Wednesday, August 31, 2016

TUMALIZE MWEZI HUU WA NANE KWA PICHA HII...USAFIRI WETU!

Nimeiangalia hii picha sana na nikaanza kuwaza nilipokuwa msichana mdogo na kapu la mihogo kichwani huku jua kali lawaka na miguu ya ungua kwa juu kali.-:) Naishia  kusema ama kweli tumetoka mbali. Ila hapa inabidi pikipiki hii iende mwendo mdogo sana maana bila hivyohuyo mama ataanguka...

Tuesday, August 30, 2016

KARIBUNI TUJUMUIKE KATIKA MLO HUU AUPENDAO KAPULYA......

 Mlo ni ni kachumbali, safu ya kwanza kwenye hicho chombo cha bluu karibu na kachumbali ni mihogo,katikati ni viazi vitabu na mwisho ni ndizi....
.....na hapa ni sahani yangu ilivyojazwa na cha kuteremshia   ni kinywaji cha uhai  si kingine ni MAJI

Monday, August 29, 2016

NI JUMATATU YA MWISHO YA MWEZI HUU WA NANE(8) NA UJUMBE KUTOKA KWA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO NI HUU! KAMWE USISAHAU AINA HIZI TATU (3) ZA WATU MWAISHANI MWAKO...

1. Mtu ambaye ame/alikusaidia ulipokuwa na hali/wakati ngumu/mgumu

2. Mtu aliyekuacha ukiwa na wakati/hali ngumu/mgumu

3. Mtu aliyekuweka katika hali/wakati ngumu/mgumu.
NAWATAKIENI WOTE MLIOPITA HAPA JUMATATU NJEMA. TUPO PAMOJA!

Friday, August 26, 2016

TUMALIZA IJUMAA HII YA MWISHO WA MWEZI HUU NA MWISHO WA WIKI NA PICHA HII...HUYU KAANZA MAPEMA MNO...

Napenda kuwatakieni mwisho mwema wa juma pia Ijumaa hii ya mwisho wa mwezi huu wa nane. Huyo Ntoto kaanza mapema mno  jamani. Kaaazi kwelikweli....IJUMAA NJEMA. ujumbe wa leo:- Hatuvichukulie vitu kama vilivyo, isipikuwa kwa vile tulivyo.

Wednesday, August 24, 2016

AFRIKA YETU...TANZANIA:-MILA NA UTAMADUNI WETU... UNAWAFAHAMU WAMASAI


Kama tujuavyo Tanzania yetu ina makabila mengi sana kwa hiyo na mila pia tamaduni zitakuwa nyingi...Kwa hiyo nimeona si mbaya nikianza na Kabila la kimasai fuatana nami.....

Kwa kweli hakuna kabila hapa nchini kwetu Tanzania linalotutoa kimasomaso kama kabila la Kimasai kwa kujali na kuendeleza MILA, na kabila hili liko madhubuti kwenye kufuata mila. kuanzia kufuata mila, vyakula wanavyokula mavazi pamoja na ndoa  kwa kweli kuna haja kubwa sana kwa makabil mengine kuiga mfano wa kabila la wamasai.

Kwani ndio kabila ambalo lipo mbele katika kuenzi na kulinda tamaduni zao huwezi kutembea ukamkuta mMasai akiwa hajavaa vazi lao la kimasai tofauti na makabila mengine.  Kwani makabila mengine wanavaa mavazi yao mpaka kuwe na sherehe za kimila/ kitamaduni. Lakini hivi hivi huwezi kuwakuta wakiwa wamevaa, ila kabila hili la kimasai wenyewe mpaka kwenye harusi hawakubali kuiga na kuvaa nguo za aina nyingi

