Thursday, June 23, 2011

MIAKA NANE YA NDOA, LAKINI HAYA MAUZA UZA NINAYOYASHUHUDIA NABAKI KUJIULIZA, TATIZO NI MALEZI AU NI WAPAMBE?

Ndio, leo hii natimiza miaka nane ya ndoa, lakini nikiwa peke yangu.
Sio kwamba mwenzangu katangulia mbele ya haki, au amesafiri, la hasha,
yupo, tena hapa hapa mjini, yu buheri wa afya kabisa.
Siku kama ya leo, ilikuwa ni furaha isiyo kifani mimi na mume wangu
tulikuwa tumesimama madhabahuni tukila kiapo cha ndoa mbele ya wazazi
wetu, ndugu, jamaa na marafiki. Nakumbuka nilikuwa nimemuangalia mume
wangu usoni wakati alipokuwa akitamka yale maneno ya mwisho ya kiapo
yasemayo, “mpaka kifo kitakapotutenganisha” Alikuwa akionekana dhahiri yale maneno yalitoka katika moyo wake ambao
ulijaa upendo wa hali ya juu, upendo ambao kwangu mimi niliuona
dhahiri ni maalum kwa ajili yangu. Nilimuamini sana mume wangu tangu
aliponitamkia miezi kumi na nane iliyopita kwamba ananipenda na
angependa tuoane.
Naikumbuka vizuri sana siku nilipokutana na mume wangu, ni siku ambayo
kamwe sitakuja kuisahau katika maisha yangu, sijui nisemeje lakini
ninachoweza kukushirikisha wewe msomaji ni kwamba, huyu alikuwa ndiye
mwanaume wa kwanza kukutana naye na moyo wangu kulipuka katika penzi
zito lisilo na mfano.
Mwanzoni mwa maisha yetu ya ndoa, nilianza kuhisi jambo, kwani
nilianza kushuhudia ndugu wa mume wangu wakiwa ndio washauri wakuu wa
mume wangu. Nilijikuta kila mara nikiwa nimeachwa nje kwa kila jambo,
yaani nilikuwa sishirikishwi kabisa katika mambo muhimu ya kifamilia
jambo ambalo lilikuwa linaniuma sana.
Kwa kuwa mume wangu ana uwezo kifedha kwa kiasi fulani, amejikuta
akiwa amezungukwa na ndugu kiasi kwamba wao ndio wamekuwa wakimtegemea
kwa kila kitu mpaka kusomeshewa watoto, na wanahisi labda ndugu yao
angeweza kuwasaidia zaidi, kama sio uwepo wangu yaani kuolewa kwangu.
Nadhani hapo nyuma alikuwa akiwapa misaada mingi sana na huenda tangu
anioe kumetokea upungufu wa misaada tofauti na zamani kwa sababu ya
majukumu ya kifamilia ambayo hakuwa nayo hapo nyuma.
Katika kila ndoa kama mnavyojua kuna kutofautiana kimitizamo na
kukwaruzana kwa hapa na pale kitu ambacho hakiepukiki. Ila kitu
kilichokua kina ni sikitisha ni pale tu mwenzangu anapokua hajali
ushauri wangu na kufata ule wa ndugu zake.
Nilipokuwa najaribu kumshauri mwenzangu, anakuwa ni mkali kupindukia,
ilifika mahali nikajiona kama mtumishi wa ndani.
JUU YA KIDONDA UKAWEKWA MSUMARI WA MOTO
Nikiwa bado nasakamwa na yeye mwenyewe pamoja
na ndugu zake, na kama hiyo haitoshi mnamo Januari mwaka
huu nikampoteza baba yangu.
Ulikuwa ni msiba mzito sana kwangu, kwani, baba yangu alikua kama
ndiye baba wa mume wangu, ametusaidia sana walau kufikia hapa
tulipofika. Alikuwa ni baba mwenye busara sana na mwenye upeo wa hali
ya juu katika masuala ya kifamilia. Alikua akitatua matatizo yetu
mengi sana pale tunapokwaruzana na kutaka kusawazishwa ili maisha
yapate kuendelea.
wakati tunajiandaa na kumaliza 40 tangu baba yangu afariki, siku moja
akaja dada yangu kwa baba mkubwa ambaye ameolewa na mjomba wa
mume wangu. Dada yangu ambaye nilitarajia angekuwa upande wangu, alinitamkia bila kutafuna maneno kuwa wanafamilia ya mume wangu wamefurahi sana na pia
kufanya sherehe baada ya Baba yangu kufariki kwani sasa matakwa yao ya
mimi kuachika yatatimia, hakuishia hapo alitoa maneno mengi ya
kashfa dhidi yangu. Wakati wote mie nilibaki kimya nikiwa siamini kile
kinachotokea mbele yangu.
Baada kusema yale aliyosema na roho yake kuridhika aliondoka huku
akiendelea kunipiga vijembe. Nilibaki pale kwenye kiti kama
walivyonikuta nikitafakari juu ya kadhia ile….. Naam baada a
kutafakari mtiririko wa matukio yaliyopita kati yangu na mume wangu
tangu baba yangu afariki nilianza kuamini maneno ya ndugu zake. Kwani
tangu baba yangu afariki nilianza kuona mwenzangu anabadilika,
hanijali tena na alikuwa na majibu ya ovyo ovyo hata kama namuuliza
jambo la msingi. Nadhani alikuwa ananiheshimu japo kwa kiasi kidogo
