Wednesday, May 18, 2011

JAMANI HII NI NDOA AU NDOANO?

Haya basi ile siku imefika ni Jumatano kama nilivyotoa Taarifa... kwa hiyo basi leo tuanze na hii mada ambayo nilisha iweka yenye kichwa cha habari kama kisemavyo hapo juu.
-------------------------------------------------------------------------------------


Je? kuna upendo hapa?


Ndugu wasomaji na wanablog wenzangu, leo nina jambo moja ambalo ningependa tulijadili kwa pamoja.
Kuna msomaji mmoja wa blog hii ambaye ningependa kumuita Mlachaombwani (Sio jina lake halisi) amenitumia email akinitaka ushauri kutokana na kile alichoita jinamizi linaloitafuna furaha ktk ndoa yake.

Kusema kweli, hata mie nimejikuta nikishikwa na kizunguzungu maana mambo ya maunyumba haya yanahitaji umakini pale unapotakiwa ushauri.

Kaka Mlachaombwani anasema kuwa ameishi na mkewe kwa takribani muongo mmoja sasa na wamejaaliwa kupata watoto wawili katika ndoa yao hiyo. Maisha yao kwa ujumla ni mazuri kiasi, kwani ni familia iliyojitosheleza kwa kiasi cha mboga. Awali ndoa yao iloanza kwa bashasha zote ilikuwa na amani na utulivu na kila mmoja alimpenda mwenzake.

Lakini mwaka 2003 mkewe huyo alimbadilikia sana na akawa hawapendi kabisa ndugu zake, yaani ndugu wa mume. Hataki kuwaona wazee wa mumewe wala ndugu zake. Pamoja na ushauri toka kwa viongozi wa dini yao mkewe huyo alishasema kuwa ‘hata kama akija MALAIKA kumshauri hataweza kubadili msimamo wake kwa kuwa akishamchukia mtu basi ni mpaka kiyama’! Kibaya zaidi kafikia hatua anamnyima mumewe huyo unyumba au labda niseme chakula cha usiku, na sasa maisha yao ya ndoa yamekuwa kama vile sio wanandoa, yaani hakuna kupeana lile tendo la ndoa kama ilivyokuwa zamani wakati wanaoana.

Anasema hata kama akiamua kumpa tendo ni pale anapoamua yeye (mwanamke) yaani akipenda yeye na hii inaweza kuwa ni baada ya mwezi au baada ya miezi. Nilipomuuliza kama anapopewa, je wanafanya kwa ile hali ya mapenzi kufurahia tendo la ndoa au vipi? Akasema ni mradi kutimiza tu wajibu lakini hakuna raha yoyote ile. Ni kama vile anabakwa ama anabaka vile.

Nikukumbushe msomaji wangu kuwa ndani ya miaka hiyo kuanzia 2003 ilisababisha huyo kaka Machaombwani kuingia katika ‘mahusiano yasiyofaa’ nje ya ndoa ambayo yalisababisha kupatikana watoto wengine wawili. Nadhani ni baada ya kuona hapati haki yake hapo nyumbani.

Hata hivyo amebainisha kuwa tatizo jingine kubwa linaloitafuna ndoa yake ni wivu usiofaa aliokuwa nao mkewe huyo. Anasema mke wake amekuwa akimlinda sana akijaribu kumpeleleza kama ana wanawake wengine nje ya ndoa (nyumba ndogo?) hata baada ya mume kukiri kilichokwisha kutokea. Kwamba pamoja na kumnyima tendo la ndoa lakini bado anamuonea wivu, na kumlinda. Na cha ajabu pia pamoja na mume kusema kuwa kwa muda wa miaka 2 sasa hamjui mwanamke mwingine nje ya ndoa hataki kusikia chochote ikiwa ni pamoja na kumzuia mumewe kutoa matunzo kwa watoto hao waliozaliwa nje ya ndoa kutokana na ‘ujinga’ wa wanandoa hao.

Tatizo lingine ni matusi, yaani anamtukana hadharani mbele ya watoto bila hata ya aibu. Kuhusu malezi ya watoto, watoto wanalelewa kana kwamba wako ktk kambi ya mateso kwani ni matusi (kama vile mbwa wee, kunguni, mjinga, taahira n.k) na mangumi kwa kwenda mbele. Heshima ndani ya nyumba imepungua na hakuna amani kabisa. Kwamba unaweza kuwakuta wanacheka lakini ni vicheko vya kebehi na ukiwaona leo baada ya saa moja ukiwakuta utadhani ni maadui wa siku nyingi.

Kaka Mlachaombwani anadai kuwa amani yake yeye ni pale anapokuwa kazini, safarini au kwa marafiki zake tu, lakini nyumbani kila siku moto unawaka. Amekiri kuwa sasa wakati wake mwingi anaupotezea katika kompyuta kwa kuwa hapo ndio hupata farijiko huku akijifunza mambo mengi kadha wa kadha ili kupoteza mawazo.

Nimemuuliza kwa nini asimuache huyo mwanamke na kumfukuza kama hali yenyewe ndiyo hiyo naye amenijibu kuwa yupo kwa SABABU ya WANAWE na si vinginevyo. Anasema kuwa muda ukifika ataondoka yeye tu na kumwachia kila kitu huyo mkewe! Yaani pamoja na mahusiano haya mabaya bado yupo tu? Na atakaa kwa muda gani akiyavumilia hayo? Kuna haja ya kuondoka? Kuna haja ya kuoa mke mwingine? Afanye nini?

