Tuesday, March 11, 2014

MAISHA YA NDOA:- KWA NINI NIMEMWOA?

LEO NIMEAMKIA KUSOMA SOMA KATIKA MOJA YA HABARI NILIZOSOMA NI HII NIKAONA NIWASHIRIKISHE PIA. NI KUTOKA KATIKA KITABU:- NJIA YETU KWA MAPENDO NA NDOA. KARIBUNI......
Vincent na Regina walikuwa wa kabila moja. Na walikuwa wamesoma shule moja. Vincent alikuwa amemaliza darasa la 5 lakini ilimbidi kuacha kwa sababu hakuwa na mtu wa kumlipia karo/ada za shule. Regina naye alipaswwa kuachia darasa la 3. Wazazi wake, kama vile wazazi wa Vincent, walikuwa wakulima. Lakini kwa sababu ya uhaba wa mvua kwa miaka kadhaa iliyoopita, wazazi wake walipaswa kuhamia mahali pabaya pasipokuwa na shule karibu.
Vincent alijiunga na baba yake shambani. Regina, baada ya miaka kadhaa alikwenda kufanya kazi kwa wazungu fulani katika mji wa karibu. Alikuwa yaya. Waajiri wake walikuwa wakarimu kwake na mara nyingi walimpa vitu vingi vizuri. Kila wiki alipokea mshahara wake lakini mara nyingi zaidi yeye aliutumia mara tu alipoupokea.
Siku ya soko kila wiki, Vincent alizoea kwenda mjini na bidhaa za kuuza. Lakini kila mara alihakikisha kwamba amemwona Regina kabla ya kurudi nyumbani. Bila shaka siku nyingine Regina alipaswa kufanya hiki  na kile, hivyo hakuweza kuondoka na kufika sokoni. Siku hizo, Vincent alirudi nyumbani akisemasema manenoo yasiyosikika, hivyo mara nyingi wazazi wake walijiuliza ikiwa Vincent ni mgonjwa?
Mwishowe, Vincent na Regina walioana. Vincent alikuwa amejenga nyumba mpya nzuri kwa ajili yao wawili. Mwanzoni kila kitu kilionekana chema kabisa. Ni kweli kwamba mara kwa mara Vincent alikuwa na wasiwasi juu ya Regina. Alijua kwamba Regina alikuwa amejifunza mitindo ya kigeni kwa wale wazungu katika nyumba ile kubwa. Basi, alijisemea kwamba baada ya muda Regina atayasahau kabisa hayo yote na kuwa mmoja wao tena.
Lakini Regina hakuweza kusahau. Alikumbuka vyakula vizuri, sahani na vikombe vizuri, viti n.k. Yeye hatakuwa kamwe na nyumba ya namna hiyo. Polepole alianza kubadili mwenendo wake kwa Vincent. Alikuwa mkimya kabisa, lakini pengine ukimya wake ulibadilika hata ukamfanya afadhaike na kukasirika kwa sababu ya jambo alilosema au alilofanya Vincent.
Kadiri alivyokasirika zaidi, ndivyo alivyojitahidi kumpendeza zaidi. Hakusema chochote aliporudi nyumbani toka shambani akiwa amechoka na kusikia njaa na kukuta chakula hakijawa tayari. Alikumbuka vema aibu aliyopata siku ile ambayo baba na mama waliwatembelea, na Regina akagoma kuwapikia chakula. Usiku, walipokuwa wameondoka, alimpiga Regina, ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kufanya hivyo.
Toka siku hiyo mambo yalizidi kuwa mabaya. Regina aliishi katika nyumba kwa ukimya wa kitoto. Alimjibu Vincent kwa kuguna kila alipomwuliza swali. Hata mara nyingine alikataa kulala na Vincent mpaka naye aahidi kumtendea tendo fulani. Vincent maskini! Hakujua la kufanya. Mara nyingi sana alijisemea: "Maisha ya mjini yamemharibu, kabla yake hakuwa hivi". Alisema kwa sauti ndogo:- "Kwa nini nimemwoa?
Alizidi kutumaini kwamba Regina atabadilika. Miaka ilivyopita Mungu aliwajalia watoto wawili, mvulana na msichana. Hizi zilikuwa ndizo siku njema, wakati kila kitu kilipoonekana kinakwenda sawa tena. Regina alionekana kuwa mtu ambaye Vincent amemtumaini kuwa naye. Lakini jambo fulani likitokea basi, Regina alikuwa anabadilika upesi. Alikuwa anakataa kufagia nyumba, au kupika chakula au hata kuwatunza watoto kwa ujumla.
Wakati kama huu, Vincent alikuwa anajiuliza tena na tena:- "Kwa nini nimemwoa?
Je? hapa wa kumlaumu ni nani na wa kumsikitikia ni nani?
KILA LA KHERI...PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA!!!

2 comments:

Mussa Middy said...

Hapo wa kulaumiwa ni Regina kwasababu ameshindwa kuishi maisha waliyokubaliana na mumeo na hatimaye kutaman maisha mazuri ya mjini. Jaman jaribun kuwa makin ktk kuchagua mke cyo tu eti kwasababu mmesoma wote au mnaishi eneo moja!!!!!!!!!!!!

Yasinta Ngonyani said...

Kaka yangu Mussa! Kwanza karibu sana katika kibaraza hiki. Na pia ahsante kwa ulilosema kuishi maisha ya mke na mume si kazi ndogo. Hasa kama hakutakuwa na PENZI LA DHATI..