Wamasai wana ustadi unaohitajika kuishi katika pori la Bonde la Ufa. Wao hutembea mbali sana kutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao, nao huchunga mifugo miongoni mwa makundi ya kongoni, punda-milia, twiga, na wanyama wengine wanaoishi katika pori hilo.
Wamasai wanaamini kwamba ng’ombe wote duniani ni mali yao. Imani hiyo inatokana na hekaya inayosema kwamba hapo mwanzoni Mungu alikuwa na wana watatu, naye alimpa kila mmoja zawadi. Yule wa kwanza alipokea mshale wa kuwindia, yule wa pili alipokea jembe la kulimia, na yule wa tatu alipokea fimbo ya kuchunga ng’ombe. Inasemekana kwamba yule mwana wa mwisho alikuwa babu wa kale wa Wamasai. Ijapokuwa watu wa makabila mengine wanafuga ng’ombe, Wamasai wanaamini kwamba ng’ombe hao ni mali yao. Mwanamume mwenye ng’ombe na watoto wengi huheshimiwa na kupewa hadhi katika jamii ya Wamasai. Mwanamume aliye na ng’ombe wanaopungua 50 huonwa kuwa mtu maskini. Kwa msaada wa wake zake na watoto wake wengi, mwanamume Mmasai hutarajia hatimaye kuwa na kundi kubwa linaloweza kufikia ng’ombe 10000. Wamasai hupenda ng’ombe zao. Kila mtu katika familia hutambua vizuri sauti na utu wa kila mnyama kundini. Mara nyingi, ng’ombe hurembeshwa kwa kuchorwa alama za mistari mirefu inayojipinda-pinda na mapambo mengine kwa kutumia chuma chenye moto. Nyimbo hutungwa juu ya sura nzuri za ng’ombe mbalimbali na jinsi wanavyopendwa. Fahali wenye pembe kubwa zilizojipinda hupendwa sana, na ndama mdogo hutunzwa na kushughulikiwa kana kwamba ni mtoto aliyezaliwa karibuni. Nyumba za Wamasai hujengwa na wanawake, nazo hujengwa kwa matawi na nyasi na kisha hukandikwa kwa samadi ya ng’ombe. Nyumba za Wamasai ni zenye umbo la mstatili nazo huzunguka boma ambamo ng’ombe hulala usiku. Nje ya nyumba hizo kuna ua wa matawi yenye miiba unaowalinda Wamasai na ng’ombe zao dhidi ya fisi, chui, na simba wanaowinda usiku. Wamasai hutegemea sana mifugo yao, kwa hiyo ni lazima ng’ombe wawe na afya na nguvu. Wamasai hunywa maziwa ya ng’ombe na kutumia samadi ya ng’ombe kujenga nyumba. Wamasai huchinja ng’ombe mara chache sana.,
Wao hufuga mbuzi na kondoo wachache kwa ajili ya chakula.,Lakini ng’ombe anapochinjwa, kila sehemu ya mnyama hutumiwa. Pembe hutumiwa kutengeneza vyombo, kwato na mifupa hutumiwa kutengeneza mapambo; na ngozi zilizolainishwa hutumiwa kutengeneza viatu, nguo, matandiko, na kamba. 
Wamasai ni watu warefu, wembamba, na wenye sura nzuri. Wao hufunga mashuka yenye rangi nyangavu nyekundu na samawati. Wanawake hujirembesha kwa kuvalia mikufu mipana yenye shanga, na mapambo ya vichwani yenye rangi nyingi tofauti tofauti. Nyakati nyingine mikono na miguu hukazwa kikiki kwa nyaya nyingi nene za shaba. Wanawake na wanaume hurefusha masikio yao kwa kuvaa mapambo na vipuli vizito vyenye shanga. Madini mekundu yaliyosagwa huchanganywa na mafuta ya ng’ombe nayo hutumiwa kupamba mwili. Mida ya jioni  Wamasai  wanakusanyika ili kucheza ngoma, husimama katika duara na kusogea kwa kufuatana na mdundo. Mdundo wa ngoma ukizidi, ile mikufu mipana mizito yenye shanga kwenye mabega ya wasichana inaruka-ruka kwa kufuatana na mdundo. Kisha, moran (mpiganaji) mmoja baada ya mwingine anaingia katikati ya mduara na kuanza kurukaruka juu sana. Wacheza-ngoma wanaweza kuendelea kucheza usiku kucha hadi wote watakapochoka kabisa.