Wenzangu kwangu mimi huu ni mtihani maana hata sijui nimshauri nini kaka Mlachaombwani.

Swali langu kwa ndugu zangu wasomaji:- Je ndoa ni kupendana kati ya wanandoa au ni tendo la ndoa? Je ni kipi kinachowaunganisha wanandoa, ni upendo au ni tendo la ndoa?
Je kweli kuna upendo kati ya wanandoa hawa na ni namna gani tunaweza kuwasaidia wanandoa hawa?

Na ukibonyeza KAPULYA utakuta maelezo ya kaka Mlachaombwani. TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO....!!!

5 comments:

Fadhy Mtanga said...

hapo ndipo ninapoona watu wana akili fupi kweli. Wewe unamnyima mwenzako unyumba, kisha unamchunga asitoke nje. Unamfanya mtumwa kwako kimwili na kiakili.

Anonymous said...

Da,Yasinta.Hapa kuna kitu ambacho mimi na wewe hatuwezi kukijuwa mwanzo wa mzozo huu,kati ya hawa wana ndoa.sikuzote sisi marafiki,ndungu nk, niwatoa ushauri tu ambao kwa wahusika ni jukumu lao kuchuja na kuchambua ushauri huo.ndoa nikuvumiliana kwa kilajambo litokeapo muwapowawili.la msingi hapa si chakula cha usiku tu ndo kinafanya ndoa iwe imara.bali ni jinsi kati yenu nyinyi wawili mnavyo peana nafasi katika kutatua matatizo yenu.nafasi hiyo ni kuwa lazima mmoja wenu amjuwe vizuri mwenzi wake anataka nini(mawasiliano).na hii ni kwa pande zote mke/mume.kwa kauzoefu kangu kadogo,ndani ya nyumba wote mkiwa vijogoo hamtafika mbali.lazima mmoja akubali kuwa chini ili kuinusuru ndoa.kuwa chini haina maana unakuwa mtumwa hapana,nijinsi ambavyo wewe kama baba/mama unatoa nafasi ya kuleta maelewano kwa utaratibu sahihi,mfano dawa ya moto ni moto!huwezi kusuruhisha mgogoro wa wanandoa kama wote woko juu,panapo tokea mmoja kumpa mwenziwake nafasi ndipo maelewano ndani ya nyumba yana patikana.nasikuzote wenye maamuzi ya mwisho ni hao hao wana ndoa,kwani ndiyo watakao baki pamoja kujadiliana na kukubaliana ,wa achane ama waedelee.kumbuka pia swala la watoto nimuhimu sana,jamaa ana sababu sikuzote watoto ndiyo wanao teseka.mwisho huyo mama atakuwa ana matatizo ya kisaikolojia,hivyo akiwa ona wataalam wanaweza kumsaidia.hasa watu wanaoitwa THERAPIST.awatafute ,mwambie huyo bwana amtafutie mkewe huduma hiyo,lazima kuna kitu anacho, kamanilivyosema awali kinuhusiano na 'akili' ngoja niishie hapa. Kaka S.

emu-three said...

'usifikiri wote waliopo kwenye ndoa wanafurahia aku kufurahiana sana...' akasema jamaa yangu, nikamuuliza kwanini, akasema `utashi wa binadamu, hisia na mapenzi ynatofautiana kati ya mtu na mtu...'
'Sasa unataka kusemaje?' nikawa sijamuelewa.
'Ni kuwa kuoana ni pamoja na kuvumiliana, huyu amvumilie mwenzake naye avumiliwe..., lakini kwa hali ilivyo sasa, kila mmoja kaota mapembe, hujui ni nani na nani katika ndoa. Katika kumi, wawili tu wanaweza wakawa wanafuraha katika ndoa..' akasema jamaa yangu.
Nilivyo mdadidi sana akanifichulia siri yake na mkewe. Kwani sisi majirani tulikuwa tukiwasifu sana kuwa katika ndoa iliyobarikiwa ndio hiyo, kwani ukiwakuta mitaani, utafikiri mapacha...kumbe...duuuh, ndio huko kuvumiliana!
Ndugu mtoa mada, au mlalamikaji, ndoa inajengwa kati ya mume na mke, na ikitokea hitilafu jambo jema ni kukaa na kujadiliana, ikishindikana mnawashirikisha watu mnaowaamini, ikishindikana, ....mmmh, uue kuna jambo, kwani kila jambo hutokea ili iwe sabababu. Na kumbukeni mapenzi mazuri kati yenu ndio msingi mzuri wa kizazi chenu. Sasa kaeni mjadili , mnataka watoto wenu waishije baadaye? wawe kama nyo hivyo, au ?

EDNA said...

kweli si wote walio kwenye ndoa wanafurahia maisha ya ndoa...

Christian Sikapundwa said...

Dada Yasinta yaliyofungwa duniani na Mbinguni yamefungwa,Hao walishaapa mbele za mashaidi kuwa watapendana katika raha na shida.

Kwa hiyo huo ndiyo msalaba wa huyo mme mwenye wivi,lakini binadamu tuna mambo akiacha kumwonea wivu mme wake watasema hampendi mmewe.akimpenda sana hadi kutaka kuchoma moto nyumba ndogo watasema anamnyanyasa kipi kizuri? Ndoa ni ndoa tu iwe tendo la ndoa linafanyika au kwa wasiwasi bado ni ndoa tu kila mmoja anahaki na mwili wa mwenzake.Hilo jambo ni gumu si rahisi kama tunavyo fikiri.Ndoa ni kuvumiliana nyumba zinatunza siri sana kwa wana - ndoa.