kwa sababu ya kumuogopa baba, na kwa kuwa baba ameshafariki, sasa ni
nani nitamkimbilia ili kutaka kusawazishwa pale tutakapokuwa
tunatofautiana………..Nikajua sasa nimekwisha, nilijikuta nikitamka
maneno hayo kwa sauti, nilishtuliwa na sauti yake akinijibu, “ni bora
umelifahamu hilo mapema” hata sikujua aliingia pale ndani saa ngapi?
Hata sikumjibu, nilibaki kumwangalia tu kisha nikaguna, niliingia
chumbani na kujitupa kitandani, ambapo nilipitiwa na usingizi mzito.
Nilishtuliwa na mwenetu pekee wa kiume ambaye ndio alikuwa ametimiza
miaka 6, alikuwa amerudi kutoka shule. Niliamka na kumkumbatia
mwanangu huku machozi yakinitoka. Mwananu alishtuka na kuniuliza,
“mama unalia?” Nilimdanganya kuwa nimemkumbuka babu yake, yaani baba
yangu, mwanangu aliniambia pole na nilimuona dhahiri na yeye akiwa
amegubikwa na uso wa huzuni.
Sikujua kwamba ule ulikuwa ndio mwanzo wa Segere, kwani baada ya
kumaliza 40 ya baba siku kama ya 5 hivi, nakumbuka ilikuwa ni Februari
18, 2011, ulizuka ubishani kati yangu na mume wangu ambao ulizua mzozo
mkubwa tu. Nilijikuta nikapandwa na hasira na kumbwatukia yale maneno
yote niliyoambiwa na ndugu zake.
Mwenzangu katika hali ya taharuki alikasirika sana na nilishangaa
kumuona akichukua baadhi ya nguo zake chache na vyeti vyake akatia
kwenye gari na kuondoka zake, kwa kuwa ilikua usiku wa manane
nikampigia mama mkwe simu kumueleza, maana lolote laweza tokea. Kwa
ufupi mama hakuchukua hatua yeyote ile, na wala hakuja kwangu kujua
sababu ya mume wangu kuondoka katika mazingira ya kutatanisha.
Hata hivyo nililala nikijipa moyo kuwa huenda atarudi kwani alikuwa
amekunywa pombe kidogo, na labda kutokana na hasira na ndio maana
akaamua kuondoka, ingawa jambo lile kwa kweli lilinishtua kwa sababu
tangu tumeoana haijawahi kutokea tukatofautiana kiasi cha mume wangu
kuikimbia nyumba yake. Ndugu msomaji labda unaweza ukashangaa
nikikueleza kwamba mpaka leo hii ambapo ndoa yetu inatimiza miaka 8
sijamtia machoni mume wangu.
Juhudi za kumsihi mama mkwe atusuluhishe zimegonga mwamba kwani
alinitamkia waziwazi kwamba amemchukua mtoto wake na anaishi naye
nyumbani kwake mpaka hasira zitakapo muisha! Alienda mbali zaidi na
kudai kwamba haoni sababu ya kukaa kikao maana hakuna mtu katika ukoo
wangu ambaye wanaweza kumuita na kuongea naye!
Kauli hiyo iliniuma sana. Nilijiuliza, hivi ina maana mimi kufiwa na
wazazi wangu hakuna ndugu yangu anayestahili kuthaminiwa na ndugu wa
mume wangu? Je ina maana hata yale maneno waliyonieleza kuwa
wamefurahia baba yangu kufariki ni kweli?
NAJIULIZA!
Je nifanyaje? Nianze mchakato wa kudai talaka ili niwe huru? Kwa kweli
sina uhakika hata kama tukisuluhishwa sidhani kama tutaweza kuishi kwa
amani, maana kuishi na mtu huku ukiwa unajiuliza je tukigombana
ataondoka tena? na hiyo kama ataondoka nitakuwa na hali gani? mgonjwa?
sina kazi? sina uwezo wa kutunza mtoto? Maswali ni mengi kwa kweli.
Jambo hili linaniumiza sana maana nilijua nimekwisha pata asilimia
kubwa ya vitu ambavyo nilikua navihitaji katika maisha kwa mfano
tayari nimeshapata mume, mtoto, kazi nzuri kwa hiyo nilichokua nawaza
ni maisha ya kiroho, lakini sasa imenilazimu nirudi tena kujipanga
upya.
Dada Yasinta nimeona nikutumie mkasa wangu huu ili kuwashirikisha
wadau wa kibaraza chako cha MAISHA NA MAFANIKIO, kibaraza ambacho mimi
ni msomaji mzuri na nimekuwa nikifuatilia mijadala mingi unayoiweka
hapo ambayo inawavutia wasomaji wengi ambapo maoni na michango
inayotolewa ni darasa tosha.
Ni imani yangu wasomaji wa kibaraza hiki watatumia busara zao na kutoa
maoni na mitizamo yao kwa uhuru na haki bila kupendelea upande wowote.
Sikueleza hayo hapo juu ili kujidhalilisha, bali kutaka kupata
suluhisho ya kile ambacho nakabiliana nacho nikiamini kwamba sisi kama
binaadamu kuna wakati tunahitahi ushauri kutoka kwa wenzetu ili tumudu
kukabiliana na changamoto za maisha.
Natanguliza shukrani zangu za pekee kwako na kwa wadau wote wa Blog
popote pale Duniani.

