Haya ni maoni ya MAKULILO,Jr kwenye mada ya UBAGUZI WA RANGI TANZANIA/AFRIKA nimeona niyaweke hapa wote ili tujadiliane.
MAUAJI YA ZERUZERU (ALBINO) TANZANIA NAYO NI UBAGUZI WA RANGI
Nimekaa na kufanya tafakari ya kina kuhusiana na mauaji ya ndugu zetu Albino yanayoendelea kuisakama Tanzania. Dhana mbili zinajitokeza katika tafakari hiyo. Moja ni dhana nzima ya ubaguzi wa rangi na pili ni tathimini yangu kuhusu mikakati ya serikali ya Tanzania kuwahakikishia usalama ndugu zetu Albino.
Ukiangalia ubaguzi wa rangi uliokuwepo Afrika Kusini enzi za Makaburu, watu walipangwa katika makundi kutokana na rangi zao; weupe ( Wazungu ), watu wa rangirangi (coloured ) na weusi ( Waafrika ). Huduma zote, ikiwa ni pamoja na elimu, zilitolewa kwa kuzingatia rangi ya mtu.
Kulikuwa na kumbi za starehe kwa ajili ya watu weupe, ambapo mtu mweusi hakuruhusiwa kuingia. Kuna sehemu zingine ambazo mwafrika hakuruhusiwa hata kukanyaga kabisa. Akikamatwa, alipewa kipigo kikali na hata kutupwa lupango ( jela).
Ubaguzi wa rangi, hususani dhidi ya Mwafrika, ulikuwepo hata katika nchi za Magharibi. Nakumbuka nimeona picha zilizoandika “only for blacks and dogs here.” Hii ilikuwa hatari sana, kwani mtu mweusi alinyimwa haki zake kutokana na rangi ya ngozi yake .
Sasa tujiulize.Hivi Albinno ni mtu wa namna gani? Anaweza tambuliwaje kwa muonekano wake? Sintopenda kuingia ndani zaidi kuchimba sababu za kibaiolojia zinazo mfanya mtu azaliwe Albino. Hata hivyo mtu haitaji microscope ( darubini) wala elimu ya Chuo kikuu kumtambua Albino.
Nionavyo mimi, naamini bila pingamizi lolote kuwa mauaji ya Albino yanayoendelea kuitikisa Tanzania “Kisiwa cha Amani” ni mwendelezo wa dhambi ya ubaguzi wa rangi, lakini huu ni ubaguzi mkali zaidi katika historia ya mwanadamu kushinda hata dhambi ya biashara ya utumwa.
Nasema nimkali zaidi kwani unalenga kuondoa maisha ya mwanadamu kwa ukatili wa kunyofoa viungo, tofauti na ule wa kumzuia mweusi kutembelea mitaa fulani au katika upandaji wa mabasi n.k !
Ni kwa kuangalia rangi ya ngozi yake, unaweza kumtambua Albino. Kwa bahati mbaya, Albino anayezaliwa Afrika, ni tofauti na yule wa nchi za Ulaya na Marekani, kwani Albino wa nchi hizo, hatofautiani sana na mtu wa kawaida. Rangi yake inarandana na ya mzungu . Si ajabu kama naye angefanana na mwafrika, angebaguliwa na kuuawa.
Kinachonishangaza mimi, ni kwanini Tanzania au Watanzania kwa ujumla hatusemi ukweli kuwa mauaji ya Albino yanayoendelea, ni ubaguzi wa rangi ili tuweze kupambana nao ipasavyo na Jumuiya ya Kimataifa iweze kutoa msaada sawawa na ambavyo jumuiya ya Kimataifa, hususani Tanzania, ilivyojitoa muhanga kung’oa mzizi wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini?
Kwa mtazamo wangu, Watanzania tumeaminishwa kuwa Tanzania ni kisiwa cha Amani na hivyo sisi ni bora zaidi kuliko Taifa lolote kiutamaduni na kimaadili. Hii si kweli na huu ni mtazamo potofu ambao tusipokuwa makini, utatufikisha pabaya.
