Sijui nianze vipi hili jambo limekuwa likinitatanisha sana afadhali niliweka wazi ili nisaidiwa nisije nikapasuka kichwa kwa kuwaza. Ni hivi: babu, baba, kaka au nisema wanaume kwa ujumla kwa nini wanapenda kujitoa katika mambo mengi. Nisemapo hivi nina maana mara nyingi utasikia, yule mwanadada/mwanamke ni mhuni/malaya sana Je huu uhuni/umalaya anafanya na nani?. Anajifanyia peke yake?. HAPANA kwa sababu kuna wanaume wasiotosheka, wenye tamaa wanawaacha wake zao nyumbani na kwenda pembeni. Na baadaye wanageuka na kusema wanawake wahuni. Mnajua mimi bado sijaelewa kabisa nani ni mhuni hapa. Kwasababu sijawahi kusikia hata siku moja , ikisemwa mwanaume yule mhuni.
Najua wanaume wengi watasema/jitetea ya kuwa hawatosheki na wake zao kwa sababu ya migogoro nyumbani hiyo ndiyo sababu wanatoka nje. Lakini kumbuka hii ni kisingizio tu cha kutoka nje( kuwa na nyumba pembeni)
Inasemekana wanaume hawawezi kuvumilia angalia wanaume waliooa wanaozungukwa na makarani wengi au wafanyakazi wengine ambao ushawishi na mvuto wao wa kimwili unaonekana kila saa katika wakati wa kufanya kazi basi hapo kishawishi tayari.
Nimeona niambatanishe na MADA hii hapo chini kwani inalenga jambo hilo hilo kutoka kwa http://kaluse.blogspot.com/
WANAUME WOTE WANA NYUMBA NDOGO?
Kuna idadi kubwa sana ya wanawake kuliko mimi na wewe tunavyoweza kufikiri, wanaoamini kwamba wanaume wote wana nyumba ndogo. Je wewe mwanamke ndivyo unavyoamini? Je wewe mwanaume umeshawahi kuambiwa hivyo na mkeo au mpenzi wako? Kama bado basi wewe una bahati.
Kwa nini wanawake hawa wanaamini hivyo? Kuna sababu kubwa moja tu ambayo ndiyo yenye kufanya imani hii kushika mizizi, nayo ni malezi. Wanawake kama ilivyo wanaume wamelelewa kwa kuamini kwamba wao ni dhaifu na wanaume ni imara. Wamelelewa kwa kufundishwa kwamba wao hawana haki zote ndani ya nyumba kama ilivyo kwa wanaume.
Katika kuamini huku wanawake wamejikuta wakiwa ni aina ya watumishi ndani ya ndoa na wamejikuta wakiwa ni watu wa jikoni ndani ya ndoa na waamejikuta wakiwa watu wa kupewa amri na kuzipokea ndani ya ndoa. Katika mkabala huo wanawake wamejikuta wakiwa hawana kauli wala sauti hata katika maswala ya kimaumbile.Kwa mfano ni mwanamume ndiye anayetakiwa kusema ‘leo sijisikii’ na siyo mwanamke na ni mwanaume anayetakiwa kusema ‘leo nahitaji’ na siyo mwanamke.
Mwanamke anapokua na mahusiano na mwanaume mwingine nje, anapewa haraka jina la ‘Malaya sana’ wakati mwanaume anaweza kupewa jina la sifa “mkali” au “mtu wa watoto” hata kama ana mahusiano na wanawake kumi. Hii sio nasibu ya mambo bali matokeo ya malezi yetu.
Kwa kupewa nafasi kama hii mwanaume amekua huru kushiriki tendo la ndoa kwa kadri atakavyo kwenye familia zetu. Nyumbani hua tunaona jinsi watoto wakiume wanapokua na marafiki wa kike lisivyo jambo la ajabu , bali tu pale watoto wa kike wanapo jaribu kuwa na marafiki wa kiume hata wale makaka ambao wao huwachezea madada wa wengine huko nje huwa wakali sana kwa madada zao.
Kwa mkabala kama huo, kwenye jamii yetu mwanamke kua mcheshi, mzungumzaji huru na mkaribishaji mzuri kuna maana moja tu kwamba huyu ni malaya, bali kwa mwanaume sifa hizo hubaki hivyohivyo na pengine kuongezewa uzito. Hata kama ndani ya sifa hizo kumejificha ufuska ulio kubuhu, hakuna atakayejali sana.
Kuna ukweli kiasi fulani kwamba, wanaume wengi huwa wana ‘nyumba ndogo’ au zaidi ya rafiki mmoja wa kike. Hali hii imepelekea hata watu kuamini kwamba wanaume wana hamu kubwa na tendo la ndoa kuliko wanawake, jambo ambalo limekanushwa na tafiti nyingi zilizofanywa kuhusiana nalo.