Ni mimi msomaji wako.
Dada Gly

16 comments:

Mija Shija Sayi said...

Kwa ufupi amekupunguzia mengi....!!

Hadi hapo mume wako anadhani, wewe kuwa naye ni kwa sababu wewe(mke)ndio unamuhitaji yeye(mume) zaidi kuliko mnavyohitajiana...

Ingekuwa mimi ndio wewe..ningepiga magoti na kumshukuru Mungu kwa kuniondolea tatizo...

Anonymous said...

Dada yangu,mama yangu.pole sana kwa matatizo ya wewe na mummeo.kwa kwejinsi ulivyo jieleza naweza kupata picha kamili ya jinsi unavyoumia moyo.ningekuwa mimi ndiyo wewe,) ninge usikiliza moyo wangu na nafsi yangu vina vinana niamulianini. ningemshukuru mungu na baadaye kuamuaa vile ninavyo taka mimi (wewe).ningekata shauri kutoutesa tena moyo wangu,kwa mtu asiye nithamini.nisinge sikiliza ushauri kutoka kwa mtu yeyeyote unao nielekeza kuendelea kumvumilia kwasababu tu eti yeye ni mwanume.vilevile ukifuata viapo vya kanisani( kwenye tabu na raha)siyo hivyo hayo nimakusudi tatizo la kaka zenu wa kitanzania wakipendwa sijuwi wana kuwa wehu,unakuta jamaa na mke mzuri sana kwa sura umbile hata tabia,lakini bado jamaa lina mtesa mtoto wa watu,huu ni ushenzi.anyway fanya maamuzi kutoka rohoni kwako usifikirie watu watasemanini,fikiria wewe unasema nini na unataka nini.watu wapo tu. pole san .Kaka S.

Rik Kilasi said...

Kwa mtindo huu ni kweli ndoa ndoano! Dada pole sana kwa yaliyokukuta.wanasema karibia kila kitu hutokea kwasababu fulani cha msingi mshukuru Mungu kwanza kwani hujui amekuepusha na nini.Aidha ushauri unaopata hapa uchukulie kama changamoto ya yale unayotaka kuyafanya, itakua ngumu sana kwa mtu baki kukuamlia ufanye nini na kwakua wewe unajua mlikotoka na mumeo na mpaka mmefika hapo na wewe inaonyesha kwasasa ndio unamuhitaji ila yeye hana mpango na wewe (kitu ambacho sio haki na mapenzi kwaujumla yamekwisha)

Mimi ningekua wewe ningefungua ukurasa mpya wa maisha huku nikimuomba Mungu maisha yaendelee.Hujakatwa mikono kwahiyo unaweza endeleza maisha Mungu hamtupi mja wake! Inasikitisha sana ila tu jipe moyo.