Tuesday, August 23, 2016

SENENE NI WADUDU WANAOTUMIKA SANA NA KABILA LA WAHAYA MKOANI KAGERA KAMA KITOWEO.....

Senene (Ensenene, kwa Kihaya) ni miongoni mwa wadudu wanaotumiwa sana na kabila la Wahaya mkoani Kagera kama kitoweo, pengine kuliko kabila lolote tangu enzi za mababu.
Pamoja na wadudu hao kuheshimika katika kabila la Wahaya, historia kamili ya asili ya wadudu hao bado haijulikani.
Mwanzoni senene waliliwa na wanaume peke yake. Wanawake walionywa wawe na haya siku zote na wasivunje mwiko kwa kula senene na vitu vyote vilivyokatazwa. Wanawake wote walikuwa na utii wakiheshimu mila na desturi za kabila lao hivyo kutokana na haya hiyo waliitwa “WAHAYA”. 
Wasichana walipeleka zawadi ya senene kwa wachumba wao kama ishara ya kuonyesha upendo na utayari wa kuolewa na mchumba huyo. Msichana ambaye hakufanya hivyo uwezekano wa kuolewa na mchumba wake ulikuwa mdogo, hivyo senene walitumika kama ishara ya upendo na uaminifu.
Zipo aina nyingi za senene lakini wale wanaozungumziwa hapa wamegawanyika katika kundi lijulikanalo kama Orthopterous. Hawa ni jamii ya panzi wapole ambao hawana tabia ya kuharibu na kuteketeza makazi yao kwa chakula kama walivyo nzige wengine. Senene huzaliana kwa wingi katika mwambao wa maziwa makuu baada ya kutaga mayai yao ardhini kipindi cha kiangazi.
Baada ya kutaga mayai na kuangua mzunguko wa maisha yao huishia kati ya mwezi Oktoba na Desemba ambapo kipindi hiki huwa ni msimu wa mvua za vuli zijulikanazo kwa wahaya kama Omusenene. Hiki ni kipindi ambacho senene huruka wakiwa katika makundi wakihitimisha safari ya maisha yao.
Pamoja na kutumika kama kitoweo pia jamii imeanza kufaidika na senene kama chanzo cha kujipatia kipato, jambo ambalo limeufanya mkoa wa Kagera hasa Bukoba kujulikana sana kitaifa na kimataifa, pia kutokana na uchunguzi wa madaktari imeonekana kuwa senene wanaongeza vitamin “C”

Monday, August 22, 2016

WIKI MPYA,JUMATATU MPYA NA CHANGAMOTO MPYA...MWONEKAN MPYA WA PICHA YA KAPULYA WENU:-)

Kwanza ilikuwa hivi ....



Baadaye dada yangu Mariam akaona juna vitu vinakosekana  kama uonavyo  alivyoorodhesha katika picha....
Miaka imepita na jana ndipo nilipotumiwa hii picha kwa mfano huu. Hakika sikuitambua kabisa. Na bado sijitambui  maana hiyo si tabia yangu...Je wewe msomaji unauonaje huu mfano wa hii picha ya Kapulya ya mwisho?

Saturday, August 20, 2016

NAWATAKIENI JIONI HII YA JUMAMOSI YA LEO IWE NJEMA ...

Jumamosi njema kwa atakayepita hapa na msosi ndio huu hapa tena wa kutosha tu...JUMAMOSI NJEMA..WOTE MNAPENDWA!

Wednesday, August 17, 2016

KUMBUKUMBU :- LEO NI MIAKA KUMI NA MBILI (12) KAMILI TANGU MAMA YETU MPENDWA ALANA NGONYANI ATUTOKE!!

