Wednesday, June 1, 2011

TUONDOE SEHEMU ZA MIILI YETU ZILIZOKUFA.

Kupitia Jongoo huyu alijifunza kitu muhimu maishani


Mzee mmoja, Salim Keni wa Makongorosi huko Chunya mkoani Mbeya, anasema kuwa siku moja alishangazwa sana na kauli ya mtoto wake wa miaka kumi. Anasema alikuwa amekaa nje ya nyumba yake jioni. Hapo alipokuwa amekaa alikuwa akiangalia jongoo. Jongoo huyo alikuwa ameumia sehemu yake ya nyuma, ambayo sasa ilikuwa imekauka, yaani imekufa.

Sehemu ya mbele ambayo ilikuwa ni nzima iliunganishwa na sehemu hiyo ya nyuma au ya mkia kwa kiuzi kidogo sana. Tunaweza kusema kwamba sehemu hiyo ya mkia ilikuwa inakokotwa na ile ya mbele. Hali hiyo ilimfanya jongoo yule kupata shida sana ya kusogea. Ukweli ni kwamba, hata kama sehemu ile ya nyuma ya jongoo yule ingeondolewa wala asingebaini, kwani ilikuwa sio sehemu ya mwili wake tena-ilishapoteza uhai.

Lakini aliendelea kuikokota kama vile bado alikuwa akiihitaji. Wakati Mzee Salim akimshangaa jongoo yule, mtoto wake huyo ambaye ni mtundu sana alifika hapo, ambapo naye alimuona jongoo huyo.
Alikaa chini karibu na baba yake na kumkodolea macho kabla hajatoa kauli hiyo ya kushangaza. ‘Sasa baba, huyu mdudu si anapata shida bure, kwa nini asiache hii sehemu ya nyuma ili atembee vizuri, kwa sababu yenyewe imekauka…..’

Kabla baba yake hajajibu, mtoto yule alichukua kijiti na kutenganisha sehemu ya mbele na ile ya nyuma ya jongoo yule. Baada ya kufanya hivyo, jongoo yule aliweza kuongeza kasi ya kutembea na alionekana wazi kwamba amekuwa huru.

Mzee Salim alishikwa na butwa kwani hakuwa amepata muda wa kufikiri hivyo wakati akimtazama yule jongoo. Ni kweli kabisa, mtoto wake alikuwa amemfunulia kitendawili kikubwa sana cha maisha. Ya nini kutembea na sehemu ya mwili ambayo haina kazi, ambayo imekufa, ambayo angeweza kuiacha na kuwa huru zaidi?

Mtoto yule aliona wazi kabisa pamoja na akili yake ya kitoto kwamba, kama mdudu yule angemudu kuiacha sehemu ya mwili wake ambayo ilikuwa tayari imekufa angeweza kuishi katika uhalisia.

Uvumbuzi wa mtoto yule ni uzumbuzi wetu sote. Ni lini nasi tutaamua kuacha sehemu zetu ambazo zimekufa ili tuweze kuishi katika uhalisia? Sehemu zetu za miili zilizokufa ni zipi? Ni maumivu ya kimaisha yaliyopita. Ni mizigo ya mashtaka ya dhamira zetu na haja yetu ya kutaka kulipiza visasi. Ni masikitiko na majuto ya mambo yaliyopita, ambayo bado yanatuumiza hadi leo, mambo ambayo hayana maana yoyote tena kwetu.

Wengi wetu tunatembea au kuishi na mizigo mizito sana ya mambo yaliyopita, mambo ambayo ukweli ni kwamba hayana maana yoyote kwetu. Lakini kwa sababu tumeamua kutembea nayo, hutuzuia kwenda kama tunavyotaka, hutuzuia kufurahia maisha na hutuzuia kuwa huru katika mambo yetu mengi kimaisha.

Bila shaka tukiwa jasiri kama mtoto yule na kubaini sisi wenyewe kwamba tunatembea na sehemu zetu ambazo zimekufa, tutakuwa tayari kuziondoa na kuwa huru. Ni vizuri kujiuliza kama kuna mambo yaliyopita ambayo yanatuzuia katika kufanya na kufikia malengo yetu, ambayo yanatunyima furaha na kutufanya tujione kama watumwa. Je mambo hayo yana maana gani kwetu wakati yameshapita? Ni wazi yamekua, tunayabeba bure.