Wanaume kwa sababu za kamalezi na ubabe ulio katika mazoea ya kimapokezi tangu kale, wanaamini kwamba wao ndio wenye uhuru wakuchagua kama waendelee kua na mmoja au hapana. Kwa hiyo,kwa sababu wao ndiyo ambao wamejipa funguo ya maamuzi hufanya uharibifu mwingi.
Kwa kuwa wanaume wanaamini kwamba wanapaswa kuabudiwa na wanawake, linapotokea tatizo dogo tu la kindoa huamua kutoka nje, kwa sababu wanawake kwao ni vyombo vya starehe vinavyoweza kununuliwa mwanamume anapojisikia. Lakini pia hii ni kwa sababu, kutoka nje kwao ni aina ya sifa wakati mwingine.
Kutokana na malezi haya ambayo yanahalalisha mwanaume kuwa “kijogoo” wanaume wengi wamekua na urahisi wakutokua waaminifu . Lakini hata hivyo,hakuna ukweli kwamba wanaume wote wana nyumba ndogo. Nadhani unajua tofauti kati “wote” na “wengi”
Ni vigumu kusema idadi halisi kwa maana asilimia, kwani hakuna utafiti rasmi ambao umefanywa, lakini kwa utafiti usio rasmi imethibitika kwamba kwa hapa Jijini Dar es salaam, kuna uwezekano mkubwa kwamba katika kila wanaume kumi, saba wana ‘nyumba ndogo’ au rafiki wa kike zaidi ya mmoja.
Idadi hii ni kubwa sana na kuna haki kwa watu kuamini kwamba kila mwanamume ana ‘nyumba ndogo’. Lakini bila shaka umefika wakati kwa wanaume kujiuliza kama tabia hiyo ina manufaa yoyote kwao na kama huko sio kuwazalilisha wake au wapenzi wao. Je, wake zao wangekua wanafanya hivyo wao wangejisikia vipi,au wanadhani wanawake hawana hisia kama binadamu?
5 comments:
Mmmhhh! Ni kama hadithi ya kuku na yai. Yaani kujua kipi cha kulaumiwa iwapo atatotolewa kuku asiye na sifa ambazo mtotoleshaji anataka. Sijui na Yai ama Kuku? Ni nani wa kubeba lawama hapa? Nakumbuka mataifa makubwa yanaposema acheni vita huku yanatoa silaha. Basi najiuliza kama ni sahihi kwa wanaume kuwalaumu wanawake ilhali wao ndio wanaoonekana kuwashawishi. Lakini pia najiuliza kama ni sahihi kwa kinamama wanaojua kuwa wanalaumiwa kimakosa kuendelea kusema NDIO katika kitu chenye uwezekano mkubwa wa kuwadhalilisha.
Kwani kinakaka/baba wakiacha "kuwatokea kinadada kutakuwa na DADA mhuni? Na kinadada/mama nao wakikataa kufanya "vyombo vya starehe" kutakuwa na KAKA mhuni kweli?
Kutamani kumeumbwa ili kuweka hitaji la kusonga katika KILA CHEMA UTAMANICHO, lakini kwa matumizi mabaya ya hisia zetu, tunajikuta tukiitumia vibaya tamaa. Na ni lazima tutambue kuwa kwa kila kitu tumiacho vibaya, twajiandalia maafa. Hata dawa zikiwa abused badala ya kuwa used inakuwa balaa.
Hivi ni nani mwenye makosa? Ni nani chanzo cha tatizo? Ni nani wa kuleta usuluhishi?
Na ni kweli kuwa wanaume nwote wana nyumba ndogo?
Naacha
Uhuni, wote wanawake kwa waume wanaweza kuwa wahuni kutokana na matendo yao.
Mada ihusuyo Wanaume kuwa na Nyumba Ndogo,sio jambo jema. Kila mtu anatakiwa utosheke na ulienaye
LMFAO! haki ya mungu yaani hiyo heading imeniacha hoi sana. Tamaa tupu!
Mi naona hii ni kubalance mambo maana wanaume tuko wachake hata tukiwa na wawili wawili bado wanawake watabaki, halafu katika hao wanaume wachache ondoa ambao sio marijali,mashoga na mapadri kwa hiyo ili kila mwanamke awe na mwenzi wake inabidi tugawane kila mwanaume apate wanawake 6, na kwakuwa dini zingine haziruhusu ndoa zaidi ya moja basi solution ni nyumba ndogo.
haahahhaha! i was just joking jamani kuna ukimwi tujichunge kaa na wako mmoja tu
Post a Comment