Baraka Mfunguo said...

Talaka sio suluhisho ya tatizo. Msingi wa tatizo ni kujua tatizo baina yako na yeye. Mwisho wa siku inakuja kujulikana. Katika maisha kuna changamoto nyingi na hili kwako ni changamoto na si kwako tu hata sisi wengine tuliokishuhudia kisa hiki kupitia blogu ya Ruhuwiko na wale wanaotarajia na waliokwisha funga ndoa.

Kimsingi majuto huja baada ya tukio. Na ndio maana tukaita MAJUTO NI MJUKUU. Jishushe ili mambo yaende. Inawezekana kwamba kila mmoja wenu anaonekana ni mjuaji kuliko mwenzake. Tafakari mustakabali wa maisha yenu ya ndoa na mwenzako. Mkabidhi MUNGU changamoto ulizonazo lakini kamwe usisubiri mtu wa nje kuja kukutoa katika changamoto hiyo. KABILIANA NAYO NASI TUTAKUUNGA MKONO.

raynjau said...

Can Marriage
Withstand
the Storm?
--------------------------------
“What God has yoked together let no man put apart.”—MATTHEW 19:6.
----------------------------------
When Marital Disagreements Arise
HOMES that looked sturdy were swept off their foundations, their structures ripped to shreds. As monster storms hit large areas around the globe recently, the quality and durability of countless buildings were put to the ultimate test
A storm of another nature, however, is wreaking havoc on the foundation and structure of the age-old institution of marriage. “For better or worse, marriage has been displaced from its pivotal position in personal and social life,” states family historian Stephanie Coontz.
Can you see the effects of such a trend? Do you feel that marriage is losing its honored place in society? If so, why is this happening? And what hope does anyone have of securing or maintaining a happy marriage? First, though, what is putting marriage in danger?
Marriage Under Attack
The attacks on marriage are not new; they go back to the beginning of human history. Qualities and attitudes that developed in our first human parents have led to the marriage crisis we experience today. Adam and Eve sinned when they gave in to selfish cravings, and thus “sin entered into the world.” (Romans 5:12) The historical record of the Bible states that soon after this, “every inclination of the thoughts of [man’s] heart was only bad all the time.”—Genesis 6:5.
Not much has changed since then. Among the corrosive inclinations that plague marriage is the uninhibited pursuit of selfish gratification.

emu-three said...

Maisha ya ndoa tafsir yake ni pana, na wengi husema hayana `fomula' au utaratibu mmoja, kila mtu ana njia yake, kwani wanadamu hutofautiana katika kutafakari na kuwa na maamuzi anuai.
Mume na mke wanapooana tunategemea kuwa na nguvu imeongzwa katika familia au kati ya mume na mke, na hili kiukweli utaliona kama hujaoa au kuolewa kwa muda mrefu.
Swali kubwa, je nitampataje wa aina niitakayo...hili ndilo swali la kila mtu anapofikia hatua ya kumtaka mwenzake.
Kuna maoni nilitoa kuwa kabla hujaingia kwenye hicho kizimba cha ndoa, ujaraibu kutafakari wewe ni nani na umtakaye unataka aweje..hili litapunguza `msuguano' ingawaje msuguano katika ndoa upo, hata mpendane vipi.
Kwa tatizo lako mpendwa, mitihani ipo katika ndoa, na huwezi amini wapo ambapo unawakuta mitaani wanacheka wanakumbatiana, lakini wakiwa ndani..ni huzuni kwa kwenda mbele...ina maana wanavumilia huku wanaumia.
Ndoa ni kati ya mume na mke, na nyie wawili ndio mnaoweza kujenga au kuvunja ndoa...jadilianeni , peaneni muda, tafuta vijarida, msome kwa pamoja, ikizidi mnatafuta washauri...ambao mnawaamini hasa watu wa dini, au wataalamu wa ndoa..wapo na wanasaidia! Lakini hili litawezekana ikiwa nyie wawili mumekubaliana ...mumeamua kuijenga ndoa yenu.
Wanandugu wawe tu kama wageni, wawe tu kama washauri, lakini maamuzi ni yenu wawili.
Kama alivyosema mwenzangu , kila jambo hutokea ili iwe sababu, hayatokeii tuu hivihivi..ukiona mambo ni machungu, muombe mungu wako na fungua ukurasa mwingine, kwani huo msamiati wa `talaka' usingekuwepo ila kwa machungu, taabu, dhiki na mengineyo...ila hilo liwe ni jambo la mwisho kwani watoto wanahitaji upendo wa baba na mama, isije ikawa vita vya tembo wanaumia ni nyasi.
Nitaisoma tena hii habari maana unaposoma kwenye intenet cafe muda ni mdogo wa kutafakari...
Nami nafikiria jinsi ya kukutungia kisa, kutokana na mkasa huu: Nitembelee kijiweni kwangu, ILI KAMA utaniruhusu niandae kisa kinachoshabihisan na tatizo lako humoo ndani tunaweza kupata mafunzo