Kuna ambao wanalia hadi leo kufuatia vifo vya wapenzi wao vilivyotokea mika kumi iliyopita. Kuna wanaohangaika kutaka kulipa visasi vya yale mabaya waliyotendewa miaka kadhaa nyuma. Kuna wale ambao wanasumbuliwa na mawazo ya jinsi walivyofilisika au kusalitiwa na jamaa au wapenzi wao. Hii yote ni mizigo ya bure, ni sehemu za miili au maisha yao ambazo zimekufa, lakini wanaziburuza.

Nimekuwa nikiandika hapa mara kwa mara kwamba mambo yaliyopita hayapaswi kutuumiza, kutuondolea furaha na kutufanya tujihisi wanyonge na tusio na thamani, kwa sababu mambo haya hayana maana yoyote tena kwetu. Hata kama utafikiri kwa miaka mia kuhusu jambo Fulani ambalo tayari limekutokea, huwezi kulibadili hata kwa chembe ndogo sana, sanasana unalipa uzito ili likutese zaidi.

Ili uishi hasa, uishi kwa kadiri ya utashi wa kanuni za kimaumbile, inakupasa uondoe sehemu ya mwili wako ambayo imeshakufa. Bila kuiondoa sehemu hiyo, ni lazima utaelemewa sana.
Habari hii iliwahi kuandikwa katika Gazeti la Jitambue.


Kama kawaida leo ni Jumatano ambayo ni siku ya kipengele chetu cha marudio ya mada/makala /picha nk mbalimbali na leo mada hii inatoka kwa mzee wa Utambuzi na Kujitambua .

6 comments:

Rachel Siwa said...

Asante sana da Yasinta nimekupata vyema kwa kisa hiki cha jongoo!

Hakika tuondoe sehemu za miili yetu zilizokufa!! ili tuishi kwa Amani,Upendo, Furaha .........

Simon Kitururu said...

Mmmh!

Goodman Manyanya Phiri said...

Mtoto yule ni RIGHT-BRAINED, kinyume na baba yake aliekuwa LEFT-BRAINED. Mtoto anatawaliwa na jazba lakini baba ni fikra tupu.


Ndiyo, mtoto amempa jongoo uhuru wake; lakini angeweza pia kumtoa roho kabla ya siku zake kwenda kwa Mola!


Hata mtu akibeba mzigo asiyestahili kubeba, sababu itakuwepo tu kwanini anafanya hivyo na sababu hiyo inaweza ikawa kubwa kuliko huo mzigo!

Goodman Manyanya Phiri said...

Baba yangu mzazi aliwahi kunipa hadithi moja ya huko kwao, Rumphi (Malawi) alikotokea.


Na alisema siku moja mfalme kijana na mwenye akili nyingi aliwapatia Bi Vizee na mababu wenye miaka mingi suluhisho: Wauliwe kwani hawana kazi yoyote ile katika jamii bali kula na kunya tu! (kumradhi lugha, ni hadithi tu!)


Nakweli, kila kijana alimshambulia na kumwua bibi au babu yake aliekaa tu nyumabani kwa uzee. Lakini kijana mmoja tu katika ufalme mzima alificha babu yake.

Siku moja joka likajisokota kwa mfalme usingizini mwili mzima na jeshi ambalo lilikuwa ni vijana tupu likaja na mikuki na wengine bunduki ili kumwua nyoka na kuokoa maisha ya Mfalme.


Baadaye wakaona haitawezekana kwani mkuki na risasi vitakula nyama sawa tu ya nyoka kwa ya binadamu, kwa hiyo mfalme huenda akajeruhiwa naye vibaya labda hata kufa katika kuwua nyoka huyo.


Suluhisho?


HAMNA SULUHISHO KWA MFALME KIJANA NA VIJANA WENZAKE! Lakini kijana mwenye babu hai akamkimbilia pale ufichoni kumwuliza sasa vipi, Babu, tufanyeje?



Babu alifika kwa Mfalme na kamba. Mwisho wa kamba palikuwa na chura. Joka kumwona chura alimuachia mfalme kufukuza nyama tamu ile na hapo ndipo jeshi lilipoweza kumwua nyoka.


Mfalme alimshukuru na kumpongeza kijana kwa kunusurisha maisha ya babu yule pia akajirudi kusema hamna kiungo katika maisha ya jamii au mtu binafsi kilielemaa kiasi kwamba hakina kazi!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

hadith ya manyanya imetulia, japo ni kweli wazee wamepitwa na wakati

natuurmanjak said...

Maisha ya kujifurahisha na kupata kujua kama tanzania.
Mimi ni wa blog yako, tangu blog yako ni ya thamani!
Mimi nataka kikundi kujifunza zaidi!
wengi salamu kutoka Ubelgiji na Guido ... natuurmanjak