KUZALIWA 2/10/1952-KUFA 17/8/2004
Mama ni miaka kumi na mbili  sasa tangu ututoke. Umetuacha na majonzi pia maumivu moyoni mwetu. Tunaukumbuka sana uwepo wako, tukiamini Mungu angekuacha japo kwa miaka michache. Midomo yetu haiwezi kuelezea jinsi tulivyokupenda. Lakini Mwenyezi Mungu anajua ni jinsi gani tulivyokupenda. Na jinsi gani tunakukumbuka, mapenzi yako, wema wako. Pia kama mama kwa mwongozo wako katika nyumba yetu, ambayo sasa ni upweke mtupu bila wewe.
Tunakukumbuka sana,  sisi wanafamilia wote pamoja na ndugu wote na pia marafiki. KIMWILI HAUPO NASI, BALI KIROHO UPO NASI DAIMA. MWENYEZI MUNGU AIPUMZISHE ROHO YAKO MAHALA PEMA PEPONI. AMINA!!!

Tuesday, August 16, 2016

KATIKA MAISHA NI BARAKA KUBWA SANA KUFIKIWA NA WAGENI:- KWA HIYO NASI JANA JUMATATU TULIPATA HIYO BARAKA

 Mlo wa pamoja, kulikuwa na vyakula mbalimbali kama vile  nyama choma nk. Ilikuwa ni  furaha sana kwa kweli....
Baada ya kula muda wa kuondoka wagen ulifika lakini hakuwa vizuri kuondoka tu bila kuacha ukumbusho wa. Ndiyo kama muonavyo ila wawili walikuwa wapiga picha...
Nawatakieni siku njema!

Monday, August 15, 2016

TUANZE WIKI HII/JUMATATU HII NA HILI NENO KUSAMEHE:- KUSAMEHE NI MTIHANI/JITAHIDI USHINDE!

Katika tembea tembea nimekutana na hii makala kuhusu kusamehe....nikaona Elimu hii nisiwanyima ndugu zanguni..karibu muunganie nami.... 


Katika maisha hakuna jambo gumu kama kusamehe na hakuna kitu chenye faida kama kusamehe. Kuna watu katika maisha wapo ili tuumie na TUJIFUNZE. Wengine wapo ili tukisha umia wao watuumize zaidi ili tukose imani kwa wengine!
Lakini katika wote, wapo ambao kazi yao ni kutufariji, wao Inawezekana walipitia magumu kama yetu hivyo wana fahamu njia ya kutokea lakini kwa sababu tuliumizwa zaidi hatutaki kuwaamini hata wao. Ukisamehe unaweza kuamini upya!
Ni kweli katika maisha bila watu kama hao hatuwezi kuitwa "imara". Umewahi KUJIULIZA kwanini mtu anaitwa MVUMILIVU?? Kipimo chake ni kipi?? Uwezo wa kusamehe na kusonga mbele bila malalamiko ndiyo UVUMILIVU HALISI.
HAUNA jambo gumu kama kusamehe maumivu ambayo yanajirudia kichwani, yana choma moyo kama panga kali...... Vuta picha mtu anakuumiza alafu vilevile anataka akumalize kabisa! Alafu baada ya kuumbuka anaomba msamaha!
Vuta picha umemfumania mkeo au mume wako alafu una ambiwa samehe! Vuta picha mtu kamuua mzazi wako au ndugu yako kisha una ambiwa samehe! Moyo unauma, akili inakataa, mwili unawaka hasira lakini bado una ambiwa samehe, jikaze tu!
Wengine walikusababisha uishi maisha ambayo unaishi kwa sasa, unatamani hata wafe! Lakini una ambiwa samehe! Msamaha ni nini hasa?? Unalia ukijipiga kifua, msamaha ni nini?? Machozi ya uchungu yanakutoka kujaribu kuosha hasira yako lakini moyo unakataa!
Utaimba nyimbo zote za kujifariji lakini moyo unasema HAPANA NIMEUMIZWA SANA. Unashindwa kula na kulala vizuri kwa sababu umeumia! Mbaya zaidi hisia zikiumia ni hatari kuliko Simba aliye katwa mguu! Na wengi wana umizwa sana kwa sababu ya kitu kimoja tu IMANI.
Wengi leo wame umizwa sana na Mama mkwe, shangazi, wazazi, ndugu, marafiki, wapenzi, majirani na kadhalika! Lakini tiba ni moja tu, KUSAMEHE. Kutokusamehe ni sawa na kumsaidia shetani kufanya kazi maana mawazo yako yatakuwa sawa na shetani anavyo waza (uharibifu).
Kusamehe ni tiba ya presha, ni tiba ya kichwa na moyo. Kusamehe ni dawa ya maisha na pia ni baraka kwako! KUSAMEHE kunamfanya MUNGU akuamini ili upande daraja la imani la kiwango kingine cha juu zaidi.
Nakumbuka katika maisha yangu, nimewahi KUUMIZWA mara nyingi tu katika mambo tofauti tofauti, lakini mara zote napata somo jipya. Pamoja na kujifunza sana lakini kuna muda ilinibidi NISAMEHE KWA MACHOZI, yaani nasamehe nikiwa natokwa machozi kwa lengo la kuuponya moyo wangu!
Ni kweli umeumia lakini Samehe sasa, samehe leo, samehe kesho, samehe siku zote! Binadamu wana umiza sana sana sana tena sana lakini jivike moyo mkuu, samehe ili maombi yako yakubaliwe na MUNGU. Kumbuka msamaha ni tiba, ni amani ni upendo ni faida.
NB: Kwa yeyote aliye wahi kuniumiza kwa namna yoyote ile NIMEMSAMEHE, kwa yeyote yule anaye ona nimemuudhi na anisamehe, kwa yeyote yule ambaye huwa anahisi sijamsamehe na afahamu sasa kwamba NIMEMSAMEHE asitazame ukubwa wa kosa au mazingira ya ugomvi, atazame utumishi na huruma ya MUNGU ndani yangu, amen.
CHANZO: Na Charles Francis M,