Anonymous said...

dada pole sana,
ndoa ni ngumu sana, tena shukru wewe umeachwa kwenye nyumba mimi nilifukuzwa na akaoa mwingine hata nguo zangu alikatalia nilivyoenda kuchukua nilipelekwa police na mdogo wake kwamba nimeenda kuiba, nna miaka sita hatuko pamoja alishaoa na wamezaa watoto wawili na mimi tulizaa watoto wawili, lakini juzi nimeitwa mahakamani amefungua kesi nimemtelekeza miaka sita, anataka nimpe talaka arudishiwe mahari, wewe acha wanaume wengine sijui walilaaniwa na nani, mpaka sasa sitamani kuingia kwenye ndoa tena, kwa hiyo tunakesi mahakamani mpaka sasa.

chib said...

Duh!!

Bi Mkora said...

Tatizo lako halina tofauti na matatizo wanayokumbana nayo wanawake wengi wa kiafrika kutokana na wana ndugu au wana ukoo kuingilia mambo ya familia ya ndugu/mtoto wao. Lakini tatizo kubwa liko kwa mwanaume mwenyewe ambaye ameshindwa kubalance haki za ndugu/clan/wazazi wake na haki za familia yake. Je hakuambiwa huko kanisani kuwa atawaacha ndugu zake ili awe mwili mmoja na wewe?na mnaomwambia alikiunganisha mungu mwanadamu asikitenganishe ni nani anayekiuka hayo maandiko kama si mume mwenyewe na ndugu zake.

Viweje mwanaume mzima akaacha mkewe na kitanda chake eti akakimbilia kwa mama au ndugu zake, ni mwoga au ni zuga zake za kwenda kuishi na mwanamke mwingine t? maana kama alibeba vyeti vyake ina maana alishaanza mipango ya kukuacha siku nyingi akanunua na kitanda cha kulalia, akatafuta na mtu wa kulala nae, na hili la kukimbiwa kitanda chako si la kuvumilia maana siku hizi kuna maradhi waweza pata ushawishi ukakaribisha mtu kupasha joto kitanda cha mtoro matokeo yake ukabeba maradhi, au yeye huko alikoenda kulala kwenye kitanda kingine aweza kubeba maradhi.

Nikupe siri wanaume wengi wakishapata wanawake wengine huanza vibweka taratibu na kama anasupport ya ndugu zake basi huwaonyesha huyo bibie mpya na wao humsifia kuwa huyu mzuri kuliko yule na yuafaa sana na matokeo yake huwa kama yaliyokukuta. Cha kufanya waone viongozi wako wa dini waliokufungisha hiyo ndoa, waelezee matatizo yako, kubali usuluhishi kama atakubali lakini ukae mguu ndani mguu nje maana inaelekea jamaa ana akili za kushikiwa, hivyo jiandae kwa lolote, na vile vile akikubali kurudiana shubiri chungu kupima na kutunza afya yako lazima usije acha yatima kwa kuendekeza peremende!

Lau kama hataki usuluhishi kwa kuwa huko keshafika mwisho wa reli, mwambie mmalizane muachane kisheria kwani shubiri ni dawa ingawa ni chungu, ili uweze kuendelea na maisha yako ama sivyo utabaki kuumia kila siku na hilo gume gume lilowashinda mitume. MWANAUME HAKIMBII MATATIZO YA NYUMBANI KWAKE hata iweje, labda akufumanie na mwanaume mwingine, lakini huyo ni COWARD!

Anonymous said...

mimi ningependa kuchangia kama ningejua upande wa pili washilingi maana inawezakuwa huyu mama aliyetaka ushauri sii ajabu yeye peke yake ndiye chanzo ya tatizo maana huwezi jua mume wake naye angepatikana aseme mapungufu ya mke wake ingekuwa vizuri kwa hiyo mimi sina lakumshauri zaidi ajichunguze yeye kwanza

Dada Gly said...

wapendwa nashukuru kwa maoni yenu, nimepita tu kidogo leo nitaendelea kukusanya ushauri wenu ninaahidi kurudi tena kueleza hatma yangu. M3 wasailiana na Kapulya atakupa e-mail yangu tuwasiliane. Nawashukuru wote hasa rafiki yangu wa hiari.