Kwa uzoefu wangu, kitendo cha ubaguzi kikifanywa na Taifa jingine mfano Burundi, Kongo, Afrika Kusini, Ujerumani, M arekani ama Israeli, tunawanyooshea kidole kuwa wamepotoka huku tukitamka wazi kuwa nchi hizo zinafanya ubagauzi wa rangi. Je, kwa nini kitendo hicho kikitendeka Tanzania kama cha mauaji ya Albino, tunapata kigugumizi kutamka wazi kwamba ni kitendo cha ubaguzi wa rangi na tunaanza kutafuta majina mengine kama vile “unyanyasaji wa Albino” na k.n yasiyotoa picha halisi ya mambo yanayoendelea?
Kwani ubaguzi wa rangi lazima kitendo kifanywe na mtu mweupe ( mzungu ) dhidi ya mweusi ( mwafrika ) ili kistahili kuitwa ubaguzi wa rangi? Vipi kama kitendo hichohicho kitafanywa na mtu mweusi dhidi ya mtu mweupe ( mzungu / albino ), hakiwezi kuitwa kitendo cha ubaguzi wa rangi?
Au kama mtu mweusi atafanya kitendo cha kumbagua mweusi mwenzake kutokana na rangi yake kama vile mweusi sana , mweusi tiii! mweusi wa kati, nacho hakiwezi kuitwa ubaguzi wa rangi? Na vipi kama mtu mweupe ( mzungu ) akimbagua na kumnyanyasa mweupe mwingine kama vile Mchina , Mwarabu n.k, kitendo hicho kitaitwaje?
Kwa uzoefu wangu, hasa baada ya kuangalia matukio ya hivi karibuni ambapo Waafrika Kusini waliamua kuwavamia na kuwaua wahamiaji kutoka nchi nyingine za Afrika, Tanzania ilikuwa mstasri wa mbele kukemea vitendo hivyo. Tanzania ilitoa tamko kali na kwa uwazi kabisa ikisema, “ Dhambi ya ubaguzi bado inaitafuna Afrika kusini.”
Nikaanza kuangalia mambo mengine ninayoyashuhudia kila kukicha huku Marekani. Mtu akifanyiwa kitendo fulani, kwa mfano, ikiwa ni mweupe kakifanya, hukimbilia kusema ni ubaguzi wa rangi.
Sasa mimi najiuliza. Je endapo Mtanzania mweusi mmoja ataenda nchi yoyote ya Magharibi kama vile kusoma au kufanya kazi halafu akauliwa na kunyofolewa viungo kama wanavyofanyiwa Albino, Tanzania itasemaje? Haina ubishi , kila mtu atasema “amebaguliwa na kuuwawa kutokana na rangi yake.”
Swali langu la msingi ni hili: Kitendo cha Albino kunyofolewa viungo vyake kinyama na hatimaye kuuawa na mtu mwenye rangi nyeusi kisa rangi yake ni tofauti na cha mtanzania mweusi aliyebaguliwa na kuuawa ugenini hususani katika nchi za magharibi? Kwa nini mauwaji ya Albino yasitajwe kama ubaguzi wa rangi? Maana Albino naye hutambuliwa kwa rangi yake!
Kama tumefikia hatua ya kuuana kutokana na rangi zetu; moja nyeusi, nyingine ya rangirangi ( coloured ) na wote ni binadamu tena watanzania, tuanaelekea wapi ndungu zangu?
Serikali ya Tanzaia inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupambana na janga hili la mauaji ya albino. Uamuzi wa kugawa simu kwa albino wote, pengine waweza kusaidia kwa kuwawezesha kupiga simu polisi wanapovamiwa.
Lakini Serikali inawasaidiaje albino waishio kijijini ambako hakuna umeme? Simu hiyo inachajiwa kwa teknolojia gani? Je simu hizo hizitakuwa kivutio kingine na hivyo kuwafanya wavamiwe zaidi?
Kama imefikia hatua albino hawezi kutembea peke yake au kutembea baadhi ya masaa hususani jioni, kama imefikia hatua Mbunge maalum ambaye ni albino lazima apewe ulinzi maalum ili asinyofolewe viungo vyake, falsafa ya Tanzania kama kisiwa cha amani iko wapi?