Sunday, August 14, 2016

UJUMBE WA JUMAPILI YA LEO 14/8/2016

Katika sehemu nyingi za kazi utakuta kuna baadhi ya watu hawawapendi wenzao. Lakini wewe fanya kazi haupo /haukuja kufuata /kutafuta urafiki na wao.
............................................................................................................................
TUENDELEE NA SALA HII KUTOKA KWANGU KUJA KWENU:-
Eee Mungu wangu nakuomba uwalinde familia, rafiki na jamii yote. Nakuomba uwalinde wakati wote na uwape afya njema, furaha na uwashushie baraka zako. AMINA.
JUMAPILI  IWE  YENYE BARAKA NA UPENDO KWAKO/KWENU! NA IKUMBUKWE KWAMBA NI JUMAPILI YA KUPAA KWA MAMA YETU MPENDWA BIKIRA MARIA 

Friday, August 12, 2016

NAPENDA KUWATAKIENI MWISHO MWEMA WA JUMA ....LEO TUPO MKOANI IRINGA...

Watumiaji wa kinywaji aina ya Ulanzi wakifurahia kinywaji hicho katika mkoa wa Iringa. IJUMAA NJEMA NDUGU ZANGU....

Thursday, August 11, 2016

PICHA YA WIKI: TANZANIA -MALAWI BARABARA KUU KARIBU NA MBEYA.....

Nimependa mandhari ya hii barabara kiai kwamba natamani kuendesha ...maana ipo safi sana...na ndiyo maana nimeamua iwe picha ya wiki hii....

Tuesday, August 9, 2016

MWONEKANO MPYA WA KAPULYA WENU... WA MWAFRIKA HALISI KABISA...


Hapa sijui mapozi au ndo furaha 
Baada ya kuangalia sana nikaona nywele zangu si nyeusi si isipokuwa zimepata ugeni ...angalia tu utaona :-) Unajua nini nimependa sana hiyo na naahidi sitamfukuza mgeni huyo kwani kuna wengine wanamtafuta ...Ila duh sijui nitaweza kuchana kila siku maana ni kipilipili/ulezi hasa

Monday, August 8, 2016

KUANZA KUPOTEA KWA DESTURI YA UKARIBU WA KIFAMILIA KUNAVYOATHIRI MALEZI

Malezi katika mazingira yetu ya ki-Afrika ni suala nyeti. Kwa kutambua umuhimu wa malezi katika kujenga jamii yenye ustawi, wa-Afrika tumekuwa na desturi ya kuelekeza nguvu zetu nyingi katika malezi ya wanetu. Kwa mfano, tangu mtoto anazaliwa, ilikuwa ni lazima alale kitanda kimoja na wazazi wake kwa muda unaozidi miaka miwili. Mtoto mchanga hakuachwa alale kwenye kitanda chake mapema kwa sababu za msingi zilizokubalika katika jamii zetu.