Anonymous said...

Pole sn dada yngu! Maisha ya ndoa magumu na yanahitaji uvumilivu sn. Mkasa wko unafanana na wngu ila me ha2jaachana naye! Mm nimeachwa 2 nyumbani nimekuwa km housegirl sina ninachoshirikishwa wala kupewa taarifa anashauriana na mama yke tu. Ila me nashukuru ndugu zake pamoja na wifi zangu ndio wafariji wngu. Alinunua gari cjapewa taarifa ila kwa maombi yngu mungu akatenda miujiza likaibiwa ila yy hajui km ni laana yngu na masononeko yngu. Mambo yke ynamuendea kombo sasa anataka kuuza kiwanja. Muombe mungu atatenda muujiza. Ni mm 2la

Anonymous said...

pole sana mpenzi ,inauma sana na hasa ukifikiria ulikotoka naye,muhimu ni wewe kushukuru mungu kwa yote yaliyotokea na umkabidhi mungu yote na kwa namna mumeo alivyokutenda umtakie mwisho mwema endelea kusali muombe mungu wako ukimkabidhi maisha yako kazi zako na kumkabidhi mungu mwanao,mlilie mungu kila siku ipo siku ataonyesha muujiza kwako na utafanikiwa hayo yote ni mapito na mungu anasema ktk biblia yeye atakuwa ni shahidi wa mume au mke wa ujana wako pia biblia inasema kila chozi litapimwa na ukumbuke pia malipo ni hapahapa duniani hukumu ni kwa mwenye enzi mungu omba mungu ukiamini atakusaidia,hiyo issue yako ni typical kama ndoa yangu hivi sasa imetubidi kumueleza baba padre aliyetufungisha ndoa ili tutengane tena kidogo bora mumeo mimi mume wangu alikuwa anaingiza hadi vitoto ndani kwangu chumbani ktk kitanda chetu alininyanyasa mno na mtoto,lakini nimelia na mungu nimefunga na kuomba nikimkabidhi kwa mungu kila leo,nilichoamua kabla ya kutaka kutengana ni kucheki afya yangu nimekutwa mzima ninamshukuru mungu kwa hilo,ameona nianze life peke yangu ila ndugu yaku muamini mungu na masononeko yako na chozi lako ulilolitoa kwasababu yake ipo siku vitalipwa hapahapa duniani,pole sana be strong.

Anonymous said...

Ndoa kwa kweli siwezi hata kuisimulia, sikuwahi kuiona raha ya ndoa ndani ya miaka 6, hiyo haitoshi mwaume akanigeuka mpaka hela ya chakula akawa ananinyima na nlikiuwa na watoto wawili. nilikonda mpaka watu wakfikiria nimeathirika yeye anatumia vidonge ndo maana yeye mnene. na hiyo pesa tuliitafuta yote tulipofanikiwa mwenzangu akanigeuka. nilivumilia nikachoka nikasema inatosha sikuumbwa nae mpaka nifie kwake acha nikafie kwingine. mwanzaoni iliniwia vigumu kuzoea lakini baadae nilizoea nikamuomba mungu nikamwabia wewe ndo uliyenileta hap duniani unajua mwisho wangu. nilisoma kakozi fulani nikamuomba mungu akanipa kazi, sasa hivi nimenenepa kama siyo niliyekuwa mke wake, anashangaa. sitamani kuolewa tena maana nahisi hawa wenzentu tabia zao zinafanana. muombe Mungu atakusaidia na utamsahau. kama Mungu alipanga huyo ndo mme wako atarudi na atabadilika, lakini kama sio mpango wa mungu utamsahau na mungu atatenda muujiza mpaka utashangaa

Anonymous said...

kama na wewe hunatatizo lolote na unakazi yako tulia enderea na kazi kama yy ndoanamakosa au anakukosea najua utafanikiwa tulia mwondoe kwenye mawazo yako ingawa ni vigumu lakini mwishowe jibu utalipata

Anonymous said...

hermes outlet
cheap jordans
goyard
supreme
off white jordan 1
kyrie 7 shoes
golden goose outlet
hermes outlet
bapesta shoes
off white shoes