Haya ni maoni ya MAKULILO,Jr kwenye mada ya UBAGUZI WA RANGI TANZANIA/AFRIKA nimeona niyaweke hapa wote ili tujadiliane.
MAUAJI YA ZERUZERU (ALBINO) TANZANIA NAYO NI UBAGUZI WA RANGI Nimekaa na kufanya tafakari ya kina kuhusiana na mauaji ya ndugu zetu Albino yanayoendelea kuisakama Tanzania. Dhana mbili zinajitokeza katika tafakari hiyo. Moja ni dhana nzima ya ubaguzi wa rangi na pili ni tathimini yangu kuhusu mikakati ya serikali ya Tanzania kuwahakikishia usalama ndugu zetu Albino.
Ukiangalia ubaguzi wa rangi uliokuwepo Afrika Kusini enzi za Makaburu, watu walipangwa katika makundi kutokana na rangi zao; weupe ( Wazungu ), watu wa rangirangi (coloured ) na weusi ( Waafrika ). Huduma zote, ikiwa ni pamoja na elimu, zilitolewa kwa kuzingatia rangi ya mtu.
Kulikuwa na kumbi za starehe kwa ajili ya watu weupe, ambapo mtu mweusi hakuruhusiwa kuingia. Kuna sehemu zingine ambazo mwafrika hakuruhusiwa hata kukanyaga kabisa. Akikamatwa, alipewa kipigo kikali na hata kutupwa lupango ( jela).
Ubaguzi wa rangi, hususani dhidi ya Mwafrika, ulikuwepo hata katika nchi za Magharibi. Nakumbuka nimeona picha zilizoandika “only for blacks and dogs here.” Hii ilikuwa hatari sana, kwani mtu mweusi alinyimwa haki zake kutokana na rangi ya ngozi yake .
Sasa tujiulize.Hivi Albinno ni mtu wa namna gani? Anaweza tambuliwaje kwa muonekano wake? Sintopenda kuingia ndani zaidi kuchimba sababu za kibaiolojia zinazo mfanya mtu azaliwe Albino. Hata hivyo mtu haitaji microscope ( darubini) wala elimu ya Chuo kikuu kumtambua Albino.
Nionavyo mimi, naamini bila pingamizi lolote kuwa mauaji ya Albino yanayoendelea kuitikisa Tanzania “Kisiwa cha Amani” ni mwendelezo wa dhambi ya ubaguzi wa rangi, lakini huu ni ubaguzi mkali zaidi katika historia ya mwanadamu kushinda hata dhambi ya biashara ya utumwa.
Nasema nimkali zaidi kwani unalenga kuondoa maisha ya mwanadamu kwa ukatili wa kunyofoa viungo, tofauti na ule wa kumzuia mweusi kutembelea mitaa fulani au katika upandaji wa mabasi n.k !
Ni kwa kuangalia rangi ya ngozi yake, unaweza kumtambua Albino. Kwa bahati mbaya, Albino anayezaliwa Afrika, ni tofauti na yule wa nchi za Ulaya na Marekani, kwani Albino wa nchi hizo, hatofautiani sana na mtu wa kawaida. Rangi yake inarandana na ya mzungu . Si ajabu kama naye angefanana na mwafrika, angebaguliwa na kuuawa.
Kinachonishangaza mimi, ni kwanini Tanzania au Watanzania kwa ujumla hatusemi ukweli kuwa mauaji ya Albino yanayoendelea, ni ubaguzi wa rangi ili tuweze kupambana nao ipasavyo na Jumuiya ya Kimataifa iweze kutoa msaada sawawa na ambavyo jumuiya ya Kimataifa, hususani Tanzania, ilivyojitoa muhanga kung’oa mzizi wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini?
Kwa mtazamo wangu, Watanzania tumeaminishwa kuwa Tanzania ni kisiwa cha Amani na hivyo sisi ni bora zaidi kuliko Taifa lolote kiutamaduni na kimaadili. Hii si kweli na huu ni mtazamo potofu ambao tusipokuwa makini, utatufikisha pabaya.
Kwa uzoefu wangu, kitendo cha ubaguzi kikifanywa na Taifa jingine mfano Burundi, Kongo, Afrika Kusini, Ujerumani, M arekani ama Israeli, tunawanyooshea kidole kuwa wamepotoka huku tukitamka wazi kuwa nchi hizo zinafanya ubagauzi wa rangi. Je, kwa nini kitendo hicho kikitendeka Tanzania kama cha mauaji ya Albino, tunapata kigugumizi kutamka wazi kwamba ni kitendo cha ubaguzi wa rangi na tunaanza kutafuta majina mengine kama vile “unyanyasaji wa Albino” na k.n yasiyotoa picha halisi ya mambo yanayoendelea?