MAMA AKIWA KAMBEBA MWANAE
Aidha, mtoto daima alikulia mikononi mwa watu wazima aliowafahamu vyema. Watu hawa ama aliishi nao kwenye boma la wazazi wake au walitoka miongoni mwa jamaa inayomzunguka. Muda mwingi mtoto alibebwa mgongoni kwa mama yake au dada zake. Desturi ya kubeba watoto mgongoni ilifanya suala la ukuaji wa mtoto kufuatiliwa kwa karibu sana na imethibitika kisayansi kusaidia kujenga muunganiko wa kihisia kati ya mzazi na mtoto. Jambo hili, hata hivyo, halieleweki kwa wageni wa bara hili wanaodhani ni aina nyinine ya udhalilishaji wa mtoto.

Chakula cha pamoja ni kitamu sana

Wakati wa jioni, familia zilikuwa na desturi ya watoto kukaa na wazazi wao kijinsia. Baba aliota moto na watoto wa kiume akiwasimulia mambo mbalimbali ya kimaisha. Kadhalika, mama naye alifanya kazi za jikoni kwa ushirikiano wa karibu na watoto wa kike. Chakula kilipokuwa tayari kililiwa kwa ushirikiano. Muda wa chakula ulifahamika, na kwa kweli, kila mtoto aliwajibika kuwepo kupata chakula. Kwa kuwa chombo kilichotumika kulia chakula mara nyingi kilikuwa kimoja basi kila mmoja katika familia alilamizika kula kwa ushirikiano na wenzake.

Desturi hii ya kukaa karibu na watoto na kufanya mambo mengi kwa pamoja iliwasaidia wazazi kuwafundisha watoto maarifa na ujuzi wa aina mbalimbali. Vile vile, ukaribu huu ulikuza uhusiano wa karibu wa kifamilia. Kadhalika, karibu huu uliwahakikishia watoto usalama wao. Kisaikolojia walijua hawana wasiwasi kwa sababu baba na mama wapo na wangepigana na yeyote anayetishia usalama wao. Watoto waliwategemea wazazi wao.

Upo ushahidi wa kiutafiti kwamba kutegemewa kwa mzazi ni nguzo kuu ya malezi. Kwamba mtoto huiga mengi wa mzazi ikiwa anaamini mzazi huyo ni wa kutegemewa na yuko upande wake. Hali hii ilimfanya mtoto asiwe na wasiwasi na usalama wake pale yalipojitokeza mazingira ya kutengana kimwili na kwa hivyo wazazi kwa kweli hawakulazimika kuwa na watoto muda wote. Kama tutakavyoona katika mfululizo huu, hali hii ya mtoto kumwamini na kujisikia salama mikononi mwa mzazi inategemea sana uwepo endelevu wa mzazi kimwili na kihisia tangu siku za mwanzo za maisha ya mtoto.

Hata hivyo, kadri mwanadamu anavyozidi ‘kuendelea’ na ‘kustaarabika’, ndivyo desturi hii ya kupatikana kwa wazazi nyumbani inavyozidi kukosa umaarufu. Kwa mfano, ipo dhana inajengeka katika jamii kwamba maendeleo halisi ni vitu. Matokeo ya imani hii ni kutufanya tutumie muda mwingi ‘kuhusiana na vitu’ zaidi kwa gharama ya mahusiano na ustawi wa familia zetu.

Kadhalika, zipo changamoto nyingine za kijamii zinazotishia desturi ya familia. Kuna masuala kama kazi/ajira zinazowatenganisha wazazi na familia, misukosuko ya kimahusiano inayozaa talaka na/ama kulazimisha malezi ya mzazi mmoja, ujio wa shule za bweni kwa watoto wadogo pamoja na matatizo kadha wa kadha yanayofanya watoto wadogo wakue katika mazingira magumu yasiyo na uangalizi mzuri. Haya tutayaangalia wakati wake ukifika.

