Monday, April 18, 2011

WANAUME NA KAULI HIZI: 'HUYO SIO WA KUOA, NI WA KUCHEZEA TU'

Bila shaka wewe msomaji unayesoma hapa utakubaliana na mimi kuwa umeshawahi kuzisikia kauli hizi kutoka kwa wanaume pale anapozungumziwa mwanamke mzuri kwa sura na umbo.

Kwa kawaida vipimo vya uzuri wa mwanamke kwa wanaume vimegawanyika. Wanaume wengi hupima uzuri wa mwanamke kwa sura au umbo, lakini linapokuja swala la kuoa, suala la tabia na mwenendo hupewa nafasi kubwa.

Na ndio maana wakati mwingine unaweza kushangaa kukuta mwanaume ambaye ni hodari wa kuchagua wanawake wazuri, lakini ukija kumuona mke aliyemuoa, utakuta ni mbaya kwa sura na umbo, lakini kwa upande mwingine utakuta mke huyo ni mzuri katika maeneo mengine kama vile, tabia nzuri,upendo, wema, na anayemudu malezi ya watoto katika familia.

Sifa nyingine ni zile za kumkubali mwingine kirahisi, kuwa tayari kusaidia yanapojitokeza matatizo katika familia, mpenda amani na kumfanya mume wake aone kuwa hakukosea kumchagua yeye kuwa mke wake. Kwa kifupi wanawake wa aina hii hata kama wangekuwa ni wabaya kwa sura na umbo bado wako kwenye nafasi ya kuonekana kuwa ni wazuri, na huolewa kirahisi zaidi.

Wanawake wazuri kwa sura na umbo ambao tabia na mienendo yao hairidhishi wako kwenye nafasi kubwa ya kuishi bila kuolewa, na kwa bahati mbaya zaidi wanawake wengi wanaohesabika kuwa ni wazuri, tabia na mienendo yao ni ya kutilia mashaka. Wanaume wengi huvutiwa na wanawake hao kujenga uhusiano nao hasa wa kimwili tu na si vinginevyo, na ndio maana wanawake wazuri kwa sura na umbo wanalo soko kubwa sana kwa wanaume, lakini huishia kuchezewa zaidi kuliko kuolewa.

Wanaume nao kwa upande wao wamejenga dhana kwamba wanawake wazuri sana sio wa kuoa na hivyo kuwaogopa. Wanaamini kwamba wanawake wazuri sana ni wasumbufu, kitu ambacho kina ukweli kwa kiasi fulani. Wanaume wanaamini kwamba wanawake wazuri sana kwa sura na umbo huwasababishia waume zao maradhi ya moyo,shinikizo la damu na wakati mwingine hata kuwafanya kupata matatizo fulani ya kiakili, na hiyo inatokana na waume hao kuwa katika mashaka ya wake zao kuchukuliwa na wanaume wengine wakati wowote kutokana na uzuri wao. Hata hivyo wanawake wazuri nao huwaendesha waume zao wakijua kuwa ni wazuri na soko lao liko juu na waume zao nao huwanyenyekea wakihofia kuachwa.

Na ndio maana usishangae kuona kuwa wale wanawake ambao watu wamekuwa wakiamini kuwa ndio wabaya kwa sura au umbo lakini tabia na mienendo yao ni mizuri ndio wanaoolewa na hata ndoa zao zinadumu, tofauti na za wale wanaoonekana kuwa ni wazuri sana kwa sura na umbo na ambao tabia na mienendo yao si mizuri, ndoa zao hazina umri mrefu.

12 comments:

Raymond Mkandawile said...

Nimelipata somo hilo dada yake...hasa ukizingatia ndiyo nipo kwenye mchakato wa kutafuta mwenza.big up sana.

Goodman Manyanya Phiri said...