Kwani ubaguzi wa rangi lazima kitendo kifanywe na mtu mweupe ( mzungu ) dhidi ya mweusi ( mwafrika ) ili kistahili kuitwa ubaguzi wa rangi? Vipi kama kitendo hichohicho kitafanywa na mtu mweusi dhidi ya mtu mweupe ( mzungu / albino ), hakiwezi kuitwa kitendo cha ubaguzi wa rangi?
Au kama mtu mweusi atafanya kitendo cha kumbagua mweusi mwenzake kutokana na rangi yake kama vile mweusi sana , mweusi tiii! mweusi wa kati, nacho hakiwezi kuitwa ubaguzi wa rangi? Na vipi kama mtu mweupe ( mzungu ) akimbagua na kumnyanyasa mweupe mwingine kama vile Mchina , Mwarabu n.k, kitendo hicho kitaitwaje?
Kwa uzoefu wangu, hasa baada ya kuangalia matukio ya hivi karibuni ambapo Waafrika Kusini waliamua kuwavamia na kuwaua wahamiaji kutoka nchi nyingine za Afrika, Tanzania ilikuwa mstasri wa mbele kukemea vitendo hivyo. Tanzania ilitoa tamko kali na kwa uwazi kabisa ikisema, “ Dhambi ya ubaguzi bado inaitafuna Afrika kusini.”
Nikaanza kuangalia mambo mengine ninayoyashuhudia kila kukicha huku Marekani. Mtu akifanyiwa kitendo fulani, kwa mfano, ikiwa ni mweupe kakifanya, hukimbilia kusema ni ubaguzi wa rangi.
Sasa mimi najiuliza. Je endapo Mtanzania mweusi mmoja ataenda nchi yoyote ya Magharibi kama vile kusoma au kufanya kazi halafu akauliwa na kunyofolewa viungo kama wanavyofanyiwa Albino, Tanzania itasemaje? Haina ubishi , kila mtu atasema “amebaguliwa na kuuwawa kutokana na rangi yake.”
Swali langu la msingi ni hili: Kitendo cha Albino kunyofolewa viungo vyake kinyama na hatimaye kuuawa na mtu mwenye rangi nyeusi kisa rangi yake ni tofauti na cha mtanzania mweusi aliyebaguliwa na kuuawa ugenini hususani katika nchi za magharibi? Kwa nini mauwaji ya Albino yasitajwe kama ubaguzi wa rangi? Maana Albino naye hutambuliwa kwa rangi yake!
Kama tumefikia hatua ya kuuana kutokana na rangi zetu; moja nyeusi, nyingine ya rangirangi ( coloured ) na wote ni binadamu tena watanzania, tuanaelekea wapi ndungu zangu?
Serikali ya Tanzaia inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kupambana na janga hili la mauaji ya albino. Uamuzi wa kugawa simu kwa albino wote, pengine waweza kusaidia kwa kuwawezesha kupiga simu polisi wanapovamiwa.
Lakini Serikali inawasaidiaje albino waishio kijijini ambako hakuna umeme? Simu hiyo inachajiwa kwa teknolojia gani? Je simu hizo hizitakuwa kivutio kingine na hivyo kuwafanya wavamiwe zaidi?
Kama imefikia hatua albino hawezi kutembea peke yake au kutembea baadhi ya masaa hususani jioni, kama imefikia hatua Mbunge maalum ambaye ni albino lazima apewe ulinzi maalum ili asinyofolewe viungo vyake, falsafa ya Tanzania kama kisiwa cha amani iko wapi?
Ndugu zetu wa Marekani wanaelekea kuishinda dhambi ya ubaguzi wa rangi, kwani hatimaye wamefikia hatua ya kumchagua mtu mweusi kuwa Rais wao kwa kuangalia uwezo wake, hoja zake na si tena kigezo cha rangi kama Dr. Martin Luther King Jr aliposisitiza katika ndoto yake ( I HAVE A DREAM). Mwaka 2010 kama mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa albino, tutakuwa tayari kumpigia kura endapo atakuwa na sifa za kutuongoza? Tafakari, Chukua hatua.
Nawasilisha hoja!
MAKULILO, Jr.
Fulbright Visiting Scholar
Blog: www.makulilo.blogspot.com
E-Mail: msauzi101@yahoo.com
West Virginia, US