Ndugu zetu wa Marekani wanaelekea kuishinda dhambi ya ubaguzi wa rangi, kwani hatimaye wamefikia hatua ya kumchagua mtu mweusi kuwa Rais wao kwa kuangalia uwezo wake, hoja zake na si tena kigezo cha rangi kama Dr. Martin Luther King Jr aliposisitiza katika ndoto yake ( I HAVE A DREAM). Mwaka 2010 kama mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa albino, tutakuwa tayari kumpigia kura endapo atakuwa na sifa za kutuongoza? Tafakari, Chukua hatua.
Nawasilisha hoja!
MAKULILO, Jr.
Fulbright Visiting Scholar
Blog: www.makulilo.blogspot.com
E-Mail: msauzi101@yahoo.com
West Virginia, US
7 comments:
Asante Da Yasinta kwa kuweka mada yangu.Wadau tusaidiane kujenga hoja na kuchukua hatua.
MAKULILO, Jr.
KAKA MAKULILO JR! Tupo pamoja,tunataka kitu kimoja na tukiungana tutakuwa PAMOJA.Ahsante wewe.
Da Yasinta karibu na huku tuzungumze-www.varsitycollegetz.ning.com. Hii mada ya Makulilo pia ilijadiliwa huku. Baadae.
Mi naona kuna aina tofauti ya ubaguzi hata huo wa rangi...coz if a white person does the same thing to a black person like what some tanzanians do to albinos... i think it's gonna b based on the background, culture n way of livin dat someone else is against it...
....so i think its different..wit albinos we are comin from the same culture, background and country but wit albino killings it is based on particular type of beliefs. I dnt knw abt others but dats my opinion.
huwa naumia sana ninaposikia mauaji ya hawa wenzetu (Albino) nikiwafikiria najifananisha kama vile mimi nikiwa kwenye mbuga yenye wanyama wakali kuanzia nyati, mamba, simba, chui, chatu, nyoka wenye sumu n.k halafu niishi humo wakati sijui ni nani kati yao ataniua, sasa hayo ndio maisha ya albino hapa nchini mwetu na eneo hatari zaidi ni kanda ya ziwa
Mauaji ya albino na hata yale ya vikongwe ni irationality of the highest order!Ingawa tafiti nyingi bado hazifanyika kuangalia huu unyama wa mauaji ya albino lakini watu huelezea kuwa linaletelezwa na masuala ya ushirikina, hasa kutokana na kwamba albino wanaouawa hukutwa hawana baadhi ya viungo vyao vya mwili. Kwa tafsiri ya haraka haraka hapa ni kwamba, waganga na waaguzi wa kienyeji ndio ambao kwa namna moja au nyingine hutoa hamasa ya mauaji. Ingawa tiba za jadi zina umuhimu wake (kama alternative form of medicine), lakini kuna watoaji huduma hiyo ambayo wanaharibu fani hii. Kama vile ambavyo WM Mh. Mizengo Pinda alivyowahi kutamka (ule utata wa kufuta leseni za watoa tiba),njia ya haraka ya kufikirika ni kuwamonitor hawa watoa tiba kwa njia itakayofanya shughuli zao kuwa wazi zaidi na kuadhere kwenye ethics za huduma za afya. Mganga au Muaguzi anayekwambia ukalete kiungo cha binadamu huyo si mganga, atakulia hela yako tu bure. Kwa upande mwingine, mimi naona haihitaji hata kwenda shule, suala hili linasababishwa na tamaa ya kutaka utajiri na mafanikio ya haraka!Kutokana na hilo, binadamu tumegeuka wanyama, utu tumeutupa kapuni!
Ukitumia vitabu vya nadharia ya kisosholojia, tunaelezwa na nadharia za aina zote mbili kwa namna tofauti chanzo cha haya mauaji.Zile zinazomwangalia mwanadamu (at individual level- micro theories) na zile zinazoangalia mfumo na jamii kwa ujumla (macro theories.
Kwa ufupi, kati ya zile zinazomwangalia mwanadamu, kuna moja ambayo inaona kuwa chanzo ni ile hali ya wanadamu wenyewe kutoa maana ya vitu kupitia mchakato wa tafsiri (creation of meaning through interpretative process). hapa ina maana kuwa kwa kuwa waganga, waaguzi na wenye tamaa wameshatoa maana, kinachofuata ni mtu mmoja baada ya mwingine naye kushare ile maana kupitia kuchangamana (interaction).