Kwa hiyo, ili kukabiliana na changamoto hizi mpya, upo umuhimu mkubwa wa kujadili tafiti zilizochunguza athari za mazingira haya mapya ya kimalezi ambayo kwa kiasi kikubwa hayakuwepo huko nyuma. Kwa mhutasari, tunaweza kutaja suala kuu linalojitokeza kwa haraka. Kwamba uhusiano kati ya mzazi na mtoto unaathiri mahusiano ya mtoto huyo na watu wengine. 

Sunday, August 7, 2016

JUMAPILI YA LEO TUTEMBELEA KWETU LITUMBANDYOSI:- HATIMAYE WANALITUMBANDYOSI NASI TUMEPATA PADRE....

 Jina lae ni FURAHA HENJEWELE SAMBALITOLA
 Shughuli za upadirisho zipo motomoto
Ndani ya kanisa letu la Litumbandyosi 4/8/2016...TUMWOMBEE AWE NA AFYA NJEMA ILI AWEZE KUIFANYA KAZI YA MUNGU VIZURI. HONGERA SANA WANALITUMBA.

Saturday, August 6, 2016

NAWATAKIENI WOTE MTAKAOPITA HAPA MAPUMZIKO MEMA YA MWISHO WA JUMA....

Mdada inaonekana ni mpenzi wa maua...:-)  Haya muwe na Jumamosi njema panapo majaliwa tutaonana...Kapulya...

Friday, August 5, 2016

NAIPENDA AFRIKA YANGU NA UTAMADUNI WAKE.....

Mara nyingi sana huwa nakutana na maswali mengi sana...kama vile:- Hivi kwa nini waafrika mnaweza kubeba mtoto mgongoni na kubebamzigo kichwani kwa wakati mmoja? au mnawezaje kubabe ndoa la maji kichwani bila kuanguka? Huwa nawaangalia na kufurahi tu kwa raha na kujivuna ...Je wewe umewahi kufikiria hili? Lakini sijui huku tuendeko kama hasa hili la kubeba watoto mgongoni litaendelea...

Thursday, August 4, 2016

MAISHA NA MAFANIKIO:- JIKUBALI

 MFANYABIASHARA WA KUUZA MBOGA ZA MAJANI AKIKOKOTA BAISKELI 

Maisha ya watu wengi sana yanashindwa kufanikiwa kwa sababu watu hawajikubali. Ngoja nikuambie kitu leo:- Kila mwanadamu aliyeumbwa hapa duniani, ameubwa na kitu tofauti na mtu mwingine. Hii ina maana kwamba kila mwanadamu ana kitu tofauti kikubwa ambacho anaweza kukifanya hapa duniani kuliko mtu mwingine. Japo sikuambii wewe ni bora kuliko watu wengine, lakini ninachokuambia wewe una kitu bora zaidi cha kufanya katika  maisha yako kuliko watu wengine.
Tatizo kubwa wanalolifanya  watu wengi wasiweze kufanya vile ambavyo wanataka ni kutokujikubali. JIKUBALI. Tunaweza tukazaliwa tumbo moja, tukasoma darasa moja, lakini wote tukawa na kitu ambacho kitatutofautisha. Kinachokufanya uendelee kuwa hivyo ulivyo ni kwa sababu tu haujikubali na haujiamini kuwa wewe ni mtu tofauti.
Ngoja nikumnie kitu kingine  tena,  wewe ni mtu tofauti sana, na unaweza kufanya vitu vikubwa sana kwenye hii dunia. Lakini kitu pekee unapaswa kukifanya kuanzia  leo ni KUJIKUBALI. Usikubali mtu akukatishe tamaa, JIKUBALI, usikubali mtu akuambie hauwezi...JIKUBALI, asikuambie mtu hauwezi kufanya hicho unachofanya . ANZA KUJIKUBALI unapojikubali mambo mengine yanakuwa rahisi. Hata kama leo unahaingaika na magonjwa kiasi gani usikubali kuambiwa nawengine JIKUBALI WEWE, ukijikubali utapata nafuu.
Kulikuwa na dada mmoja mzuri sana, lakini kasoro yake ilikuwa moja tu alikuwa na matege. Alichokifanya dada huyu ni kuvaa nguo fupi ili watu waone matege yake....ALIJIKUBALI na watu wakamkubali.
Tatizo kubwa tulilokuwa nalo sisi au watu wengi ni kutoJIKUBALI. Kujificha ule uhalisia wao, kujificha ule mwonekano wao halisi wa wao na hii inawafanya maisha yai kutokubalika kabisa. Ushauri wangu JIKUBALI ULIVYO halafu kila siku songa mbele. ukijikubali na wengine watajikubali. Ndugu yangu jikubali kwa hali yoyote uliyo nayo leo ili ikufanye usonge mbele.