@ Mkandawile

Nilitumia muda kuongea na Mkandawile kwani ukoo wao nahisi naulewa sana. Pia nafurahi sana kutafutiwa SISTER-IN-LAW (shemeji???). Kwa wasiojuwa chimbuko: Mkandawile hawa wanatokea nchini Afrika Kusini/Swaziland ambamo lipo kabila la Waswazi na mwanzilishi wake Mfalme Sobhuza-I ambaye chimbuko lake alikuwa Mtonga wa Msumbiji. Mfalme alipofika Swaziland/Afrika Kusini alikuta eneo la Waswazi wa leo wapo wenyeji waliojulikana kama “Makhandzambili”, maana yake “Wale sisi Watonga kuliewakuta mbele”. Baada ya kufika kwa Waingereza Afrika Kusini ukaanza mzozo na vita vya makabila kutokana na kukamatwa kwa watumwa na Waingereza na watu wengi sana wakaondoka Afrika ya Kusini kwelekea Afrika Mashariki. Wengi wao walitokea kwa kabila laMakhandzambili. Kufika huko Afrika Mashariki wenyeji huko hawakua na uwezo wakutamka “Khandzambili” na badala yake jamaa hawa wakaitwa “Mkandawili”.


Ndani ya tundu sasa:


Mkuu, Mkandwile: Inategemea tena nia zako za kuowa ni zipi.

Kama moja yake ni kuzaa, zingatia kwamba je, unayemuaza kazaliwa peke yake kwa wazazi wake (hatari) au wako wengi (busara).

Kama moja ya nia zako ni kupata msaidizi katika shughuli zako, basi tazama alama katika mwili wake za uchapakazi... ziko nyingi sana alama na sitakwambia hapa... fikiria mwenyewe.

Kama unataka mchaMungu, sikiliza kwa makini unapokwenda kumtembelea kwao: anaposhusha sauti kila kukitokea matatizo kwao juwa huyo siMchamungu, bali ni msiri asiependa ukweli na ukimwoa utakiona cha mtemakuni.


Sura, kabila (hata akiwa Mzungu, Mchina, Mhindi, Mkaburu au kabila lolote lile), umbo hata akiwa kipofu au kilema cha namna gani si mhimu kabisa.


Ya mwisho: kumbuka kwamba yule utakaemchagua, umechaguliwa VILEVILE na Mungu wako. Usimdharau hapo baadaye. Ukifanya hivyo, nakuhakikishia utakuja kujiunga nasi wakongwe katika raha ya ndoa!

Goodman Manyanya Phiri said...

@NaNgonyani

Nakushukuru sana kwa kuanzisha mjadala kama huu. Wengi wanaogopa kuanzisha. Lakini ni vizuri sana tujadiliane kuhusu mambo haya ya kuleta duniani vizazi vijao.

Kwa maoni yangu: hamna mwanamke mbaya duniani. Wote ni wa zuri tu.


Kuhusu kauli ya wanaume nani achezewe nani aolewe, ni haki yao ya maoni; kama vile wanawake nao wanatuzungumza sisi wanaume.

Labda nyongeza kwa ['wanawake wabaya na wazuri']: Mwanamke mbaya ni yule tu asiejali mpenzi wake anampikia chakula gani...yaani mwanaume anampikia hata takatata au anamwambia "tuende tukale hotelini".

Huyo basi hataolewa kabisa! (najua nitashambuliwa na niko tayari kula risasi)

Anonymous said...

Dada ulosema ni ukweli kabisa. Naona wanawake wengi wazuri tu lakini wapo wapo na si kuwa hawataki kuolewa ni kwa sababu either wanaogopwa au hawana maadili. Kikubwa wadada tujitahidi kutunza heshima zetu. Tena unapokuwa mzuri sana ndo unatakiwa utulie kweli kwani watu ni wepesi wa kuona maovu ya wadada wazuri.

Unknown said...

dah hili nalo neno.Linaukweli sana tu.na nimeshalisikia mara nyingi tu.

Anonymous said...

