga za kigeni kama kabeji, saladi, biringanya na aina nyingine. Kwa ujumla kilimo cha mvua za mwaka huwa katika sehemu zalizoinuka na wakati wa kiangazi wananchi hulima mabondeni. Hivyo shughuli za kilimo ni za wakati wote katika mwaka. Mvua za mwaka huanza mwezi Novemba na kumalizika mwezi mei.

Kilimo kimekuwa kwa miaka mingi cha mtu mmoja mmoja au mtu na jamii yake wakishirikiana na jirani wa karibu katika kilimo cha bega kwa bega au “Chama”. Mapato na hali ya maisha ya wakazi kwa ujumla si ya kuridhisha sana. Ingawaje wananchi wanapata chakula kwa wingi cha kuwashibisha lakini kuna uhaba wa vyakula vya aina ya nyama ambayo ni muhimu kujenga miili ya binadamu hasa akina mama wajawazito, watoto na vijana. Vyakula aina ya nyama, samaki, mayai, dagaa, kunde, maharagwe na maziwa ndivyo vinavyojenga miili yetu. Ili watu wajengeke vema kiafya kuna haja ya kuwapa akina mama wajawazito, watoto na vijana vyakula vya aina nilivyotaja kwa wingi.

Kabla ya vita kuu ya pili, wananchi walikuwa na mifugo ya aina mbalimbali, kama ngómbe, mbuzi, kondoo, kuku, njiwa, na bata. Na kwenye mapori kulikuwa na wanyama wa aina mbalimbali kama funo, tambaramba, nguruwe, ngungusi, kwale, kanga, nyani, ngedere, chui na simba na wengineo. Wanyama hawa walikuwa wakiwindwa kwa nyavu, mitego na pengine kwa bunduki za migobole. Hivyo kutokana na mifugo na wanyama wa porini, wananchi waliweza kula nyama mara kwa mara wakati walipotaka. Hivi sasa ufugaji wa wanyama umepungua sana na kadhalika idadi ya wanyama wa porini. Hali hii inaleta shida kubwa ya kupata nyama huko vijijini.

Watu wachache wanofuga wantama hao ni kwa ajili ya posa, misiba, harusi au wakati mwingine kwa ajili ya kuwapata watu kuwalimia mashamba yao ya binafsi. Ufugaji wa kuku na bata nao ni wa kijadi. Kuku huzurura ovyo mashambani wakitafuta panzi, kupelkua mchwa na kutafuta chembe za nafaka mashambani. Hali hiyo hiyo ipo kwenye ufugaji wa bata.

Watu wachache hufuga nguruwe nao pia ni kiasi kidogo sana na matumizi yake makubwa ni kuwalipa watu wanolima wakati wa masika. Kuna uwezekano wa kuongeza ufugaji huu kwani chakula cha nguruwe si vigumu kupatikana.

Kijiji cha Likuyu Fusi kina mafundi wachache wa useremala wenye mashine za kuranda, kupasua mbao, kutengeneza milango, madirisha, meza, viti na madawati nk. Mafundi hawa ambaohupata msaada wa mara kwa mara toka misheni, hufanya kazi zao binafsi ingawaje huwaajiri vijana wa kuwafunza kazi. Siku hizi karibu kila kijiji kilichoandikishwa kimekopeshwa na Benki ya maendeleo vijijini, mashine za kusaga na kukoboa nafaka, matrekta ya kulimia na malori. Hata hivyo ni watu wachache wenye kuzingatia kazi za kilimo, kwani idadi kubwa ya wakazi wa sehemu hizi hutegemea kazi za kuajiriwa na misheni au mahali pengine katika mashirika na Serikali. Katika vijiji nilivyovitaja wapo pia mafundi wa uhunzi wenye kutengeneza mashoka, mikuki, visu, nyengo,vinu n.k. Vitu hivi hutengenezwa kwa kiasi kidogo sana ili kupata fedha za kununua mahitaji na kulipa gharama mbalimbali za maisha. Katika kila kijiji kilichoandikishwa na vile vya asili zimefunguliwa shule moja kutegemea idadi ya watoto walioko. Zaidi ya hayo zipo huduma za madhehebu mbalimbali ya dini katka kila kijiji. Ingawa bado watu wengi hutegemea masoko yaliyoko katika vituo vya misheni, siku hizi kila kijiji kimeanzisha shughuli za soko kama vile uuzaji wa pombe na vyakula, na mazao mbalimbali toka mashambani kwao. Hata hivyo serikali za vijiji zinatakiwa kufanya jitihada kubwa kupunguza tatizo la wizi wa mali za vijiji ambao hutokana na kuwa na majengo hafifu ya kutunzia mali hizo, pamoja na utunzaji mbaya wa mahesabu yake. Wengi wa viongozi wa vijiji hawana ujuzi wa shughuli hizo, na hawapo tayari kutoa nafasi kwa wale wenye uwezo. Hilo ni tatizo la kudumu katika baadhi ya vijiji na limesababisha vijiji hivyo kushindwa kuendelea. Bado ipo haja ya kuwa na msukumo mkubwa sana wa kuwaelimisha wakazi kuhusu uendeshaji wa shughuli za kijiji katika upande wa uchumi.