Wednesday, August 3, 2016

LEO TUANGALIE BAADHI YA ZILIPENDWA....

Je? Unavikumbuka hivi? Ila naona kama vinarudi tena.  Vya kale ni dhahabu....

Monday, August 1, 2016

KITUO CHA MABASI CHA MFARANYAKI KUANZA KAZI HIVI KARIBUNI

Kituo kikuu cha mabasi cha Songea kinaendelea kuwa  Msamala
Kituo cha mabasi cha mjini kati ambacho kilizinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwezi Juni mwaka huu kinatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai 29 mwaka huu baada ya kazi ya kukarabati kukamilika.
Ofisa habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo anasema taarifa ambayo imetolewa na mkurugenzi wa manispaa ya Songea Tina Sekambo kwa wakuu wa idara na vitengo katika manispaa hiyo ni kwamba kazi ya kukamilisha ua linalizunguka kituo hicho ipo ukingoni.

Midelo anasema vikao vya Baraza  la madiwani na wataalam wa manispaa hiyo vilipitisha utaratibu utakaotumika ambapo sasa mabasi makubwa ya abiria yatakayokuwa yanaingia mjini Songea yanaruhusiwa kuingia katika stendi hiyo kushusha abiria kwa muda mfupi kisha kurudi kwenye stendi kuu ya mabasi ya Msamala.
Kwa mujibu wa ofisa habari huyo ukarabati wa Kituo hicho cha Mabasi ulianza Novemba 25 mwaka 2014 ambapo hatua ya kwanza imehusisha ujenzi wa eneo la kuegesha na  mabasi uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 499.

Amesema hatua ya pili utahusisha ujenzi wa majengo ya biashara  utakaogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni   5.25 na kwamba  Majengo hayo  ya biashara   yatajengwa na  Wafanyabiahara na wadau mbalimbali  kwa  njia  ya jenga endesha kabidhi.

Licha ya kukamilika kwa ukarabati wa mradi wa kituo cha mabasi,mchumi mkuu wa manispaa ya Songea Raphael Kimary amezitaja changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi kuwa ni pamoja na kuchelewa kwa fedha kutoka Wizarani, mabadiliko ya hali ya hewa yaliyosababisha mvua nyingi kunyesha  hivyo  kusababisha  kuchelewa kukamilika   Mradi  huu kwa wakati.

Baadhi ya wadau wa usafirishaji mkoani Ruvuma  wameunga mkono ushauri wa wataalam na madiwani wa manispaa ya Songea kuwa kituo kikuu cha mabasi kinaendelea kubakia Msamala ili kupanua mji na kuongeza mapato katika manispaa ya Songea.

Pascal Msigwa mfanyabiashara wa mjini Songea amesema serikali kupitia Baraza la madiwani na watalaam wameamua uamuzi wa busara kufanya kituo cha mabasi cha zamani kuwa ni sehemu ambayo mabasi  yatakuwa yanashuka abiria na kurudi kulala Msamala kwa kuwa kituo hicho ni kidogo na hakiwezi kukidhi idadi kubwa ya mabasi yaliopo mjini Songea hivi sasa.
Mwisho.
Habari hii nimeipata  maendeleo ni vita. AHSANTE.