Kwa zile zinazoiangalia jamii, napenda sana kutumia falsafa na nadharia za mwanazuoni Karl Marx. labda kama angekuwa hai leo angesema, mauaji ya albino yanaletelezwa na mfumo. Mfumo wa kibepari ambao siku zote unawafanya watu kutafuta zaidi (ku-maximize profit). Kutafuta huku kunawafanya watumie kila aina ya njia, watu wengi wanawaona albino kama viumbe dhaifu kitu ambacho si kweli kabisa, lakini pia kutokana na mwonekano wao, ukichanganya na haja nyingine, wanatumiwa ili watu fulani waendelee kushikilia nafasi walizo nazo na kujiongezea/ kujipatia utajiri. Marx angeshauri labda, mfumo ambao unasababisha gap kubwa kati ya walio nacho na wasio nacho kuvunjwa na wanaonyonywa, na hapo jamii isiyo ya kinyonyaji, iliyostaarabika, yenye utu na inayozingatia haki za binadamu ingechukua nafasi yake.
Tujiulize, kwa Tanzania hili linawezekana? Naamini kwa nguvu zetu, YES WE CAN!
Yasinda na Makulilo,
Japokuwa nakubaliana kuwa kitendo cha mtu mmoja kumua mtu mwingine kwa lengo lolote lile ni dhambi kubwa SIKUBALIANI na hoja ya Makulilo kwamba kuuawa kwa albino Tanzania ni dhana ya ubaguzi wa rangi. Dhana ya ubaguzi wa rangi msingi wake mkubwa ni kwamba mtu mmoja anamini kwamba yeye ni bora kuliko mtu mwingine ambapo inakwenda katika level ya watu wa race moja ni superior kuliko race nyingine hapa ndipo chanzo ubaguzi na ndiyo msingi mkubwa wa ubaguzi wa rangi. Watanzania wanaoua albino hawafanyi hivyo kwa kuamini kwamba wao ni bora. Kinachotokea ni kwamba wanaamini kwamba (kwa fikra mbovu) kwamba wakipata viongo vya albino basi watatajirika. Hii haina tofauti na imani kwa mikoa ya au kanda ya shinyanga ambapo wazee akina mama wanauawa kwa misingi kwamba ni wachawi. Hii nayo huwezi kuweka kwamba ni ubaguzi wa rangi japokuwa ni ni vitendo ambavyo kwa mtu ambaye yupo civilized ni hali mbaya sana.
Pia tofauti nyingine ni kwamba ubaguzi wa rangi shina lake ni refu sana yaani ulianza miaka na miaka na hata kabla ya utumwa. Na hauishi kiraurahisi wakati actually albino kuuawa ni tendo jipya ambalo limekuja baada baadhi ya watu kufukiri kwamba wanaweza kupata hela mapema. Na kama serikali itafanya juhudi utakwesha mapema sana kama polisi watafanya kazi nzuri.
Kusema na kutaka kulinganisha matendo haya kwa matendo ya ubaguzi wa africa kusini au marekani au Europe na hata Israel kweli ni kukosa kuelewa dhana kubwa ya ubaguzi katika nchi hizi. Mimi naamini kabisa asilimia kubwa ya watanzania hawaamini kwamba albinos are inferior. Ndiyo unaweza kusema kwamba kuna tatizo lakini watanzania wengi hatuamini kwa namna yeyote ile kwamba albino ni watu ambao wapo chini kwa namna yeyote ile. Wakati ubaguzi wa rangi upo rooted kwenye racism ambayo initial assumption ni kwamba race moja au kundi fulani ni superior kuliko wengine. Wachina/Japanese hadi leo bado wanaamini kwamba mtu mweusi ndiyo hivyo kwamba yupo chini na wachina wengine au wajapane wanaendelea na hilo.
Anyway, nafikiri niishie hapo kwa sasa maana muda umekwisha. Samahani kama sielewi. Mshamba wa Iringa aka Evaristo.
Post a Comment