Tuesday, February 11, 2014

MKE ANAPOMJALI NA KUMKUBALI MUME HUMUONGEZEA KUJIAMINI…

Mke anapomjali na kumkubali mume humuongezea kujiamini…
Mahusiano kati ya mume na mke nyumbani huweza kumfanya mume afanikiwe kwenye shughuli zake au aanguke. Kwa nini? Ni kwamba, mtu ambaye anakataliwa na mtu au watu wanaomhusu huwa anakosa kujiamini, huwa anafikia mahali ambapo hujichukia hata yeye mwenyewe.
Mke anapomkosoa mume, anapomlalamikia kila mara na kuwa na ghubu, bila kujali kama mume huyo amekosa au hapana, mume hufikia mahali huanza kujitilia mashaka kama kweli ana uwezo wa kufanya mambo, kama kweli ana thamani anayodhani kuwa anayo. Kujiuliza huku mara nyingi kuna maana ya mwanaume kuanza kupoteza kujiamini na hata kuanza kuwa na uhusiano mbaya na watu anaohusiana nao mahali pengine kama kazini. Unaweza kumgundua mtu ambaye ana mke mlalamikaji, mkosoaji na mwenye ghubu kwa kuangalia jinsi anavyojitathmini. Kama mke ni mkosoaji na mwenye ghubu kwa mumewe ni lazima mume atakosa kujiamini katika kufanya mambo yake mengi, ni lazima ataanza kuwa na uhusiano mmbaya na watu wengine kutokana na hukohuko kutojiamini kwake ambako kumesababishwa na ghubu na kukosoa kwengi kwa mkewe. Mwanaume ambaye ana mke mkosoaji na mwenye ghubu hutokea kutowapenda watu wengine na kukosoa wengine inatokea kuwa sehemu muhimu kwa maisha yake, anatokea kuwa na hasira za karibukaribu na ni vigumu sana kwa mtu wa aina hii kuelewana na watu.
Baadhi ya makampuni huko Marekani, kabla hayajampandisha mtumishi wake cheo, humchunguza mke wa mtumishi. Hawachunguzi kama ni mzuri wa sura au kama anajua mapenzi au kupika vizuri. Mara zote huchunguza kama mwanamke huwa anampa mumewe moyo, kama hamkosoi na kumlalamikia na kama hana ghubu. Wanapogundua kwamba mke wa mtumishi siyo mkosoaji
wala mwenye kulalamika-lalamika humpa cheo mtumshi kwa imani kwamba atakuwa ni mtu mwenye kujiamini. Lakini wanapogundua kwamba mke ni mwenye kukosoa, mwenye ghubu na
mlalamikaji, kamwe hawampi mtumishi cheo, kwa sababu wanaamini kwamba, mtumishi huyo hawezi kuwa makini, atakuwa hajiamini.
.......................................................................................................................................................
Swali langu hapa je hii ni pale tu mwanamke anapomjali mume na ndio iwe hivi? Je? mwanamke astahili kujaliwa na kukubaliwa ili kuongeza kujiamini?..au ndo kusema mwanamke anajiamini sana kuliko mwanamume?..swali kutoka kwa KAPULYA...
Habari/mada hii nimetumiwa na mkereketwa/msomaji wa Maisha na Mafanikio kwa kutaka tu mimi nisome lakini mimi nimeona ina mafundisho ndani yake nikaona ni bora niiweke hapa ili wengine wafaidike na ELIMU hii.

5 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Je na mume akimjali mkewe mambo yanakuwaje hasa kazini? Wakati ukiandaa jibu jaribu kupiga picha za akina mama vigogo kwenye CCM kama vile akina Anna Makinda, Sophia Simba, Anna Abdallah na wengine wenye vifua serikalini kama Mary Nagu. Nadhani ni vizuri mama kumjali baba na baba kumjali mama iwapo wote wanapendana vilivyo na hawatishwi na vyeo wala kipato yaani si malimbukeni na malimpyoto. Ila kama ni kinyume mhhh!

Yasinta Ngonyani said...

Prof: Mhango...Hilo swali lako nami ningependa sana kujua jawabu lake. Ni kweli ni vizuri kujaliana si mmoja tu. Ila kwa dunia ya sasa naona kama inaelemea kwa mmoja sijui ndo ubabe?

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Da Yacinta angalia usinichonganishe na maprof. Ingawa kweli prof ni mwalimu,nami na mwalimu ila bado sijafikia ngazi hiyo japo njia iko wazi na ni suala la muda. Tuombeane uzima.
Nimeuliza swali nawe ukanijibu kwa swali. Acha nikupe jibu kibongo bongo. Je wewe unaonaje na kwanini na vipi?

Serina said...

Yasinta unayoyasema yana ukweli kiasi, lakini inakuaje dunia ya leo? Leo kakosa mke, kesho kakosa mme...kujaliana yafaa iwe pande zote mbili. Mmme kutunzwa na mkewe si jambo la ajabu karne hii, ni onyesho la pendo. Lakini mtu asipojiamini maana haoni mchanjo wake kwenye maendeleo ya kijamii yakiwa makubwa au atarajia 'kuabudiwa' kwa lote lidogo lile sijui inakuwaje tena. Kumbuka msemo...nyani haoni kundule
Majadiliano ya maana haya.

Anonymous said...

naafiki manadiliano yote ila mada ina ukweli kwa zaidi ya asilimia 80. nampa big up mtoa mada .ndeankas