Monday, August 1, 2016

KITUO CHA MABASI CHA MFARANYAKI KUANZA KAZI HIVI KARIBUNI

Kituo kikuu cha mabasi cha Songea kinaendelea kuwa  Msamala
Kituo cha mabasi cha mjini kati ambacho kilizinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwezi Juni mwaka huu kinatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai 29 mwaka huu baada ya kazi ya kukarabati kukamilika.
Ofisa habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo anasema taarifa ambayo imetolewa na mkurugenzi wa manispaa ya Songea Tina Sekambo kwa wakuu wa idara na vitengo katika manispaa hiyo ni kwamba kazi ya kukamilisha ua linalizunguka kituo hicho ipo ukingoni.

Midelo anasema vikao vya Baraza  la madiwani na wataalam wa manispaa hiyo vilipitisha utaratibu utakaotumika ambapo sasa mabasi makubwa ya abiria yatakayokuwa yanaingia mjini Songea yanaruhusiwa kuingia katika stendi hiyo kushusha abiria kwa muda mfupi kisha kurudi kwenye stendi kuu ya mabasi ya Msamala.
Kwa mujibu wa ofisa habari huyo ukarabati wa Kituo hicho cha Mabasi ulianza Novemba 25 mwaka 2014 ambapo hatua ya kwanza imehusisha ujenzi wa eneo la kuegesha na  mabasi uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 499.

Amesema hatua ya pili utahusisha ujenzi wa majengo ya biashara  utakaogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni   5.25 na kwamba  Majengo hayo  ya biashara   yatajengwa na  Wafanyabiahara na wadau mbalimbali  kwa  njia  ya jenga endesha kabidhi.

Licha ya kukamilika kwa ukarabati wa mradi wa kituo cha mabasi,mchumi mkuu wa manispaa ya Songea Raphael Kimary amezitaja changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi kuwa ni pamoja na kuchelewa kwa fedha kutoka Wizarani, mabadiliko ya hali ya hewa yaliyosababisha mvua nyingi kunyesha  hivyo  kusababisha  kuchelewa kukamilika   Mradi  huu kwa wakati.

Baadhi ya wadau wa usafirishaji mkoani Ruvuma  wameunga mkono ushauri wa wataalam na madiwani wa manispaa ya Songea kuwa kituo kikuu cha mabasi kinaendelea kubakia Msamala ili kupanua mji na kuongeza mapato katika manispaa ya Songea.

Pascal Msigwa mfanyabiashara wa mjini Songea amesema serikali kupitia Baraza la madiwani na watalaam wameamua uamuzi wa busara kufanya kituo cha mabasi cha zamani kuwa ni sehemu ambayo mabasi  yatakuwa yanashuka abiria na kurudi kulala Msamala kwa kuwa kituo hicho ni kidogo na hakiwezi kukidhi idadi kubwa ya mabasi yaliopo mjini Songea hivi sasa.
Mwisho.
Habari hii nimeipata  maendeleo ni vita. AHSANTE.

No comments: