Tuesday, October 28, 2008

JE? HUU NI UUNGWANA KUWADANGANYA WATU HIVI?

Sofia Mhagama mwenye umri wa miaka 16 ameenda Dar es Salaam na Shangazi yake Emilia Soko kutoka katika kijiji cha Mpandangindo mkoani Ruvuma. Sofia ni mtoto watatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba. Wazazi wa Sofia hawana kipato cha kutosha kuhudumia familia nzima. Baba yake Sofia, mzee Mhagama ni mzee mashuhuri sana kijijini Mpandangindo. Shangazi yake Sofia aitwaye Emilia Soko alihamia Dar es Salaam kutoka Mpandangindo miaka ya themanini mwanzoni. Tangu Shangazi Emilia alipohamia mjini amekuwa akitembelea kijijini kwao Mpandangindo mara kwa mara. Kila wakati shangazi Emilia alipokuwa anakuja kijijini kuleta zawadi nyingi kutoka mjini pamoja na vitu vingi vya kisasa ambavyo ni shida sana kupatikana kijijini. Kila mtu kijijini aliona kuwa maisha ya Shangazi Emilia yamebadilika sana toka ahamie mjini na kuwa bora zaidi kutokana na vitu na misaada aliyokuwa anawapa wazazi wake kijijini.

Baada ya miaka Shangazi Emilia alitembelea tena kijijini kwao Mpandangindo kwa ajili ya kusherekea sikukuu ya krismas pamoja na wazazi kama ilivyo kawaida yake alikwenda pia kuwatembalea familia ya mzee Mhagama, baba yake Sofia. Shangazi Emilia alimwelezea mzee Mhagama masikitiko yake juu ya hali ngumu ya maisha ambayo inamkabili mzee Mhagama na familia yake. Emilia alimwambia kaka yake kwamba angependa kujitolea kumsaidia mtoto mmoja wa kike, Sofia. Mama yake Sofia hakuelewa kwa nini Emilia amemchagua Sofia wakati kulikuwa na wadogo zake ambao wangefaidika kielimu maana Sofia alikuwa anasaidia kazi za pale nyumbani. Sofia alikuwa anatambulika sana kwa kipaji cha kuimba kijijini pale. Mama Sofia alihisi kuwa hiyo inaweza kuwa ndio sababu kubwa Emilia kumchagua mwanae Sofia. Mzee Mhagama hupenda sana kumsifia binti yake kwa marafiki zake wakati akiwa anakunywa ulanzi, hupenda kusema "mtoto wangu Sofia ana sauti nyororo ya kumtoa nyoka pangoni". Wazazi wa Sofia walikubali kwa shingo upande kumtoa binti yao Sofia maana walikuwa wanampenda sana binti yao.
Sofia kwa sasa anaishi nashangazi yake mjini Dar es Salaam. Shangazi yake aliwaahidi wazazi wa Sofia kwamba akifika mjini, Sofia atapata kazi inayomlipa vizuri na nafasi ya kwenda shule. Kwa bahati nzuri kuna ndugu wengine wa Sofia wanaoishi Dar, kwa hiyo Sofia alijua kuna watu wa kuwategemea wakati wa shida akifika Dar, Sofia hakujua jinsi jiji la Dar lilivyo kuwa ya kwamba ni vigumu kutembea mwenyewe na hata kwenda kuwatafuta ndugu zake ambao wako Dar. Shangazi yake Sofia, naye alivunja ahadi yake: Sofia hakuruhusiwa kwenda shule na amefanywa kuwa mtumishi wa ndani kwa shangazi yake bila malipo. Sofia anafanyishwa kazi masaa mengi na kama akikataa hupigwa na kutishiwa kufukuzwa nyumbani kwa shangazi yake na kuachwa mitaani. Sofia anatamani sana kurudi kwao Mpandangindo kwa familia yake na pia kwenda shule, lakini hawezi.

Swali je? hii ni haki kufanya hivyo?

6 comments:

Christian Bwaya said...

Yasinta ningependa kuuliza kabla ya kuchangia. Hivi kisa hiki ni cha kweli kabisa ama ni hadithi?

luihamu said...

habari,
amani iwe nawe.
nimesoma kisa lakini niseme nini?

kuna mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema hakuna kiumbe kibaya duniani kama Bin Adamu kwasababu ya mambo yake.

Yasinta Ngonyani said...

Bwaya Hii ni hadithi ya kweli kabisa wala sijatunga. haya sasa karibu uchangie.

Luihamu asante kwa maoni.

MARKUS MPANGALA said...

kwanza nasherekea kurejea kwa bwana Luihamu. ni faraja na raha sana. kuhusu kisa hiki naona haya kunena ila naamini dada Yasinta uko kamili kama unavyo vingine tuhabarishe basi

Christian Bwaya said...

Inasikitisha. Nashindwa kuendelea ziadi ya kujiuliza: Kwa nini ifikie hapa?

Yasinta Ngonyani said...

Inabidi tuwaokoe watoto wanaodanganywa ni kweli inasikitisha sana na hasa ukizingatia ni wanandugu ndio wengi wanofanya hivi au marafiki