Da Yasinta,umenena lakini mimi kidogo nitatofautiana nawewe katika kubainisha kauli hii /hizi .saikolojia ya mwanaume nihatarisana, ina wingi wa vitisho,ubabe kejeli pindipo swala la mwanamke linapo ongelewa,iwe kwa mazuri au mabaya.ukimsikia mwanaume anasema huyo si wa kuoa juwa basi kunakitu kilitokea kuhusu huyo mwanamke anayesemwa si wakuoa bali ni wakuchezea.hakuna mwanume anaye taka kuoa mwanamke mbaya kwa sura,ila tu hushindwa kumpata au wengi wetu hushindwa katika kinyanganyilo cha kumpata mrembo huyo.na amini nakwambia wanawake wazuri hawanatatizo sana kama watu wanavyo wasema.ni sisi wanaume ndiyo tuna wafikisha hapo kwani utakuta mtu/mwanaume anasema umeliona toto hilo ,nitafanya kila kitu nilipate.hapo kwenye neno kilakitu ndo hapo huwa tunakosea wanaume.inamaana utaanza kumpa vitu ambavyo wewe unafikiri vita mvutia kwako kumbe ndo unaharibu,kunakuwa hakuna penzi la kweli.matokeo yake vile vitu ulivyo mzowesha vikiisha binti anakukimbia kwa sababu halikuwa penzi la ukweli. sikuzote hakikisha hulazimishii penzi uwe mwanaume/mwanamke athali zake nikubwa unapo lazimishia penzi.wanaume tuna bahati ya kuwa na nafasi ya kuchagua mke unaye taka kumuowa, kitu ambacho ni kigumu sana kujuwa je upande wapili ndivyo hivyo(dada zetu)ufikiriwavyo.anyway ngoja niishie hapa. kaka s

Rachel Siwa said...

Asante da Yasinta kwa somo zuri nakuunga mkono kwa uliyonena!!!!Nikuite Kungwi!!!!!!!

Raymond Mkandawile said...

Kaka Goodman nashukuru sana kwa introduction yako nzuri nimeipenda sana kwani ndiyo hasa yenyewe.
Pia nashukuru sana kwa mwongozo wako ktk kipindi hiki nilichonacho cha mchakato wa kuoa,nimejifunza mengi sana na nitaendelea kujifunza mengi zaidi kwako na kwa wengine wakongwe katika ndoa.Nitafurahi iwapo utaendelea kunishauri zaidi tumia email hii;raymonds19@yahoo.com au tembelea; http://www.mkandawilejr.com

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Wanawake wazuri wazuri wameolewa, yamebaki manungxyz (naogopa kumalizie nisije kwidwa bure). Vinginevyo somo limedurusiwa na kueleweka vilivyo. Asante Da Yacinta kwa kuibua hili.

Goodman Manyanya Phiri said...

@Raymond

Asante kwa kushukuru; nami nimekwishajiunga na blogu yako. Pia napatikana daima 24/7 kwa namna hizi:


manyanyaphiri@gmail.com


SHORT MESSAGING SERVICE (sms)+27833087713

Asanteni wote!

Unknown said...

Ahsante sana dada Yasinta kwa somo hili kwani linaukweli ndani yake.

Anonymous said...

wanawake/wasichana wengi siku hizi wako single kutokana na wanaume wengi kuwa ni presha ndani ya nyumba,mtu anaona bora uishi peke yako.Binafsi ni mwanamke nina only six years ya ndoa na watoto 2,lakini kero ninazozipata na huyu mume wangu hua nakumbuka maisha niliyokuwa naishi na wazazi wangu,strees-free life!!!ila leo kila kukisha ni kakufanyia hivi,mwanaume mzima anakununia,usipombembeleza anaweza akamaliza week hajakusemesha,unajigonga kwake kwa kumfanyia mambo mazuri lakini wapi,gubu mtindo mmoja,unajikuta unamwomba msamaha hata kosa huna,yani ni hedache kwa kweli bora kuishi single au single parent kama unahitaji kuwa na mtoto.Anyway muwe mnatuombea wengine wenye matatizo kwenye ndoa,maana mi najua kuna watu wengine yani unawaona tu wanaenjoy kwenye ndoa,ohh God tusaidie na wengine,angalau tu wenzi wetu watuonyeshe upendo,maana kama alikupenda akasema tuoane why leo upendo unatoweka bila sababu za msingi!au ndio mtu anakuwa amezaliwa tu na kisiraniau ni nini,eh kwaheri bwana,nitaendelea kumlilia huyu Mungu maadamu anapatikana!