Wednesday, June 6, 2012
Wanafunzi hawa wanafanyishwa vibarua
Ije jumatano ya KIPENGELE CHETU CHA MARUDIA NDIO LEO NA LEO NIMEONA KWA VILE WIKI ILIYOPITA TULIZUNGUMZIA KIDOGO KUHUSU ELIMU BASI TUENDELEE KIDOGO NA MADA HII YA SHULE NA ELIMU.
Wanafunzi wa shule ya msingi Ndingine mwambao mwa ziwa Nyasa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakifanyishwa kazi ya kusomba tofali muda wa masomo
LICHA ya serikali kupiga marufuku walimu kuwafanyisha vibarua wanafunzi wakati wa masomo,bado baadhi ya shule hasa katika maeneo ya vijijini,zinaendelea na tabia hiyo hali ambayo inachangia kuzorotesha elimu nchini.
Uongozi wa shule ya msingi Ndingine iliyopo kata ya Ngumbo mwambao mwa ziwa Nyasa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma bado unaendelea kuwafanyisha vibarua wanafunzi licha ya afisa elimu wa wilaya hiyo kupiga marufuku jambo hilo.
Uchunguzi ambao umefanywa na mwandishi wa habari hizi katika kijiji cha Ngumbo hivi karibuni ulibaini wanafunzi baadhi wakiondolewa madarasani tena majira ya asubuhi na kwenda kufanyishwa kibarua cha kubeba tofali za kuchoma kutoka kwenye tanuli lililokuwa mtoni hadi mahali ambapo nyumba inajengwa umbali wa kilometa tatu.
Wanafunzi wa darasa la tatu na la sita kutoka shule hiyo walishuhudiwa wakisomba tofali hadi nne kichwani huku wakilalamika kuwa wanafanya kazi ambayo hawanufaiki nayo licha ya kuambulia maumivu kutokana na mzigo na umbali.
Baadhi ya wanafunzi wanasoma darasa la sita walipohojiwa ,walidai kuwa mwalimu amewaambia huo ni mradi wao ambao utawawezesha kupata fedha kwa ajili ya sherehe za mahafali ya kumaliza elimu ya msingi hapo mwakani watakapomaliza darasa la saba.
Hata hivyo wanafunzi wa darasa la tatu walilalamika kuwa wao wamelazimishwa na mwalimu kwa kuwa hawapati chochote na kwamba fedha zote wanachukua walimu,ingawa tofali zinachangia kuchafua sare zao za shule ambazo wakirudi nyumbani inawalamu wazazi kununua sabuni ili kufua nguo zao.
Miongoni mwa wazazi waliohojiwa kuhusiana na watoto wao kuendelea kufanyiwa kazi za vibarua,waliomba serikali ya wilaya kuwachukulia hatua walimu wa kata za Ngumbo na Liwundi kwa kuwa wamezoea kuwafanyisha kazi wanafunzi wao licha ya wazazi na walezi kukataa.
“Sisi wazazi kwenye vikao tulishakubaliana tutachangia shilingi 2000 kila mzazi ,walimu waache tabia ya kuwafanyisha kazi watoto wetu badala yake waendelea na kusoma lakini walimu bado wanaendelea kuwafanyisha kazi mbalimbali wanafunzi kama vile kuchota maji ya walimu,kubeba tofali,kukata matete,kubeba kuni pamoja na kazi nyingine nyingi’’,alisema Martha Nchimbi mkazi wa Mkili.
Hata hivyo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ndingine Aidan Mbilinyi alipohojiwa kuhusiana na kuwafanyisha kazi za vibarua wanafunzi alidai kuwa katika shule yake wanafunzi hawafanyishwi vibarua badala yake wazazi wanachangia kila mwaka shilingi 2000 kwa ajili ya sherehe za mahafali ya darasa la saba .
Katika kikao cha walimu wakuu wote wa wilaya ya Mbinga ambacho kiliitishwa na idara ya elimu chini ya mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Septemba 23 mwaka huu pamoja na mambo mengine waliazimia kuacha kuwafanyisha vibarua wanafunzi vikiwemo kusomba tofali na kuvuna kahawa.
Afisa elimu wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali amekemea tabia ya walimu wakuu kuendelea kuwafanyisha kazi wanafunzi na kusisitiza kuwa kuanzia sasa atachukua hatua za kinidhamu kwa walimu wakuu wote ikiwa ni pamoja na kuwashusha vyeo vyao.
“Maazimio yalipitishwa tangu mwezi Septemba mwaka huu marufuku wanafunzi kufanyishwa vibarua,shule zibuni miradi ya kujitegemea itakayowawezesha kupata fedha,pia walimu kuwapatia wanafunzi maarifa ya kujitegemea kwa mfano kulima bustani baada ya saa za masomo’’,alisisitiza.
Mkali aliyataja mambo ambayo yamechangia kushuka kwa elimu na ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi wilayani Mbinga kuwa ni pamoja na wanafunzi kufanyishwa vibarua,utoro na ulevi kwa baadhi ya walimu,walimu kutofundisha siku zote 195 zilizopangwa na wizara,walimu wakuu kutofuatilia ufundishaji,ukaguzi wa maandalio na kazi za watoto.
Takwimu zilizokusanywa katika shule 321 katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kuanzia darasa la tatu hadi la saba zinaonesha kuwa wanafunzi 15,128 kati ya 116,966 hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu
Makala hii nimeipata hapa JAMIIFORUM IMEANDIKWA NA Albano Midelo hapo decemba 13th 2011 pia kwa kuweza kusoma habari nyingi inayofanana na hii ingia hapa. TUKUTANO TENA JUMATANO IJAYO PANAPO MAJALIWA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
3 comments:
Hapa sasa tuseme elimu ni ufunguo wa maisha au kufuli la maisha?
Mimi ningesema ni kufuli la maisha...wazazi wanasema mwanangu kaenda shule kupata elimu kumbe anafanya kazi kwa mwalimu...nakumbuka hizi kazi nimezifanya sana kuchota maji, kulima shamba la mwalimu, kufagia na pia hata kulea watoto wao... nakajua hizi kazi siku hizi hazipo kumbe
hizi kazi nakumbuka nimezifanya sana pia, walimu wanasema zinmjenga mwanafunzi kuwa Imara, sina uhakika na hilo, je! walimu wanasemaje kuhusu hilo??? mimi huruma sana kuhusu wanafunzi, tena mikoani huwa kuna baridi sana, utakuta wanafunzi wanatetemekaaaa, lakini wapo tu na mizigo, au kubeba matofali ya walimu
Post a Comment