Jengo la Mahakama lililojengwa wakati wa Nduna Laurent akiwa mtawala wa jadi, bado linaendea kutumika kama mahakama na ofisi ya Mahakama ya Mwanzo.

Wakazi wa vijiji nilivyotaja wanahudumiwa na hospitali kubwa ya Peramiho na Songea. Hata hivyo katika kila kijiji lipo sanduku la huduma ya kwanza ambayo huangaliwa na Serikali ya Kijiji. Zipo barabara kubwa zinazopita katika maeneo ya baadhi ya vijiji lakini hali ya vijiji hivyo bado havijafikia hatua ya kujitegemea katika huduma za usafiri kwa wakazi wake. Malori ya mikopo na matrekta hutumika kwa muda mfupi kutokana na kuharibika mara kwa mara kwa kukosa uangalizi mzuri.

Kama nilivyoeleza hapo juu kuwa eneo la Likuyu Fusi limebahatika kuwa na mito ya kudumu kwa hiyo hakuna tatizo la kukosa maji. Hata hivyo kwa msaada wa Serikali na Misheni baadhi ya vijiji vimepelekewa maji kwa mabomba. Mipango hiyo inaendelea katika vijiji vilivyobaki.

Wakazi wa Likuyu Fusi ni Wangoni wenye asili mbalimbali. Nduna Laurent alikuwa mjuzi wa kupambanua asili zao. Alikuwa anasimulia kuwa siyo kila mtu ni Mngoni wa asili. Watu wengine wanaitwa Wangoni kwa sababu zao mbalimbali. Mathalani, yapo makabila yaliyokuwepo katika nchi hii kabla ya Wangoni wageni hawajaingia Wilaya ya Songea. Makabila hayo ni Wandendeule, Wamatengo,Wamwera,Wahyao, Wamatumbi na Wapangwa, Baadhi ya watu toka katika makabila haya walipewa Ungoni kwa ajili ya kutekwa katika vita vya makabila, na wengine kwa ajili ya kuzaliwa katika mali ya mtu, na wengine walinunua kabila. Mathalani, Mtepa Gama alipokuwa vitani aliteka watumwa wanne, wawili wanawake na wawili wanaume, Hawa wote kila mmoja wao alikuwa na jina lake la ukoo, kama Komba, Hyera, Ngonyani, Kihaule n.k. Watumwa hawa baada ya kutekwa waliruhusiwa kuendelea kutumia majina yao au walitaka waweze kutumia jina la mtu aliyewateka. Ili kulinda usalama wao watumwa hao waliamua kutumia jina la ukoo wa Mtepa ambaye aliwateka na hivyo walijulikana kuwa ni watu wa Mtepa. ITAENDELEA.......

2 comments:

Bennet said...

Hii inaonyesha jinsi gani ambavyo ulitaka kuijua asili yako kwa undani zaidi lakini pia nakusifu kwa jinsi ulivyo fanikiwa kupata hizi taarifa muhimu, nina uhakika hazikutokana na chanzo kimoja bali ni watu mbali mbali

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli kabisa safari yangu ya TZ mwaka huu imenipa faida sana pamoja na kutembelea Bookshop ya Peramiho. Na halafu niliposoma shule ya msingi kati ya masomo niliyoyapenda ni Historia na Jiografia. Ukweli ndio huo kakangu.